Vipimo na uchunguzi
Pamoja na kumchunguza mgonjwa kuhusu kuwepo kwa dalili na viashiria vya ugonjwa huu wa Uti wa mgongo, daktari pia anaweza kufanya vipimo vifuatavyo;
- Kuchunguza damu ya mgonjwa kwa ajili ya kuangalia uwepo wa vimelea vinavyosababisha ugonjwa na pia kufahamu ni aina gani ya vimelea hao. Hali kadhalika, damu inaweza pia kutumika kuotesha vimelea maabara ili kugundua aina ya vimelea na dawa gani nzuri zinazofaa kwa ajili ya matibabu (culture and sensitivity).
- Kipimo kinachofanyika kwa kuchukua maji ya uti wa mgongo wa mgonjwa na kuyachunguza maabara ili kutambua uwepo wa vimelea, aina ya vimelea na dawa zinazofaa kutibu vimelea hao (Lumbar puncture).
- Kwa baadhi ya maeneo yenye vifaa kama CT-scan na MRI, mgonjwa pia huweza kuchunguzwa kwa kutumia vifaa hivi ili kufahamu uwepo wa ugonjwa, sehemu lilipo na madhara yaliyosababishwa na ugonjwa huu wa uti wa mgongo. Hata hivyo vipimo hivi haviwezi kutambua aina wala dawa ya kutibu vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo.
Matibabu ya ugonjwa wa Uti wa Mgongo
Kwa wagonjwa waliopoteza fahamu ni vizuri kuhakikisha wanapumua vizuri, na njia za hewa ziko wazi. Halikadhalika, iwapo itathibitika kuwa bakteria ndiyo wanaosababisha ugonjwa huu, mgonjwa anaweza kupewa mojawapo ya dawa hizi za antibiotiki kama cefotaxime au Cefriaxone. Aidha baadhi ya madaktari hupendelea kuongeza dawa za steroids kama dexamethasone kama sehemu ya matibabu.
Iwapo itathibitika ugonjwa huu umesababishwa na virus, dawa kama Acyclovir huweza kutumika. Hali kadhalika, ikithibitika kuwa vimelea waliosababisha ugonjwa huu ni wa kundi la fungus, dawa kama Amphotericin B au flucytosine zaweza kutumika. Mgonjwa pia hupewa Paracetamol kwa ajili ya kushusha homa na kuondoa maumivu ya kichwa.
Madhara yanayoweza kuletwa na ugonjwa wa uti wa mgongo
Ugonjwa wa uti wa mgongo unaweza kusababisha
- Kuamshwa kwa chembechembe za damu zinazo sababisha damu kuganda kitaalamu – Disseminated Intravascular Coagulopathy (DIC).
- Kuvuja damu kwa katika tezi za adrenalin na kupelekea kutokea kwa ugonjwa ambao kitaalamu unaitwa – waterhouse friderichsen syndrome.
- Kwa watoto, ugonjwa huu unaweza kusababisha mtoto kuwa na kichwa kikubwa - hydrocephalus.
Picha kwa hisani ya http://www.humanosphere.org