Image

MSIMAMO WA SIKIKA KUHUSU MGOMO WA MADAKTARI

  4 July 2012
MSIMAMO WA SIKIKA KUHUSU MGOMO WA MADAKTARI
UTANGULIZI
SIKIKA ni shirika lisilo la kiserikali linalotekeleza shughuli mbali mbali zenye lengo la kuchochea upatikanaji wa huduma za afya zenye uwiano, viwango na ubora unaokubalika, gharama nafuu na zilizo endelevu. SIKIKA imekuwa mstari wa mbele kufanya tafiti katika sekta ya afya na kuhimiza utekelezaji wa sera, uwajibikaji na upatikanaji wa huduma bora nchini Tanzania.
Kama neno ‘afya’ lilivyo tafsiriwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Mwaka 1948, sera ya afya ya Taifa (Tanzania Health Policy) ya mwaka 2007, nayo pia inatambua ‘afya’ kama hali ya ukamilifu wa binadamu kiakili, kimwili, kijamii na siyo tu kutokuwepo kwa maradhi. Afya bora ni mhimili wa maendeleo ya mtu binafsi, familia na taifa zima kwa ujumla hasa katika harakati za kuondoa umasikini uliokithiri katika taifa letu.
Katika nchi yetu, mfumo wa utoaji huduma katika sekta ya afya umegawanyika katika ngazi tatu yaani ngazi ya afya ya msingi kama vile zahanati na vituo vya afya, ngazi ya pili kama vile hospitali za wilaya au mikoa na ngazi ya hospitali za rufaa kama vile hospitali ya Muhimbili, Mbeya, Bugando, KCMC na hospitali maalumu kama taasisi ya magonjwa ya kansa ya Ocean Road au hospitali ya magonjwa ya akili ya Milembe. Hospitali hizi za rufaa hushughulika na magonjwa ambayo ama yameshindikana katika hospitali za ngazi za chini au wataalamu waliopo katika ngazi hizo na vifaa vilivyopo haviwezi kutoa huduma stahili kwa magonjwa hayo. Hivyo basi, iwapo kutakuwa na matatizo yanayoathiri utendaji wao wa kazi wa kila siku na kwa kuwa wagonjwa walioletwa katika hospitali hizi za rufaa hawawezi kurudishwa kule walikotoka (ngazi za chini), wagonjwa hawa wasio na hatia ndiyo waumiao kutokana na matatizo hayo.
Migomo ya watumishi katika sekta ya afya ni mojawapo ya matatizo yanayoweza kuathiri utendaji kazi wa wataalamu wa afya, siyo tu katika hospitali za rufaa hata pia katika hospitali za ngazi za chini. Kwa historia ya migomo hii, Mwananchi anayehitaji huduma za afya hana mchango wa moja kwa moja katika kusababisha migomo ya watumishi wa afya. Mwananchi ameiweka serikali madarakani na analipa kodi ili serikali hiyo itoe huduma bora za kiafya kwake ili awe na nguvu za kujiletea maendeleo yake na taifa kwa ujumla.
MGOMO WA MADAKTARI
Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na migomo ya mara kwa mara kuanzia kwa wanafunzi wa vyuo vikuu mpaka kwa wafanyankazi wa serikali. Mwaka 2001, tulishuhudia mgomo mkubwa wa wanafunzi wa chuo cha Sayansi za tiba Muhimbili wakishinikiza uboreshwaji wa mazingira ya kusomea hasa masomo kwa vitendo. Mwaka 2005, tukashuhudia mgomo mkubwa wa madaktari wa hospitali ya Muhimbili na sehemu nyinginezo waliokuwa wakidai uboreshwaji wa maslahi yao, mgomo ambao uliathiri utoaji huduma katika hospitali nyingi hasa za rufaa. Kuelekea Mwaka jana, vuguvugu la mgomo wa madaktari lilipelekea kuwepo kwa mgomo mwanzoni wa mwaka huu ambao umekuwa ukiendelea kwa vipindi tofauti hadi sasa.
Japo serikali imekuwa ikitafuta njia za mkato kuendeleza huduma katika hospitali ya Muhimbili kama vile kuleta madaktari waliostaafu ama madaktari kutoka jeshini ambao hawakidhi mahitaji ya huduma katika hospitali hiyo ya Taifa, huduma katika hospitali nyingine zisizonufaika na njia hizi za mkato hudorora siku hadi siku kwa kipindi chote cha migomo huku wananchi wakiendelea kupata taabu.
Vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kama vile kutekwa na kupigwa kwa Mwenyekiti wa kamati maalumu ya Jumuiya ya madaktari iyosimamia madai yao, Dr. Stephen Ulimboka, ubabe, vitisho na matumizi ya nguvu dhidi ya madaktari wanaodai haki zao badala ya kutatua matatizo hayo kwa njia ya amani, siyo tu vinakiuka Katiba ya nchi inayojichanganua kimataifa kama nchi ya amani bali pia vimepunguza morali ya watumishi hawa kutoa huduma kwa wananchi ambao kama tulivyosema awali hawana mchango wa moja kwa moja katika kusababisha mgogoro huu.
Madai ya Madaktari.
Katika mgomo huu unaoendelea, madai ya madaktari, mbali na dai la awali la kusisitiza kuondolewa kwa viongozi wakuu katika wizara ya afya wanaokwamisha maendeleo ya sekta hii, madai yao yamejikita katika sehemu kuu mbili ambazo ni uboreshwaji wa mazingira ya kazi na vifaa vya tiba na Uboreshwaji wa kipato, kinga na afya za madaktari (Mishahara, posho na Bima ya afya).
Uboreshwaji wa mazingira ya kufanyia kazi na vifaa vya tiba
Kulingana na maelezo ya madaktari, hii ndiyo hoja kubwa katika madai yao ambayo inalenga kuhimiza serikali kukarabati miundombinu ya afya, kuongeza vitanda na kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kutendea kazi. Katika tamko la jumuiya ya madaktari Tanzania lililotolewa kwa waandishi wa habari tarehe 28 Juni 2012, sehemu ya tamko hilo inasema:
“…Madaktari wamechoka kuona huduma za afya nchini zikizidi kudorora mwaka hadi mwaka…
… Tumechoka kuona wagonjwa wakilala chini na watoto wakilala wanne katika kitanda kimoja…
…Tumechoka kuona msongamano mkubwa wa wagonjwa katika hospitali zetu huku kukiwa hakuna
mpango wowote wa uboreshaji…
…Tumechoka kuona wagonjwa wakikosa dawa, vipimo sahihi na watumishi wa afya wakifanya kazi katika mazingira magumu yanayoviza ubora wa huduma na misingi ya taaluma…
… Kwahiyo, kwa moyo wetu leo, tumejitolea kutetea uboreshaji wa sekta ya afya ….’’
Sera ya Taifa ya afya ya mwaka 2007 katika kipengele kinachohusu rasilimali watu inasema;
‘… Uboreshaji wa mazingira ya kazi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi vya kutosha kwa
watumishi wa afya…
… Kuweka vivutio katika sehemu zenye mazingira magumu na hatarishi ili kuwavutia wataalamu kwenda kufanya kazi katika sehemu hizo…’
Katika madai ya awali ya madaktari, walisikitishwa na wimbi kubwa la viongozi wa kisiasa na serikali wanaotibiwa nje ya nchi. Zaidi ya hayo, madaktari walibaki kuwa waidhinishaji wa rufaa za kwenda kutibiwa nje ya nchi. Hali hii, siyo tu inaweza kuongeza mwingilio wa maamuzi ya kitaalamu kwa shinikizo za watawala wa kisiasa kwa kuwashinikiza madaktari kutoa rufaa kinyume na maadili yao, bali pia inapunguza nia ya kisiasa ama ‘political will’ ya viongozi wa kisiasa na serikali katika kushughulikia kero za afya za wananchi kwa kuwa ‘wao’ wana uhakika wa matibabu nje ya nchi. Hali hii siyo tu inaondoa usawa wa kimatibabu kati ya viongozi na wananchi, na serikali kutumia fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kuboresha sekta ya afya hapa nchini bali pia nchi hushindwa kuwa na miundo mbinu ya uhakika ya kushughulikia magonjwa ya dharura ambayo muda hautaruhusu kutibiwa nje ya nchi. Nchini Malawi kwa mfano, kifo cha Rais Bingu wa Mutharika, kutokana na shinikizo la damu tarehe 5 Aprili mwaka huu kilihusishwa na serikali yake kushindwa kuboresha miundombinu na huduma za afya nchini mwake.
Katika utafiti wa Sikika kuhusu upatikanaji wa madawa na vifaa tiba uliofanyika katika wilaya 71 mwaka 2011, waganga wakuu wa wilaya waliohojiwa, walithibitisha kutokuwepo kwa gozi (gauze) katika asilimia 48 ya wilaya zote huku asilimia 44% ya wilaya zikiwa na gozi zisizotosheleza mahitaji. Katika ngazi ya vituo vya afya na zahanati, asilimia 63% hazikuwa na gozi huku asilimia 27% ikiwa haina gozi za kutosha. Kukosekana au kuwa na idadi pungufu ikilinganishwa na mahitaji uliendelea kuwepo kwa kati ya miezi mitatu hadi sita. Vivyo hivyo, katika ngazi za wilaya, glovu (surgical gloves) hazikuwepo katika asilimia 28% ya wilaya, dawa za kutibu malaria aina ya ALU asilimia 32% ya wilaya na sindano za Quinine asilimia 13% ya wilaya zote zilizoshiriki katika utafiti. Katika ngazi ya vituo vya afya na zahanati, asilimia 17% hazikuwa na glovu, asilimia 30% hazikuwa na ALU, asilimia 23% hazikuwa na sindano za Quinine na asilimia 17% haikuwa na vidonge vya Amoxcycillin. Katika utafiti huo pia, Sikika iligundua kuwa katika ngazi ya wilaya asilimia 93% ya wilaya hupata dawa na vifaa tiba chini ya maombi na mahitaji halisi na katika ngazi ya vituo vya afya na zahanati asilimia 90% hupata dawa na vifaa vya tiba chini ya maombi na mahitaji halisi.
Yapo madhara makubwa yatokanayo na upungufu wa dawa na vifaa vya tiba. Madhara hayo yaweza kupelekea kuona wagonjwa waliozidiwa au walio na dharura pekee (critical patients & emergencies) hali ambayo inajitokeza katika zahanati na vituo vya afya vingi. Madhara mengine ni kuongezeka kwa usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa kutokana na kupata kiasi kidogo, kuongezeka kwa madhara ya magonjwa yatokanayo na kutopata tiba sahihi (complications) kama ulemavu kwa watoto ambao wamekosa tiba sahihi ya malaria, kuongezeka kwa malalamiko toka kwa wananchi dhidi ya watumishi wa afya na mbaya zaidi kupungua kwa morali ya kazi kwa watumishi wa afya na kufanya kazi kinyume na misingi au maadili ya kitaalamu kama walivyosema madaktari hapo juu, ‘mazingira magumu yanayoviza ubora wa huduma na misingi ya taaluma’.
Wengi wetu ni mashahidi wa huduma zisizoridhisha katika hospitali za serikali, msongamano wa wagonjwa wodini hasa akinamama na watoto, ukosefu wa mara kwa mara wa vifaa vya tiba na matatizo mengine.
Tanzania hupoteza takribani asilimia 6% ya wagonjwa wanaohitaji huduma za CT Scan kwa mwaka. Hata hivyo, kifaa cha CT Scan katika hospitali ya Muhimbili kimeharibika kwa zaidi ya miezi saba sasa bila matengenezo ikiwalazimu wagonjwa wanaohitaji majibu ya kipimo hicho ili wapate tiba stahili, kwenda katika hospitali binafsi. Gharama za kipimo hicho katika hospitali ya Muhimbili ni takribani shilingi 170,000/= lakini katika hospitali binafsi ni kati ya shilingi 200,000/= hadi 500,000/=. Mbali ya hayo, katika ufuatiliaji wa Sikika wa mwaka 2011 kwenye wilaya 6 za mkoa wa Dar Es salaam, Pwani na Dodoma, kati ya vituo 38 vinavyotoa huduma kwa watu waishio na VVU (Care and treatment Centers) ni vituo 13 tu vilivyokuwa na mashine za CD4+ zinazotumika kuangalia maendeleo ya tiba kwa watu waishio na VVU na kati ya hizo ni mashine tano (5) ndizo zilikuwa zikifanya kazi. Ni wajibu wa serikali kuboresha mazingira ya kazi ya watumishi wa afya na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba kwa muda wote, kwa sababu hii Sikika tunaungana na madaktari katika kudai uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa watumishi wa afya, kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatika hasa maeneo ya vijijini ili kuboresha afya za wananchi kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Uboreshaji wa kipato, kinga na afya za madaktari (Mshahara, posho, Bima ya afya).
Madai mengine ya madaktari ni uboreshwaji wa mapato yao ikiwa ni pamoja na mishahara, posho ya kuitwa kazini baada ya saa za kazi (on call allowance), posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu (hardship allowance) na posho ya makazi. Vile vile madaktari wanadai posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (risk allowance) na chanjo ambayo ni muhimu ili kuzuia uwezekano wa madaktari kupata magonjwa ambayo wanaweza kuyasambaza kwa wagonjwa wengine ambao tayari wana matatizo yao ya kiafya.
Madai ya nyongeza ya mishahara
Katika madai yao ya mishahara, madaktari walipendekeza kiwango cha shilingi milioni 3.5 kwa mwezi. Hata hivyo, wakati akiongea na madaktari Tarehe 9/2/2012, waziri mkuu Mh. Mizengo Pinda alitoa ufafanuzi wa madai yanayohusu maslahi ya watumishi wa afya bila kutoa majibu ya moja kwa moja ya kiwango gani kitalipwa na serikali kama mishahara na posho kwa sababu ‘wataalamu’ walikuwa wanafanyia kazi suala hilo ili waweze kumshauri, na hadi sasa serikali haijatamka kiwango halisi itakachoweza kulipa. Pia waziri mkuu hakuweza kueleza moja kwa moja kuhusu madai ya uboreshaji wa mazingira ya kazi na upatikanaji wa vifaa tiba. Kwa sasa, mshahara wa daktari ni Tshs 957,700/= na baada ya makato ya kodi hubaki na Tshs 680,000/= kwa mwezi. Katika ufuatiliaji wa Sikika wa Disemba 2011 hadi January 2012, katika hospitali ya Regency, ilibainika kuwa hakuna daktari anayepata mshahara chini ya shilingi milioni mbili (gross pay) na Agha Khan hospitali, daktari mwenye uzoefu wa chini ya miaka minne alikuwa akilipwa shilingi milioni 1.8 kuachilia mbali mafao mengine kama vile bima ya afya, posho za nyumba n.k. Sikika inatarajia kuwa serikali pia itaboresha mishahara ya madaktari na mafao mengine ili kuongeza tija katika hospitali za umma.
Madai ya Posho
Katika madai yao, madaktari wamependekeza viwango vifuatavyo kwa posho mbali mbali: posho ya muda wa ziada wa kazi (call allowance) asilimia 5% ya mshahara kama ilivyo kisheria kwa kada yoyote; posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu asilimia 40% ya mshahara; posho ya makazi asilimia 40% au nyumba kama ilivyo kisheria na posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi asilimia 30% au chanjo (Homa ya ini-hepatitis, HIV/AIDS, TB)
Hoja za Serikali
Serikali imeendelea kusisitiza ufinyu wa bajeti na kwamba, kuwaongezea mishahara madaktari peke yaokutaondoa ulinganifu na kuongeza migogoro katika sekta nyingine. Hata hivyo, sehemu ya sheria yakazi ya mwaka 2004 (Employment and Labour Relations Act, Kifungu cha 6: (20) (4)), inasomeka hivi“Mwajiri atamlipa mwajiriwa walau 5% ya mshahara wa msingi wa mwajiriwa kwa kila saa aliyofanya kazi usiku’’.Kwa mahesabu rahisi, daktari alipaswa kupata angalau Tshs 47,000/= kwa saa anapofanya kazi usiku.Hata hivyo waraka wa serikali wenye Kumb. No. C/AC.17/45/01/F/73 wa tarehe 21 February 2012kutoka kwa George D. Yambesi (Katibu Mkuu Utumishi) kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara yaAfya na Ustawi wa Jamii wenye kichwa, ‘Malipo ya kuitwa kufanya kazi baada ya saa za kazi (On callallowance)’ unaelekeza kulipa viwango vifuatavyo kwa siku kwa watumishi wa afya kuanzia tarehe 9February 2012 (Siku 12 Nyuma); Wataalamu bingwa Tshs 25,000/= na madaktari wa kati Tshs20,000/=. Katika nchi ya jirani ya Kenya kwa barua yenye Kumb No. MSPS/2/1/3A Vol.III/(77), yatarehe 12 January 2012 toka ofisi ya Waziri Mkuu kwenda kwa Katibu Mkuu wa wizara husika,madaktari, wataalamu wa kinywa na wafamasia wanalipwa takribani Tshs 38,000/= kama posho ya ‘call allowance’ hali ambayo inaweza kusababisha kupungua kwa rasilimali watu katika sekta ya afya nchini Tanzania (Brain Drain) kwa kukimbilia nchi jirani kufuata kipato kizuri hasa wakati huu wa soko huria la ajira katika shirikisho la Afrika Mashariki.
Sikika imekuwa mstari wa mbele kupinga pesa zinazotumika kama posho za vikao kwa watumishi ambao tayari wanalipwa mishahara kwa kazi husika. Hata hivyo, katika waraka wenye Kumb. No. C/AC.17/45/01/125 wa tarehe 11 Februari 2010 wenye kichwa ‘Waraka wa Utumishi wa Serikali Na.2 wa mwaka 2010: Posho ya vikao (Sitting Allowance) Serikalini,’ viwango ‘vipya’ vya posho ya vikao vilivyotajwa ni Mwenyekiti/Katibu 200,000/=, Wajumbe 150,000/= na sekretarieti 100,000/=. Posho hizi kubwa si tu kwamba zinadhihirisha matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi bali pia zinapunguza nguvu kazi katika sekta ya afya kwani watumishi wengi wanahangaika kutafuta nafasi ya kushiriki katika vikao badala ya kufanya kazi zao.
Hoja ya ‘ulinganifu’ au ‘lawama’ kwa sekta nyingine haina nguvu kwani nchini Marekani kwa mfano, pato la daktari ni zaidi ya mara 100 ya kima cha chini cha mshahara kwa saa katika nchi hiyo, na nchini Botswana, ambako Madaktari wengi Watanzania hukimbilia kwa sababu za kimaslahi, mshahara wa daktari ni sawa na Tshs kati ya milioni 3.2 hadi 5.8 kwa mwezi. Hoja hii pia, kwamba madaktari wakipewa mshahara mkubwa italeta malalamiko katika kada nyingine inadhihirisha jinsi ambavyo serikali inawakandamiza kimaslahi watumishi wake. Hili lilidhihirika wakati wa mgomo wa walimu mwaka 2010, Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) bwana Nicholas Mgaya, alisema … ‘Tumedai kwamba Kima cha chini cha mishahara kiwe ni Tshs 315,000/=. …………lakini serikali ikang’ang’ania Tshs 135,000/= kiasi ambacho bado ni kidogo’’ (Daily News, August, 2010). Vivyo hivyo, utafiti wa “Motivation of Health Care Workers in Tanzania: A Case Study of Muhimbili National Hospital” uliotolewa katika Jarida la East African Journal of Public Health Volume 5 Number 1, April 2008 ulionesha kuwa Asilimia 88 ya watumishi waliamini kuwa mwajiri wao hawajali (madaktari asilimia 82.4, wauguzi asilimia 90.7 na watumishi wengine asilimia 87.9). Hata hivyo sababu tatu kubwa zilizoonekana kuwafanya watumishi hao kutokuwa na motisha mzuri wa kazi ni mishahara, mazingira ya kazi, na vifaa duni vya kazi na asilimia 30 ya wauguzi walikuwa hawajaridhika na kazi zao kiasi cha kutaka kuacha kazi hizo. Hali ya kuwa serikali imekuwa haikubali mapendekezo ya watumishi wake au hata mapendekezo ya tume zinazoundwa na serikali yenyewe hasa katika uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi wa sekta ya afya kwa ujumla, inatufanya Sikika tuungane na madaktari katika madai yao.
Katika bajeti ya sasa 2012/213, kipengele cha uendelezaji wa rasilimali watu katika sekta ya afya kimetengewa bilioni 23.4 na matumizi ya kawaida (recurrent expenditure) yametengewa Tshs bilioni 24.5). Hata hivyo kati ya fedha iliyotengwa kuendeleza rasilimali watu, bilioni 21.6 sawa na asilimia 92.3% inategemea msaada wa wafadhili. Hali hii ya utegemeji inapingana na sera ya afya ya Taifa inayotamka kuwa serikali iwe mfadhili mkuu wa sekta ya afya.
Wakati huo huo, mpango mkakati wa sekta ya afya (Health Sector Strategic Plan III) umeweka malengo ya bajeti ya sekta ya afya kufikia asilimia 10% ya bajeti yote ya serikali mwaka 2015. Hii inapingana na azimio la Abuja (asilimia 15) ambalo Rais wetu alitia saini na inapingana pia na sera ya afya ya mwaka 2007 inaposema, ‘Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya sekta ya afya …hadi kufikia azimio la Abuja….ilikukidhi mahitaji muhimu ya kisekta’ . Kwa ukiukwaji wa makubaliano ya azimio la Abuja na kutoitekeleza sera ya afya ya Taifa kama inavyotakiwa, yote haya yanadhihirisha kuwa serikali haina nia ya dhati ya kusimamia maamuzi yake katika ngazi za kimataifa na kitaifa. Tukirejea tena katika sera ya afya ya mwaka 2007 inasema, ‘kuwepo kwa watumishi wa kutosha wenye ujuzi katika ngazi zote za kutolea huduma kulingana na vigezo vilivyokubalika’. Udaktari ni mojawapo ya fani ambazo katika nchi nyingi zimepewa jina la ‘scarce skills’ yaani ujuzi adimu. Kwa miaka kadhaa sasa, idadi kubwa ya wanafunzi wa shule katika ngazi za chini wameendelea kuyakimbia masomo ya sayansi na wanafunzi wanaodahiliwa kusomea masomo ya udaktari ni wale ambao kiwango chao cha ufaulu katika masomo ya fizikia, kemia na biologia kiko juu sana, hivyo madaktari kulipwa mishahara mikubwa ili waweze kuokoa maisha ya watanzania si tatizo, kwa maoni ya Sikika.
Tena, hoja ya ufinyu wa bajeti inakosa nguvu katika madai haya kwani, katika tafiti za Sikika tumeonyesha jinsi ambayo serikali imeendelea kuwa na matumizi mabovu ya fedha za walipa kodi na ukosefu wa vipaumbele katika matumizi yake.
Katika chapisho la Sikika lenye kichwa, ‘Matumizi yasiyo ya lazima, Taarifa fupi kuhusu mpango wa serikali katika kuangalia Upya matumizi’ toleo no. 2 la July 2010 lililotolewa kwa ushirikiano wa Policy forum linaonyesha kuwa matumizi yasiyo ya lazima serikalini yalikuwa bilioni 684 mwaka 2008/09, billioni 530 mwaka 2009/10 na bilioni 537 mwaka 2010/11. Zaidi ya hayo,, matumizi katika posho mbali mbali yaliongezeka toka bilioni 171 mwaka 2008/09 hadi bilioni 269 mwaka 2010/11. Gharama za kusafiri nje na ndani ya nchi zilikuwa bilioni 155 mwaka 2008/09 na bilioni 124 mwaka 2010/11. Gharama za mafuta ya kuendeshea na kulainisha magari ya kifahari ya serikali (Mbali na ununuzi) zilikuwa zaidi ya bilioni 52 mwaka 2010/11 na manunuzi ya magari ya serikali yaligharimu Bilioni 15.3 mwaka 2010/11 pekee. Mbali ya hayo, serikali imekosa vipaumbele katika matumizi yake mfano ni matumizi ya zaidi ya bilioni moja kwenye wizara ya afya wakati wa sherehe za Nane Nane..
Katika sekta ya afya pekee, matumizi yasiyo ya lazima (unnecessary expenditure) yaliongezeka toka bilioni 16.1 mwaka 2010/11 hadi bilioni 22 mwaka 2011/12, na inakadiriwa kufikia bilioni 25 katika bajeti ya 2012/13, posho mbalimbali zikiongoza katika matumizi. Posho hizo zinalenga watu wachache sana hasa watawala na hazina tija katika utoaji wa huduma za afya. Posho zimefanya utendaji kazi uwe hafifu na kupunguza uwajibikaji ilhali watumishi wasio katika nafasi za kitawala wakiendelea kuambulia maslahi madogo
Taarifa za CAG pia zinadhihirisha matumizi mabovu na usimizi mbovu wa rasilimali za taifa kwa mfano msamaha wa kodi uliongezeka toka bilioni 680 mwaka 2009/2010 hadi Trilioni 1.016 kwa mwaka wa 2010/11. Hii inawakilisha asilimia 18% makusanyo yote ya pato la Taifa na ni kiwango kikubwa sana kuliko nchi nyingi za Afrika. Matumizi yasiyokusudiwa bilioni 8, bilioni 31 zimelipia vifaa ambavyo havikufika na Malipo yanayotia shaka bilioni 1.4.
Rasimali watu katika Sekta ya Afya
Tumeshuhudia matamko ya hospitali kadhaa hospitali za mikoa ya Mbeya, Dodoma, Morogoro, Kilimanjaro na Mwanza zikiwafukuza madaktari waliogoma badala ya kushiriki katika kutatua mgogoro huu ili warejee kazini na kuepuka kupoteza nguvu kazi yenye upungufu mkubwa katika sekta ya afya. Shirika la afya duniani (World Health Organization), linapendekeza kwamba kila daktari anatakiwa ahudumie watu wasiozidi 5,000. Kwa mujibu mkutano mkuu wa chama cha madaktari Tanzania (MAT) tarehe 10 hadi 11 August, 2010 pale Mlimani city, uwiano wa daktari mmoja kwa idadi ya watu ulikuwa 1:300 wakati wa uhuru na hali ikawa mbaya kwa kasi hadi uwiano wa 1: 30,000 mwaka 2010. Kwa upande wa wafamasia kwa mfano, wakati kukiwa na vituo vya kutolea dawa 4,185 vya serikali na 1,056 vya binafsi nchini mwaka 2009, kulikuwa na wataalamu 1,506 pekee waliopata mafunzo ya ufamasia na wafamasia 703 wenye shahada ya ufamasia. Katika utafiti wa Sikika wa HRH Tracking Study 2010, ulionyesha kuwa asilimia 54% ya wilaya zote zilizoshiriki katika utafiti zilikuwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa afya. Hata hivyo, idadi ya watumishi wanaopangiwa vituo vya kazi na kuripoti ni asilimia 70% kwa wilaya za vijijini na asilimia 93% kwa wilaya za mijini. Zaidi ya hayo, wilaya nyingi hazipati wafanyakazi kulingana na maombi yao, kwa mfano katika utafiti huu, wilaya nyingi zilipata ni asilimia 35% ya wafanyakazi katika maombi yao, huku hali ikiwa mbaya maeneo ya vijijini.
Katika mpango wa kukuza rasilimali watu unaoisha mwaka 2013, bajeti ya jumla ya mpango huo ilikiwa bilioni 470, wastani wa bilioni 91 kwa mwaka. Mwaka 2011/12, wizara ya afya na ustawi wa jamii iliomba bilioni 66.3 ili kutekeleza mkakati wa rasilimali watu kisekta, hata hivyo serikali ilitenga bilioni 13.2 pekee na hadi kufikia January 2012, asilimia 20% (bilioni 2.7) pekee ndiyo iliyokuwa imetolewa kwa wizara.
Wakati mkakati wa kuboresha sekta ya afya (HSSP III) ukionyesha upungufu wa rasilimali watu kufikia 92,000, mpango wa ukuzaji wa afya ya msingi (Primary Health Service Development Program 2007- 2017) unahitaji watumishi wa afya 137,813 kuutekeleza. Hata hivyo, udahili katika vyuo vya afya kwa mwaka 2010 ulikuwa wanafunzi 6,949 pekee, na iwapo udahili hautaongezeka, tutahitaji miaka 21 ili kuziba pengo la watumishi katika mpango wa kukuza afya ya msingi (PHSDP) iwapo mambo yatabaki kama yaliyo. Hii inaonyesha kuwa tutaendelea kuwa na upungufu wa watumishi wa afya kwa miaka mingi ijayo. Hata hivyo, katika mwendelezo wa hotuba zake za kila mwisho wa mwezi, Tarehe 01/07/2012, mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, siyo tu amedhihirisha kutokutilia maanani upungufu mkubwa wa wataalamu wa afya unaoisumbua nchi yetu, bali pia kama kiongozi wa nchi, ameonyesha jinsi ambavyo serikali ilivyo tayari kupoteza rasilimali hii adimu kwa kushindwa kutatua mgogoro kati yake na madaktari, ambao iwapo wataamua kuacha kazi wote, itatuchukua miaka mingi kuziba pengo hilo.
 
Hitimisho
Kwanza, kutokana na mapungufu mengi tuliyoeleza hapo juu, Sikika inaona kuwa madai ya madaktari ni ya msingi na tunaamini kuwa serikali inaweza kuboresha huduma za afya na maslahi ya wafanyakazi hasa ikidhibiti matumizi yasiyo ya lazima, ikidhibiti ufujaji wa kodi za wananchi kwa baadhi ya watendaji wake, ikipunguza misamaha ya kodi na ikitekeleza mikakati iliyopo katika sera zake kikamilifu.
Pili, Sikika inaungana na madaktari, wanaharakati na wananchi kulaani vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu aliofanyiwa mwenyekiti wa kamati maalumu ya jumuiya ya madaktari Dr. Stephen Ulimboka na kupendekeza uundwaji wa tume huru yenye mchanganyiko wa wananchi katika kuchunguza tukio hilo.
Tatu, Sikika inaihimiza serikali kuacha kutumia vitisho na ubabe katika kutatua mgogoro wake na madaktari. Vitendo hivi vinaweza kupunguza morali na ufanisi wa madaktari kiutendaji na pengine kupelekea wengine kuhama sekta ya afya au kukimbilia nje ya nchi. Badala yake serikali ifanye mapatano na wataalamu hawa muhimu, ili waweze kurejea kazini haraka kutoa huduma kwa wananchi wanaoendelea kuumia kwa kukosa huduma.
 
 
 
P.o.Box 12183 Dar Es Salaam,
 
Phone: +255222666355/57 Fax: +255222668015
E-Mail: info@sikika.or.tz web: www.sikika.or.tz
 
 

 

 

 

Imesomwa mara 14793 Imehaririwa Jumamosi, 07 Julai 2012 14:38
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.