Image

Madawa ya Kulevya - Aina na Athari zake kwa Mtumiaji

Tatizo la madawa ya kulevya limetokea kuwa janga kubwa duniani kote, watu wengi wameathirika na janga hili. jinsia zote wanaume, wanawake, na vilevile rika zote vijana na wazee pia.

Hapa tutaongelea aina mbili za madawa ya kulevya yaani Cocaine na Heroin.

Cocaine

Hutokana na majani ya mmea uitwao kitaalamu Erythroxylum coca bush.

Aina hii ya dawa ya kulevya hutolewa kwa mifumo ifuatayo

 • Unga ambapo mitaani hujulikana kama ‘coke’ na hutumika kwa kuvutwa puani kama unga, au kuyeyushwa na maji na kuchomwa kwenye mshipa wa damu.
 • Crack ambapo mitaani hujulikana kwa jina hilohilo crack au rock, na hutengenezwa kwa kuchanganywa na kemikali. Na hutumika kwa kuvutwa kama sigara.

Cocaine pindi inapoingia kwenye damu huenda kwenye ubongo na kuzuia ufyonzwaji wa vihisishi vifuatavyo: dopamine, norepinephrine na serotonin, kutoka kwenye ubongo. Hivyo ubakia kwenye ubongo. Na vihisishi hivi husababisha ile hali ya furaha, mchangamfu na kujisikia mwenye nguvu kitaalamu euphoria. Na huweza kuwa kwenye hali hii kwa nusu saa tu.
Mara tu baada kutumia dawa hii dalili zifuatazo hutokea

 • Mishipa ya damu husinyaa (constricted blood vessels)
 • Joto la mwili huongezeka
 • Mapigo ya moyo huongezeka
 • Shinikizo la damu
 • Dilated pupils

Matumizi ya muda mrefu ya dawa hii ya kulevya huleta madhara yafuatayo, Pamoja na kwenda kwenye ubongo husambaa sehemu nyingine za mwili na mzunguko wa damu

 • Moyo - Kwenye moyo huweza kuleta Shambulizi la moyo (heart attack) na vilevile mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio (Arrhythmia) hivyo unaweza kufa ghafla tu.
 • Ubongo - Mishipa ya damu kwenye ubongo inaweza kusinyaa na kupelekea kupata Kiharusi, hata kwa kijana. Vilevile unaweza kupata ugonjwa wa akili (substance abuse pyschosis).
 • Mapafu na mfumo wa hewa - Uvutaji kupitia pua huweza kupelekea tatizo sugu la kutokwa damu puani kila wakati na mafua yasiyo pona, kupoteza mfumo wa harufu, na ikivutwa kama sigara kuharibu mapafu moja kwa moja.
 • Mfumo wa chakula - Cocaine husababisha kusinyaa kwa mishipa ya damu kwenye tumbo na utumbo hivyo kusababisha vidonda na kuweza kuharibu kabisa mfumo huu kwa utumbo kuoza.
 • Mafigo - kutokana na shinikizo la damu mafigo yanaweza kushindwa kufanya kazi vizuri, vilevile cocaine inaweza kuleta madahara moja kwa moja kwenye mafigo kitaalamu Rhabdomyolysis.
 • Ngono - ingawa cocaine huweza kutumika kama njia ya kuongeza hamu ya ngono huweza kusababisha kushindwa kumaliza kile ulichokianza. Matumizi sugu ya dawa hii ya kulevya huleta madhara kwa jinsia zote yani kwa wanaume na wanawake.
 • Na vilevile huweza kufanya kuwa tegemezi wa dawa hii.
 • Kwa wanaotumia sindano na kushea wanaweza kupata maambukizi ya virusi ya hepatitis na vya ukimwi.

Nini hutokea baada ya matumizi ya muda mrefu ya kokeni?

Baada ya kutumia cocaine kwa muda mrefu punde unapoacha tu kutumia dalili zifuatazo hutokea;

 • Unyogovu
 • Uchovu
 • Kushindwa kuzingatia na kutokuwa makini
 • Kukosa uwezo wa kuwa na furaha au kusikia raha
 • Kuongezeka kwa tama zaidi ya kutumia cocaine
 • Kujisikia kuumwa, maumivu, baridi na kutetemeka.

Ikitokea mtu akitumia zaidi ya kiwango kinachotakiwa kwa muda mfupi yaani overdose, kifo cha ghafla huweza kutokea kutokana na madhara yafuatayo;

 • Moyo kushindwa kufanya kazi
 • Kiharusi
 • Degedege mara kwa mara
 • Mfumo wa hewa kushindwa kufanya kazi

Heroin

Hujulikana vilevile kama diamorphine, hutokana na mmea huitwao kitaalamu opium poppy. Heroin kwa mfumo wa Morphine hutumiwa hospitalini kama dawa ya maumivu makali ya ghafla (acute pain) kwenye maumivu makali ya kifua wakati wa shambulizi la moyo, na kwa maumivu ya mtu aliyepata ajali, vilevile baada ya upasuaji, na maumivu sugu kwenye kansa. Hivyo hutolewa kwa kuangalifu mkubwa.

Aina hii ya dawa ya kulevya huweza kutumika kwa kuvuta kwa pua, kuvuta kama sigara na kwa kuchoma kwenye mshipa. Siku hizi watu hutumia njia ya haja kubwa na kwenye uke, ambapo kuta hufyonza heroin na kuanza kufanya kazi ndani ya sekunde arobaini.

Heroin mara tu baada ya kuingia kwenye damu kuenda kwenye mfumo wa neva na kukandamiza ufanyaji kazi wake, ndio huweza kutumika kupunguza maumivu.

Dalili za mtu aliyetumia heroin

Dalili ambazo hutokea mara tu anapotumia Heroin:

 • Kujisikia mwenye furaha na raha
 • Kupishana Kusikia hali usingizi na tahadhari
 • Midomo kuwa mikavu
 • Misuli kuishiwa nguvu
 • Kuhema polepole
 • Warm skin flushing
 • Mikono na miguu kuwa mizito
 • kope za macho kulegea

Nini madhara ya matumizi ya muda mrefu ya heroin?

Madhara ya matumizi ya muda mrefu wa dawa hii ya kulevya hutokana zaidi na matumizi ya sindano na vifaa vingine visivyo salama

 • Maambukizi kwenye kuta na milango ya moyo
 • Maambukizi ya ini na virusi (kama hepatitis C na HIV),
 • Maambukizi ya figo
 • Maambukizi ya mfumo wa hewa
 • Maambukizi ya ngozi na majipu

Dalili ambazo hutokea mara tu unapoacha kutumia heroin

 • Kutotulia
 • Maumivu ya misuli na mifupa
 • Kutapika
 • Dalili hizi hufikia kilele ndani ya masaa 48 hadi 72 na hufika kikomo baada ya wiki.
Imesomwa mara 16099 Imehaririwa Jumatatu, 04 Machi 2019 10:01
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana