23 Mach 2018

Si mara chache tumewahi kushuhudia au kusikia mtu au kundi la watu likiugua ghafla baada ya kula chakula katika mkusanyiko au sherehe. Bila shaka nawe ni mmojawapo wa waliowahi kukumbwa na hali hii.

Aidha tumewahi pia kusikia au kushuhudia hata baadhi ya watu wakiamini kulishwa sumu baada ya kula chakula katika shughuli au sherehe fulani. Hali hii imewahi kuzusha tafrani na sintofahamu miongoni mwa wanajamii kwa vile si wengi wanaofahamu hasa chanzo cha hali hiyo.

Lakini usumu au maambukizi katika chakula (food poisoning) ni nini hasa?

Food poisoning ni hali ya kuchafuka kwa chakula kunakotokana na uwepo wa vimelea mbalimbali kama vile bacteria, virusi, au parasites au sumu zao ndani yake. Hali hii hutokea wakati unapokula chakula au kunywa vinywaji/maji yaliyochanganyika na vimelea hawa hususani vya bacteria wa jamii ya Staphylococcus au Escherichia coli (E. coli).

Ieleweke kuwa food poisoning haimaanishi sumu inayowekwa na mtu/watu kwenye chakula bali hutokana na vijidudu vya magonjwa mbalimbali kama vile bacteria.

Vihatarishi vyake

Kwa kawaida food poisoning hutokea zaidi baada ya kula vyakula vilivyoandaliwa kwenye mikusanyiko kama vile cafeteria za shule au kazini, kwenye misiba, matanga, hitma, maulid, ngoma, harusi, mahoteli, na mikusanyiko mingine yeyote ambayo inahusisha ulaji wa chakula cha pamoja; ambapo mtu mmoja au kundi la watu hupatwa na usumu huo na kuwa wagonjwa.

02 Mai 2017

Ripoti ya utafiti iliyochapishwa katika jarida la Health Physiology na kuchapwa katika wavuti ya WebMD inadai kuwa watu wazima wenye tabia ya kufanya mazoezi ya kuendesha baiskeli au kujinyosha viungo vyao huongeza uwezo wa kukumbuka zaidi kuliko wale wasiofanya kabisa.

 

Utafiti huo unadai kuwa pamoja na kwamba kimuundo ubongo haufanani na misuli lakini kadri mtu anavyozeeka kuingia utu uzima, ufanyaji mazoezi husaidia kuimarisha uwezo wake wa kukumbuka na hata kufikiria mambo mapya.

Jambo la kutia moyo ni kuwa huna haja ya kufanya mazoezi mazito kwa vile mazoezi mepesi tu kama ya kunyoosha nyoosha viungo yanatosha kuleta kabisa matokeo ya kuridhisha.

Uchunguzi huo ambao ulihusisha watu wazima waume kwa wake waliokuwa wakiendesha baiskeli au mazoezi ya kunyoosha viungo kwa muda wa saa mbili kwa wiki kwa muda wa miezi sita ulionesha kuwepo kwa maendeleo makubwa katika uwezo wao wa kukumbuka mambo na hata kufikiria mambo mapya.

Mmoja wa watafiti hao Kirsten Hotting kutoka chuo kikuu cha Hamburg, Ujerumani anasema kuwa mtu anayefanya mazoezi ya aina mbalimbali kwa pamoja ana uwezekano wa kupata matokeo mazuri zaidi.

Ripoti hii inaweza kutafsiriwa kama changamoto kwa watu walio katika nafasi mbalimbali za kutoa maamuzi kiuongozi kuwa tabia ya ufanyaji mazoezi inaweza kuimarisha sana uwezo wao wa kukumbuka mambo na kufikiria mambo mapya, na hivyo kuzidi kuongeza tija katika utendaji wao wa kila siku. Aidha hii ni changamoto hata kwa watu wengine kuanzisha utaratibu wa kujifanyia mazoezi mepesi kwa ajili ya kuimarisha afya ya akili na mwili kwa ujumla.

Ripoti ya utafiti huu inapatikana katika Jarida la Health Psychology

01 Mai 2017

 Nikiwa kama mjukuu kipenzi wa bibi yangu, huwa napenda sana kutumia muda wangu wa mapumziko kujadiliana naye mambo mbalimbali yanayohusu jamii, iwe yaliyokuwa yanatokea hapo awali au yanayoendelea kutokea. Ilikuwa ni siku ya jumapili baada ya kutoka kwenye mihangaiko, niliingia ndani na kumuita bibi kwa jina lake la utani ‘Nyaksi’ ili twende nje tukapunge upepo na mazungumzo ya hapa na pale.

Nikipata Ushauri wa Afya toka kwa Dk Mayala

   Kama ilivyo ada yangu, huwa napenda sana kutafiti mambo mbalimbali, nikamuuliza bibi, eti bibi nimewahi kusikia kuwa wakati wa enzi zenu mlikuwa hamruhusiwi kula mayai wakati wa ujauzito kwa kuwa mtoto atazaliwa bila nywele? Bibi Nyaksi huku akitabasamu akanigeukia na kusema, "umeshaanza, kwanza usikumbushe enzi zile bado nipo mbichi" akimaanisha wakati yupo msichana. Wote tukatabasamu kwa pamoja. Nyaksi akaendelea kusema sio mayai tu, bali vyakula vyote nyenye virutubisho kwa wingi ambavyo ninyi vijana wa leo mnaviita ‘purotini’, akiitamka protini kwa lafudhi ya kizee. Nyaksi alisema tulizuiliwa kula vyakula hivyo kwa mlengo wa mwiko, akaendela kusema, unajua Babu (jina langu alilopenda sana kuniita Nyaksi) wazee walitumia mwiko ili kututisha lakini ukweli ni kuwa wakati ule hakukuwa na tekenolojia (akimaanisha teknolojia) hivyo kama utakula vyakula vyenye virutubisho sana vitamfanya mtoto awe mkubwa, na hivyo kama utashindwa kujifungua kwa njia ya kawaida basi hakutakuwa na njia nyingine ya kukusaidia. Nyaksi akaendelea ninyi vijana wa siku hizi mna raha, hospitali nyingi, madaktari wengi huku mna njia nyingi mbadala ikiwemo ya upasuaji na nyinginezo. 

   Nilimuacha Bibi Nyaksi amalizie maneno yake, halafu nikamuuliza, kama sisi tuna teknolojia na njia nyingi za kisasa, sasa inakuwaje urefu wa maisha wa vizazi vyetu unazidi kupungua kadri teknolojia inavyozidi kukua? Nyaksi alicheka sana, huku akipigapiga makofi ili kuvuta hisia alisema " hakuna kizuri kisicho na kasoro". Baada ya hapo tukaacha kuongelea masuala ya afya na kuketi chini ili kupunga upepo uliokuwa ukivuma kwa kasi kutokea Kinyanyiko. 

   Kipindi chote naburudika na upepo uliokuwa unavuma ukitokea kwenye mabonde ya Kinyanyiko nilikuwa natafakari mambo mengi kuhusu maneno ya Nyaksi. Misemo yake ilikuwa inazungukazunguka kichwani kwangu , huku maneno "Hakuna kizuri kisicho na kasoro " na " ninyi mnaishi kwenye ulimwengu wenye tekinolojia" vikijitokeza mara kwa mara. Lakini je, hizi teknolojia zinatunufaisha vipi? Zipi faida na hasara zake? Hivyo nikawa nachorachora chini nikiainisha viambatanishi vyote vya hii tunayoiita teknolojia, nikarudi haraka nyumbani na kuchukua iPad yangu kuanza kuandika makala hii ambapo tutaiangalia teknolojia kwa mapana na jinsi gani teknolojia inavyoweza kuongeza ufanisi katika medani ya afya. 

27 Apr 2017

Bima kwa Ujumla

Bima ni mfumo wa kumwahidi kumrejeshea mwanachama hali ya afya, kipato, maisha na ustawi pindi anapopata janga au anapopoteza kitu chake cha thamani hasa ikiwa amelipia michango ya marejesho (premiums).

Bima hulenga kumkinga mwanachama dhidi ya janga lisilotegemewa, kwa mfano kinga dhidi ya Ajali, Kulazwa Hospitalini, Moto, Mafuriko, Wizi, nk. Aghalabu, matukio hayo yasipokingwa, hurudisha nyuma maendeleo ya mtu au familia nzima.

Kwa kawaida kuna aina mbili za mfumo wa Bima

  • Huduma za Bima zilizo Rasmi – (Formal) kama Bima ya Afya, Bima ya Majengo, Bima ya Gari, Bima ya Maisha
  • Bima zisizo rasmi – kama Bima za Mazishi, Bima za makundi ya kuweka na kukopa, Bima ya Mfuko wa Afya ya Jamii n.k.

Tunavyofahamu

Tofauti na nchi nyingine za Afrika Mashariki kama Rwanda na Kenya, Watanzania wengi hawana huduma ya bima na wengi hawafahamu faida za kuwa na utaratibu wa bima. Wengi hawana huduma yoyote ya bima (92%) na huku asilimia ya Bima Rasmi ikiwa 6.4% na isiyo rasmi ikiwa asilimia 1.9% . (1) (FSDT/Finscope Survey 2009)

Pia, utafiti uliofanywa mwaka 2009 na The First Microinsurance Agency Limited iliyopo Dar es Salaam ikiwahusisha watu 600 na ikifanywa na kundi la Steadman ulionesha kuwa walio wengi wanapendelea sana kuwa na Bima ya Afya. Hii inafuatiwa na Bima ya Elimu na Bima ya Maisha. (2) (Market Research on the Demand for Health and Life Insurance in Tanzania. Steadman Group, 2008).

Mifumo iliyopo nchini

Kwa sasa, Bima zilizopo nchini Tanzania ni zifuatazo:

  • Bima za Afya
  • Bima za Ajali
  • Bima za Mali
  • Bima za Ajali
  • Bima za Majengo
12 Apr 2017

Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 47 kutoka jimbo la Michigan nchini Marekani amepata ugonjwa adimu sana(rare disease) wa mifupa baada ya kunywa chai iliyotengenezwa kwa aina mia moja ya majani ya chai kwa wingi (lita 3 kwa siku) kwa miaka 17 mfululizo, watafiti kutoka Marekani wamesema.

Mwanamke huyo alikwenda hospitali kuonana na Daktari baada ya kuwa na maumivu makali kwenye kiuno,mikono,miguu na kiuno kwa miaka mitano.

Baada ya kufanyiwa kipimo cha X-ray iligundulika mama huyo ana ugonjwa huo adimu ambao huonyesha dalili za kuongezeka kwa uzito wa mifupa ya uti wa mgongo(dense spinal vertebrae) pamoja na kushikana(calcifications of ligaments) kwa viunganishi vya mifupa ya kwenye mikono’’ alisema mmoja wa watafiti Dr. Sudhaker D. Rao, Daktari bingwa wa magonjwa vichocheo vya mwili na virutubisho vya mifupa na vya mwili (Endocrinologist and bone and mineral metabolism physician) katika hospitali ya Henry Ford Hospital,Marekani.

Dr. Rao alihisi mama huyo ana ugonjwa wa mifupa unaojulikana kama skeletal fluorosis unaosababishwa kwa kutumia kwa wingi madini aina ya fluoride (Fluoride hupatikana kwenye maji au chai)

Kiwango cha madini ya fluoride katika damu ya mama huyo kilikuwa juu mara nne zaidi ya kiwango kinachohitajika kwenye mwili wa mwanadamu.

Ugonjwa wa skeletal fluorosis huonekana sana kwenye maeneo ambayo kiasili yana madini ya fluoride kwa wingi kama baadhi ya maeneo nchini India na China (katika nchi nyingi kiwango kidogo cha fluoride huweka kwenye maji, dawa za meno kama kinga dhidhi ya ugonjwa wa meno unaojulikana kama cavities)

‘’Mgonjwa alipewa rufaa ya kuja kuniona kwa sababu madaktari walie muona mwanzo walidhani ana saratani ya mifupa, lakini baada ya mimi kuona X-ray za mgonjwa,mara moja nilitambua kuwa ni ugonjwa wa skeletal fluorosis kutokana na kuwahi kuona wagonjwa wa aina hiyo nilipokuwa kwetu nchini India’’alisema Dr. Rao

28 Feb 2012

 Mnamo mwaka 2007, watafiti nchini Marekani walifanikiwa kutoa ripoti inayojaribu kuhusisha ukosefu wa usingizi na upungufu wa homoni ya testosterone miongoni mwa wanaume watu wazima.

Kwa kawaida kiwango cha homoni ya testosterone hupungua kadiri mwanaume anavyozidi kuwa mtu mzima, na kwa baadhi ya wanaume, kupungua huku kwa testosterone huweza kusababisha ulegevu wa mwili, kukosa hamu ya ngono na hata kuvunjika mifupa ya mwili.

Watafiti wanasema kuwa, wapo baadhi ya wanaume walio kwenye miaka 80 bado huweza kuwa na kiwango cha juu cha testosterone sawa na kile kinachopatikana kwa wanaume vijana. Hata hivyo sababu kubwa inayofanya kuwepo na utofauti katika viwango vya testosterone miongoni mwa rika hizo mbili bado hazieleweki sawasawa, ingawa watafiti wanasema kuwa ukosefu wa usingizi miongoni mwa watu wazima na wazee unaweza kuwa chanzo kimojawapo cha kuwepo kwa hali hiyo.

"Matokeo ya utafiti wetu yanaongeza uwezekano kuwa wanaume watu wazima na wazee ambao hupata muda mfupi sana wa kulala nyakati za usiku huwa na kiwango kidogo sana cha homoni ya testosterone wakati wa asubuhi," anasema mtafiti Plamen Penev, wa kutoka Chuo Kikuu cha Chicago, nchini Marekani.

Wakati wa utafiti, wataalamu waliofanya uchunguzi huo walipima kiwango cha homoni ya testosterone katika damu kila asubuhi cha wanaume watu wazima wenye umri kati ya miaka 64 na 74 waliojitolea kushiriki kwenye utafiti huo. Aidha, mtindo wao wa kulala pamoja na kupata usingizi pia vilichunguzwa kila siku kwa muda wa wiki nzima.

Matokeo ya uchunguzi huo yalionesha kuwa kiasi cha usingizi walicholala kilikuwa na uhusiano wa karibu sana na kiwango cha testosterone katika damu wakati wa asubuhi. Wale waliopata usingizi mzuri na kwa muda mrefu (walau saa nane) walikuwa na kiwango kikubwa cha testosterone wakati wale waliopata usingizi wa kubabaisha (saa nne) walikutwa na kiwango cha chini cha homoni hiyo. Wastani wa muda wa kulala ulikuwa masaa sita.

"Pamoja na kwamba matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa urefu wa muda wa kulala wa mtu waweza kuwa kiashiria cha mabadiliko ya homoni katika mwili yanayohusiana na umri, matokeo ya utafiti huu yanatoa tu picha ya nini kinachotokea mwilini kama mtu asipopata usingizi wa kutosha. Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika ili kuthibitisha umuhimu wa uhusiano kati ya usingizi na mabadiliko ya homoni katika mwili," anasema Dr. Penev.

Wataalamu wa masuala ya afya ya usingizi wanashauri watu wazima kupata wastani wa angalau saa saba mpaka nane za kulala kila usiku ili kuwa na afya bora. Ripoti kamili ya matokeo ya utafiti huu inapatikana katika toleo la mwezi April, 2007 la jarida la afya la Sleep.