Image

Ugonjwa wa Tete Kuwanga (Chicken Pox)

Tete kuwanga ni ugonjwa  ambao unaombukiza na kusababishwa na virusi vinavyojulikana kama Varicella zoster virus.Maambukizi ya tete kuwanga huonekana sana kwa watoto wadogo ingawa hata watu wakubwa pia hupata maambukizi ya ugonjwa huu. Tete kuwanga hupatikana duniani kote.Katika nchi zenye kupata majira ya baridi, maambukizi ya ugonjwa huu huonekana sana wakati wa kipindi cha majira ya baridi na kipindi cha masika. 
 
Watoto walio na umri wa miaka 4-6 wako kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya tete kuwanga na ndio katika umri huu ambapo maambukizi ya ugonjwa huu yapo kwenye kiwango cha juu sana.Inakadiriwa ya kwamba, tete kuwanga huambukiza kwa kiwango cha asilimia 90.
 
Watoto wengi hupata maambukizi ya tete kuwanga kabla ya kufikia umri wa kubaleghe ingawa asilimia 10 ya vijana bado wanakuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi ya tete kuwanga. Katika nchi za tropiki,maambukizi ya tete kuwanga huonekana kwa watu wakubwa na  huenda yakawa maambukizi ya hatari sana.

Maambukizi ya tete kuwanga hupatikana vipi?

Tete kuwanga huambukizwa kupitia njia ya hewa au endapo mtu atagusana mwili na mgonjwa wa tete kuwanga(kupitia majimaji yanayotoka kwenye vipele vya mgonjwa).Mtu yoyote yule anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kutoka kwa mgonjwa wa tete kuwanga kwa njia ya kucheka, kupiga chafya, kukohoa .Hii inatokana na kusambazwa kwa virusi ya Varicella zoster kwa njia ya hewa pindi mgonjwa anapocheka,kupiga chafya au anapokohoa.
Nini hutokea kipindi cha maambukizi (Pathofiziolojia)
 
Maambukizi ya tete kuwanga kwa mtoto husababisha mtoto kutoa kinga aina ya Immunoglobulin G (IgG), Immunoglobulin M, (IgM) na Immunoglobulin A,(IgA). Kinga hizi  pamoja na kinga zinazosaidiwa na chembechembe za mwili (Cell mediated responses)husaidia kupunguza madhara na urefu wa maambukizi haya ya awali ya tete kuwanga.Immunoglobulin G hubakia kipindi chote cha maisha na huweka kumbukumbu ya maambukizi ya tete kuwanga na hivyo kuwa chanjo dhidhi ya ugonjwa huu hapo baadae maishani.
 
Baada ya kupata maambukizi ya Varicella zoster virus, virusi hivi husambaa hadi kwenye tishu za ngozi, kamasi (mucosal) na hata kwenye mishipa ya fahamu (sensory nerves).Virusi hivi baada ya muda huwa kimya (dormant) {‘’ambapo ndio tunasema mgonjwa amepona’’} kwenye kifundo cha mishipa ya fahamu vinavyojulikana kama dorsal ganglion of sensory nerves.Kuchepuka tena kwa virusi hivi ambavyo awali vilikuwa vimekaa kimya ndio husababisha ugonjwa wa ukanda wa jeshi (herpes zoster),postherpetic neuralgia, na Ramsay Hunt Syndrome Type II.
 
Ramsay Hunt Syndrome type II inaambatana na dalili za kupooza sehemu mbalimbali za uso,maumivu kwenye sikio/masikio, kupoteza ladha ya ulimi (taste loss),mdomo kukauka, macho kuwa makavu na vipele kwenye mwili.

Dalili na viashiria vya Tete kuwanga

 Dalili za kwanza ni

• Kichefuchefu
• Kupungua kwa hamu ya kula
• Maumivu ya kichwa
• Maumivu ya misuli
• Kuumwa tumbo
 
Dalili hizi baadae hufuatiwa na hatua ya mgonjwa kutoka vipele, uchovu na homa ambayo sio kali sana, hatua hii ndio huonyesha kuwepo kwa ugonjwa wa tete kuwanga.
Vipele hivi mwanzo huonekana kama alama nyekundu ndogo kwenye uso, kichwa, tumbo,kifua, sehemu za juu za  kwenye mikono na miguu ambapo baada ya masaa 10-12 alama zile nyekundu hugeuka kuwa uvimbe, uvimbe huu kisha hujaa maji na kupasuka. Baadae vipele vipya (blisters) huanza kuchipuka  kwa makundi kwenye sehemu za tupu ya mwanamke (vagina), kope (eyelids) na mdomoni ambavyo hupasuka na kuwa vidonda vidogo vidogo kwenye sehemu hizi.
 
Hatua hii ya kutokea vipele huanza kuonekana kuanzia siku ya 10-21 baada ya mtu kupata maambukizi ya Varicella zoster virus na huambatana na kuwashwa sana mwili.Vipele vinaweza kutokea kwenye viganja vya mkono, nyayo na hata kwenye pua, lips, masikio, njia ya haja kubwa.
 
Vipele venye majimaji (blisters) hutokea siku ya 4-7 baada ya hatua ya kutoka vipele kuanza na hupotea kuanzia siku ya 5 na kuendelea.
Mtu ambaye ana maambukizi ya tete kuwanga huweza kuambukiza watu wengine siku moja au mbili kabla ya kuanza kutoka vipele na kuendelea kuwa na uwezo wa kuambukiza wengine kwa  siku 4-5 baada ya vipele kutokea.
Dalili ya kwanza ya tete kuwanga kwa watoto ni vipele kabla ya  dalili nyingine  nilizotaja awali hapo juu kufuata.Kwa watu wakubwa, vipele husambaa katika maeneo mengi mwilini kwa wingi na homa huwa ya muda mrefu sana na pia huweza kupata homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Varicella zoster virus.
 
Baadhi ya watoto ambao walipata chanjo ya ugonjwa huu hapo awali huweza kupata tena maambukizi ya tete kuwanga ingawa yanakuwa sio makali sana(hutoka vipele 30 kwa wastani) lakini watoto hawa bado wana uwezo wa kuambukiza wengine ugonjwa huu.Kwa kawaida mtoto hutokea wastani wa vipele 250 hadi 500 wakati wa maambukizi ya ugonjwa wa tete kuwanga.
Ugonjwa huu ni nadra sana kuwa na madhara makubwa ingawa madhara huweza kuonekana kwa wagonjwa walio na upungufu wa kinga mwilini, wenye kuugua magonjwa sugu au wanawake wajawazito ambao hawakupata chanjo ya ugonjwa huu.

Vipimo vya uchunguzi

  • Utambuzi wa ugonjwa huu hufanywa kwa kuangalia dalili na viashiria vya ugonjwa huu(Kichefuchefu, kupungua kwa hamu ya kula,maumivu ya kichwa,maumivu ya misuli, kuumwa tumbo na vipele)
  • Kupima majimaji ya ndani ya vipele kwa kutumia direct immunoflorescent test
  • Kipimo cha damu kuangalia wingi wa Immunglobin M (IgM), ambapo kiwango chake huongezeka panapotokea maambukizi mapya au kuangalia uwepo wa Immunoglobulin G (IgG) ili kuthibitisha kuwepo kwa maambukizi hapo awali.
  • Kipimo cha ultrasound kwa wanawake wajawazito ili kuangalia dalili za kuwepo kwa maambukizi ya ugonjwa huu kwa kiumbe kilichomo tumboni (Fetal Varicella Infection).Inashauriwa kuchelewesha kipimo hiki kwa wiki 5 toka mama apate maambukizi ya tete kuwanga ili kuweza kutambua kama mtoto ameathirika au la.
  • Kipimo cha kuangalia vina saba (DNA) ya virusi vya Varicella zoster virus kwa mama wajawazito kwa kuchukua maji kwenye chupa ya uzazi ya mama (amniotic fluid). Kipimo hiki kina madhara kama kusababisha mimba kutoka au mtoto kupata Fetal Varicella Syndrome

Matibabu

Matibabu ya ugonjwa huu yanalenga kupunguza athari za dalili na viashiria vya ugonjwa huu na si kuua virusi vinavyosababisha ugonjwa huu
 
Matibabu ya tete kuwanga yanahusisha
  • Kuwakata watoto kucha ili kuepusha kujikuna na hatimaye kukata vipele hivyo kuongeza kutokea kwa vipele mwilini
  • Dawa za maumivu kama paracetamol n.k
  • Antihistamines-Dawa za kupunguza kuwashwa mwili
  • Calamine lotion ingawa hakuna tafiti zilizofanyika kuthibitisha ubora wa matumizi yake dhidhi ya ugonjwa huu.Dawa hii ni salama
  • Kuongeza kiwango cha usafi wa mwili, kuosha mwili kwa maji ya uvuguvugu
  • Kukaa sehemu zenye baridi ili kupunguza kuwashwa mwili
  • Kuepuka kujikuna vipele
  • Dawa dhidhi ya virusi (antiviral medication) kama acyclovir au valacyclovir ambazo hutolewa saa 24-48 baada ya vipele kuanza,dawa hizi hupunguza kusambaa kwa virusi lakini haziui virusi hao.Dawa hizi hutolewa kwa wale ambao wana upungufu wa kinga mwilini na kwa wanawake wajawazito.Watoto chini ya miaka 12 au wale wenye umri wa zaidi ya mwezi mmoja hawaruhusiwi kutumia dawa hizi kama hawana tatizo la upungufu wa kinga mwilini ili kuwaepusha na madhara wanayoweza kupata kutokana na matumizi ya madawa haya.

 Madhara ya tete kuwanga kwa wajawazito

Maambukizi ya tete kuwanga wakati wa ujauzito yanaweza kuathiri mtoto hasa kama mama atapata maambukizi haya wiki 28 baada ya kushika mimba.Wanawake ambao wana kinga dhidhi ya ugonjwa huu hawawezi kupata tete kuwanga kipindi cha ujauzito na wasiwe na wasiwasi kuhusu mtoto wao kupata madhara.Madhara ya tete kuwanga kwa mtoto ni kutokana na uwezo wa Varicella zoster virus kuwa na uwezo wa kuvuka kondo la uzazi (placenta) kutoka kwa mama mwenye tete kuwanga na hivyo kumuathiri mtoto.
Maambukizi ya tete kuwanga kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kipindi cha ujauzito hujulikana kama fetal varicella syndrome au congenital varicella syndrome na huambatana na;
  • Madhara kwenye ubongo wa mtoto-Kichwa maji (hydrocephalus), kichwa kuwa kidogo, maambukizi ya ubongo (encephalitis),aplasia of brain
  • Madhara ya macho kama mtoto wa jicho (cataract), optic cup, optic stalk,microphthalmia, cataracts, chorioretinitis, optic atrophy n.k. 
  • Madhara ya mishipa ya fahamu
  • Madhara ya kibofu cha mkojo, miguu, njia ya haja kubwa,vidole kutoota vizuri n.k.
  • Matatizo ya ngozi kama hypopigmentation na n.k.
Watoto wenye umri wa mwezi mmoja au watoto wachanga wanatakiwa kulindwa wasipate tete kuwanga kwa kuweka mbali na wagonjwa wa tete kuwanga kwa siku 10-21. Uwezekano wa mtoto kupata tete kuwanga ni mkubwa iwapo mama atapata maambukizi ya tete kuwanga siku saba kabla ya kujifungua au wiki moja baada ya mtoto kuzaliwa.
 
Imesomwa mara 24826 Imehaririwa Jumanne, 11 Julai 2017 11:03
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.