Ni moja kati ya magonjwa sugu ambayo sio ambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine. Vilevile ni kati ya magonjwa ambayo ni endelevu.
Kuna magonjwa makuu manne yasiyo ambukizi
- Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu-shambulizi la moyo na kiharusi
- Kansa au saratani
- Kisukari
- Magonjwa sugu yasababishayo kuziba mfumo wa upumuaji kitaalamu COPD’s
Kulingana na taarifa za shirika la afya duniani
- Watu milioni 36 kila mwaka huathiriwa na magonjwa yasiyo ambukizi
- Karibu asilimia 80 sawa na watu milioni 29 hufa kutokana na magonjwa yasiyo ambukizi katika nchi za vipato vidogo na vya kati.
- Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ndio husababisha vifo zaidi watu milioni 17 kwa mwaka, ikifuatiwa na kansa watu milioni 7, mfumo wa upumuaji watu milioni 4, na kisukari milioni 1.
- Magonjwa haya yote huweza kusababishwa na vifuatavyo: utumiaji wa tumbaku, kutofanya mazoezi kabisa, utumiaji wa pombe kupita kiasi, utumiaji wa vyakula visivyo bora.
Ugonjwa wa moyo unaosababishwa na simanzi au kuachana na mpenzi/mwenza wako yoyote yule hujulikana kitaalamu kama Takostubo au broken heart syndrome.
Ugonjwa huu husababishwa na kudhoofika ghafla kwa misuli ya moyo kwa muda mfupi na hauuhusiani na tatizo la kukosekana kwa damu ya kutosha katika moyo.Tatizo hili hujulikana kama broken heart syndrome kwa sababu hutokana na mtu;
- Kufiwa na mpenzi/mwenza wake
- Kuachana na mpenzi/mwenza wake
- Kuwa na wasiwasi mara kwa mara kwa muda mrefu
Vilevile tatizo hili huweza kupelekea moyo kushindwa kufanya kazi ghafla (Acute heart failure), moyo kupiga bila mpangilio usio wa kawaida (lethal ventricular arrhythmia) .
Dalili
- Maumivu makali ya kifua
- Matatizo ya upumuaji au kuhema kwa shida
- Uchovu
- Mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio
Je tatizo hili husababishwa na nini?
Tatizo hili huweza kusababishwa na mambo yafuatayo:
- Habari ya kufiwa na mpenzi wako
- Kutambua unaugua ugonjwa sugu kama vile saratani
- Kupoteza hela nyingi
- Sherehe ya kushtukiza (surprise parties)
- Kutakiwa kuongea hadharani
- Ukiwa na matatizo kama ugonjwa wa pumu, maambukizi, ajali ya gari au baada ya upasuaji mkubwa.
Vipimo
- ECG
- X-ray ya kifua
- Echocardiogram
- MRI
- CAG
- Kipimo cha damu kuangalia vimeng’enyo vya kwenye moyo
- Ni muhimu kutofautisha na Shambulizi la moyo na hili tatizo
Matibabu
Hakuna tiba ya madawa iliyo maalum kwa ajili ya kutibu tatizo hili pekee. Matibabu yake yanaweza kufanana na matibabu ya shambulio la moyo, na mgonjwa anaweza kuhitaji kulazwa hospitali kwa muda ingawa si mara zote huwa hivyo.
Daktari akishathibitisha kuwa chanzo cha dalili zako ni broken heart syndrome na wala si shambulio la moyo anaweza kukupatia dawa kama vile zilizo katika kundi la angiotensin-converting enzyme (ACE) inhibitors mfano Benazapril, kundi la beta blockers kwa mfano carvedilol au kundi la diuretics kama vile frusemide (lasix). Dawa hizi husaidia kupunguza mzigo katika moyo na pia kuzuia usipate shambulio jipya.
Kwa kawaida wagonjwa wengi hupata nafuu baada ya muda wa kama mwezi mmoja au miwili hivi. Hata hivyo ni vema kumuuliza daktari wako unapaswa kutumia dawa kwa muda gani.
Kinga
Kuna uwezekano mkubwa sana wa hali hii kujirudia tena mara baada ya shambulio la kwanza. Mpaka sasa hakuna dawa zilizothibitishwa zinazoweza kusaidia kuzuia hali hii isijitokeze tena, ingawa baadhi ya madaktari wanashauri matumizi ya muda mrefu ya dawa zakundi la beta blockers kama vile atenolol, carvedilol, au dawa zenye kuzuia uzalishaji wa homoni zenye kuchochea shinikizo katika moyo.
Pamoja na matumizi ya dawa, ushauri nasaha pamoja na kubadili mfumo wako wa maisha ni mambo ya muhimu zaidi kusaidia kukukinga na tatizo hili.
Ukweli kuhusu umuhimu wa mazoezi katika kuzuia na kutibu magonjwa mbalimbali
Iwe unafanya kwa nia ya kuwa na umbo lenye muonekano mzuri, au kupoteza muda wa ziada ulionao, mazoezi ni zaidi ya unavyoweza kufikiria.
Ongezeko la tafiti katika eneo la mazoezi na magonjwa yahusianayo na mifumo ya maisha (lifestyle-related diseases) lililotokea ndani ya takribani miaka kumi iliyopita, limefumbua macho ya wengi juu ya umuhimu wa mazoezi katika kujikinga na kutibu magonjwa mbalimbali. Tafiti katika eneo hili zinaonesha kwamba mazoezi yanaweza kutumika kujikinga na magonjwa zaidi ya ishirini na kutibu magonjwa takribani kumi.
Ni jambo lililowazi kabisa kwamba babu zetu waliweza kuishi kwa miaka mingi zaidi ya kizazi tulichopo sisi. Ni dhahiri pia kwamba kizazi chetu kinashuhudia milipuko ya magonjwa ambayo babu zetu hawakuwahi hata kuyasikia. Pia mtakubaliana nami kuwa, kumekuwa na mambo mengi ya kimaendeleo yaliyotokea katika kipindi chote hiki, ambayo wanazuoni wamekuwa wakiyahusisha na milipuko ya baadhi ya magonjwa.
Yapo mambo mengi katika mifumo yetu ya maisha ya kila siku yaliyo mazuri katika muonekano na hisia, lakini ukweli ni kwamba yaweza kuwa na athari kubwa kwa afya zetu.
Kila mtu anapenda kuendesha gari wakati wote anapohitajika kwenda sehemu, pia watu wengi wanafurahia kuketi na kuangalia vipindi wavipendavyo katika runinga muda wote wapatapo wasaa. Si ajabu pia watu wengi wanapenda shughuli zisizohitaji kutembea tembea au kutumia nguvu.
Miaka ya nyuma iliaminika kuwa ugonjwa wa kuoza kwa meno si wa kuambukiza; lakini tafiti nyingi zilizofanyika zimedhihirisha ni ugonjwa wa kuambukiza. Jino lililooza linaweza kuambukiza meno yaliyogusana nalo na pia mgonjwa aliyeoza meno au mwenye wadudu wanaosababisha kuoza kwa meno anaweza kuambukiza mwenzake/wenzake.
Wadudu wanaosababisha kuoza kwa meno ni sehemu ya wadudu wakazi kinywani (oral flora). Wadudu hawa hujishikiza kwenye meno na kufanya utando, wana uwezo wa kuchachua vyakula hasa vyenye asili ya sukari na kutoa tindikali. Ni tindikali hii ambayo huvuta madini kwenye meno na kuweka matobo. Utando huu wa wadudu kwenye jino moja unaweza kuwa na wadudu nusu bilioni, miongoni mwao wakiwemo jamii ya mutans streptococci ambao kimsingi ndiyo wasababishaji wakuu wa kuoza kwa meno. Wadudu wengine ni kama Lactobacillus na Actinomyces.
Kujamiana (ama tendo la ndoa) ni moja ya mambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Ni ukweli usiofichika kwamba wengi wetu tungependa kuwa na mwenza ambaye mnaridhishana katika tendo la ndoa. Si hivyo tu, bali tendo hili huleta maelewano katika uhusiano wowote ule. Lakini, kuna faida zozote za kiafya za kufanya tendo hili? Ndiyo! Zipo faida kadhaa zinazotokana na kujamiana. Katika makala hii, mwandishi wako Dk. Khamis Hassan anajaribu kutueleza faida za kujamiana kiafya kama ambavyo imewahi kuonekana katika tafiti kadhaa zilizofanyika sehemu mbalimbali duniani.
1. Hulinda mwili dhidi ya magonjwa ya moyo:
Wanawake ambao hufika kilele (orgasm) angalau mara mbili kwa wiki kila wanapojamiana, wana uwezekano mdogo sana (30% tu) wa kupata maradhi ya moyo tofauti na wale wasiofikia kilele. Hii ni kwa vile homoni ya endorphin inayotolewa wakati wa kujamiana hupunguza msongo wa mawazo na hivyo kumuepusha mtu na magonjwa wa moyo. Aidha kujamiana angalau mara tatu kwa wiki, husaidia kupunguza uwezekano wa kupata shambulio la moyo (heart attack) na kiharusi. Uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo wakati wa kufanya mapenzi ni mdogo sana, ni asilimia 1 tu ya vifo vyote vinavyotokana na mshtuko wa moyo ndivyo uhusishwa na kujamiana. Aidha, sababu nyingine inayoongeza uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo ni kuwa na uhusiano nje ya ndoa ambapo huchangia karibu asilimia 75 ya vifo vinavyotokana na kujamiana, na karibu asilimia 90 ya vifo hivi hutokea kwa wanaume wazee. Uwezekano wa kupata shambulio la moyo wakati wa kujamiana huongezeka ikiwa mtu ana miaka zaidi ya 50, uzito uliopitiliza na matatizo ya afya. Hii ni sawa na kusema unaanza kufanya mazoezi mazito kwa ghafla wakati mwili na umri haviruhusu.
3. Hupunguza msongo wa mawazo:
Kujamiana hupunguza msongo wa mawazo na shinikizo la damu na humfanya mtu kupata usingizi mnono. Kufikia kilele ni sawa na kunywa 2-3mg za dawa ya diazepam (kumbuka diazepam hufanya mwili kupumzika, muscle relaxant), na hii ndiyo sababu kuu ya kwa nini watu hupata usingizi mzito baada ya kujamiana. Watu wanaojamiana huweza kuhimili vizuri msongo wa mawazo tofauti na wale ambao hawafanyi hivyo. Aidha watu wanaojamiana huwa na kiwango cha kawaida cha shinikizo la damu kuliko wale wasiojamiana. Pia kuwepo kwa viasili vya prostaglandins katika shahawa husaidia kupunguza msongo wa mawazo. Viasili hivi hunyonywa na sehemu za siri za mwanamke. Shahawa pia zina madini ya zinc, calcium, potassium, fructose na protini ambavyo vyote ni muhimu kwa afya njema.
Mtoto Saul amekumbwa na ugonjwa wa ajabu wa kusinzia na kutikisa kichwa. Mama yake anasema Saul hupatwa na degedege linaloweza kumchukua muda wa hadi si chini ya saa tatu kupata nafuu na kila shambulio huwa kali kiasi cha kumfanya mama abaki asijue la kufanya. Mama Saul anasema, tangu mwanaye akumbwe na ugonjwa huu amekuwa si yule anayemfahamu, amekuwa kama mtoto aliyechanganyikiwa akizungukazunguka bila kujua alifanyalo. Mama Saul anasema, kuna wakati Saul aliwahi kupotea kijijini bila kujulikana yupo wapi kiasi kwamba hivi sasa inampasa kuwafungia ndani watoto wake wengine ili wasipotee kama ndugu yao.
Mtoto Saul ni miongoni tu mwa mamia kwa maelfu ya watoto waliokumbwa na ugonjwa wa ajabu wa kusinzia na kutikisa kichwa huko nchini Uganda pamoja na Sudan ya Kusini na sasa inasemekana umeshaingia nchini Tanzania.
Mpaka sasa si madaktari wala wanasayansi wanaoelewa kwa undani chanzo halisi cha ugonjwa huu ingawa juhudi za kitafiti zinaendelea.
Ugonjwa wa kusinzia na kutikisa kichwa umepewa jina la 'Nodding disease' kwa sababu watoto wanaokumbwa na ugonjwa huu huonesha dalili ya kutingisha kichwa kama mtu anayeitikia kitu pamoja na dalili nyingine zinazofanana na za mtu mwenye kifafa zikiambatana na kusinzia.
Zipi hasa ni dalili za ugonjwa huu?
Watoto wenye ugonjwa wa kusinzia huathirika zaidi mfumo wao wa fahamu pamoja na ubongo [1] wa kupatwa na shambulizi kali la degedege, kushindwa kula chakula na kubadilika kabisa kitabia.
Mtoto huanza kuonesha hali ya kutikisa kichwa kama anayeitikia jambo, hufumba macho, kisha huinamisha kichwa chake kama anayesinzia, lakini akiwa haoneshi dalili yoyote ya kuchoka na pia huonekana kupambana ili asipoteze ufahamu. Kisha huinua kichwa chake juu na kukaza macho yake kama mtu anayetazama kitu kabla ya macho yake kuwa mazito na kope kufunga na kupitiwa na usingizi mzito. Hali hii hufuatiwa na kuanguka kwa ghafla na wakati mwingine kujiumiza mwili.
Shambulizi la degedege huchochewa na vitu tofauti kidogo na vile vinavyochochea degedege linalowapata kwa mfano watoto wenye kifafa. Imeripotiwa na baadhi ya wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huu kuwa, baadhi ya watoto walikumbwa na degedege baada ya kutokea mabadiliko ya hali ya hewa au baada ya kuoneshwa chakula ambacho hawajawahi kula hapo kabla.
Dalili nyingine ni pamoja na kitendo cha watoto kupoteza ufahamu wa wapi walipo, kuzurura zurura bila kujielewa na wakati mwingine kupotea vichakani. Katika hali ya kushangaza yameripotiwa pia matukio ya baadhi ya watoto waliokumbwa na ugonjwa huu kuchoma moto nyumba za vijiji bila kujitambua, kuchanganyikiwa na kuwa kama walioumizwa kiakili na kihisia.
Mahudhurio yao shuleni huwa hafifu, lishe huzidi kuwa duni hatimaye watoto hupatwa na utapiamlo, magonjwa nyemelezi na hatimaye kifo.
Je, Tanzania ni salama?
Miaka kadhaa nyuma kumewahi kuripotiwa milipuko kadhaa ya ugonjwa huu katika nchi za Tanzania, Liberia na Sudan lakini haikuwa mpaka mwaka 2009 ndipo mamlaka za Afya duniani zilipouchukulia kwa uzito unaostahili pale kulipotokea mlipuko wa kwanza mkubwa huko nchini Uganda.
Miaka kadhaa nyuma kumewahi kuripotiwa matukio ya ugonjwa wenye dalili zenye kufanana na huu huko nchini Tanzania [4], ingawa ugonjwa huu wa sasa wenye kuhusisha kutikisa kichwa umeripotiwa zaidi maeneo ya Sudan ya kusini na Uganda Kaskazini hususani kwenye maeneo fulani fulani [2, 3, 5].
Hivi sasa, timu ya watafiti kutoka shirika la Afya Duniani (WHO), mamlaka za Afya za Uganda pamoja na wataalamu kutoka kituo cha magonjwa ya maambukizi (CDC) cha nchini Marekani ipo nchini Uganda ikifanya utafiti kufahamu chanzo cha ugonjwa huu na jinsi ya kuutibu.
Nini hasa chanzo cha ugonjwa huu?
Chanzo halisi cha ugonjwa huu bado hakijafahamika ingawa kuna fununu fununu za hapa na pale. Watalaamu wamependekeza mambo mbalimbali kuwa yawezekana yakawa visababishi vya ugonjwa huu, yakiwemo maambukizi ya vimelea mbalimbali, ukosefu wa lishe, mazingira, na sababu za kisaikolojia. Wengine walikwenda mbali zaidi na kupendekeza uhusiano wa mabadiliko katika muundo wa vinasaba, maambukizi ya virusi wa surua, ulaji wa nyama ya nyani, matumizi ya vyakula vya msaada au hata mbegu za msaada kuwa yanaweza kuwa chanzo cha ugonjwa huu ingawa hakuna uthibitisho wa madai hayo mpaka sasa [2,3,5].
Wataalamu kutoka shirika la Afya Duniani wanasema karibu asilimia zaidi ya 90 ya watoto waliokumbwa na ugonjwa huu walikuwa wakiishi kwenye maeneo maarufu sana kwa ugonjwa wa upofu (river blindness) unaosababishwa na vimelea wanaojulikana kama Onchocerca Volvulus ambao husambazwa na aina fulani ya mbu [2,3,5].
Hata hivyo, November 2010, jopo la watafiti wa WHO lilifika eneo la kaskazini mwa Uganda kufanya uchunguzi wa chanzo na dalili za ugonjwa huu. Katika uchunguzi wao wa awali, walifanikiwa kuorodhesha watoto 38 waliokumbwa na ugonjwa huu na wale wasio na ugonjwa, na kuchunguza kama wana maambukizi ya vimelea vya Onchocerca volvulus ambapo vimelea hivi vilionekana zaidi kwa watoto waliokuwa na ugonjwa (76%) wakati ni 47% tu ya watoto wasiokuwa na ugonjwa wa kusinzia ndiyo waliokutwa navyo. Uchunguzi wao wa kistatistiki haukuonesha uhusiano wowote kati ya ugonjwa huo na vimeleo hivyo. Hali iliyoonesha kuwa pamoja na kwamba ugonjwa wa onchocerca ulikuwa umeenea sana eneo hilo, haikuweza kuthibitika moja kwa moja iwapo ugonjwa huo ulikuwa chanzo cha ugonjwa wa kusinzia [1].
Juu ya hilo, watoto wengi wenye ugonjwa huu walikutwa pia na upungufu mkubwa wa Vitamin B6, aina ya vitamini ambayo ni muhimu sana katika kuimarisha mfumo wa fahamu.
Aidha uchunguzi zaidi unaonesha kuwa lishe duni pia inawezekana ikawa chanzo kimojawapo au kihatarishi cha mtoto kupatwa na ugonjwa huu.
Ukubwa wa tatizo
Kutokana na taarifa zisizothibitishwa zilizopatikana kutoka kwa wafanyakazi wa afya walio maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huu, waathirika ni watoto walio kati ya umri wa mwaka 1 mpaka 19, ingawa kundi la watoto wenye umri wa kati ya miaka 3 mpaka 11 huathirika zaidi, na tayari umesharipotiwa katika nchi za Liberia, sudan ya Kusini, Guinea ya Ikweta, [2] na sehemu za kaskazini za Uganda na kusini mwa Tanzania [3,4]. Mlipuko huu wa sasa nchini Uganda umejikita zaidi maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo, ingawa haijathibitika bado kama ugonjwa huu unaambukizwa japokuwa wataalamu wa afya wanalichukulia hilo kwa uzito mkubwa wakitilia maanani hofu yao ya kusambaa kwa ugonjwa huo sehemu nyingine za dunia.
Ripoti kutoka baadhi ya vijiji vya maeneo ya kaskazini mwa Uganda zinasema kuwa karibu kila kaya imeripotiwa kuathiriwa na ugonjwa huu. Mpaka sasa haijulikani idadi kamili ya vifo vilivyosababishwa na ugonjwa huu ingawa kuna idadi kubwa tu ya watoto walioathiriwa vibaya kiasi cha kushindwa kujihudumia wenyewe na kuwaongezea mzigo wa huduma wazazi na walezi wao.
Ugonjwa huu unatibiwaje?
Mpaka sasa hakuna tiba ya uhakika ya ugonjwa huu. Hii ni kwa vile wataalamu bado hawafahamu chanzo halisi cha ugonjwa na jinsi unavyoambukizwa. Maisha ya watoto katika maeneo yaliyoathirika yamekuwa ya mashaka sana na kuna ripoti za baadhi ya wazazi kutupa watoto wao kwa vile hawajui ni kwa jinsi gani wanaweza kuwasaidia. Hofu yao nyingine ni kuogopa kuambukizwa kwa vile hawajui ni kwa vipi ugonjwa huu husambaa.
Ni hapa majuzi tu, mamlaka za afya za nchini Uganda ziliona umuhimu wa kufungua kituo cha kwanza cha afya kwa ajili ya kuwahudumia watoto waliokumbwa na ugonjwa huu baada ya kipindi kirefu cha kusuasua kuchukua hatua, ingawa hakuna tiba inayojulikana wala chanjo iliyogundulika mpaka sasa.
Hata hivyo katika hali ya majaribio, baadhi ya madaktari wameanza kutumia dawa za kutibu na kuthibiti kifafa kwa ajili ya kuthibiti na kutuliza degedege linaloambatana na ugonjwa huu ingawa mafanikio ya njia bado si ya kuridhisha sana, kwa vile wanasema njia hii husaidia tu kupunguza kasi ya kutokea kwa dalili na si kuzikomesha kabisa.
Tanzania ijiandae
Ripoti zisithothibiitishwa kwamba tayari ugonjwa huu umeshaingia Tanzania au kuna uwezekano mkubwa ukavuka mipaka na kuingia nchini si jambo la kulichukulia kijuujuu hata kidogo. Ni wakati muafaka sasa mamlaka zinazohusika kujiweka tayari na kujiandaa kulikabili tatizo hili kabla au pindi mlipuko utakapotokea.
Marejeo
1. Lul Reik, MD, Abdinasir Abubakar, MD, Martin Opoka, MD, Godwin Mindra, MD, James Sejvar, MD, Scott F. Dowell, MD, Carlos Navarro-Colorado, MD, Curtis Blanton, MS, Jeffrey Ratto, MPH, Sudhir Bunga, MD, Jennifer Foltz, MD, EIS officers, CDC. Nodding Syndrome — South Sudan, 2011 Weekly January 27, 2012 / 61(03);52-54. Inapatikana mtandaoni kupitia http://www.cdc.gov/mmwr/preview/mmwrhtml/mm6103a3.htm
2. Nyungura JL, Akim T, Lako A, Gordon A, Lejeng L, William G. Investigation into nodding syndrome in Witto Payam, Western Equatoria State, 2010. Southern Sudan Medical Journal 2010;4:3–6.
3. Winkler AS, Friedrich K, Konig R, et al. The head nodding syndrome—clinical classification and possible causes. Epilepsia 2008;49:2008–15.
4. Winkler AS, Friedrich K, Meindl M, et al. Clinical characteristics of people with head nodding in southern Tanzania. Trop Doct 2010;40:173-5.
5. Lacey M. Nodding disease: mystery of southern Sudan. Lancet Neurol 2003;2:714.