Image

Ugonjwa wa kifua kikuu ni kati ya magonjwa matatu yanayotokea sana kwa watu masikini duniani (Disease of poverty). Magonjwa mengine katika jamii ya disease of poverty ni malaria na Ukimwi (AIDS). Ugonjwa wa kifua kikuu huathiri asilimia 98 ya watu katika nchi zinazoendelea, ukimwi asilimia 95 na malaria asilimia 90.

Magonjwa haya matatu husababisha vifo asilimia 10 ya idadi ya watu wote duniani kwa ujumla, ambapo inakisiwa watu wote duniani ni 6.91 bilioni kulingana na kituo cha kuhesabu watu cha Marekani ( US Census Bureau).

Kwa Tanzania, watu 120,191 hukisiwa kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu kila mwaka, hii ni kutokana na taarifa ya shirika la USAID ya mwaka 2007. Kati ya watu hawa (120,191), 56,233 ni wale wanaogundulika kuwa na ugonjwa huu kupitia makohozi yaani sputum smear positive (SS+ ). Vifo vinavyotokana na ugonjwa wa kifua kikuu ni 32,000 kila mwaka nchini Tanzania.

Tanzania ni ya 15 kati ya nchi 22 ambazo zimeathiriwa sana na ugonjwa huu. Kati ya asilimia 50 ya wagonjwa wa kifua kikuu waliopimwa virusi vya ukimwi mwaka 2007, inakadiriwa ugonjwa wa ukimwi huathiri asilimia 47 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu. Ugonjwa sugu wa kifua kikuu (Multidrug resistant tuberculosis) huathiri watu 1,300 nchini Tanzania kulingana na taarifa ya mwaka 2007.

Je, ugonjwa wa kifua kikuu husababishwa na nini?

Ugonjwa wa kifua kikuu, husababishwa na bakteria wanaojulikana kama Mycobacteria tuberculosis. Kuna aina nyingi za jamii ya Mycobacterium kama Mycobacteria tuberculosis (husababisha kifua kikuu), Mycobacteria leprae (husababisha ugonjwa wa ukoma), Mycobacteria bovis (huathiri ngombe na binadamu), Mycobacteria afrikanum na kadhalika.

Ugonjwa wa kifua kikuu unaweza kuathiri mapafu, mishipa ya fahamu, mifupa, mfumo wa mzunguko wa damu, ngozi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system.

Mycobacteria bovis ambayo huathiri ngombe, inaweza kuambukiza binadamu kama atakula bidhaa zinazotokana na maziwa ya ngombe ambayo yameathirika na bakteria hawa kama vile siagi, mtindi, maziwa yenyewe, cheese, ice cream nk. Aina hii ya bakteria huathiri mapafu, tezi (lymph nodes), tumbo na sehemu nyingine za mwili.

Ni asilimia 10 tu ya watu walio na bakteria wa Mycobacteria tuberculosis ambao hawapati ugonjwa huu wa kifua kikuu.