Image

Kwa kawaida, meno ya mtoto ya utotoni (meno ya awali) huanza kutoka kuanzia miaka 6. Kwa baadhi ya watoto, huweza kuchelewa kuanza kutoka meno ya utotoni hadi wanapoanza mwaka wA 7.

Meno ya kwanza yanayoanza kutoka ni yale mawili ya chini ya kati (lower central incisors) na hufuatiwa na yale ya juu ya kati (upper central incisors) (. Baada ya hapo, hufuatiwa na meno ya kutafunia ya kwanza na ya pili.

Kwa kawaida, meno ya ya awali hukaa bila kutoka mpaka pale meno ya kudumu yanapotaka kuanza kuchomoza, hivyo hulisukuma jino la utoto na kusababisha kutoka. Endapo mtoto atatoka meno mapema au jino litatoka kwa sababu ya ajali au kuoza, basi jino la kudumu litaziba pengo hilo baada ya muda kufika. Hii inaweza kusababisha meno kutokuwa na mpangilio mzuri kwakuwa wakati linachomoza kulikuwa na meno mengine ya utotoni, hivyo unashauri kuwasiliana na daktari wa kinywa na meno kwa ushauri zaidi.

Pale mtoto anapoanza kutoka meno, tafadhali zingatia kanuni bora za Afya ya kinywa na meno kama ;

  • Kuhakikisha anasubua meno angalau mara mbili kwa siku. Mkazanie kwa sababu umakini unahitajika.
  • Msaidie mtoto kusugua meno kila siku
  • Hakikisha anakula chakula bora na kupunguza matumizi ya vyakula vitamu
  • Weka miadi na daktari wa kinywa nameno

Kwa mazingatio haya, utaweza kuhakikisha afya bora ya kinywa na meno ya mtoto wako. Pia, unaweza kusoma makala zaidi juu ya Afya ya kinywa na meno wakati wa makuzi ya mtoto

Afya bora ya kinywa na meno kwa mtoto ni muhimu sana na ina uhususiano wa moja kwa moja na afya yake kwa ujumla. Humuepusha mtoto kupata maumivu, uwezekano wa uambukizo, kumfanya aweze kutafuna vizuri ili kupata virutubisho muhimu kwa ajili ya kujenga kinga dhidi ya magonjwa, na kusaidia ukuaji. Afya nzuri ya kinywa na meno pia itamfanya mtoto aweze kuhudhuria masomo ipasavyo na hivyo kupata matokeo mazuri.

Umuhimu wa meno ya utoto

Wazazi /walezi wengi hujiuliza kwanini wahangaike kutunza meno ya utoto ambayo yanatarajiwa kung’oka na kuota ya ukubwa. Meno ya utoto ni muhimu kutokana na sababu zifuatazo:
Humsadia mtoto kutafuna na hivyo kumwezesha kupata virutubisho muhimu
Hutunza nafasi kwa ajili ya meno ya ukubwa
Hali ya afya ya meno ya utoto huathiri hali ya afya ya meno ya ukubwani
Husadia uumbaji wa maneno (kuongea)

Kama mzazi / mlezi unatakiwa kuwa mstari wa mbele kutunza meno ya mtoto wako kwani, watoto hupenda kujifunza kutokana na mfano wa wazazi.

Zifuatazo ni dondoo muhimu kwa wazazi/walezi kwa ajili ya kutunza afya bora ya mtoto:

Umri wa kuzaliwa mpaka miezi 6

  • Mnyonyeshe mtoto maziwa ya mama pekee hadi umri wa miezi sita.
  • Maziwa ya mama ni muhimu sana kwa ukuaji na kinga dhidi ya magonjwa.

Umri wa miezi 7 hadi miezi 18

  • Usimlaze mtoto akiwa na chuchu ya maziwa au chuchu ya mama mdomoni ili kuzuia ugonjwa wa kuoza kwa meno (rampant caries)
  • Mpatie mtoto maji badala ya juisi akiwa na kiu.
  • Iwapo utampa mtoto juisi ya boksi unashauriwa kuongeza kiwango cha maji sawa na kile cha juisi ili kupunguza kiasi cha sukari kilichomo ndani ya juisi.
  • Ukitengeneza juisi nyumbani kwa ajili ya mtoto, jiepushe kuiongezea sukari.
  • Jino la kwanza litakapoota, anza kusafisha kinywa cha mtoto kutumia kitambaa laini kilicholoweshwa kwenye maji safi au mswaki laini bila dawa.
  • Panga miadi ya kwanza ya kumwona daktari wa meno (first appointment) wakati mwanao hana maumivu au shida yoyote ili kujenga mahusiano mazuri kati ya mtoto na daktari

Umri wa miezi 18 hadi miaka 6

  • Dhibiti ulaji wa vyakula vyenye sukari na zingatia ulaji wa vyakula vinavyojenga afya ya mtoto kama matunda, mboga mboga, karanga, maziwa na samaki.
  • Safisha meno ya mtoto kutumia maji safi na mswaki laini na dawa ya meno (zingatia kiwango cha dawa: kiasi cha mbegu ya kunde) asubuhi na jioni kila siku.
  • Mtoto asukutue mdomoni ili kupunguza kiwango cha dawa itakayobaki.
  • Chunguza mara kwa mara meno ya mtoto ili kugundua dalili za mwanzo za ugonjwa wa kuoza kwa meno (rangi kuwa nyeupe au kahawia zaidi katika eneo husika baada ya kukausha) na pia matatizo mengine kama uvimbe, vijipu au kutoka damu kwenye fizi.
  • Mpeleke mtoto kwa daktari wa meno angalau mara moja kwa mwaka na mara unapogundua tatizo lolote kinywani mwake.

Umri wa miaka 6 hadi 12

  • Msimamie mtoto kusafisha kinywa na meno mara mbili kwa siku.
  • Mtoto ateme dawa itakayobaki ila asisukutue na maji baada ya kupiga mswaki.
  • Mjengee mtoto tabia ya kusukutua na maji kila baada ya kula vyakula vyenye sukari kama keki, chokoleti au juisi.
  • Chunguza mara kwa mara meno ya mtoto ili kugundua dalili za mwanzo za ugonjwa wa kuoza kwa meno na matatizo mengine kinywani.
  • Mpeleke mtoto kwa daktari wa meno angalau mara moja kwa mwaka na mara unapogundua tatizo lolote kinywani mwake.

Umri wa miaka 12 na zaidi

  • Mtoto anaweza kuanza kusafisha kinywa na meno bila ya usimamizi.
  • Dhibiti ulaji wa vyakula vyenye sukari na zingatia ulaji wa vyakula vinavyojenga afya ya mtoto kama matunda, mboga mboga, karanga, maziwa na samaki.
  • Mpeleke mtoto kwa daktari wa meno angalau mara moja kwa mwaka na mara unapogundua tatizo lolote kinywani mwake.

CREDIT: Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS)

Wakati wa muongo uliopita mahitaji ya kuboresha muonekano au kurembesha meno yameongezeka kwa kiwango kikubwa hasa katika nchi zilizoendelea. Hii imechochewa na kupatikana kemikali mpya za meno (dental meterials) na vifaa kwa kasi ikiendana na kuboresha vile vya zamani. Sehemu nyingine iliyosababisha madaktari na mainjinia wa meno kuyafanya meno kuwa meupe ni sehemu ya fani ya taaluma ya meno chini ya urembeshaji wa meno, fani hii uhusika na kuboresha muonekano wa meno hasa yale yanayoonekana wakati wa kutabasamu na kuongea.

Inahusisha matibabu kama kuyafanya meno yenye rangi kuwa meupe, kunyoosha meno yaliyojipanga vibaya pamoja na kukarabati meno yaliyovunjika na yale yaliyoumbika visivyo (malformed teeth). Huko Uingereza na sehemu nyingine za magharibi wanawake walio wengi wanatumia maelfu ya paundi/euro kuboresha muonekano wa meno yao hali ambayo inaanza pia kuingia huku kwetu.

Nini husababisha meno kugeuka rangi?
Meno kugeuka rangi husababishwa na kimojwapo au muunganiko wa vitu vifutavyo: -

  1. Vyakula na vinywaji kama vile vinyaji vyenye kaboni, wine na sigara.
  2. Utumiaji wa maji yenye kiwango cha juu cha madini aina ya magadi (fluoride) na utumiaji wa magadi katika kulainisha vyakula wakati wa kuandaa vyakula vigumu kama maharage na makande. Utafiti uliofanywa na Prof. Mabelya na wenzake nchini Tanzania umeonesha kuwa kubadilika kwa rangi ya meno kutokana na magadi kwa kiwango kikubwa husababishwa na matumizi ya magadi katika mapishi ya vyakula hasa makande kule maeneo ya mkoa wa Kilimanjaro/Moshi kuliko inavosababishwa na matumizi ya maji.
  3. Maumbile yasiyo sahihi ya sehemu ngumu za jino (enamel and dentine defects). Iwapo sehemu ngumu ya meno imeumbwa ikiwa laini ni rahisi kufyonza rangi na jino kuota likiwa limegeuka rangi au kubadilika baada ya kuota.
  4. Matumizi ya madawa kwa mama mjamzito ambaye tayari meno ya mtoto aliye tumboni yameanza kuumbwa lakini hayajapata madini ya kutosha na hata watoto wachanga ambao meno yao hayajakomaa.
  5. Kufa kwa kiini cha jino hasa kutoka na kujigonga wakati wa ajali au kupigana ngumi usoni (pulp necrosis), jino likigongwa kwa nguvu damu huvuja ndani ya kiini cha jino na baadaye huchachuliwa na kutoa kemikali ambayo hupenya kwenye vitundu vidogo vidogo kwenye dentine na kujidhihirisha kama kijivu, zambarau au hata nyeusi. Hali hii yaweza tokea mapema baada ya kupata ajali lakini wakati mwingine inaweza kuchukua miaka kadhaa hata arobaini kipindi ambapo mtu hakumbuki kuwa aliwahi kutwangwa ngumi.

Kuyafanya meno yenye rangi yasimpendeza mwenye nayo kuwa meupe (Bleaching or teeth whitening)

Huku ni kuyafanya meno yenye rangi kuwa meupe au kuongeza weupe wa yale yenye rangi ya kawaida kufikia kiwango cha weupe atakacho muhitaji kwa kutumia kemikali maalum. Rangi ya kawaida ya meno kwa walio wengi ni uweupe kama wa maziwa (milky white). Rangi yeyote nje ya hiyo si ya kawaida (abnormal color or discoloration).