Image

Fangasi wapo kila mahali, kwenye miti, mimea, mchanga, ndani majumbani mwetu na hata kwenye ngozi ya binadamu.Aina nyingi ya fangasi hawasababishi madhara yoyote kwa binadamu isipokuwa wachache tu. Kuna aina milioni moja na nusu za wadudu aina ya fangasi wanaotambulika duniani, kati yao ni fangasi 300 tu wanaojulikana kusababisha maambukizi kwa binadamu .1,2 Uvutaji wa hewa iliyochanganyika na  mazalia ya fangasi yanayojulikana kama fungal spores pamoja na uwepo wa uvamizi au ukuaji wa fangasi kwenye ngozi ya binadamu husababisha maambukizi ya fangasi, hivyo basi maambukizi mengi ya fangasi huanza kwenye  mapafu au kwenye ngozi ya mtu.

Takribani watu milioni 984 walipata maambukizi ya fangasi kwenye ngozi  mwaka 2010 na hivyo kufanya maambukizi haya kuwa ugonjwa namba nne katika magonjwa yote kwa mwaka huo 3.

Watu walio kwenye hatari ya kupata maambukizi ya fangasi ni kama wafuatavyo;

  • Wagonjwa wanaotumia dawa za kuua vimelea vya wadudu bila kufuata masharti ya daktari -Dawa aina ya antibayotiki (antibiotics)
  • Wale wenye kinga dhaifu - Wagonjwa wa ukimwi,wagonjwa wa kisukari, wagonjwa wanaotumia dawa za jamii ya steroid, wagonjwa wanaotumia dawa za kutibu saratani (chemotherapy drugs), immunosuppressive drugs, wagonjwa wanaotibiwa kwa mionzi na  wajawazito
  • Watoto wadogo na wazee - Ingawa watu wote wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya fangasi, hatari kubwa ipo kwenye kundi hili la wazee na watoto kutokana kuwa na kinga dhaifu

Aina za maambukizi ya fangasi

  1. Maambukizi ya fangasi nje ya mwili (Superficial mycoses) - Ni fangasi ambao husababisha maambukizi kwenye ngozi, nywele, kucha na hawaishi kwenye tishu mwilini. Fangasi aina hii hujulikana kama Dermatophytes.Fangasi hawa hushambulia sehemu tajwa hapo juu kwa kutoa vimengenyo (Extracellular enzymes) vinavyolainisha protini aina ya keratin inayopatikana katika maeneo hayo.Maambukizi haya ya fangasi yamegawanyika katika
  2. Tinea Corporis - Maambukizi ya fangasi yanayopatikana katika sehemu yoyote ile mwilini.
  3. Tinea Pedis (Athlete’s foot)-Maambukizi ya fangasi katikati ya vidole vya miguuni na kwenye nyao za miguu
  4. Tinea Unguium (Onchomycosis) - Maambukizi haya yanapatikana kwenye kucha za vidole vya miguuni na vya mikononi
  5. Tinea Capitis – Huonekana kwenye kichwa hasa kwa watoto wadogo.Husababisha mapunye kwenye kichwa, nywele kunyofoka, mabaka meusi kwenye kichwa yaliyoambatana na mcharuko (Inflammation), kutokwa na magamba kichwani, kuwashwa na kuvimba vimba  kwenye kichwa
  6. Tinea Cruris – Maambukizi ya fangasi sehemu za siri
  7. Tinea Barbae – Huonekana maeneo yenye ndevu kwenye uso na shingoni
  8. Tinea Vesicolor – Maambukizi ya fangasi kwenye ngozi ya watu wazima.Maambukizi haya hayaonekani kwenye uso ila husababisha ngozi kuwa na mabaka yenye rangi ya kahawia iliyochanganyika na rangi nyekundu (reddish brown).Tinea vesicolor huonekana sana kwenye ngozi ya watu wanaoishi sehemu zenye joto kali au wenye matatizo kwenye vichocheo vya miili yao (hormonal abnormalities) ingawa wote wanaopata maambukizi haya huwa ni watu wenye afya njema.
  9. Subcutaneous Mycoses- Maambukizi ya fangasi kwenye tishu chini ya ngozi zinazojulikana kama dermis, subcutaneous tissue, fascia na kwenye misuli.Fangasi wanaosababisha maambukizi haya hupatikana kwenye mchanga na mimea.Maambukizi haya sugu hutokea pale mtu anapokuwa na kidonda na hivyo kurahisisha fangasi kuvamia mwili.Magonjwa yanayosababishwa na fangasi kwenye tishu chini ya ngozi ni kama yafuatayo;
  • Sporotrichosis
  • Chromoblastomycosus
  • Mycetoma
  • Phaeohypomycosis 

Sporotrichosis

Husababishwa na fangasi aina ya Sporothrix schenckii.Fangasi hawa hupatikana kwenye mimea, miti, nyasi na kwenye maua aina ya waridi. Maambukizi yanayotokea kwenye mikono na miguu ingawa kwa watoto huonekana sana sehemu za usoni.Pia huweza kusambaa kwenye damu kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini.