Image

Je,ni nini cha kufanya mtoto mchanga anapolia?

Kuna vitu ambavyo mzazi unaweza kufanya ili kumpa faraja mtoto wako pindi anapolia. Yawezekana baadhi ya mambo yatakayoshauriwa hapa yasiwasaidie watoto wote, hivyo basi mzazi ama mlezi ni vizuri ukamjua mtoto wako na kufahamu kwa undani ni kitu gani hasa kinachoweza kusaidia kumtuliza.

1. Kumbeba mtoto 

Watoto wachanga huonyesha upendeleo fulani wa hisia, kama vile walivyokuwa ndani ya tumbo, hivyo basi unaweza kujaribu kumvingirisha mtoto wako katika blanketi au nguo zozote za kumbebea kama khanga au vitenge ili kuona kama atapenda hali hiyo. Watoto wengine hawapendi kuvingirishwa kwenye blanketi na hupenda aina nyingine ya kupata faraja kama vile kubebwa.

2. Kumwimbia nyimbo au sauti za kumbembeleza 

Akiwa tumboni mwa mama, mara kwa mara mtoto alikuwa akisikia mapigo ya moyo ya mama. Hali hii ndiyo sababu kubwa ya watoto wengi kupendelea kubebwa na mama zao. Hata hivyo kuna aina nyingine za sauti zinazoweza pia kusaidia kumtuliza mtoto.

3. Jaribu kumkanda au kumsugua taratibu (masaji) 

Kumkanda kanda au kumsugua mtoto taratibu mgongoni au tumboni kunaweza kumsaidia sana kumfariji mtoto. Iwapo inaonekana mtoto anapata tabu wakati wa kubeua au kucheua, jaribu kumlisha akiwa wima zaidi na kila baada ya kumlisha mweke juu ya bega lako na kumsugua taratibu mgongoni ili kumsaidia atoe gesi kwa kubeua.

4. Mpatie kitu cha kunyonya 

Kwa baadhi ya watoto waliozaliwa, haja ya kunyonya ni kubwa sana na hivyo kumpatia chuchu safi iliyotengenezwa kwa ajili hiyo au kidole kisafi cha mama inaweza kuleta faraja kubwa kwao. Kunyonya kutamsababishia mapigo ya moyo wake kuwa katika kiwango chake cha kawaida, kupumzisha tumbo lake, na kutulia.

Kwa maelezo zaidi soma Sababu za Watoto Wachanga Kulia Mara kwa Mara na Namna ya Kuwabembeleza

Imesomwa mara 2473 Imehaririwa Ijumaa, 18 Januari 2019 15:50
Sophia Mangapi

Web Developer

This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.