Image

Kuoza kwa meno (Dental Caries) ni ugonjwa wa kuambukiza

Miaka ya nyuma iliaminika kuwa ugonjwa wa kuoza kwa meno si wa kuambukiza; lakini tafiti nyingi zilizofanyika zimedhihirisha ni ugonjwa wa kuambukiza. Jino lililooza linaweza kuambukiza meno yaliyogusana nalo na pia mgonjwa aliyeoza meno au mwenye wadudu wanaosababisha kuoza kwa meno anaweza kuambukiza mwenzake/wenzake.

Wadudu wanaosababisha kuoza kwa meno ni sehemu ya wadudu wakazi kinywani (oral flora). Wadudu hawa hujishikiza kwenye meno na kufanya utando, wana uwezo wa kuchachua vyakula hasa vyenye asili ya sukari na kutoa tindikali. Ni tindikali hii ambayo huvuta madini kwenye meno na kuweka matobo. Utando huu wa wadudu kwenye jino moja unaweza kuwa na wadudu nusu bilioni, miongoni mwao wakiwemo jamii ya mutans streptococci ambao kimsingi ndiyo wasababishaji wakuu wa kuoza kwa meno. Wadudu wengine ni kama Lactobacillus na Actinomyces.

Jinsi wanavyoambukiza

Ndani ya jamii ya wadudu hawa ziko jamii zingine ndogondogo ambazo zinatofautiana kwa uwezo wa kuchachua vyakula na kutoa tindikali na hata uwezo wa kujishikiza kwenye meno. Kwa mtu mwenye wadudu wasio wakali anaweza kuambukizwa na mwenzake mwenye wadudu wakali na hivyo kuingia kwenye hatari zaidi ya kuoza meno. Tafiti zimeonesha wapenzi/wanandoa wanaweza kuambukizana kwa njia ya kubusiana. Watoto wanaochangia ice cream/ice water mashuleni pia wanaambukizana kwa njia hii. Tafiti pia zimeonesha wazazi wanaotafunia vyakula watoto wao kama sehemu ya kuvilainisha wanaweza kuwambukiza pia watoto wao.

Njia nyingine ni jino lililooza kuambukiza mengine yanayogusana nayo, tindikali inayozalishwa na wadudu katika jino lililooza inaweza kuathiri jino lililo jirani. Ndiyo maana inashauriwa ukiona jino limeanza kuoza muone mtaalamu akalitibu au akaling’oe kama halitibiki ili lisiambukize mengine.

Namna ya kujikinga

  • Njia muhimu ni kutembelea cliniki za meno angalau kila baada ya miezi sita
  • Kuzuia watoto kuchangia vyakula mudomoni
  • Kupima kuangalia kiwango na aina za bakiteria zilizi kwenye mate yake na kupata dawa ikibidi.
  • Kuhusu kubusiana sina la kusema
Imesomwa mara 36235 Imehaririwa Alhamisi, 27 Aprili 2017 15:17
Dr. Augustine Rukoma

Dr Dr. Augustine Rukoma ni daktari na mtaalamu wa meno, anapenda kutumia muda wake wa ziada kuandika makala na kubadilishana mawazo juu ya afya ya kinywa na Meno.

rukomadentalanswers.blogspot.com | Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana