Image

Katika hali inayoweza kutafsiriwa kuwa ni hatua nzuri katika vita dhidi ya VVU, tafiti zilizofanywa na watafiti huko Marekani na Uingereza zimeonesha kuwa unywaji wa chai ya kijani (green tea) waweza kuwa na manufaa makubwa katika kuzuia maambukizi dhidi ya VVU.

Matokeo ya awali ya tafiti hizo ambayo yamechapishwa katika jarida la tafiti lijulikanalo kama Journal of Allergy and Clinical Immunology yameonesha kuwa chai ya kijani ina kiasili ambacho kina uwezo wa kuzuia VVU kuzaliana kwa wingi ndani ya damu ya muathirika.

Utafiti wa awali uliofanywa katika maabara umeonesha kuwa kiasili hicho kijulikanacho kitaalamu kama Epigallocatechin gallate (EGCG) kina uwezo wa kunata katika chembe chembe nyeupe za damu zijulikanazo kama CD4 ambazo kwa kawaida hutumiwa na VVU kuzaliana na hivyo kuzuia uwezekano wa VVU kuingia ndani ya chembe chembe hizo na hivyo kupunguza kasi yao ya kuzaliana.

Mmojawapo wa watafiti hao, Profesa Mike Williamson wa Chuo Kikuu cha Sheffield cha nchini Uingereza alisema katika mahojiano kuwa, utafiti wao umeonesha kuwa unywaji wa chai ya kijani unaweza kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi ya VVU na pia kupunguza uwezekano wa VVU kuzaliana na kuongezeka katika damu ya muathirika.

Hata hivyo watafiti hao wameonya kuwa ni mapema mno kwa jamii kuanza kuyatumia matokeo ya utafiti huo na kwamba tafiti zaidi hususani zinazohusisha binadamu au wanyama zinapaswa kufanywa ili kuyapa matokeo ya utafiti huo uzito unaostahili.

Waliongeza kuwa imeonekana mara nyingi viasili vinavyoweza kuonesha matokeo mazuri katika maabara, vinaweza visilete matokeo yanayokusudiwa kama utafiti huohuo utafanywa kwa binadamu ama wanyama.

Hawakusita kuonesha kuwa matokeo ya utafiti wao yasichukuliwe kuwa chai ya kijani ni tiba au njia ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU badala yake inaweza kutumika kama njia nyongeza ya kusaidia dawa za kupambana na VVU na hivyo kupunguza kasi ya kuzaliana kwa VVU.

Watafiti nchini Marekani wameonesha uwezekano wa bakteria wanaosababisha vidonda vya tumbo (gastric ulcers) kuhusishwa na kusababisha ugonjwa wa Parkinson. Kwa mujibu wa taarifa ya watafiti hao, ilionekana kuwa panya waliotumika kwa ajili ya utafiti huo walionesha kuwa na dalili za ugonjwa wa Parkinson baada ya kudungwa bakteria wa Helicobacter pylori.

“Maambukizi ya bakteria hawa kwa panya yalihusika kwa kiasi kikubwa kuleta dalili hizo’ Ilisema sehemu ya ripoti ya utafiti huo iliyowasilishwa katika mkutano wa chama cha wanamikrobaiolojia wa Marekani (the American Society for Microbiology).

Ugonjwa wa Parkinson ni ugonjwa unaoathiri ubongo na kumfanya mgonjwa kutetemeka, kupungua kwa uwezo wa kutenda na kutembea kwa kuchechemea.

Katika utafiti huo, wanasayansi waliwadunga na kuwaambukiza bateria aina ya H. pylori panya waliokuwa na umri wa kati, wakiwakilisha binadamu wenye umri kati ya miaka 55 hadi 65, umri ambao ugonjwa wa Parkinson hujitokeza zaidi. Baada ya kuwafuatilia kwa kipindi cha miezi sita, panya hawa walionesha kuwa na dalili zinazofanana na zile za Ugonjwa wa Parkinson kama vile kupungua kwa uwezo wa kujongea, na kupungua katika ubongo kwa kiwango cha dopamine, kemikali inayohusika, pamoja na mambo mengine, na kusaidia uwezo wa kujongea wa mwili na viungo vyake. Hata hivyo mabadiliko haya hayakuonekana kwa panya waliokuwa na umri wa kati au panya wachanga.

Mmoja wa watafiti, Dr Traci Testerman, wa Chuo kikuu cha Sayansi za Afya cha jimbo la Louisiana alisema kuwa matokeo ya utafiti huo yametoa mwanga wa kuwepo uwezekano wa bakteria wa H. pylori kuhusika katika kusababisha ugonjwa wa Parkinson kwa binadamu. Aliongeza matokeo kuwa panya wazee waliathirika zaidi kuliko panya wachanga yanaonesha kuwa kitendo cha kuzeeka kinaongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa Parkinson kwa panya kama ilivyo pia kwa binadamu.

Page 2 of 2