Image
nasikitisha kuona ingawa dhamira zetu ni nzuri kwa kuwapa watoto watakayo msimu huu, sisi wazazi ni sehemu ya tatizo. Hebu tazama njia muhimu saba unazoweza kutumia kumwepusha mtoto kuharibikiwa.
1. Mfundishe kuridhika. Mtoto akiridhika na alichonacho hawezi kutamani/kudai asivyonavyo. Mtoto wa umri wowote anaweza kujifunza kushukuru kwa zawadi aliopewa, kuridhika nayo na kuzoea kusema asante. Mtoto anayefahamu mambo haya ni vigumu kuyumbishwa na tamaa kwani anajisikia fahari kwa yale aliyonayo.
 
2. Jenga misingi ya zawadi kwa familia. Namna bora ya kudhibiti matarajio ya mwanao ni kujiwekea sababu za kupeana zawadi. Kwa mfano, mnaweza mkajipangia kuwa zawadi iwe mojawapo ya hizi: "kwa ajili ya kuvaa, kwa ajili ya kusoma na hitaji maalumu." Vinginevyo hakuna zawadi. Vievile zawadi si lazima inunuliwe, unaweza mwandikia, umchoree picha ama umtengenezee zawadi. Namna hii utamfundisha kuwa zawadi si lazima itoke dukani kwa fedha bali ni ishara ya upendo toka kwako.
 
3. Wekeza muda. Likizo ni wakati mzuri wa wewe kuweka mambo mengine yote pembeni ukatulia na mwanao. Amini usiamini, anataka mawazo yako yasiyogawanyika zaidi ya zawadi unazohangaika nazo. Unapopata muda wa faragha na mtoto unaimarisha uhusiano wa kihisia kati yenu na kupata ushirikiano mkubwa toka kwake. Zaidi ya yote, mtoto atajifunza kwamba furaha hutokana na kukaa pamoja na uwapendao si kushinda madukani (mkinunua zawadi).
 
4. Usihofu kutomridhisha. Wazazi mara nyingi tunahamu ya kufanya 'dunia' kuwa mahali pazuri kwa watoto wetu. Kama kumnunulia simu dhidi ya dhamira zetu au kupika mboga saba tofauti kila mlo ili mtoto aweze kuchagua ale nini aache nini, n.k. Alimuradi tu mtoto aneemeke! Kwa bahati mbaya, wakati sisi tunaondoa 'matuta' ili watoto wapete, tunawafundisha kuchukulia maisha kirahisi bila kujua tunawanyima uzoefu muhimu ambao 'ugumu' wa maisha unaweza kutufundisha (ujasiri, uvumilivu, utayari kukabili changamoto). Lakini nini cha kufanya wakati mtoto akikupandishia mabega kwa kutaka bwerere hizi? Kuwa jasiri: MPUUZE. Punde si punde, mtoto wako atajifunza kwamba maisha yanazo changamoto na kwamba hazitatuliwi kwa kupandisha mabega na kudeka.
 
5. Fundisha matumizi ya fedha. Sote tunajua pesa hazichumwi kwenye miti - ama kwenye pochi zetu - Je mtoto wako anajua hili? Ufunguzi pochi kwa kila analodai/anachotaka mtoto ni kitovu cha uharibifu. Unamwambia, utapata utakacho wakati wowote. Badala yake na kwa kuzingatia umri wa mtoto, toa posho za wiki zenye mlengo kumfundisha kuachana na matumizi yasiyo ya lazima, kama midoli/mwanasesere, kwenda sinema na marafiki, n.k. Ikiwezekana haya ajifunze kuyagharimia kutokana na kubana matumizi katika posho yake.
 
6. Mpe majukumu. Mara kadhaa tunajikuta tunawafanyia watoto kila kitu hata mambo wanayopaswa kutekeleza wenyewe. Kumfungia kamba za viatu (Baby Class) hadi 'kumwomba' mwalimu arekebishe daraja lake la Fizikia (A' Level). Hata kama tuna nia njema, hapa tunamfundisha uzembe - kwamba yupo mtu wa kufanya majukumu yake. Mpangie majukumu na mfunze kujisimamia, namna hii atakuwa mtu wa kuwajibika.
 
7. Nidhamu. Moja ya tabia walizonazo watoto waloharibikiwa ni kudhani kwamba taratibu na sheria kamwe haziwagusi. Tunawajengea nadharia hii kwa kutowafundisha gharama za kutotii sheria/taratibu. Mbaya zaidi ni pale tunaposhindwa kutoa adhabu stahiki wanapokosea. Badilika leo, toa makatazo na yafuatilie na adhabu kulingana na umri wa mtoto.
 
Source: Sema Tanzania
Katika #Malezi ya mtoto ni muhimu kujua njia bora na sahihi inayomjengea mtoto misingi bora ya maisha yake ya baadae. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali juu ya malezi ya watoto, kuna aina kuu nne za malezi.
1. Malezi ya kimabavu: Wazazi katika aina hii ya malezi huamini watoto lazima wafuate sheria na maelekezo yote wanayopewa bila kupuuza wala kukaidi.
 
2. Malezi ya mamlaka (demokrasia): Kama ilivyo kwa wazazi wenye malezi ya kimabavu, wazazi wenye malezi ya mamlaka huweka sheria na miongozo, lakini hutoa nafasi kwa watoto wao kujieleza na kuelezea mitazamo yao.
 
3. Malezi huru: Wazazi wenye malezi huru ni wavumilivu, na hawawafuatilii watoto wao sana. Huingilia na kuonekana pale tu panapojitokeza tatizo kubwa dhidi ya watoto wao.
 
4. Malezi huria: Wazazi wenye malezi huria, kimsingi hutarajia watoto wajilee wao wenyewe. Wazazi hawatumii nguvu nyingi kutafta mahitaji ya watoto wao. Wakati mwingine wazazi hawa, hawafahamu juu ya maendeleo ya watoto wao.
Aina zote za Malezi zinaathiri tofauti tabia ya mtoto. Tafiti zinaonyesha kuwa Malezi ya mamlaka (demokrasia) yana manufaa kwa watoto zaidi ya aina nyingine.
 
Je, ni aina ipi kati ya hizi umekua ukitumia kukuongoza katika safari yako ya Malezi?
 
Kama una swali lolote kuhusu malezi ya mtoto usisite kupiga namba 116, Huduma ya Simu kwa Mtoto inayopatikana kupitia mitandao yote Tanzania bila malipo.
 
Source: Sema Tanzania