Image

Matumizi Sahihi na Utaratibu wa Kuanza Dawa za Kufubaza Makali ya Virusi vya Ukimwi - ARV

 

Moja kati ya vitu vya msingi vya kuzingatia ukiwa muathirika wa ugonjwa wa VVU/UKIMWI ni matumizi sahihi ya dawa.Watu wengi wamepotoshwa na taarifa za uongo kuwa  dawa hizi hupunguza nguvu za kiume hivyo wagonjwa wengi wa UKIMWI hawatumii dawa  hizi na badala yake hutumia mitishamba au kutokutumia dawa kabisa.

Tafiti nyingi zimefanyika na kuonyesha kwamba dawa hizi zina uwezo mkubwa wa kuzuia magonjwa yatokanayo na UKIMWI na kuzuia vifo. Aidha dawa  hizi zimeonyosha uwezo mkubwa wa kupunguza maambukizi ya mama kwa mtoto.Matumizi ya dawa  za kufubaza makali ya virusi vya VVU/UKIMWI kwa waathirika wa ugonjwa huu yanahusishwa na  kupungua kwa hatari ya kueneza maambukizi ya virusi vya VVU/UKIMWI wakati wa kushiriki tendo la ndo  kwa sababu ya uwezo wake wa kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI.

KUKMBUKA dawa hizi sio tiba ya virusi vya VVU/UKIMWI.

Utaratibu wa Kuanza Dawa

Kulingana na miongozo ya matibabu ya VVU/UKIMWI anashauriwa kuanza dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI mara tu anapogundulika kuwa ni muathirika wa virusi vya VVU/UKIMWI na kupewa ushauri nasaha. Hii husaidia sana kupunguza makali ya virusi hivi.

Utaratibu wa kuanza dawa huambatana na kujisajili kwenye za kliniki za CTC ambazo zipo kwenye takribani vituo vyote vya afya nchini. Ukishajisajili utapewa namba pamoja na kadi ambayo itakuwa na taarifa zako zote muhimu kama muda au tarehe ya kumuona dakatri, aina na kiwango cha dawa  unachotumia , wingi wa virusi vya VVU kwenye damu (viral load) na kiwango cha CD4.

Endapo uligundulika na virusi vya VVU/UKIMWI na umeshaanza kupata magonjwa nyemelezi, basi utaanza matibabu ya magonjwa hayo na kuanzishiwa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi ndani ya wiki mbili.

Kuna baadhi ya magonjwa ikiwemo kifua kikuu (PTB)   pamoja na ugonjwa wa kukakamaa shingo (Cryptococcoal Meningitis) huwa kuanza kutumia dawa haraka sio vizuri kwani inaongeza hatari ya kupata mchafuko wa kinga ya mwili (Immune Reconstitution Inflammatory Syndrome- IRIS) ambayo huzidisha dalili za magonjwa nyemelezi.

Hali hii hutokea kwa sababu madawa ya kufubaza virusi vya UKIMWI husaidia kuongeza kinga ya mwili na hivyo mwili huanza vita na magonjwa nyemelezi ambayo mwanzo mwili ulikuwa hauna uwezo wa kuyadhiti hii huleta mchafuko wa kinga ya mwili na kuzidisha  dalili zilizopo au kusababisha dalili mpya za magonjwa nyemelezi.

Matumizi Sahihi ya Dawa za Kufubaza Makali ya Virusi vya VVU/UKIMWI (ARV)

Matumizi sahihi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya VVU/UKIMWI ni muhimu sana kwani usipofanya hivyo unaweza kupata madhara makubwa zaidi ikiwemo ugonjwa wa UKIMWI kuja kwa kasi zaidi, hali hii huchangia sana mgonjwa kupoteza maisha. Hivyo hakikisha unapata maelekezo yote kuhusu utumiaji wa dawa kutoka kwa daktari wako.

Dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI zipo kwenye makundi mbalimbali. Tafiti tofauti pamoja na miongozo ya matibabu ya VVU/UKIMWI zimependekeza matumizi ya dawa zifuatazo; Tenofovir disoproxil fumarate(TDF), Lamuvidine(3TC), Dultegravir(DTG) kama dawa za kwanza dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI (first line treatment).

Yapo makundi mbalimbali ya mchanganyiko wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya VVU/UKIMWI ambayo  yanaweza kutumika kulingana na kundi analotoka mgonjwa  mfano watoto wadogo, mama mjamzito au kulingana na jinsi ambavyo dawa hizi  hufanya kazi kwa mtu binafsi n.k

Dawa hizi za mchanganyiko hupatikana kama dawa moja  ambayo humezwa kila siku. Dawa hii ya mchanganyiko wa madawa mbalimbali ina nguvu sana hivyo unashauriwa kula lishe bora wakati wote ili kupunguza maudhi madogo madogo yanayotokana na dawa hizi.

Hata hivyo,imeripotiwa kuwa baadhi ya waathirika hupata madhara kutokana na matumizi ya dawa hizi zilizochanganywa  kwa pamoja, endapo mgonjwa atapata madhara ya dawa hizi, basi anashauriwa kumuona daktari haraka iwezekanavyo kwa ajili ya uchunguzi wa kina ili kugundua  ni aina gani  ya dawa inayomsababishia mgonjwa madhara.

Pindi unapougua epuka kununua madawa na kutumia bila kumuona daktari wako. Hii ni kwa sababu kuna baadhi ya dawa huingiliana na dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI katika utendaji kazi hivyo hupelekea kupungua kwa nguvu ya dawa au dawa kubaki mwilini kwa muda mrefu sana (toxicity). Mambo yote hayo tajwa yana madhara kwa mtumiaji.

Pia unashauriwa kupunguza na kuacha unywaji wa pombe.

Muhimu: Hakikisha unameza dawa kwa kufuata maelekezo ya daktari na epuka kuruka ruka kumeza dawa au utoro wa kuhurudhia kliniki ili kuepuka  madhara  zaidi.

 

 

Imesomwa mara 27728 Imehaririwa Jumanne, 13 Aprili 2021 22:53
TanzMED Admin

TanzMED ni mjumuiko wa wataalamu wa fani mbalimbali za Afya na IT wa kitanzania ambao wamejitoa katika kuhakikisha kuwa jamii ya kitanzania na Afrika kwa ujumla inafaidika kwa kupata habari na ushauri juu ya masuala ya afya yanayozunguka jamii hizo.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.