Image

Matumizi ya mafuta ya nazi kuzuia ugonjwa wa kusahau (Alzheimer's disease)

Makala hii iliandikwa na Dada Subi wa tovuti ya wavuti.com akizungumzia kuhusu umuhimu wa kufanyika kwa utafiti juu ya dhana ya kuwepo kwa uwezo wa mafuta ya nazi katika kutibu na kuzuia ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer's unaowaathiri zaidi wazee.  Ungana naye katika maoni yake haya.

Baadhi ya watafiti wanasema kiwango fulani cha mafuta ya nazi ni muhimu kwenye chakula kwa kuwa husaidia kupunguza ugonjwa wa kusahau  "Alzheimer's" ambao mara nyingi humjia mwanadamu kadiri umri unavyosogelea uzeeni.

Watafiti wanathubutu kusema, huenda mafuta haya ya nazi yakazuia kabisa kupata ugonjwa huo kwa baadhi ya watu.

Ingekuwa vyema na sisi Tanzania tukafanya utafiti kwa jamii ya watu wanaotumia kwa wingi mafuta ya nazi katika mapishi yao, hasa wale waishio mikoa ya mwambao wa pwani ambapo zao ma mnazi hustawi vizuri na kwa wingi.

Pengine hii ikawa pia sababu kujibu suala la kwa nini yapo matukio mengi ya Wazee na Vikongwe wengi kuuawa kikatili katika mikoa kadhaa nchini Tanzania ambayo zao la nazi ni nadra kuonekana sokoni, achilia mbali kutumika kama kiungo katika mapishi na/au matumizi ya kuchua na marashi.

Nimewaza hivyo kwa kuwa wazee wetu wanaouawa mara nyingi utetezi unaotolewa na wauaji ni kuwa mzee alikuwa na "dalili" za uchawi kwa kuwa pengine alikuwa akisema mwenyewe kama mwehu, akiondoka usiku na kutokomea pasikojulikana, alikuwa akivua nguo mbele ya kadamnasi, alikuwa mwoga au kuonekana mwenye wasiwasi wakati wote n.k., bila watu hao kufahamu kuwa kwa ujinga* wa masuala ya afya ya akili ya binadamu yatokanayo na umri, matukio mbalimbali maishani yaliyoathiri akili na fikira, pamoja na hofu ya uzee kwa vitendo walivyotendewa wengine, wanaweza kabisa kuwa sababu ya matatizo (dalili) na kuishia kuwawahukumu baadhi ya wazee hao kifo pasina hukumu ya haki. Ninaamini kuwa, kama ambavyo wapo waliofungwa jela kwa makosa ya kudhaniwa, kusingiziwa, wasiyoyatenda na visasi, vile vile wapo wanaouawa kwa sababu zizo hizo.

Niseme kuwa, zinazotajwa kuwa sababu (naita visingizio) za kumtuhumu mtu uchawi zinalandana na dalili za ugonjwa wa kusahau "Alzheimer's  disease" ambazo niliwahi kuziandika wakati nikichangia makala za afya katika gazeti la KwanzaJamii (unaweza kuzisoma kwa lugha ya Kiingereza katika linki hii: alz.org).

Makala hii ni kwa hisani ya wavuti.com

Imesomwa mara 35439 Imehaririwa Alhamisi, 15 Agosti 2019 08:56
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana