Image

Upandikizaji wa Uboho kwenye Mifupa (Bone Marrow Transplant) Tiba ya HIV?

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wanaume wawili ambao walikuwa na maambukizi ya ugonjwa wa HIV huko nchini Marekani wameweza kuacha kabisa  kutumia dawa za kurefusha maisha yaani ARV’S   ambazo hupewa wagonjwa wa HIV baada ya kufanyiwa upandikizaji wa uboho (bone marrow transplant) katika mifupa yao.

Wanaume hao ambao walikuwa na ugonjwa wa HIV kwa miaka 30, walikuwa wakipewa tiba ya upandikizaji wa uboho kutokana kuugua saratani ya damu (Leukemia). Mmoja wa wanaume hao ameacha kutumia dawa hizo za kurefusha maisha miezi minne iliyopita na mwingine ameacha kuzitumia wiki saba zilizopita.

 

Watafiti  wa Marekani wamesema baada ya wagonjwa hao kufanyiwa upandikizaji wa uboho, wagonjwa hao bado waliendelea kupewa dawa hizo za kurefusha maisha ili kulinda chembechembe mpya za damu kutoathiriwa na virusi vya HIV na baada ya muda zile chembechembe zao za zamani ambazo zilikuwa tayari zimeathiriwa na virusi vya HIV ziliuliwa na chembechembe mpya za damu zilizotoka kwenye uboho uliopandikizwa.

Wanasayansi wanasema bado ni mapema sana kusema ya kwamba wagonjwa hao wamepona kabisa ila mpaka sasa hakuna dalili zozote za virusi vya HIV kurudi tena kwa wagonjwa hao.

Katika kongamano la International Aids Society lililofanyika hivi karibuni huko nchini Malaysia, wanasayansi walielezwa ya kwamba hata baada ya wagonjwa hao kuacha kutumia dawa hizo za ARV’S, virusi vya HIV havikuweza kuonekana kwenye damu za wagonjwa hao.Kwa kawaida ugonjwa wa HIV unaweza kudhibitiwa tu kwa mgonjwa kutumia dawa za kurefusha maisha wakati wote wa uhai wake.

 

Utafiti huu mpya unaweza kuchangia kupatikana tiba ya ugonjwa huu wa HIV ambao umeambukiza takriban watu milioni 34 duniani kote.

Mtafiti Timothy Henrich wa Brigham and Women’s Hospital ya Boston amesema ‘’Ingawa majibu haya ya hawa wagonjwa yanatia moyo, bado hayathibitishi kama wanaume hao wamepona kweli, ila muda ndio utakaoamua kama kweli wamepona’’.

Uwezekano uliopo ni kwamba virusi hivyo vya HIV vinaweza kuwa vimejificha katika baadhi ya viungo vya mwili kama kwenye ubongo, ini, na vinaweza kuibuka tena hapo baadae.

Dk. Michael Brady wa Terrence Higgins Trust amesema’’ Upandikizaji wa uboho huwa huchanganya sana na huweza kuwa hatari kuliko dawa za kila siku.

‘’Ingawa hii si tiba lakini inatoa changamoto kwa wanasayansi kupata mwelekeo wa kupata tiba ya ugonjwa wa HIV’’ aliendelea kusema Dk. Michael Bradley

Mtu wa kwanza kabisa kupona ugonjwa wa HIV ni Mmarekani Timothy Ray Brown ambaye alifanyiwa upandikizaji wa seli za awali mwaka 2007 (Stem cells transplant) ili kutibu ugonjwa wa saratani ya damu na kuripotiwa na madaktari wake wajerumani kupona kabisa  HIV miaka miwili baadae.

Madaktari hao wa kijerumani walitumia seli za awali kutoka kwa mtu ambaye alikuwa na aina adimu ya kubadilika kwa seli asilia (genetic mutation) ambazo zina uwezo wa kujikinga dhidhi ya virusi vya HIV. Mpaka sasa hakuna mtu yoyote ambaye ameripotiwa kupona ugonjwa wa HIV isipokuwa wanaume hawa wawili wamarekani.

Mtafiti Kuritzkes anasema ‘’Iwapo maambukizi ya HIV yatajirudia tena kwa wanaume hao, basi tutawapa dawa za kurefusha maisha’’.

Kujitokeza tena kwa maambukizi ya HIV kwa wanaume hawa itaonesha ya kwamba viungo vingine vya mwili ni muhimu katika kuhifadhi virusi hivi na hivyo kutahitajika mtazamo mpya wa jinsi ya kutatua tatizo hili ili kupata tiba muafaka ya HIV’’ Alisema mtafiti Henrich

Matokea haya mapya yanatoa mwanga na kubadilisha jinsi tunavyofikiria kuhusu HIV na tiba ya viasilia (gene therapy)’’ alisema Kevin Robert Frost, mkurugenzi wa taasisi inayojihusisha na utafiti wa ugonjwa wa AIDS (The Foundation of AIDS Research).

Ingawa upandikizaji wa seli za awali sio chaguo bora kwa wagonjwa wa HIV kutokana na gharama zake pamoja na umakini unaohitajika, lakini matokeo haya yanatupa mwelekeo mpya wa jinsi ya kutibu na hata kuutokomeza kabisa ugonjwa wa HIV’’ aliendelea kusema mwanasayansi Kevin Robert Frost

HIV PT

 

 

Imesomwa mara 23762 Imehaririwa Jumatatu, 11 Juni 2018 15:41
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.