Image

Kuyafanya Meno Yenye Rangi kuwa Meupe (Teeth Whitening)

Wakati wa muongo uliopita mahitaji ya kuboresha muonekano au kurembesha meno yameongezeka kwa kiwango kikubwa hasa katika nchi zilizoendelea. Hii imechochewa na kupatikana kemikali mpya za meno (dental meterials) na vifaa kwa kasi ikiendana na kuboresha vile vya zamani. Sehemu nyingine iliyosababisha madaktari na mainjinia wa meno kuyafanya meno kuwa meupe ni sehemu ya fani ya taaluma ya meno chini ya urembeshaji wa meno, fani hii uhusika na kuboresha muonekano wa meno hasa yale yanayoonekana wakati wa kutabasamu na kuongea.

Inahusisha matibabu kama kuyafanya meno yenye rangi kuwa meupe, kunyoosha meno yaliyojipanga vibaya pamoja na kukarabati meno yaliyovunjika na yale yaliyoumbika visivyo (malformed teeth). Huko Uingereza na sehemu nyingine za magharibi wanawake walio wengi wanatumia maelfu ya paundi/euro kuboresha muonekano wa meno yao hali ambayo inaanza pia kuingia huku kwetu.

Nini husababisha meno kugeuka rangi?
Meno kugeuka rangi husababishwa na kimojwapo au muunganiko wa vitu vifutavyo: -

  1. Vyakula na vinywaji kama vile vinyaji vyenye kaboni, wine na sigara.
  2. Utumiaji wa maji yenye kiwango cha juu cha madini aina ya magadi (fluoride) na utumiaji wa magadi katika kulainisha vyakula wakati wa kuandaa vyakula vigumu kama maharage na makande. Utafiti uliofanywa na Prof. Mabelya na wenzake nchini Tanzania umeonesha kuwa kubadilika kwa rangi ya meno kutokana na magadi kwa kiwango kikubwa husababishwa na matumizi ya magadi katika mapishi ya vyakula hasa makande kule maeneo ya mkoa wa Kilimanjaro/Moshi kuliko inavosababishwa na matumizi ya maji.
  3. Maumbile yasiyo sahihi ya sehemu ngumu za jino (enamel and dentine defects). Iwapo sehemu ngumu ya meno imeumbwa ikiwa laini ni rahisi kufyonza rangi na jino kuota likiwa limegeuka rangi au kubadilika baada ya kuota.
  4. Matumizi ya madawa kwa mama mjamzito ambaye tayari meno ya mtoto aliye tumboni yameanza kuumbwa lakini hayajapata madini ya kutosha na hata watoto wachanga ambao meno yao hayajakomaa.
  5. Kufa kwa kiini cha jino hasa kutoka na kujigonga wakati wa ajali au kupigana ngumi usoni (pulp necrosis), jino likigongwa kwa nguvu damu huvuja ndani ya kiini cha jino na baadaye huchachuliwa na kutoa kemikali ambayo hupenya kwenye vitundu vidogo vidogo kwenye dentine na kujidhihirisha kama kijivu, zambarau au hata nyeusi. Hali hii yaweza tokea mapema baada ya kupata ajali lakini wakati mwingine inaweza kuchukua miaka kadhaa hata arobaini kipindi ambapo mtu hakumbuki kuwa aliwahi kutwangwa ngumi.

Kuyafanya meno yenye rangi yasimpendeza mwenye nayo kuwa meupe (Bleaching or teeth whitening)

Huku ni kuyafanya meno yenye rangi kuwa meupe au kuongeza weupe wa yale yenye rangi ya kawaida kufikia kiwango cha weupe atakacho muhitaji kwa kutumia kemikali maalum. Rangi ya kawaida ya meno kwa walio wengi ni uweupe kama wa maziwa (milky white). Rangi yeyote nje ya hiyo si ya kawaida (abnormal color or discoloration).

Kuwa na rangi isiyo ya kwaida hasa kwa meno ya mbele linaweza kuwa tatizo kubwa la urembo na kumsumbua mhusika kisaikolojia. Kuyafanya meno kuwa meupe kumelenga kuwaondolea wahusika tatizo hili japo mafanikio yake yanategemea kiwango cha rangi isiyo ya kawaida.

Kufanya meno kuwa meupe kwa kutumia kemikali, kunaweza kubadili yaliyo na rangi isiyo ya kawaida kutoka yale yaliyoathirika kwa kiwango kidogo mpaka cha kati. 

Kufanya meno yawe meupe kwa kutumia kemikali huunguza (oxidises) rangi ya jino na kuiondoa. Kemikali zinazotumika   zina hydrogen peroxide 30%-35% na baadhi carbamide peroxide 10%. Kemikali hizi huweza kuondoa rangi zilizosababishwa na vyakula, vinywaji, dawa za tetracycline, rangi kidogo iliyotokana na utumiaji wa madini ya magadi kwenye vyakula au kwenye maji (mild fluorosis) na meno yenye rangi ya njano au kijivu itokanayo na umri kuwa mkubwa. Inaweza pia kuondoa rangi itokanayo na uvutaji wa sigara na matumizi ya ugoro.

Kwa wavutaji wa sigara sharti waache pindi watumiapo kemikali hizi kwani muunganiko wa hydrogen peroxide na kemikali zilizopo kwenye moshi wa sigara unahisiwa kuongeza madhara zaidi ambayo tayari moshi wa sigara husababisha kwenye mwili wa binadamu. Haishauriwi kwa akina mama wanaonyonyesha kutumia dawa hizi pamoja na kwamba hakuna madhara yanayojulikana mpaka sasa. Kuboresha weupe kwa kutumia chemikali


Kupiga meno viraka (Veneering)
Hii hufanyika kwa kuondoa sehemu ndogo ya juu ya jino kwenye enamel kama 0.5-1mm na baadaye kupandika dawa yenye rangi nyeupe kulingana na mgonjwa anavyotaka mwenyewe. Picha inayonesha meno yaliyobadlika rangi kutokana na magadi kabla na baada ya kupigwa viraka

 
Kabla ya kiraka                                                        Baada ya kupigwa kiraka (veneer)

Kumbuka: kuna rangi zaidi ya 26 nyeupe ambazo miongoni mwake mgonjwa anaweza kuchagua anayoitaka

Imesomwa mara 18965 Imehaririwa Jumatano, 31 Oktoba 2018 14:23
Dr. Augustine Rukoma

Dr Dr. Augustine Rukoma ni daktari na mtaalamu wa meno, anapenda kutumia muda wake wa ziada kuandika makala na kubadilishana mawazo juu ya afya ya kinywa na Meno.

rukomadentalanswers.blogspot.com | Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana