Dawa za kuongeza makalio ni kitu kilichopata umaarufu wa ghafla miongoni mwa kina dada wengi duniani na hata katika jamii yetu. Siku hizi haishangazi kusikia dada mwenye makalio makubwa au yenye umbo duara akiambiwa kuwa anatumia dawa za kunenepesha makalio au ‘wowowo’ kama wanavyopenda kuita vijana kwa kiswahili cha mtaani. Aidha matangazo juu ya dawa hizi nayo yamekuwa yakiongezeka kila kukicha. Pamoja na kwamba kuna simulizi tofauti juu ya faida na madhara ya matumizi yake, idadi ya watumiaji inazidi kuongezeka siku hadi siku.

Lakini dawa za kuongeza makalio ni nini hasa? Kwa ujumla hizi ni dawa zitumiwazo na akina dada na mama kwa ajili ya kunenepesha na kuongeza ukubwa wa makalio yao na kuyafanya yawe na umbo wanalodhani linawavutia wao au/na wapenzi wao. Ukisoma maelezo ya dawa hizi, nyingi hudai kuwa na uwezo wa kuboresha umbo la makalio kwa kuyafanya yawe na muonekano wa ujana zaidi, duara, laini na yenye mvuto.

Wanawake karibu dunia nzima huamini maelezo kuwa dawa hizi zina uwezo wa kuwajengea maumbo wanayoyatamani. Wengi, kuanzia watu mashuhuri (celebrities) mpaka watu wa kawaida, wanataka makalio makubwa; yale maumbo madogo na makalio ‘yasiyojazia’ hayana nafasi tena. Wanaamini kuwa makalio ‘yaliyojazia’ yanafanya hata nguo kukaa vema mwilini, huwafanya wanaume kugeuza shingo kuwashangaa (labda kuwatamani pia) na wengine hudai yanasaidia kuongeza mvuto wa ngono kwa wapenzi wao.