Aidha watafiti wanaamini kuwa sababu iliyowafanya panya wale kupata ugonjwa wa Parkinson baada ya kudungwa bakteria wa H.pylori ni kuwa bakteria hao huzalisha aina ya kemikali ambayo ni sumu kwa ubongo wa mnyama. Wanasema bakteria hawa walionesha uwezo wa kutumia lijamu (cholesterol) kutoka katika seli za mwili wa panya na kuongeza kiasili cha sukari kutengeneza kemikali mpya ambayo hufanana sana kimuundo na kemikali nyingine inayopatikana katika baadhi ya mimea inayohusishwa na kusababisha ugonjwa wa Parkinson.
Hata hivyo watafiti wanasema, matibabu ya H.pylori kwa mgonjwa wa Parkinson ambaye tayari ameshaingia katika hatua za mwisho za ugonjwa huo hayasaidii kuleta unafuu wowote kwa vile tayari seli kadhaa za ubongo huwa zimeathirika na kufa kabla hata dalili za Parkinson kujitokeza. Aidha seli nyingine zaidi za ubongo hufa kadiri ugonjwa unavyoendelea na mbaya zaidi seli hizi za ubongo hazina uwezo wa kukua upya pindi zikishaharibika.
Hata hivyo ripoti hiyo inaonekana kuleta tashwishwi miongoni mwa makundi kadhaa yanayojihusisha na ugonjwa wa Parkinson. Chama cha hisani cha Ugonjwa wa Parkinson cha nchini Uingereza kilisema kuwa matokeo ya utafiti huo hayana budi kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa.
Mkurugenzi wa kituo kimoja cha utafiti wa Parkinson huko Uingereza, Dr Kieran Breen alisema inajulikana na kuaminika kuwa ugonjwa Parkinson husabaishwa na mkusanyiko wa mambo kadhaa zikiwemo sababu za mazingira pamoja na nasaba ya muhusika mwenyewe. Aliongeza kuwa kuna ushahidi kuwa bakteria hao wana uwezo wa kuzuia ufyonzwaji wa Levodopa, dawa inayotibu ugonjwa Parkison, katika kuta za tumbo na utumbo mdogo lakini hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa kuwepo kwao kwenye tumbo kunasababisha Parkinson.
Aidha alisema pamoja na kuwa utafiti huo umeleta chachu na changamoto kubwa, matokeo yake hayana budi kuchukuliwa kwa tahadhari na akashauri tafiti zaidi kufanyika ili kuthibitisha matokeo hayo.