Image

Makala hii iliandikwa na Dada Subi wa tovuti ya wavuti.com akizungumzia kuhusu umuhimu wa kufanyika kwa utafiti juu ya dhana ya kuwepo kwa uwezo wa mafuta ya nazi katika kutibu na kuzuia ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer's unaowaathiri zaidi wazee.  Ungana naye katika maoni yake haya.

Baadhi ya watafiti wanasema kiwango fulani cha mafuta ya nazi ni muhimu kwenye chakula kwa kuwa husaidia kupunguza ugonjwa wa kusahau  "Alzheimer's" ambao mara nyingi humjia mwanadamu kadiri umri unavyosogelea uzeeni.

Watafiti wanathubutu kusema, huenda mafuta haya ya nazi yakazuia kabisa kupata ugonjwa huo kwa baadhi ya watu.

Ingekuwa vyema na sisi Tanzania tukafanya utafiti kwa jamii ya watu wanaotumia kwa wingi mafuta ya nazi katika mapishi yao, hasa wale waishio mikoa ya mwambao wa pwani ambapo zao ma mnazi hustawi vizuri na kwa wingi.

Pengine hii ikawa pia sababu kujibu suala la kwa nini yapo matukio mengi ya Wazee na Vikongwe wengi kuuawa kikatili katika mikoa kadhaa nchini Tanzania ambayo zao la nazi ni nadra kuonekana sokoni, achilia mbali kutumika kama kiungo katika mapishi na/au matumizi ya kuchua na marashi.

Nimewaza hivyo kwa kuwa wazee wetu wanaouawa mara nyingi utetezi unaotolewa na wauaji ni kuwa mzee alikuwa na "dalili" za uchawi kwa kuwa pengine alikuwa akisema mwenyewe kama mwehu, akiondoka usiku na kutokomea pasikojulikana, alikuwa akivua nguo mbele ya kadamnasi, alikuwa mwoga au kuonekana mwenye wasiwasi wakati wote n.k., bila watu hao kufahamu kuwa kwa ujinga* wa masuala ya afya ya akili ya binadamu yatokanayo na umri, matukio mbalimbali maishani yaliyoathiri akili na fikira, pamoja na hofu ya uzee kwa vitendo walivyotendewa wengine, wanaweza kabisa kuwa sababu ya matatizo (dalili) na kuishia kuwawahukumu baadhi ya wazee hao kifo pasina hukumu ya haki. Ninaamini kuwa, kama ambavyo wapo waliofungwa jela kwa makosa ya kudhaniwa, kusingiziwa, wasiyoyatenda na visasi, vile vile wapo wanaouawa kwa sababu zizo hizo.

Niseme kuwa, zinazotajwa kuwa sababu (naita visingizio) za kumtuhumu mtu uchawi zinalandana na dalili za ugonjwa wa kusahau "Alzheimer's  disease" ambazo niliwahi kuziandika wakati nikichangia makala za afya katika gazeti la KwanzaJamii (unaweza kuzisoma kwa lugha ya Kiingereza katika linki hii: alz.org).

Makala hii ni kwa hisani ya wavuti.com

Polio ni ugonjwa wa kuambukiza usababishwao na virusi, huathiri neva na kusababisha ulemavu.

Kutokana na taarifa za shirika la afya duniani:

  • Polio huathiri zaidi watoto wa umri wa chini ya miaka mitano
  • Ulemavu hutokea kwa mmoja kati ya maambukizi 200
  • Mpaka 2013 ni nchi tatu ambazo bado kuna mlipuko wa ugonjwa huu wa kupooza Afghanistan, Pakistan na Nigeria. Ila kutokana na Taarifa kutoka wizara ya afya ya Tanzania ilipokea taarifa kutoka shirika la afya duniani kuwa kuna mlipuko katika nji jirani ya Kenya, wilaya ya Fafi.

Je ni zipi dalili za ugonjwa huu?

Dalili hizi hudumu kwa kati ya siku 1 hadi 10

  • Homa
  • Maumivu ya kichwa
  • Kutapika
  • Uchovu
  • Maumivu ya shingo
  • Maumivu ya mgongo
  • Maumivu ya mikono na miguu
  • Misuli kukakamaa

Je ni matatizo gani mtu huweza kupata baada ya maambukizi haya?

  • Kupooza misuli
  • Ulemavu wa miguu

Kati ya maambukizi yanayowasumbua wanawake wengi duniani ni maambukizi ya fangasi. Inakisiwa asilimia 75 ya wanawake wote duniani hupata maambukizi haya katika kipindi cha uhai wao. 

Maambukizi ya fangasi katika sehemu za siri za mwanamke husababishwa na uwepo wa fangasi wanaojulikana kitaalamu kama Candida albicans. Maambukizi haya pia hujulikana kama yeast infection au thrush. Fangasi hupatikana kama vimelea vya kawaida katika mdomo, mpira wa kupitisha chakula sehemu inayojulikana kama pharynx, katika kibofu cha mkojo, uume na hata kwenye uke. 

Mfumo mzuri wa kinga wa mwili pamoja aina fulani za bakteria wanaoishi pamoja na fangasi hawa husaidia sana katika kuthibiti maambukizi yanayoyosababishwa na aina hi ya fangasi. 

Nini hutokea?

Kwa kawaida, Candida albicans huishi kwenye uke na sehemu nyingine (kama zilivyoelezewa hapo juu) bila kusababisha madhara yoyote yale isipokuwa pale mazingira ya eneo husika yanapobadilika kama vile mabadiliko katika hali ya pH ya  eneo husika (ifahamike ya kwamba pH ya kawaida ndani ya  uke ni 4.0 - 4.5) au uwiano wake na vimelea  (microorganisms) wengine unapoharibiwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile matumizi ya madawa aina ya antibiotics, kupungua kwa kinga mwilini kutokana na magonjwa mbalimbali n.k.

Maambukizi haya ya fangasi yanaweza kugawanywa katika sehemu kuu mbili

  • Maambukizi yasiyo makali yaani uncomplicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi  mara moja hadi nne kwa mwaka na dalili zake huwa si mbaya sana na maambukizi haya husababishwa na fangasi wa jamii hii ya Candida albicans.
  • Maambukizi makali yaani complicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi zaidi ya mara nne kwa mwaka, dalili zake kuwa mbaya zaidi au kama maambukizi  yatakuwa yametokea kipindi cha ujauzito, ugonjwa wa kisukari, upungufu wa kinga mwilini. Aina hii kusababishwa na vimelea vya aina nyingine tofauti na Candida albicans. 

Vihatarishi

Watu walio katika hatari ya kupata maambukizi ya fangasi hawa ni  wale wenye

Mchungaji Mstaafu Ambilikile Mwasapile ni jina lililojipatia umaarufu sana katika miezi ya hivi karibuni nchini Tanzania na eneo la nchi za maziwa makuu. Umaarufu wake unatokana na madai kuhusu uwezo wake wa kutibu maradhi sugu mbalimbali  kwa kutumia dawa ya ‘kiimani’ iliyotengenezwa kwa kutumia majani ya mti maarufu sana katika mazingira ya eneo hilo unaojulikana kama mugariga. 

Lakini mugariga ni nini? Tabia zake ni zipi? Je una uwezo wowote wa kutibu maradhi yanayodaiwa kuwa sugu? Ni mti wa kale au umegunduliwa juzi juzi tu?

Mugariga au Carissa edulis kama unavyojulikana kitaalamu au ‘mtanda-mboo’ kwa Kiswahili fasaha si kitu kigeni duniani. Ni mti ambao umekuwepo tangu zama na zama. Kiasili, mti huu unapatikana maeneo mengi sana duniani hasa yale yenye uoto wa kitropiki kama vile Kenya, Tanzania, Sudan, Ethiopia, Thailand, Botswana, Namibia, Myanmar na Afrika ya Kusini (1).

Mti huu upo kwenye familia ya mimea ya Apocynaceae, familia ambayo inajumuisha genera zipatazo 163 za mimea zenye takribani aina 1850 za miti (2). Familia ya Apocynaceae inajumuisha aina kadhaa za miti ambazo zina matumizi mbalimbali kulingana na sehemu zinapopatikana. Kwa mfano kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 1970 na Kokwaro na wenzake huko nchini Kenya (3), ilionekana kuwa aina ijulikanayo kama Acokanthera schimperi imekuwa ikitumiwa kwa miaka mingi na wenyeji wa maeneo ulipofanyika utafiti huo kama sumu kwa kupaka kwenye ncha za mishale na mikuki kwa ajili ya kutumika kama silaha. Hata hivyo, zipo aina kadhaa katika familia hii ya mimea ambazo si sumu na zimekuwa zikitumiwa kwa matumizi mbalimbali yakiwemo chakula.

Matumizi ya mti wa Carissa edulis yanatofautiana kati ya jamii na jamii. Kwa mfano inasemekana baadhi ya jamii nchini Ghana hutumia mti huu kama chachandu ya kuongeza ladha katika chakula, wakati nchini Sudan na Kenya, mti huu hutumika kutengenezea siki au jam. Aidha zipo jamii kadhaa hukohuko Kenya zinazotumia mti huu kama dawa ya kufukuza nyoka kwa kuweka mizizi yake iliyokaushwa juu ya paa la nyumba.

Pamoja na matumizi yaliyoelezwa hapo juu, matumizi makubwa kabisa ya mti ambayo ndiyo msingi mkuu wa makala hii ni katika kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu pamoja na wanyama.

Ili tuweze kufahamu vizuri utendaji wake kazi katika matibabu, hebu kwanza tuangalie kilichomo (ingredients) katika mti huu.

Kemikali zilizomo kwenye mti huu (ingredients)


Vifuatavyo ni viasili vilivyowahi kukutwa katika mti wa
 Carissa edulis baada ya tafiti mbalimbali za wataalamu wa afya pamoja na mitishamba.

  1. Mizizi yake imegundulika kuwa na kiasili cha Sesquiterpene ambacho huzalisha viasili vya carissone, cryptomeridiol, germacarane na β-eudesmane. Kwa ujumla viasili vya sesquiterpenes vinajulikana kuwa na tabia au uwezo wa kutibu magonjwa au hali zote zinazohusiana na mcharuko mwili (anti-inflammatory effects), vimelea (antimicrobial effects) na saratani na uvimbe (antineoplastic effects).
  2. Mbegu za matunda yake zimeonekana kuwa na viasili vya lignans kama vile carissanol, secoisolariciresinol, nortrachelogenin na olivil. Kutokana na umbo lake la kikemikali, viasili hivi hususani carissanol vimeonekana kuwa na tabia au uwezo wa kuua vimelea (antimicrobial effects) na kusaidia kuua seli zisizohitajika mwilini (antioxidant effects) sifa ambayo inaipa uwezo mkubwa wa kupambana na seli za saratani.
  3. Vichipukizi vyake vina viasili vya quebrachytol ambavyo kina tabia za kuimarisha kinga ya mwili kwa kutegemeza tando za seli (membrane stabilization effects) na kuua seli zisizohitajika zikiwemo za saratani (antioxidant effects). Pia zina cardioglycosides ambavyo hufanya kazi kwenye pump ya Na+-K+ na kuweza kuua minyoo.
  4. Shina na majani yameonekana kuwa na aina fulani ya kemikali ya alkaloid
  5. Magamba ya mizizi yake yamegunduliwa kuwa na viasili vya 2-Hydroxy acetophenone ambacho kina uwezo wa kufanya kazi katika mishipa ya damu na kuifanya itanuke (vasodilation effects) na hivyo kuwa na sifa kubwa ya kusaidia kushusha shinikizo la damu na kuongeza nguvu za kiume.

Matumizi katika tiba

Wenyeji wa jamii kadhaa nchini Ghana wamekuwa, kwa miaka kadhaa sasa, wakichanganya magamba ya mizizi na baadhi ya viungo na kutumia kwa ajili ya kutibu maumivu ya mgongo na maumivu ya sehemu nyingine za mwili. Aidha nchini Guinea, jamii zimekuwa na mazoea ya kuchemsha majani ya mti huu na kutumia kutibu maumivu ya meno. Jamii nyingine barani Africa zimekuwa zikitumia sehemu ya juu ya mizizi hii kutibu uvimbe na mcharuko mwili (inflammatory reactions). Hali kadhalika sehemu za mizizi mkuu zimekuwa zikitumika kwa ajili ya kutibu magonjwa ya zinaa kama kaswende na kisonono, kurudisha urijali na kuongeza uwezo wa kuzaa, vidonda vya tumbo au kikohozi.

Jamii nyingine zimekuwa zikitumia mti huu kwa ajili ya kutoa mimba, na kwa hapa Tanzania yapo baadhi ya makabila yanayotumia Carissa edulis kutibu ugonjwa wa malaria.

Utafiti wa hivi karibuni nchini Kenya umeonesha kuwa, mti wa Carissa edulis una uwezo wa kuua vimelea vya virus aina ya Herpes Simplex Virus ingawa haijajulikana hasa ni kwa njia gani.

Kwa mujibu wa mtafiti Lindsay na wenzake, 2000 (3) ukiacha aina (species) hii ya Carissa edulis, aina nyingine zilizo katika jamii moja na mti huu, kama vile Carissa lanceolata, imethibitika kuwa na uwezo wa kutibu bacteria vya aina mbalimbali vikiwemo Staphylococcus aureus, Escherichia coli na Pseudomonas aeruginosa bila kuwa na madhara kwa mtumiaji.

Je mti huu una madhara kwa afya za binadamu?

Mpaka sasa hakuna ushahidi wowote wa kitafiti unaoonesha kuwa matumizi ya dawa za mitishamba zinazotokana na mti wa Carissa edulis zina madhara kwa binadamu.

Je kuna ushahidi wowote wa kitafiti kuthibitisha uwezo wa Carissa edulis?

Tafiti kadhaa zilizofanywa barani Afrika na kwingineko duniani zinathibitisha hilo.

1. Uwezo wa kupambana na virus (Antiviral activities)

Mwaka 2005 , watafiti nchini Kenya (4) walitumia magamba ya mizizi ya Carissa edulis kuchunguza uwezo wa mti huu katika kupambana na virus wa jamii ya Herpes Simplex Virus (HSV) kwa kutumia panya. Matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa, dawa iliyotumika kutokana na mti huo ilikuwa na uwezo wa kuua aina (strains) zote mbili (wild na resistant) za virus hawa wa HSV. Ilionekana pia kuwa, aina sugu ya virus hawa yaani resistant strain ndiyo iliyoathiriwa zaidi ikilinganishwa na aina isiyo sugu (wild strain). Kwa maneno mengine, mti huu ulionekana kuwa na uwezo mkubwa katika kuua na kutokomeza virus walioonekana kuwa sugu zaidi kwa madawa mengine kuliko wale wasio sugu. Hata hivyo watafiti hawakuonesha ni kwa jinsi gani  (mode of mechanism) mti huu uliweza kufanya kazi hiyo na hivyo kupendekeza kufanyika kwa utafiti mwingine utakaofanya kazi hiyo hususani kwa binadamu.

2. Uwezo wa kupambana na virus vya Ukimwi (Antiretroviral effects)

Mpaka sasa hakuna utafiti wowote wa kisayansi uliofanywa kuthibitisha uwezo wa mti wa Carissa edulis katika kupambana na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi. Hivyo bado ni ngumu kuthibitisha uwezo wa mti huu katika kuua na kutokomeza virus vya Ukimwi. Hii inaleta changamoto kubwa kwa wanasayansi kuweza kubainisha hilo.

3. Uwezo wa kutibu kifafa na degedege (Anticonvulsant effects)

Mtafiti Ya’u (5) kutoka idara ya madawa ya chuo kikuu cha Ahmadu Bello, nchini Nigeria akishirikiana na wenzake walifanya utafiti kuchunguza uwezo wa mti wa Carissa eduliskatika kutibu magonjwa ya degedege na kifafa. Katika utafiti wao, walitumia magamba ya mizizi ya mti huu kuchunguza uwezo wake katika kuzuia kutokea kwa degedege kwa wanyama. Watafiti hao walipendekeza kuwa mti wa Carissa edulis una kiasili chenye uwezo wa kuzuia kutokea kwa degedege na hivyo kukubaliana na madai ya baadhi ya jamii zinazotumia mti huu kama dawa ya kutibu tatizo hilo.

4. Uwezo wa kutoa na kupunguza maji mwilini (Antidiuretic effects)

Mtafiti Nadi T (6) wa chuo kikuu cha Addis Ababa, Ethiopia akishirikiana na wenzake walifanya utafiti kuchunguza uwezo wa mti Carissa edulis katika kutoa na kupunguza maji mwilini kwa njia ya mkojo (antidiuretic effects). Katika utafiti wao, wataalamu hao walitumia magamba ya mizizi kuwapa panya na kisha kuchunguza kiasi cha mkojo kilichotolewa na panya hao pamoja na upotevu wa viasili vya Sodium, potassium na Chloride mwilini. Kadiri dozi ya dawa iliyotumika ilipoongezwa, kiwango cha mkojo na upotevu wa viasili hivyo nao pia uliongezeka. Matokeo haya ya utafiti yanaendana na mazoea ya tangu kale ya jamii mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumia mti huu kwa ajili ya kusaidia kukojoa hususani kwa watu wenye matatizo ya figo.

5. Uwezo wa kutibu kisukari (Antidiabetic effects)

Watafiti kutoka chuo kikuu cha Alexandria nchini Misri (7), wakitumia panya wa maabara, walifanya utafiti kwa lengo la kuchunguza uwezo wa mti wa Carissa eduliskatika kutibu ugonjwa wa kisukari. Katika utafiti wao, wataalamu hao walifanikiwa kugundua kuwa, majani ya mti wa Carissa edulis yalikuwa na uwezo wa kushusha na kurekebisha kiwango cha sukari kwa panya waliokuwa na kisukari ndani ya muda wa masaa matatu, sawa kabisa na dawa za Metformin na buguanides zinazotumika kutibu ugonjwa huo mahospitalini.

Hitimisho

Ingawa tafiti mbalimbali za kisayansi zimefanyika kujaribu kuonesha uwezo wa mti waCarissa edulis katika kutibu magonjwa kadhaa kwa kutumia wanyama kama panya na kuku, mpaka sasa hakuna utafiti wowote uliowahi kufanyika kwa binadamu kuthibitish hilo, pamoja na kwamba tangu enzi na enzi, watu wa jamii zilizojaliwa kuwa na mti huu wamekuwa na wanaendelea kuutumia katika kujitibu maradhi mbalimbali yanayowakabili. Ni changamoto kwa watafiti na watalaamu kufanya tafiti zaidi za kisayansi ili kutambua jinsi mti huu unavyofanya kazi katika kutibu baadhi ya magonjwa na kuthibitisha pasi shaka uwezo wake katika kutibu ugonjwa wa Ukimwi na maradhi mengine sugu.

Marejeo

  1. www.worldagroforestry.org/treedb2/AFTPDFS/Carissa_edulis.pdf
  2. Leeuwenberg, A.J.M. & Kupicha, F.K. et al. (1985) Apocynaceae FZ 7(2)
  3. Kokwaro, J.O., 1976. Medicinal Plants of East Africa. East African Literature. Bureau, Nairobi, Kenya, pp. 1–8, 25–26.
  4. Lindsay, E.A., Berry, Y., Jamie, J.F., Bremner, J.B., 2000. Antibacterial compounds fromCarissa lanceolata R. Br. Phytochemistry 55, 403–406.
  5. Festus M. Tolo, Geoffrey M. Rukunga, Faith W. Muli, Eliud N.M. Njagi, Wilson Njue, Kazuko Kumon, Geoffrey M. Mungai, Charles N. Muthaura, Joseph M. Muli, Lucia K. Keter, Esau Oishi, Mawuli W. Kofi-Tsekpo, 2005. Anti-viral activity of the extracts of a Kenyan medicinal plant Carissa edulis against herpes simplex virus. Journal of Ethnopharmacology 104 (2006) 92–99. Inapatikana mtandaoni www.sciencedirect.co
  6. Ya’u J, Yaro AH, Abubakar MS, Anuka JA, Hussaini IM., 2008. Anticonvulsant activity of Carissa edulis (Vahl) (Apocynaceae) root bark extract. J Ethnopharmacol. 2008 Nov 20;120(2):255-8. Epub 2008 Sep 4. Inapatikana mtandaoni www.sciencedirect.com
  7. Nedi T, Mekonnen N, Urga K., 2004. Diuretic effect of the crude extracts of Carissa edulis in rats. J Ethnopharmacol. 2004 Nov;95(1):57-61. Inapatikana mtandaoni www.sciencedirect.com
  8. El-Fiky FK, Abou-Karam MA, Afify EA., 1996. Effect of Luffa aegyptiaca (seeds) and Carissa edulis (leaves) extracts on blood glucose level of normal and streptozotocin diabetic rats. J Ethnopharmacol. 1996 Jan;50(1):43-7. Inapatikana mtandaoni http://www.kau.edu.sa

Ni tatizo la ngozi ambalo linaifanya ngozi kuwa nyekundu, kuvimba/kuwasha au kupata mcharuko (inflammation) baada ya kugusana na kitu kinachochangia mwili kucharuka au kupata mzio (allergic reaction)

Kuna msomaji mmoja aliuliza swali kwenye tovuti hii, na hapa na nukuu swali lake ‘’ Nina tatizo la kutoka vipele sehemu za siri siku moja baada ya kufanya mapenzi au baada ya "masterbartion". Vipele hukaa siku tatu hadi nne hutumbuka na kutoa maji, kidonda hukauka siku moja hadi mbili bila dawa. Nimepima ukimwi pamoja na kaswende lakini halikuonekana tatizo. Naomba msaada kujua tatizo langu’’ Mwisho wa kunukuu.

Muundo ya moyo  na mishipa ya damu ni mojawapo ya vinavyooathirika katika magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo. Vijusi(fetuses) kati ya 8 hadi 10 huathirika kwa kila 1000.

Magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo huweza kutoa dalili mara tu baada ya kuzaliwa, utotoni na wakati mwingine husubiri mpaka ukubwani. 

Magonjwa ya Moyo ya Kuzaliwa husababishwa na nini?

Kwa wengi sababu huwa haijulikani. Ila huwa kuna vitu hatarishi ambavyo hupelekea kuongezeka kwa uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo, vitu hivyo hatarishi ni:

  • Matatizo ya kijenetekia utotoni kama Downs syndrome, Turner’s syndrome, Marfan syndrome, 
  • Matumizi ya dawa ya kutibu chunusi (acne)  aina ya retinoic acid, madawa ya kulevya na unywaji wa pombe wakati wa ujauzito
  • Maambukizi ya virusi vya Rubella (German measles) kipindi cha kwanza cha ujauzito (1st trimester)

Kuna aina mbili za magonjwa ya moyo ya kuzaliwa

  • Cyanotic
  • Non-cyanotic

Cyanosis ni hali ya kuwa na rangi ya samawati (katika midomo,ulimi, ganja za mikono na miguuni) kutokana na kukosa oksijeni ya kutosha mwilini.

Cyanotic

Magonjwa ya moyo ya asili ambayo yanaangukia katika kundi hili ni pamoja na

  • Tetralogy of fallots
  • Transposition of great vessels
  • Tricuspid atresia
  • Total anomalous pulmonary venous return
  • Truncus arteriousus
  • Hypoplastic left heart
  • Pulmonary atresia
  • Ebstein anomaly

Non-cyanotic

Magonjwa ya moyo ya asili yaliyo kwenye kundi hili hujumuisha 

  • Ventricular septal defect (tundu katika kuta za ventrikali)
  • Atrial septal defect (tundu katika kuta za atria)
  • Patents ductus arteriousus 
  • Aortic stenosis
  • Pulmonic stenosis
  • Coarctation of the aorta
  • Atrioventricular canal (endocardial cushion defect)

Dalili za Magonjwa ya Moyo ya Kuzaliwa

Kwa ujumla, wagonjwa wa moyo wa asili huwa na dalili zifuatazo

  • Kupumua kwa shida 
  • Kushindwa kula vizuri
  • Matatizo ya ukuaji
  • Matatizo ya ukuaji wa misuli ya mikono na miguu
  • Maambukizi ya mfumo wa hewa
  • Cyanosis kwa aina ya kwanza(rangi ya samawati katika midomo,ulimi, viganja vya mikono na miguuni)
  • Ongezeko la sauti ya ziada katika sauti za moyo kutokana na tatizo (heart murmur)
  • Mabadiliko kwenye kucha hasa za vidole vya mikononi (digital clubbing)

Vipimo na Uchunguzi

Baadhi ya vipimo vinavyotumika kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa haya ni

  • Echocardiogram/transesophageal echocardiogram
  • Cardiac catheterization
  • Magnetic Resonance Imaging
  • Electrocardiogram
  • Chest x-ray

Matibabu

Matibabu hutegemea aina ya ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao, hivyo hapa nitaelezea kwa kifupi ila, maelezo zaidi nitatoa katika makala zinazokuja za ugonjwa mmoja mmoja.

Aina nyingi za magonjwa haya huwa na madhara makubwa hivyo huhitaji upasuaji kurekebisha kasoro hizo, pamoja na matibabu ya dawa (diuretics ambazo husaidia kupunguza maji na chumvi mwilini, digoxin ambayo husaidia kuongeza nguvu katika mapigo ya moyo).

Vilevile kuna tiba nyengine ambayo badala ya upasuaji kitaalamu Transcatheter ambapo kifaa cha kufunga au kupachika huwekwa kwenye catheter maalumu ambayo hupita kwenye mishipa ya damu mpaka kwenye kasoro na kurekebisha kwa kuziba tundu nakadhalika.

 

Hiatus Hernia ni tundu linalotokea baada ya sehemu ya juu ya mfuko wa kuhifadhia chakula (tumbo) kuingia kwenye sehemu ya kifua kupitia uwazi unaojulikana kama esophageal hiatus. Kwa kawaida uwazi huu  (esophageal hiatus) hupitisha mrija wa chakula kwenda kwenye tumbo yaani esophagus na si  utumbo.
 
Mara nyingi, tatizo hili huonekana kwa takribani ya 60% ya watu wenye umri wa miaka 50 na kuendelea,  ingawa pia linaweza kuwapata wale walio na umri wa chini ya huo.

Kuna aina mbili kuu za hiatus hernia

  • Sliding type : Kama jina lake linavyomaanisha, aina hii hutokea iwapo sehemu ya juu ya utumbo inaposukumwa juu na kuingia kwenye upenyo wa esophagus hiatus baada ya kutokea kwa ongezeko la presha katika maeneo ya tumbo (increased pressure in the abdominal cavity) na kurudi kama kawaida wakati presha inapopungua.
  • Fixing type: Aina hii hutokea iwapo sehemu ya  juu ya utumbo inapokuwa kwenye maeneo ya kifua na haishuki chini.

Vihatarishi vya Ugonjwa huu

Ongezeko la presha tumboni kutokana na
  • Kunyanyua vitu vizito au kuinama sana
  • Kukohoa sana au kukohoa mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali
  • Kutapika sana (violent vomiting)
  • Kupiga chafya sana (Hard sneezing)
  • Ujauzito -Kutokana na mfuko wa uzazi (uterus) kusukuma viungo kwenda juu kutokana na kuongezeka ukubwa wake.
  • Wakati wa kujifungua- Kutokana na kuongezeka kwa presha ndani ya tumbo wakati mama anajitahidi kusukuma mtoto. Si wanawake wote wanaopata tatizo hili.
  • Kujikamua wakati wa kwenda  haja kubwa (straining during constipation)
  • Uzito uliopitiliza -Kutokana na kuongezeka uzito ambao unasukuma viungo kwenye maeneo ya kifua kwenda chini na hivyo kuongeza presha  tumboni.
  • Kujisaidia haja kubwa wakati mtu amekaa - Kutokana na maendeleo ya binadamu, watu wengi sasa hivi wameanza utamaduni wa kutumia vyoo vya kukaa wakati wa kujisaidia haja kubwa, katika tafiti iliyofanywa na Dr Denis Burkitt (1), imeonekana ya kwamba kujisaidia wakati mtu amekaa hufanya mtu kujikamua zaidi na hivyo kuongeza presha ndani ya utumbo (Increased intraabdominal pressure) na hivyo kusukuma mfuko wa kuhifadhia chakula (utumbo) kupitia kwenye upenyo wa esophagus hiatus na hivyo kusababisha hiatus hernia.

Tatizo la kurithi (Heredity)

  •  Uvutaji sigara
  •  Matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine
  •  Kuwa na kiwambo hewa (diaghram) dhaifu
  •  Msongo wa mawazo (depression)
  •  Matatizo ya kuzaliwa (congenital defects).

Dalili na Viashiria

  • Maumivu ya kifua

  • Kichomi (pleurisy) ambacho kinakuwa kikali sana wakati wa kuinama au mtu anapolala chini
  • Matatizo katika kumeza chakula
  • Kupumua kwa shida Kutokana na hiatus hernia kupunguza uwezo wa ufanyaji kazi wa kiwambo hewa (diaphragm).
  • Mapigo ya moyo kwenda kasi Kutokana na mkwaruzo wa neva inayojulikana kama vagus nerve.

Mara nyingi sana hiatus hernia haioneshi dalili zozote zile isipokuwa inapokuwa kubwa sana. Maumivu na kichomi hutokana na kurudishwa kwa tindikali ya kwenye tumbo (gastric acid) kwenye kifua. Pia tindikali aina ya bile acid na hewa huwa inasukumwa juu kwenye kifua.

Vipimo vya Uchunguzi

  • Barium Swallow X-ray – X-ray ya kuangalia viungo vya ndani, mgonjwa hupewa au huchomwa sindano  yenye dawa maalum ambayo huonekana vizuri kwenye X-ray, na baada ya hapo hupigwa picha za X-ray akiwa amekaa au amesimama. Kawaida kipimo hiki huchukua masaa 3-6.
  • Esophagogastroduodenoscopy (OGD) - Mpira maalum wenye taa na camera kwa mbele unaoingizwa  mdomoni kwenye mpira wa kupitisha chakula (esophagus) na hutazama kama kuna magonjwa yoyote kwenye esophagus hadi kwenye sehemu inayojulikana kama duodenum.
  • Electrocardiography (ECG)- Kipimo cha  kuangalia kama kuna matatizo katika jinsi moyo unavyopiga
  • Chest X-ray- Kuangalia kama kuna magonjwa kama homa ya mapafu (Pneumonia), kama  kuna pafu lolote ambalo halifanyi kazi, madhara kwenye moyo (injury to the heart) na pia kuangalia matatizo yoyote yale.
  • Complete Blood Count- Kipimo cha kuangalia wingi wa damu, kuangalia aina mbalimbali za chembechembe za damu kama zipo katika maumbo yao ya kawaida, wingi wao kama ni wa kawaida.

Tiba ya Hiatus Hernia

Kama ilivyoelezwa hapo awali, hiatus hernia mara nyingi haioneshi dalili zozote na hivyo mtu anaweza kuendelea na shughuli zake za kila siku bila madhara yoyote. Tiba ya hiatus hernia inahusisha dawa na upasuaji.
 
Tiba ya Dawa
  • Dawa za kuyeyusha tindikali mwilini (antacids) hutumika kama Gelusil, Maalox nk.
  • H2 receptor antagonist –Dawa zinazopunguza kiwango cha utolewaji wa tindikali kama cimetidine, ranitidine nk.
  • Dawa ambazo huzuia utolewaji wa tindikali na kuponya tishu za esophagus (Proton Pump Inhibitors) dawa hizi ni  omeprazole, lansoprazole nk.
Tiba ya Upasuaji
Upasuaji hufanyika kwa wagonjwa wa dharura au pale ambapo mgonjwa hajapata nafuu hata baada ya kutumia dawa na hali yake inazidi kuwa mbaya. Upasuaji huu hufanywa na daktari wa upasuaji  kwa kuchana (incision)  kwenye kifua (thoracotomy) au tumbo (laparatomy) na kuvuta sehemu ya utumbo iliyopanda juu kwenye kifua ili kuirudisha katika sehemu yake ya kawaida na kupunguza ule uwazi uliopo kwenye diaphgram, kurekebisha sphincters (nyama zinazosaidia katika kufunga na kufungua uwazi kwenye diaphragm) za esophagus ambazo zimekuwa dhaifu. Pia daktari anaweza kufanya upasuaji huu kwa kuchana sehemu ndogo sana kwenye tumbo na kwa kutumia kifaa maalum chenye kumsaidia kurekebisha henia hii. Aina hii ya upasuaji hujulikana kama endoscopic surgery.
 

Madhara ya Hiatus Hernia

Madhara ya hiatus hernia hutokana na kurudishwa juu kwa tindikali aina ya gastric acid na hivyo kusababisha ugonjwa unaojulikana kama Gastroesophageal Reflux Disease (GERD).
Madhara haya ni
  • Kichomi
  • Ugonjwa wa esophagitis
  • Barretts esophagus
  • Saratani ya kwenye mpira wa kupitisha chakula (esophageal cancer)
  • Kuoza kwa meno (dental erosion)
  • Strangulation of the stomach (kunyongwa kwa sehemu ya juu ya tumbo na hivyo kusababisha sehemu hii kukosa damu ya kutosha na hivyo tishu zake kufa na kuoza (ischemic and necrosis)
  • Kuzuia pafu kujaa hewa na hivyo kushindwa kutanuka na kusababisha mtu kupumua kwa shida sana.

Jinsi ya kujikinga

  • Kuacha kunywa pombe
  • Kuacha matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine
  • Kupunguza uzito uliopitiliza.
  • Kula milo midogo mara nyingi kwa siku
  • Epuka vyakula vinavyoongeza kichomi kama chocolate, vitunguu, vyakula vikali, vinywaji venye limau, ndimu nk.
  • Kula chakula cha usiku masaa matatu kabla ya kwenda kulala
  • Pumzika kwa kukaa baada  ya kula usilale chini.
  • Nyanyua sehemu unayoweka kichwa chako wakati wa kulala kwa angalau 15cm (6 inches)
  • Punguza msongo wa mawazo
  • Acha kuvuta sigara.

Marejeo

Burkitt DP (1981). "Hiatus hernia: is it preventable?". Am. J. Clin. Nutr. 34 (3): 428–31. PMID 6259926
Sontag S (1999). "Defining GERD". Yale J Biol Med 72 (2-3): 69–80. PMC 2579007. PMID 10780568
 
 

Hatari ya Kukakamaa kwa mwili  huongezeka kwa mtu mwenye kiharusi  au vihatarishi vya kiharusi kutokana na utafiti uliofanywa Rotterdam uholanzi.

Sehemu ya ubongo kitaalamu Cerebral cortex inapokandamizwa  aidha na kihararusi cha mishipa kuchanika na kuvujisha damu au mishipa inapoziba husababisha Kukakamaa kwa mwili. Hali yoyote isababishayo upungufu wa damu kufika katika sehemu za ubongo hupelekea Kukakamaa kwa mwili  kutokea, na moja wapo ya sababu hizo ni magonjwa ya moyo.

Kwa takribani miongo mitatu sasa, tumeshuhudia ongezeko kubwa la mlipuko wa ugonjwa wa mkanda wa jeshi linaloendana na ongezeko la hususani ugonjwa wa UKIMWI. Hali hii imefanya baadhi ya watu kuamini kuwa, ugonjwa huu ni dalili ya wazi kabisa ya mtu kuwa na VVU, imani ambayo kwa kiasi kikubwa ina ukweli ndani yake ingawa si kwa wote wanaopatwa nao.

Mkanda wa jeshi au shingles au herpes zoster kwa majina ya kitabibu ni ugonjwa unaosababishwa na virus wa aina ya Varicella-zoster ambao pia husababisha ugonjwa wa tetekuwanga au chickenpox. Ugonjwa huu huathiri ngozi ambapo huambatana na vipele na michubuko kama ya kuungua yenye kuambatana na maumivu makali .

Visababishi
Kama tulivyokwisha tangulia kueleza hapo juu, ugonjwa huu husababishwa na virus aina ya Varicella-zoster ambao pia husababisha ugonjwa wa tetekuwanga. Baada ya mtu kupatwa na tetekuwanga, virus hawa hubaki katika hali ya kupooza/kutokuwa na madhara (dormant) katika neva fulani za mwili. Baada ya miaka kadhaa, iwapo itatokea kinga ya mwili ikashuka kwa sababu yoyote ile, virus hawa hupata tena nguvu/kuwa na madhara (active), kuibuka na kusababisha ugonjwa wa mkanda wa jeshi.

Kwa kawaida shambulio la mkanda wa jeshi hutokea mara moja maishani ingawa laweza kujirudia.

Vihatarishi
Mkanda wa jeshi unaweza kumpata mtu wa umri wowote ule ingawa watu walio katika makundi haya wapo katika hatari kubwa zaidi:
• Wenye umri wa zaidi ya miaka 60
• Mtu aliyewahi kuugua ugonjwa wa tetekuwanga kabla ya umri wa mwaka mmoja
• Watu ambao kinga yao ya mwili imepungua kwa sababu mbalimbali kama vile matumizi ya aina fulan za dawa, magonjwa kama vile maambukizi ya VVU (HIV/AIDS), saratani na utapiamlo.

Je mkanda wa jeshi huambukizwa?
Hapana ugonjwa huu hauambukizwi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine! Lakini iwapo itatokea mtoto au mtu mzima ambaye hajawahi kupatwa na ugonjwa wa tetekuwanga maishani mwake na ambaye pia hajawahi kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo akakutana na mtu mwenye ugonjwa wa mkanda wa jeshi, mtoto au mtu huyo atapatwa na ugonjwa tetekuwanga na siyo mkanda wa jeshi.

Dalili
Dalili ya awali kabisa ya mkanda wa jeshi ni maumivu makali sehemu fulani/ upande mmoja wa mwili yakiambatana na hali ya ganzi na hisia za kuungua kwenye ngozi. Maumivu pamoja na hisia za kuungua huwa makali sana na hutokea kabla ya vipele/michubuko kutokea kwenye ngozi.
Kawaida, vipele au michubuko huusisha eneo fulani la mwili kuanzia kwenye uti wa mgongo kuzunguka kuelekea eneo la tumbo au kifua. Michubuko pia inaweza kutokea kwenye maeneo yanayozunguka uso, macho, mdomo au masikio.

Dalili nyingine ni pamoja na :
• Maumivu ya tumbo
• Homa
• Maumivu ya mwili mzima
• Vidonda sehemu za siri
• Maumivu ya kichwa
• Maumivu ya viungo
• Kuvimba kwa mitoki/ matezi
Iwapo neva za maeneo ya uso zitaathiriwa, mgonjwa anaweza kupatwa na matatizo ya kuona, kuonja, au kusikia.

Vipimo
Ni nadra sana kufanya Vipimo maalum kwa ajili ya utambuzi wa ugonjwa huu, isipokuwa kwa nchi zilizoendelea. Kwa ujumla utambuzi wa ugonjwa huu hufanyika kwa kuchukua historia ya mgonjwa na kuchunguza sehemu ya ngozi iliyoathiriwa.
Vipimo vya damu yaani FBP huonesha ongezeko la chembe nyeupe za damu na antibodies dhidi ya virus wa tetekuwanga.

Matibabu
Matibabu ya mkanda wa jeshi hujumuisha matumizi ya dawa kama vile Acyclovir, Famciclovir na Valacyclovir kwa ajili ya kuua virus wanaosababisha ugonwja huu. Dawa hizi husaidia kupunguza maumivu, kuzuia madhara zaidi ya ugonjwa huu na kupunguza muda wa ugonjwa.
Dawa hizi hutolewa angalau saa 72 baada ya mgonjwa kuanza kuhisi maumivu na hali ya kuungua. Ni vema dawa zianze kutumika kabla ya vipele/michubuko kujitokeza.
Jamii ya dawa za corticosteroids kama vile prednisolone husaidia kupunguza maumivu na uvimbe kwa badhi ya wagonjwa. Dawa nyingine zinazofaa kutumika ni pamoja na jamii ya antihistamines kwa ajili ya kupunguza muwasho, dawa za maumivu, calamine lotion kwa ajili ya kupunguza muwasho. Aidha mgonjwa anashauriwa kupata mapumziko ya kutosha

Matarajio
Mkanda wa jeshi kwa kawaida huchukua kati ya wiki mbili hadi tatu kupona wenyewe. Aidha ni nadra sana kwa ugonjwa huu kujirudia tena. Iwapo neva zinazothibiti mwendo katika mwili zitakuwa zimeathirika, mgonjwa anaweza kupatwa na kupooza kwa muda au kwa kudumu kwa sehemu ya mwili iliyoathiriwa. Wakati mwingine, maumivu yanayosababishwa na mkanda wa jeshi yanaweza kudumu kwa miezi mpaka mwaka hata baada ya mgonjwa kupona kabisa. Maumivu haya yanayojulikana kama postherpetic neuralgia kwa kawaida huwakumba wagonjwa wenye umri wa zaidi ya miaka 60 na husababishwa na uharibifu katika neva za mwili.

Madhara
Madhara ya mkanda wa jeshi ni pamoja na kupatwa na shambulio jingine la ugonjwa huu, maambukizi ya bakteria, upofu iwapo eneo la jicho litahusika, ukiziwi, maambukizi katika utando wa ubongo (encephalitis), uwepo wa vimelea kwenye damu (sepsis) au ugonjwa unaoitwa Ramsay Hunt Syndrome iwapo utahusisha neva za uso.

Kinga
Epuka kabisa kugusa eneo lenye vipele au michubuko kwa mtu mwenye mkanda wa jeshi au tetekuwanga iwapo hujawahi kuugua au kupata chanjo ya tetekuwanga.
Ni vema kupata chanjo dhidi ya virus wa Varicella zoster kama inapatikana katika nchi au eneo ulilopo . Tafiti zimeonesha kuwa, watu wazima wanaopata chanjo hii wana uwezekano mdogo sana wa kupata madhara ya mkanda wa jeshi kuliko wale wasiochanjwa.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Marekani cha Boston umesema  unywaji wa chai vikombe viwili kwa siku huongeza uwezekano wa mwanamke kupata ujauzito. Katika utafiti uliohusisha wanawake 3,600 umeonyesha ya kwamba wanawake wanaokunywa vikombe viwili vya chai kwa siku wana asilimia 27 ya kupata ujauzito ikilinganishwa na wanawake ambao hawanywi  chai. Pia utafiti huo umeonyesha ya kwamba wanawake wanotumia  vinywaji baridi  viwili kwa  siku kama coca cola, hupunguza uwezekano wao wa kushika mimba kwa asilimia 20 na haijalishi kama vinywaji hivyo  vina sukari au la. 

Mtafiti  mkuu Profesa Elizabeth Hatch amesema alifanya utafiti huu ili kutaka kujua kama kuna uhusiano wowote wa kemikali aina ya caffeine inayopatikana kwenye chai, kahawa  na uwezo wa kushika mimba kwa wanawake.Utafiti huu ulifanywa kwa kuwahusisha wanawake wa kutoka  nchi ya Denmark   kutokana na nchi hiyo kuwa na mfumo wa kuwapa raia wao namba za uraia wa kudumu wakati wa kuzaliwa na hivyo kuwa rahisi kwa Profesa Hatch kuwafuatilia kwa njia ya intaneti kwa muda wa mwaka mmoja. 

Profesa Hatch amesema “Hatujui wanawake hawa walikuwa wakinywa chai ya aina gani, hatujui kama walikunywa chai bila kuongeza kitu chengine kwenye chai, kama waliongeza maziwa au limao kwenye chai, bali inaonekana kuna uhusiano wa caffeine na uwezo wa kushika mimba au uwezo huo umetokana na mfumo wa maisha wa wanawake hao au ni kutokana na  virutubisho vya chai hiyo”. 

Ukurasa 1 ya 3