Image

Mazoezi: Dawa Halisi na Rahisi

Ukweli kuhusu umuhimu wa mazoezi katika kuzuia na kutibu magonjwa mbalimbali

Iwe unafanya kwa nia ya kuwa na umbo lenye muonekano mzuri, au kupoteza muda wa ziada ulionao, mazoezi ni zaidi ya unavyoweza kufikiria.

Ongezeko la tafiti katika eneo la mazoezi na magonjwa yahusianayo na mifumo ya maisha (lifestyle-related diseases) lililotokea ndani ya takribani miaka kumi iliyopita, limefumbua macho ya wengi juu ya umuhimu wa mazoezi katika kujikinga na kutibu magonjwa mbalimbali. Tafiti katika eneo hili zinaonesha kwamba mazoezi yanaweza kutumika kujikinga na magonjwa zaidi ya ishirini na kutibu magonjwa takribani kumi.

Ni jambo lililowazi kabisa kwamba babu zetu waliweza kuishi kwa miaka mingi zaidi ya kizazi tulichopo sisi. Ni dhahiri pia kwamba kizazi chetu kinashuhudia milipuko ya magonjwa ambayo babu zetu hawakuwahi hata kuyasikia. Pia mtakubaliana nami kuwa, kumekuwa na mambo mengi ya kimaendeleo yaliyotokea katika kipindi chote hiki, ambayo wanazuoni wamekuwa wakiyahusisha na milipuko ya baadhi ya magonjwa.

Yapo mambo mengi katika mifumo yetu ya maisha ya kila siku yaliyo mazuri katika muonekano na hisia, lakini ukweli ni kwamba yaweza kuwa na athari kubwa kwa afya zetu.

Kila mtu anapenda kuendesha gari wakati wote anapohitajika kwenda sehemu, pia watu wengi wanafurahia kuketi na kuangalia vipindi wavipendavyo katika runinga muda wote wapatapo wasaa. Si ajabu pia watu wengi wanapenda shughuli zisizohitaji kutembea tembea au kutumia nguvu.

Ukweli ni kwamba katika jamii zetu za kiafrika, mambo yaliyotajwa hapo juu ni vielelezo halisi vya mtu kuwa na maisha mazuri, na kinadharia hakuna mtu asiyependa maisha mazuri. Kinachosahauliwa ni kwamba mfumo huu wa maisha ambao mara nyingi huendana na upatikanaji mkubwa wa chakula, unatupelekea katika kushindwa kutumia miili yetu ipasavyo pamoja na virutubisho tunavyokula katika vyakula mbalimbali.

Miili yetu imetengenezwa ili iweze tumika katika kiwango fulani, na kuitumia chini au juu ya viwango hivyo, husababisha magonjwa mbalimbali.

Kwa ufupi ni kwamba, magonjwa yanayohusishwa na mifumo ya maisha hutokea pale mwili unapotumiwa chini au juu ya kiwango chake, au pale mwili unapopokea virutubisho chini au juu ya viwango vinavyohitajika. Kwa mfano katika jamii tuliyopo sasa hususani mijini, kiasi cha watu wanaoweza kuwa na maisha mazuri kinaongezeka. Vilevile teknologia inaongezeka hivyo kupelekea watu kula zaidi na kutembea kidogo, kwa maana ya kuendesha magari na kuketi kutizama runinga kwa muda mrefu.

Hii inaufanya mwili kutunza virutubisho ambavyo kwa hali ya kawaida vingetumika kama mtu angetembea au kufanya kazi itumiayo nguvu kiasi. Mwili hauhitaji kiasi kikubwa cha virutubisho hivi na baada ya muda mrefu vinakuwa kama sumu na hivyo kusababisha magonjwa kama vile kisukari kisichotegemea insulini (Type 2 diabetes).

Kwa kufanya mazoezi, mtu anauwezesha mwili wake kutumia virutubisho ipasavyo, kwa maana ya kwamba hakuna kinachohifadhiwa mwilini kinyume na matakwa ya mwili. Ifahamike kuwa mazoezi si lazima yawe ya kwenda kwenye sehemu maalum za mazoezi kama gym.

Tafiti zimeonyesha kuwa kutembea kwa saa moja zaidi ya shughuli zako za kawaida kwa siku tatu mpaka tano kwa juma, kunasaidia kujikinga na magonjwa kama kisukari kisichotegemea insulin, na magonjwa ya moyo. Wanasayansi katika chuo kikuu cha karolinska nchini Sweden, wameonyesha katika utafiti kwamba, kutembea kwa kawaida kwa muda wa angalau saa moja kwa siku kwa muda wa siku tano kunaweza kushusha viwango vya sukari vya wagonjwa wa kisukari kufikia kiwango cha kawaida kwa asilimia zaidi ya sabini. Tafiti zimeonyesha pia kwamba, mazoezi yaweza kumkinga mtu na magonjwa kama saratani na msongo wa mawazo (depression).

Kuna ushahidi wa kutosha pia kuhusiana na uwezo wa mazoezi katika kutibu na kuzuia magonjwa ya viungo kama baridi yabisi (arthritis).

Utafiti mkubwa uliofanywa na wanasayansi kutoka katika Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba cha Muhimbili, Dar es salaam nchini Tanzania wakishirikiana na wenzao wa Japani, kimeonyesha kwamba watu wenye tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara, wana kinga zaidi ya kutopata magonjwa ya kisukari na moyo, ukilinganisha na wale wasiofanya mazoezi kabisa.

Inafahamika pia kuwa babu zetu waliishi kwa kuwinda na kulima hivyo magonjwa kama kisukari kisichotegemea insulin, hayakuwepo kabisa. Na imeonekana pia kwamba jamii zinazoishi na kujulikana kama wawindaji na wakulima mpaka leo zina kiasi kidogo sana cha magonjwa kama ya kisukari, moyo na kansa ukilinganisha na jamii zinazoishi maisha tunayoyaita ya kisasa.

Baadhi ya magonjwa yanayoweza kuzuiwa au kutibiwa na mazoezi ni pamoja na Kisukari, unene wa kupindukia, magonjwa ya moyo, saratani na magonjwa ya viungo (Arthritis). Magonjwa mengine ni msongo wa mawazo (depression), kisukari cha mimba, na magonjwa mengi ya mfumo wa homoni. Mazoezi yanatambuliwa kama dawa katika nchi mbalimbali.

Uzuri wa mazoezi kama dawa ni kutokana na uhalisi wake na ukweli kwamba mtu haitaji kununua. Pia hakuna madhara yaliyoripotiwa kwa kutumia mazoezi kama matibabu. Tujenge utaratibu wa kujifanyia mazoezi kwani mazoezi ni dawa halisi na rahisi.

Imesomwa mara 27931 Imehaririwa Alhamisi, 18 Julai 2019 17:07