Image

Ugonjwa wa ajabu wa kusinzia wagharimu maisha ya watoto Uganda; Tanzania ijiandae

Nodding disease

Mtoto Saul amekumbwa na ugonjwa wa ajabu wa kusinzia na kutikisa kichwa. Mama yake anasema Saul hupatwa na degedege linaloweza kumchukua muda wa hadi si chini ya saa tatu kupata nafuu na kila shambulio huwa kali kiasi cha kumfanya mama abaki asijue la kufanya. Mama Saul anasema, tangu mwanaye akumbwe na ugonjwa huu amekuwa si yule anayemfahamu, amekuwa kama mtoto aliyechanganyikiwa akizungukazunguka bila kujua alifanyalo. Mama Saul anasema, kuna wakati Saul aliwahi kupotea kijijini bila kujulikana yupo wapi kiasi kwamba hivi sasa inampasa kuwafungia ndani watoto wake wengine ili wasipotee kama ndugu yao.

Mtoto Saul ni miongoni tu mwa mamia kwa maelfu ya watoto waliokumbwa na ugonjwa wa ajabu wa kusinzia na kutikisa kichwa huko nchini Uganda pamoja na Sudan ya Kusini na sasa inasemekana umeshaingia nchini Tanzania. 

Mpaka sasa si madaktari wala wanasayansi wanaoelewa kwa undani chanzo halisi cha ugonjwa huu ingawa juhudi za kitafiti zinaendelea. 

Ugonjwa wa kusinzia na kutikisa kichwa umepewa jina la 'Nodding disease' kwa sababu watoto wanaokumbwa na ugonjwa huu huonesha dalili ya kutingisha kichwa kama mtu anayeitikia kitu pamoja na dalili nyingine zinazofanana na za mtu mwenye kifafa zikiambatana na kusinzia. 

Zipi hasa ni dalili za ugonjwa huu?
Watoto wenye ugonjwa wa kusinzia huathirika zaidi mfumo wao wa fahamu pamoja na ubongo [1] wa kupatwa na shambulizi kali la degedege, kushindwa kula chakula na kubadilika kabisa kitabia. 

Mtoto huanza kuonesha hali ya kutikisa kichwa kama anayeitikia jambo, hufumba macho, kisha huinamisha kichwa chake kama anayesinzia, lakini akiwa haoneshi dalili yoyote ya kuchoka na pia huonekana kupambana ili asipoteze ufahamu. Kisha huinua kichwa chake juu na kukaza macho yake kama mtu anayetazama kitu kabla ya macho yake kuwa mazito na kope kufunga na kupitiwa na usingizi mzito. Hali hii hufuatiwa na kuanguka kwa ghafla na wakati mwingine kujiumiza mwili. 

Shambulizi la degedege huchochewa na vitu tofauti kidogo na vile vinavyochochea degedege  linalowapata kwa mfano watoto wenye kifafa. Imeripotiwa na baadhi ya wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huu kuwa, baadhi ya watoto walikumbwa na degedege baada ya kutokea mabadiliko ya hali ya hewa au baada ya kuoneshwa chakula ambacho hawajawahi kula hapo kabla. 

Dalili nyingine ni pamoja na kitendo cha watoto kupoteza ufahamu wa wapi walipo, kuzurura zurura bila kujielewa na wakati mwingine kupotea vichakani. Katika hali ya kushangaza yameripotiwa pia matukio ya baadhi ya watoto waliokumbwa na ugonjwa huu kuchoma moto nyumba za vijiji bila kujitambua, kuchanganyikiwa na kuwa kama walioumizwa kiakili na kihisia.

Mahudhurio yao shuleni huwa hafifu, lishe huzidi kuwa duni hatimaye watoto hupatwa na utapiamlo, magonjwa nyemelezi na hatimaye kifo.

Je, Tanzania ni salama?
Miaka kadhaa nyuma kumewahi kuripotiwa milipuko kadhaa ya ugonjwa huu katika nchi za Tanzania, Liberia na Sudan lakini haikuwa mpaka mwaka 2009 ndipo mamlaka za Afya duniani zilipouchukulia kwa uzito unaostahili pale kulipotokea mlipuko wa kwanza mkubwa huko nchini Uganda. 

Miaka kadhaa nyuma kumewahi kuripotiwa matukio ya ugonjwa wenye dalili zenye kufanana na huu huko nchini Tanzania [4], ingawa ugonjwa huu wa sasa wenye kuhusisha kutikisa kichwa umeripotiwa zaidi maeneo ya Sudan ya kusini na Uganda Kaskazini hususani kwenye maeneo fulani fulani [2, 3, 5].

Hivi sasa, timu ya watafiti kutoka shirika la Afya Duniani (WHO), mamlaka za Afya za Uganda pamoja na wataalamu kutoka kituo cha magonjwa ya maambukizi (CDC) cha nchini Marekani ipo nchini Uganda ikifanya utafiti kufahamu chanzo cha ugonjwa huu na jinsi ya kuutibu. 

Nini hasa chanzo cha ugonjwa huu?
Chanzo halisi cha ugonjwa huu bado hakijafahamika ingawa kuna fununu fununu za hapa na pale. Watalaamu wamependekeza mambo mbalimbali kuwa yawezekana yakawa visababishi vya ugonjwa huu, yakiwemo maambukizi ya vimelea mbalimbali, ukosefu wa lishe, mazingira, na sababu za kisaikolojia. Wengine walikwenda mbali zaidi na kupendekeza uhusiano wa mabadiliko katika muundo wa vinasaba, maambukizi ya virusi wa surua, ulaji wa nyama ya nyani, matumizi ya vyakula vya msaada au hata mbegu za msaada kuwa yanaweza kuwa chanzo cha ugonjwa huu ingawa hakuna uthibitisho wa madai hayo mpaka sasa [2,3,5]. 

Wataalamu kutoka shirika la Afya Duniani wanasema karibu asilimia zaidi ya 90 ya watoto waliokumbwa na ugonjwa huu walikuwa wakiishi kwenye maeneo maarufu sana kwa ugonjwa wa upofu (river blindness) unaosababishwa na vimelea wanaojulikana kama Onchocerca Volvulus ambao husambazwa na aina fulani ya mbu [2,3,5]. 

Hata hivyo, November 2010, jopo la watafiti wa WHO lilifika eneo la kaskazini mwa Uganda kufanya uchunguzi wa chanzo na dalili za ugonjwa huu. Katika uchunguzi wao wa awali, walifanikiwa kuorodhesha watoto 38 waliokumbwa na ugonjwa huu na wale wasio na ugonjwa, na kuchunguza kama wana maambukizi ya vimelea vya Onchocerca volvulus ambapo vimelea hivi vilionekana zaidi kwa watoto waliokuwa na ugonjwa (76%) wakati ni 47% tu ya watoto wasiokuwa na ugonjwa wa kusinzia ndiyo waliokutwa navyo. Uchunguzi wao wa kistatistiki haukuonesha uhusiano wowote kati ya ugonjwa huo na vimeleo hivyo. Hali iliyoonesha kuwa pamoja na kwamba ugonjwa wa onchocerca ulikuwa umeenea sana eneo hilo, haikuweza kuthibitika moja kwa moja iwapo ugonjwa huo ulikuwa chanzo cha ugonjwa wa kusinzia [1]. 

Juu ya hilo, watoto wengi wenye ugonjwa huu walikutwa pia na upungufu mkubwa wa Vitamin B6,  aina ya vitamini ambayo ni muhimu sana katika kuimarisha mfumo wa fahamu. 

Aidha uchunguzi zaidi unaonesha kuwa lishe duni pia inawezekana ikawa chanzo kimojawapo au kihatarishi cha mtoto kupatwa na ugonjwa huu. 

Ukubwa wa tatizo
Kutokana na taarifa zisizothibitishwa zilizopatikana kutoka kwa wafanyakazi wa afya walio maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huu, waathirika ni watoto walio kati ya umri wa mwaka 1 mpaka 19, ingawa kundi la watoto wenye umri wa kati ya miaka 3 mpaka 11 huathirika zaidi, na tayari umesharipotiwa katika nchi za Liberia, sudan ya Kusini, Guinea ya Ikweta, [2] na sehemu za kaskazini za Uganda na kusini mwa Tanzania [3,4]. Mlipuko huu wa sasa nchini Uganda umejikita zaidi maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo, ingawa haijathibitika bado kama ugonjwa huu unaambukizwa japokuwa wataalamu wa afya wanalichukulia hilo kwa uzito mkubwa wakitilia maanani hofu yao ya kusambaa kwa ugonjwa huo sehemu nyingine za dunia.

Ripoti kutoka baadhi ya vijiji vya maeneo ya kaskazini mwa Uganda zinasema kuwa karibu kila kaya imeripotiwa kuathiriwa na ugonjwa huu. Mpaka sasa haijulikani idadi kamili ya vifo vilivyosababishwa na ugonjwa huu ingawa kuna idadi kubwa tu ya watoto walioathiriwa vibaya kiasi cha kushindwa kujihudumia wenyewe na kuwaongezea mzigo wa huduma wazazi na walezi wao. 

Ugonjwa huu unatibiwaje?
Mpaka sasa hakuna tiba ya uhakika ya ugonjwa huu. Hii ni kwa vile wataalamu bado hawafahamu chanzo halisi cha ugonjwa na jinsi unavyoambukizwa. Maisha ya watoto katika maeneo yaliyoathirika yamekuwa ya mashaka sana na kuna ripoti za baadhi ya wazazi kutupa watoto wao kwa vile hawajui ni kwa jinsi gani wanaweza kuwasaidia. Hofu yao nyingine ni kuogopa kuambukizwa kwa vile hawajui ni kwa vipi ugonjwa huu husambaa.

Ni hapa majuzi tu, mamlaka za afya za nchini Uganda ziliona umuhimu wa kufungua kituo cha kwanza cha afya kwa ajili ya kuwahudumia watoto waliokumbwa na ugonjwa huu baada ya kipindi kirefu cha kusuasua kuchukua hatua, ingawa hakuna tiba inayojulikana wala chanjo iliyogundulika mpaka sasa. 

Hata hivyo katika hali ya majaribio, baadhi ya madaktari wameanza kutumia dawa za kutibu na kuthibiti kifafa kwa ajili ya kuthibiti na kutuliza degedege linaloambatana na ugonjwa huu ingawa mafanikio ya njia bado si ya kuridhisha sana, kwa vile wanasema njia hii husaidia tu kupunguza kasi ya kutokea kwa dalili na si kuzikomesha kabisa. 

Tanzania ijiandae
Ripoti zisithothibiitishwa kwamba tayari ugonjwa huu umeshaingia Tanzania au kuna uwezekano mkubwa ukavuka mipaka na kuingia nchini si jambo la kulichukulia kijuujuu hata kidogo. Ni wakati muafaka sasa mamlaka zinazohusika kujiweka tayari na kujiandaa kulikabili tatizo hili kabla au pindi mlipuko utakapotokea. 

Marejeo
1. Lul Reik, MD, Abdinasir Abubakar, MD, Martin Opoka, MD, Godwin Mindra, MD, James Sejvar, MD, Scott F. Dowell, MD, Carlos Navarro-Colorado, MD, Curtis Blanton, MS, Jeffrey Ratto, MPH, Sudhir Bunga, MD, Jennifer Foltz, MD, EIS officers, CDC. Nodding Syndrome — South Sudan, 2011 Weekly January 27, 2012 / 61(03);52-54. Inapatikana mtandaoni kupitia http://www.cdc.gov/mmwr/preview/mmwrhtml/mm6103a3.htm
2. Nyungura JL, Akim T, Lako A, Gordon A, Lejeng L, William G. Investigation into nodding syndrome in Witto Payam, Western Equatoria State, 2010. Southern Sudan Medical Journal 2010;4:3–6.
3. Winkler AS, Friedrich K, Konig R, et al. The head nodding syndrome—clinical classification and possible causes. Epilepsia 2008;49:2008–15.
4. Winkler AS, Friedrich K, Meindl M, et al. Clinical characteristics of people with head nodding in southern Tanzania. Trop Doct 2010;40:173-5. 
5. Lacey M. Nodding disease: mystery of southern Sudan. Lancet Neurol 2003;2:714.

 


Imesomwa mara 20995 Imehaririwa Jumatano, 21 Machi 2012 07:43
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.