Image

Je wajua,madhara ya Pumu(Asthma) kwa wanawake wajawazito?

Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa ambao huathiri sehemu ya kupitisha hewa kwenda kwenye mapafu ya binadamu zinazojulikana kitaalamu kama bronchioles.

Mtu mwenye pumu huwa na mcharuko mwili sugu (chronic Inflammation) kwenye mirija yake ya kupitishia hewa (bronchioles tubes) hali ambayo husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hii, kujaa kwa ute mzito (mucus) na kupungua kwa njia ya kupitishia hewa, hali ambayo humfanya muathirika kushindwa kuvuta na kutoa hewa nje na hivyo kupumua kwa shida sana. Hali hii inaweza kudumu kwa muda mfupi au mrefu kiasi cha kuhitaji tiba ili kumuwezesha mgonjwa kupata nafuu.

Kutokana na  kuwepo kwa msuguano na uzuiaji wa kupitisha hewa wakati wa kupumua hwa nje, pumu hujulikana pia kama obstructive lung disease . Mtu aliye na pumu, huwa nayo kipindi chote cha maisha yake.  

Nini madhara ya pumu kwa mama wajawazito?

Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa takribani theluthi moja ya wajawazito wenye pumu hupata nafuu kipindi cha ujauzito, theluthi  nyingine hupata matatizo kipindi hiki na theluthi iliyobakia huwa na hali ya kawaida kama kabla ya ujauzito. Kwa kawaida dalili za pumu hujirudia kama awali miezi mitatu baada ya kujifungua. 

Dalili za pumu kwa mjamzito zinaweza kuwa mbaya zaidi kuanzia wiki ya 24-36 (mwezi wa sita mpaka wa nane). Ni mara chache sana mjamzito anapata shambulizi la pumu wakati wa kujifungua. Inakisiwa kuwa, ni asilimia 10 tu ya wajawazito wenye pumu wanaopata shambulizi la pumu wakati wa kujifungua.

Baadhi ya dawa zinazotumika wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua huongeza madhara ya pumu, hivyo ni vizuri  kumueleza daktari kwamba una pumu kabla ya kupewa dawa. Aidha  na si vyema kunywa dawa kwa mazoea.

Wanawake wenye pumu isiyoweza kuthibitiwa kipindi cha ujauzito hupata madhara ya kuzaa mtoto njiti (premature baby), kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo, kifafa cha mimba, shinikizo la damu (Hypertension), na iwapo atapata shambulizi hatari wakati wa ujauzito mtoto anaweza kufa kwa kukosa hewa ya oksijeni.

Soma hapa Ugonjwa wa Pumu (Bronchial Asthma), Chanzo, Dalili na Tiba kupata makala nzima kuhusu Pumu

Imesomwa mara 3212 Imehaririwa Jumanne, 02 Oktoba 2018 16:45
Sophia Mangapi

Web Developer

This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.