13 Ago 2017

Utafiti wasema unywaji wa angalau soda mbili kwa wiki huongeza hatari ya kupata kansa ya tezi kongosho,viwanda vyadai utafiti una walakini.

Mapema mwaka huu iliripotiwa na majarida kadhaa sehemu mbalimbali duniani kuwa, kwa mujibu wa utafiti mpya, unywaji wa angalau chupa mbili za vinywaji baridi (soda) kila wiki huongeza uwezekano wa kupata kansa ya tezi kongosho.

Tezi kongosho lipo nyuma ya tumbo likiwa na kazi ya kuzalisha homoni ya insulin ambayo hufanya kazi ya kuchochea seli zinyonye sukari kutoka katika damu mara baada ya mtu kula au kunywa kitu chenye sukari. Pia hutoa vimeng’enyo ambavyo husaidia katika usagaji wa vyakula vyenye mafuta na protini.

Walio fanya utafiti huo wanasema kuwa watu wanywao chupa mbili au zaidi za vinywaji baridi kama soda kwa wiki wana uwezekano wa karibu alimia 87 wa kupata kansa ya tezi kongosho ikilinganishwa na wale wasiotumia vinywaji vya aina hiyo. Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la Cancer Epidemiology, Biomarkers & Prevention linalomilikiwa na chama cha tafiti za saratani cha Marekani.

Hata hivyo makampuni yanayohusika na utengezaji wa vinywaji baridi wameupinga utafiti huo wakidai kuwa ulikuwa na walakini na makosa mengi, huku wakiegemea katika matokeo ya tafiti zilizowahi hapo kabla ambazo zilionesha kutokuwepo kwa uhusiano wowote kati ya unywaji soda na kansa ya kongosho.

07 Jun 2017

Watafiti nchini Japan wamegundua jinsi seli za mfumo wa fahamu zinavyoweza kutumika kama seli mbadala zinazofaa kupandikizwa kwenye seli kongosho ili kutibu kisukari. Ripoti ya utafiti huo ambayo imechapishwa kwenye jarida la kitafiti la EMBO Molecular Medicine, inaonesha kuwa seli zinazovunwa kutoka katika mfumo wa fahamu zinaweza kupandikizwa katika tezi kongosho na hivyo kumaliza tatizo la ukosefu wa seli za beta ambazo huitajika kwa ajili ya uzalishaji wa insulin.

Kisukari ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa kichocheo cha insulin kinachozalishwa na tezi kongosho, na ambao huathiri karibu watu milioni 200 duniani. Mpaka sasa hakuna tiba yeyote ya ugonjwa huu, hali inayowafanya wagonjwa wa kisukari kutegemea zaidi matumizi ya dawa au njia nyingine mbadala kuthibiti kiwango cha sukari mwilini.

Utafiti huo ulioongozwa na Dr Tomoko Kuwabara kutoka taasisi ya tafiti za Afya ya AIST ya Tsukuba nchini Japan, ulilenga katika kuchunguza jinsi seli za binadamu zinavyokua na kijiwagawa kulingana na kazi mbalimbali za mwili, na pia kuchunguza uwezekano wa kutumia seli mbalimbali kutekeleza kazi zilizo nje ya majukumu yake ya kawaida.  

Katika kufafanua, Dr. Kubawara anasema kuwa kwa vile kisukari ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa aina moja ya seli, ugonjwa huu unaweza kutibika kwa kutumia njia ya upandikizaji wa seli mpya zitakazotumika kuzalisha kichocheo cha insulin.

Anasema, hata hivyo kwa vile kupandikiza seli za beta kutoka tezi kongosho za watu wengine ni ngumu kwa sababu ya ukosefu wa watoaji, njia muafaka ni kutumia seli za mfumo wa fahamu wa mgonjwa mwenyewe katika kufanikisha upandikizaji huo.

21 Apr 2017

Aina mpya ya vimelea vya ugonjwa wa kisonono au "gono" ambavyo vinahimili dawa (resistant to drugs) zinazotumika kutibu ugojwa huu imegundulika duniani. Taarifa iliyotolewa na shirika la afya duniani (WHO) hivi karibuni imesema, ugonjwa wa kisonono unaoathiri mamilioni ya watu ulimwenguni umeanza kuwa sugu dhidhi ya dawa zinazotumiwa kuutibu na hivyo kuna hatari ya kutoweza kutibika kabisa.

Shirika la afya duniani limetoa wito kwa serikali na madaktari kuongeza ufuatlijiaji wa aina hii ya kisonono kutokana na ugonjwa wa kisonono kuwa na athari nyingi kama mcharuko (inflammation), ugumba, matatizo wakati wa ujauzito na hata vifo vya kina mama wajawazito.

“Aina hii mpya ya vimelea vya kisonono vinaonyesha usugu dhidhi ya dawa zote za antibiotiki tunazotumia dhidhi yake ikiwemo dawa za jamii ya cephalosporins ambazo ni dawa za mwisho katika kutibu ugonjwa wa kisonono, “ alisema Dk. Manjula Lusti-Narasimhan, mmoja wa wanasayansi wa shirika la afya duniani katika kitengo cha magonjwa ya zinaa.

Miaka michache ijayo, aina hii mpya ya kisonono itakuwa sugu dhidhi ya dawa zote ambazo tunazo saizi “aliendelea kusema Dk. Manjula Lusti-Narasimhan wakati wa mahojiano na shirika la habari la The Associated Press kabla WHO haijatangaza rasmi hatua na mwongozo mpya wa kukabiliana na tishio la aina hii mpya ya kisonono.

Inakisiwa watu milioni 106 ulimwenguni kote huathiriwa na ugonjwa wa kisonono kila mwaka.Ugonjwa wa kisonono pia huongeza hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa Virusi vya Ukimwi (VVU).

“Ugonjwa sugu wa kisonono sio tatizo la bara la Ulaya au Afrika pekee bali ni tatizo la dunia nzima kwa sasa,’'alinukuliwa akisema Dk. Manjula Lusti-Narasimhan.

Kwa mara ya kwanza, vimelea sugu vya ugonjwa wa kisonono dhidhi ya dawa aina ya cephalosporins viliripotiwa katika nchi ya Japan, ikifuatiwa na Uingereza, Hongkong na Norway.

Wanasayansi wanaamini matumizi mabaya ya dawa aina ya antibiotiki pamoja na uwezo wa vimelea vya ugonjwa wa kisonono kubadilika na kuzoea mazingira mapya ndio chanzo kikuu cha kutokea kwa ugonjwa sugu wa kisonono na hivyo muda si mrefu ugonjwa huu utakuwa janga kubwa dunia nzima kama hatua za haraka hazitachukuliwa.

Kuna uwezekano wa vimelea hivi sugu vya kisonono vinasambaa kwa sasa duniani bila kuweza kugundulika kutokana na nchi nyingi kutokuwa na ufuatiliaji na utunzaji kumbukumbu mzuri wa wagonjwa wake.

Shirika la afya duniani limesema nchi zinatakiwa kuongeza ufuatiliaji wa wagonjwa wake pamoja na kudhibiti matumizi holela ya dawa za antibiotiki mpaka pale taarifa kamili za ugonjwa huu zitakapojulikana.

“Elimu ya masuala ya kujamiana pamoja na matumizi sahihi ya mipira ya kondomu inahitajika ili kutokomeza kabisa ugonjwa huu sugu wa kisonono. Hatuwezi kuutokomeza kabisa ugonjwa huu bali tunaweza kuzuia usambaaji wake,”alisema Dk. Manjula Lusti-Narasimhan.

 

10 Apr 2017

Utafiti mpya uliofanyika nchini Marekani umesema ya kwamba kula machungwa na zabibu kunaweza kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi (Stroke).

Utafiti huo uliangalia faida za matunda chachu (Citrus Fruit) pekee kwa mara ya kwanza tofauti na tafiti nyingi ambazo tumezizoea zinazoangalia umuhimu wa matunda na mboga za majani kwa afya kiujumla.

Utafiti huu umehusisha maelfu ya wanawake wanaoshiriki katika tafiti ya manesi Nurse’s Health Study lakini wataalamu wanaamini faida hizo za machungwa na zabibu pia zinapatikana kwa wanaume.

Timu ya watafiti katika chuo cha Norwich Medical School katika Chuo Kikuu cha East Anglia wamechunguza umuhimu wa kemikali aina ya flavonoids ambayo ni jamii ya antioxidant (kemikali zinauwa kemikali hatari za kwenye mwili) inayopatikana katika matunda, mboga za majani, chocolate nyeusi na wine nyekundu.

Utafiti huu ulifuatilia takwimu za miaka 14 za wanawake 69,222 ambao walikuwa wakishirki katika tafiti kwa kuandika kiwango chao cha kula matunda na mboga za majani kwa kila kipindi cha miaka 4.

Timu hiyo ya utafiti iliangalia uhusiano wa aina sita ya flavonoids - flavanones, anthocyanins, flavan-3-ols, flavonoid polymers, flavonols na flavones na hatari ya aina mbalimbali za kiharusi kama Ischaemic, Hemorrhagic na Total Stroke.

Ilionekana wanawake waliokula kiwango kikubwa cha flavanones kwenye matunda chachu walikuwa na asilimia 19 ya uwezekano wa kupunguza kiharusi kulinganisha na wanawake ambao walikula kiwango kidogo cha matunda hayo.

Kiwango kikubwa cha flavanones kilikuwa 45mg kwa siku kulinganisha na kiwango kidogo cha 25mg kwa siku.

Utafiti huu ulichapishwa katika jarida la Medical Journal Stroke umesema flavanones hupatikana kwa asilimia 82 kwenye machungwa na juisi ya machungwa na hupatikana kwa asilimia 14 kwenye zabibu na juisi ya zabibu. Hata hivyo watafiti hao wamesema kwa wale wenye kusudio la kuongeza kiwango kikubwa cha flavanones itawalazimu kula tunda la chungwa kwa wingi na si juisi za machungwa zinazotengenezwa kiwandani kutokana na kiwango kikubwa cha sukari kinachopatikana katika juisi hizo za viwandani.

07 Apr 2017

Wanaume wanaovuta bangi wapo kwenye hatari ya kupata watoto wenye matatizo ya kiakili kama kutomudu masomo ya darasani, wamesema wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Pennsylvania, nchini Marekani. Utafiti huu mpya umesema ya kwamba madhara ya bangi kwenye vina saba (DNA) yanaweza kurithishwa kupitia shahawa na hivyo kuathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto.

Cha kushangaza ni kwamba madhara haya ya bangi kwenye ubongo wa mtoto huonekana sana kwa watoto wa kiume kuliko watoto wa kike au mtoto yoyote yule atakayezaliwa na mama ambaye alikuwa mvutaji bangi.

Wakati wanasayansi bado wanajaribu kutafuta ni kwa muda gani athari za bangi kwenye vina saba zinaweza kuwepo hata kama mvutaji ameacha kuvuta bangi miaka mingi iliyopita lakini tafiti hii ni muendelezo wa tafiti za hapo awali ambazo ziliwahi kueleza kuhusu madhara ya bangi kwenye vina saba kwa miaka mingi hata kama mvutaji ameacha kuvuta bangi. Profesa R. Christopher Pierce, mtaalamu wa sayansi ya akili (Neuroscience) katika chuo kikuu cha Pennsylvania pamoja na timu yake ya watafiti ambayo ndio walitafiti nadharia (hypothesis) hii ya kwamba ‘’uvutaji bangi huathiri vina saba kwa miaka mingi hata baada ya mtumiaji bangi kuacha kuvuta bangi’’.

Watafiti hawa walipima nadharia yao kwa kutafiti panya 16 wanaume ambao walipewa uwezo wa kutumia bangi wao wenyewe kwa kuwachanganyia bangi kwenye maji yao ya kunywa kwa muda wa siku 60.Panya wengine wa kiume walikunywa maji ya kawaida kwa muda huo wa siku 60.

Panya hawa walijamiana na panya majike na baadae kugundulika ya kwamba utumiaji bangi kwa mzazi hauna uhusiano wowote na uzito wa mtoto anaezaliwa, jinsia au ukuaji wa mtoto.

Hata hivyo kati ya watoto wote wa panya 46 waliozaliwa, watoto wa kiume ambao walitokana na wazazi ambao walitumia maji yenye mchanganyiko wa bangi walionekana kuwa na matatizo ya kiakili. Baada ya uchunguzi zaidi, watafiti hawa waligundua ya kwamba jeni (genes) ambazo ni muhimu kwa kumbukumbu za kiumbe zimebadilishwa (mutation) kutokana na matumizi ya bangi.

Asilimia ya watoto wa kiume ambao baba zao walitumia maji yaliyochanganya na bangi walikuwa na kiwango kidogo cha molekuli (molecule) aina ya D-serine ambayo ni muhimu kwa ajili ya kumbukumbu. Baada ya watafiti hawa kuwachoma molekuli hii ya D-serine kwenye sehemu ya ubongo ya watoto wa kiume wa panya inayojulikana kama hippocampus kutokana kuwa na kiwango kidogo cha D-serine, waligundua ya kwamba uwezo wao wa uelewa uliongezeka kwa kiwango kikubwa tofauti na hapo awali.

07 Apr 2017

Wanasayansi wamegundua seli asilia (Stem Cells) kwenye mayai ya mwanamke (Ovaries) ambazo baadae zinaweza kutengeneza kiwango kikubwa kisicho na ukomo cha mayai ya uzazi ya awali (Oocytes).

Kwa kawaida mwanamke huwa na mayai mengi ya uzazi ya awali (Oocytes) wakati akiwa kwenye tumbo la mamake yaani bado akiwa kijusi (Fetus) ambapo anakadiriwa kuwa na mayai milioni 7, na mayai hayo kupungua hadi kuwa milioni 1 wakati anazaliwa na kufikia mayai 300,000 wakati wa kuvunja ungo au kubaleghe.

Mayai haya huisha kabisa akifika umri wa miaka 40 hadi miaka ya mwanzoni ya 50 (yaani kipindi cha ukomo wa kupata hedhi), na hii ndio huchangia mwanamke kutokuwa na uwezo tena wa kushika mimba ambao ni tofauti na wanaume ambao bado wanakuwa na uwezo wa kutoa shahawa hata wakiwa wazee.

Utafiti huo uliofanywa na wanasayansi katika hospitali ya Massacheutts nchini Marekani ambapo wanasayansi hao waliweza kuzitenganisha seli hizo kwenye maabara na kutengeneza mayai ambayo wamesema yanauwezo wa kurutubishwa (fertilized) na kuwa mimba.

Kutokana na utafiti huu, wataalamu wengi wa afya wamesema matokeo ya utafiti huu yatabadilisha kabisa tiba ya ugumba kwa wale wanawake wasioweza kushika mimba na pia yanaweza kusaidia wanawake kuwa na uwezo wa kushika mimba kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.

24 Apr 2012

Kimengenyo (enzyme) ambacho ni protini aina ya CYP2E1 kimegundulika kuwa ndio chanzo kinachochangia wanawake kupata saratani ya matiti kwa wanawake wanaotumia vilevi. Kwa muda mrefu wanasayansi walikuwa wakitafuta uthibitisho wa uhusiano wa kunywa pombe na saratani ya matiti, lakini sasa wameweza kupata uhusiano huo. Protini hii hupatikana kwenye matiti ya wanawake na hivyo kuwaweka kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti kama watakuwa wanakunywa sana vilevi kama pombe, whiskey, wine na nk.

Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Autonomous University of the State of Morelos cha nchini Mexico, umeonyesha ya kwamba protini hiyo ya aina ya CYP2E1 inauwezo wa kukivunja vunja kilewesho (ethanol) na kusababisha kutolewa kwa kemikali hatari zinazojulikana kama free radicals.

Watafiti hao wamesema ugunduzi wao utasaidia katika kuvumbua kipimo kitakachosaidia kujua ni wanawake gani walio na protini hii ya CYP2E1 na hivyo kuwasaidia kujikinga dhidhi ya saratani ya matiti.

Kemikali hizi hatari uhusishwa na kutokea kwa baadhi ya magonjwa kama saratani mbalimbali, ugonjwa wa kisukari, uharibifu wa mishipa ya damu aina ya ateri (arteries), kuchangia mtu kuzeeka na nk.

Swali kuu walilojiuliza watafiti wakati wa utafiti huo ni , Je kuwa na protini hii ya CYP2E1 kwa wingi huchangia mwanamke kupata ethanol-induced toxicity na hivyo kumhatarisha kupata saratani ya matiti?

Matokeo yetu yalionyesha ya kwamba seli za kutoka katika matiti ya mwanamke (mammary cells) zilizowekwa kilewesho cha aina ya ethanol, hutoa kemikali hatari kwa wingi, husababisha kuwepo kwa oxidative stress, huharakisha ufanyaji kazi wa seli na hivyo kuongeza kiwango cha ukuaji wa seli hizi kwa wingi na kusababisha saratani ya matiti” alisema Profesa Maria de Lourdes Rodriguez-Fragoso, kutoka chuo kikuu cha The Autonomous University of the State of Morelos cha nchini Mexico.

“Kama wewe ni mwanamke ambaye una kiwango kikubwa cha protini hii ya CYP2E1 katika matiti yako na unakunywa pombe basi utakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti ikilinganishwa na mwanamke ambaye ana kiwango kidogo cha protini hii katika matiti yake.” Aliendelea kusema Profesa Maria de Lourdes Rodriguez-Fragoso.

Uchunguzi uliofanywa kutoka kwenye tishu za matiti ya wanawake wenye afya njema ambao wamefanyiwa upasuaji wa kukuza matiti yao umeonyesha viwango tofauti vya protini hii katika wanawake hawa.

“Hii inamaanisha ya kwamba wanawake wanatafautiana kwa umengenywaji wa pombe na hivyo inabidi kila mwanamke kuchukua hatua tofauti katika kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti” Alisema tena Profesa Maria de Lourdes Rodriguez-Fragoso.

Protini hii ya aina ya CYP2E1 hupatikana katika seli za matiti ya mwanamke zinazojulikana kama mammary epithelial cells ambapo pia ndio chanzo cha seli/chembechembe nyingi za saratani ya matiti na kusababisha watafiti hao kuanza kushuku uhusiano wake na saratani ya matiti.

Ili kuthibitisha shauku yao kwamba protini hii husababisha saratani ya matiti, watafiti hao walichukua tishu za matiti zilizo na viwango tofauti vya CYP2E1 na kuziweka kwenye pombe. Matokeo yalionyesha ya kwamba seli zenye kiwango kidogo cha protini aina ya CYP2E1 hazikuathiriwa sana ikilinganishwa na seli ambazo zilikuwa na kiwango kikubwa cha protini hiyo.

Utafiti huu ni ushindi mkubwa katika vita dhidhi ya saratani ya matiti kwani utasaidia kupunguza kiwango cha saratani hii kwa wanawake.

Kwa makala zaidi kuhusu saratani ya matiti na athari zake bonyeza hapa Saratani ya matiti.

 

28 Feb 2012

Utafiti uliofanywa nchini Marekani hivi karibuni umetoa matokeo ya kushangaza kwa kusema ya kwamba matumizi ya dawa za usingizi huongeza hatari ya kupata saratani pamoja na mtu kufa mapema. Utafiti huo umesema wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa ya usingizi wako kwenye hatari ya kupata magonjwa ya saratani.

Utafiti huo ambao ulifanywa na watafiti wa kitengo cha usingizi katika kituo cha Jackson Hole Centre for Preventive Medicine in Wyoming and the Scripps Clinic Viterbi Family Sleep Centre kilichopo jijini California nchini Marekani ili kuangalia hatima ya watu wanaotumia dawa za usingizi aina ya benzodiazepines kama temazepam, diazepam (valium), dawa mpya aina ya zolpidem, zopiclone, zaleplon, dawa za jamii ya barbiturates na zile zinazotumiwa kutibu mcharuko mwili (allergy) na ambazo huleta usingizi.

Matokeo ya utafiti huo yanasema wale wanaotumia dawa za usingizi (Hypnotics) walizoandikiwa na Daktari wako kwenye hatari ya 4.6 kufa ndani ya miaka 2 na nusu ukilinganisha na watu ambao hawatumii dawa za usingizi. Wale ambao wanatumia dozi ndogo ya dawa za usingizi yaani wanaotumia wastani wa vidonge 4-18 kwa mwaka wako kwenye hatari ya mara 3.6 zaidi kufa kulinganisha na wale ambao hawatumii dawa za usingizi.

Wale wanaotumia dozi kubwa yaani vidonge 18-132 kwa mwaka wako kwenye hatari kubwa ya mara 4.4 zaidi kufa, na wale wanaotumia zaidi ya vidonge 132 kwa mwaka wako kwenye hatari ya mara 5.3 zaidi kufa kulinganisha na wale ambao hawatumii dawa za usingizi. Asilimia 93 ya wale walioshiriki katika utafiti huu walikuwa ni wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa za usingizi.

Pia wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa hizi wako kwenye hatari ya asilimia 35 kupata saratani kubwa. Kwa wale wanaotumia dawa aina ya zolpidem wako kwenye hatari ya mara 5.7 kufa huku wale wanaotumia dawa aina ya temazepam wako kwenye hatari ya mara 6.7 kufa kulinganisha na wale wasiotumia dawa za usingizi.

Utafiti huo umesema wale walio kwenye hatari ya madhara haya ya dawa za usingizi ni wale walio katika umri wa miaka 18-55 ingawa sababu halisi haikuelezwa katika matokeo ya utafiti huo. Wagonjwa 10,500 wanaotumia dawa za usingizi walishiriki katika utafiti huo wakilinganishwa na watu 23,500 ambao hawatumii dawa za usingizi walioshiriki katika utafiti huo.

Watafiti hao walisema tiba ya kutotumia dawa yaani ya tiba ya utambuzi wa tabia (cognitive behavior therapy) inaweza kuwa na manufaa zaidi kuliko matumizi ya dawa za usingizi na hata matumizi ya dawa za usingizi kwa muda mfupi yanapaswa kuangaliwa kwa makini. Watafiti hao wakiandika katika jarida la British Medical Journal walisema “Faida chache zinazopatikana kutokana na matumizi ya dawa za usingizi ambazo zilitafitiwa kwa kina na makundi ambayo hayana maslahi yoyote na dawa hizi haziwezi kuhalalisha madhara yatokanayo na matumizi ya dawa hizi za usingizi”.

Matokeo ya utafiti huu ni changamoto kubwa katika fani ya afya hasa ukizingatia ya kwamba watu wengi hutumia dawa za usingizi kutokana na kupatikana kiurahisi katika maduka mbalimbali ya dawa katika Afrika Mashariki. Pia ni changamoto kubwa sana kutokana na dawa hizi kutumika wakati wa upasuaji, kutibu magonjwa ya akili, kutibu mcharuko mwili, msongo wa mawazo na hata kwa wazee.

Kulingana na matokeo haya ni vizuri kuangalia upya matumizi ya dawa za usingizi na utafiti zaidi unahitajika kufanyika kabla ya kutoa msimamo kuhusu matumizi ya dawa za usingizi.

11 Jul 2011

Watafiti nchini China wana matarajio makubwa kwamba nguruwe wanaozalishwa kijenetikia (Genetic modified cloned piglets) wanaweza kuwa suluhisho la matatizo ya viungo ambavyo vitaweza kupandikizwa kwa binadamu wenye kuhitaji viungo kutokana na viungo vyao kushindwa kufanya kazi baada ya kuathiriwa na magonjwa yasiyotibika.

Mkuu wa kitengo cha utafiti cha Metabolic disease research centre cha  Nanjing University Nchini China bwana Zhao Zijian amesema “Nguruwe hawa wa kijenetikia wanaleta matumaini mapya kwa wagonjwa wanaohitaji viungo ambao wamekosa mtu wa kuwapa”.

Kundi la watafiti hao limekuwa likifanya utafiti kuhusu teknolojia ya GM tokea mwaka 1998 wakiwa na matarajio ya kubadilisha viashiria vya asili (genes) kwa nguruwe vinavyosababisha binadamu kukataa viungo kutoka kwa nguruwe.

‘’ Kama vile binadamu walivyo na makundi tofauti ya damu ambapo mtu  hawezi kupewa damu kutoka kwa mtu mwengine mwenye kundi tofauti ambalo haliendani na damu yake, basi viungo vya nguruwe vilikataliwa na binadamu kabla sijabadilisha chembechembe za sukari na kiasilia cha asili tofauti” alisema bwana Dai Yifan, naibu mkurugenzi katika kitengo hicho cha utafiti.

Bwana Dai ambaye alifanikiwa kuzalisha nguruwe hawa wa kijenetikia kwenye maabara ya Revivicor Inc nchini Marekani na kuchukua chembechembe au seli za hawa nguruwe na kurudi nazo nchini China mwaka jana ambapo anatarajia kuzalisha maelfu ya nguruwe wa aina hiyo nchini humo.

Kundi la kwanza la nguruwe hawa litazaliwa ndani ya miezi mitano au sita katika jiji la Nanjing lililopo katika mkoa wa Jiangsu. Kundi hilo litafanyiwa utafiti zaidi ili kuweza kujua kama kweli  kuna uwezekano wa kutumia viungo vyake kama moyo, figo, ini kwa binadamu bila madhara yoyote.

“Kwa muda huu, wanasanyansi  wanatengeneza sehemu maalum ya kufanyia upasuaji nguruwe hawa ambayo  itakuwa huru kutokana na virusi  ili nguruwe hawa wasipate maradhi ambayo yanaweza kumuambukiza binadamu” alisema bwana Dai.

Wakati huo huo, madaktari wa upasuaji wameonyesha wasiwasi kutokana na utafiti huo kwa sababu,  “Wanasayansi wanaufahamu mdogo kuhusu virusi vya nguruwe hivyo inaweza kuleta janga kubwa kama viungo vya nguruwe vitapandikizwa kwa binadamu” alisema Dr Li Shichun, bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya ini kutoka hospitali ya Beijing YuAn Hospital.

Viungo kutoka kwa nguruwe vimekuwa vikifanyiwa utafiti toka mwaka 2002 nchini Marekani  ambapo vimeweza kurefusha maisha ya ngedere/tumbili kwa muda wa siku 400. Hii inaweza kuwa njia mojawapo ya kurefusha muda wa mgonjwa wakati anasubiri kupatikana kwa mtu ambaye ana viungo sahihi ambavyo vitaweza kupandikizwa kwake.

Wanasayansi kutoka kitengo cha Chinese Academy of Agricultural sciences kwa mara ya kwanza walizalisha nguruwe hawa wa kijenetikia (GM pigs) mwezi wa Novemba 2010.  Utafiti kwa binadamu haujafanyika sehemu yoyote duniani.

“Kutokana na uhaba wa viungo,  ni watu 10,000  tu kati ya milioni moja wenye maradhi ya figo na watu 300,000 wenye maradhi ya ini wanaosubiri viungo ndio wanaobahatika kupata viungo na hivyo kuokoa maisha yao kila mwaka nchini china”, alisema naibu waziri wa afya wa China, mheshimiwa Huang Jiefu.

“Watafiti  wa Nanjing University wanatarajia kuomba kibali cha kufanya utafiti wao kwa binadamu wakati nguruwe hao watakapokuwa wakubwa”, alisema bwana Dai.

Wanasayansi wamesema hawajui kama serikali ya China itatoa kibali cha kuruhusu utafiti wa upandikizwaji wa viungo vya nguruwe kwa binadamu.

Ni matarajio yetu ya kwamba utafiti huu utaleta mageuzi makubwa katika tiba hasa ya magonjwa sugu kwani itakuwa rahisi kupata viungo lakini kuna umuhimu wa kufanya utafiti wa kina  kuhusu virusi vya nguruwe na pia kujiridhisha na matokeo ya utafiti wenyewe kwa binadamu. Hii ni changamoto pia kwa wanasayansi wa Tanzania kufanya utafiti katika nyanja hizi.

02 Jul 2011

Yawezekana wanafunzi wasikubaliane na maelezo haya lakini wanasayansi wanatuthibitishia kuwa usingizi ni muhimu mno kwa mwanadamu kuweza kujifunza na kukumbuka alichojifunza.

Uwezo wa utendaji kazi wa usingizi umekuwa fumbo kwa muda mrefu lakini watafiti kadhaa wamekusanya ushahidi kuonesha kuwa kupata usingizi kwa masaa kadhaa husaidia sana katika kujifunza na kuongeza uwezo wa ubongo katika kutunza kumbukumbu.

Walau tafiti mpya mbili tofauti zinaonesha kuwa usingizi unahusika kwa kiasi kikubwa katika kujenga, kuhifadhi na kuzindua kumbukumbu na pia kuandaa ubongo kwa ajili ya kupokea kitu kipya wakati wa kujifunza.

Watafiti wakiongozwa na Paul Shaw wa Chuo Kikuu cha Washington huko St. Louis wanaripoti katika jarida la Science la June mwaka huu kuwa kitendo cha kugusa na kusisimua nyuroni kadhaa zilizopo katika sehemu ya juu ya ubongo wa aina fulani ya nzi waliotumika kwenye huo utafiti kilisababisha wadudu hao kupata usingizi.

Watafiti wanasema kuwa, kusisimua seli za ubongo zinazochochea usingizi hufanya kumbukumbu za muda mfupi (short-term memories) kubadilika na kuwa za muda mrefu (long-term memories).

Katika utafiti mwingine tofauti uliofanywa na wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison huko nchini Marekani na kuchapishwa katika jarida hilo hilo la Science, watafiti walionesha ushahidi kuwa wakati wa usingizi, mawasiliano katika ya seli mbalimbali za ubongo huchujwa kwa kiasi fulani.

Walionesha pia kuwa kuna ushahidi usio wa moja kwa moja wa kitendo hiki cha kuchuja mawasiliano kinachofanywa kati ya seli za ubongo husaidia kuandaa ubongo kupokea mafundisho na taarifa mpya ya siku inayofuata. Hata hivyo watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Washington wao walionesha ushahidi wa moja kwa moja kuhusu suala hilo.

Kurasa 1 ya 2