Image

Mazoezi kwa watu wazima huongeza uwezo wa kukumbuka

Ripoti ya utafiti iliyochapishwa katika jarida la Health Physiology na kuchapwa katika wavuti ya WebMD inadai kuwa watu wazima wenye tabia ya kufanya mazoezi ya kuendesha baiskeli au kujinyosha viungo vyao huongeza uwezo wa kukumbuka zaidi kuliko wale wasiofanya kabisa.

 

Utafiti huo unadai kuwa pamoja na kwamba kimuundo ubongo haufanani na misuli lakini kadri mtu anavyozeeka kuingia utu uzima, ufanyaji mazoezi husaidia kuimarisha uwezo wake wa kukumbuka na hata kufikiria mambo mapya.

Jambo la kutia moyo ni kuwa huna haja ya kufanya mazoezi mazito kwa vile mazoezi mepesi tu kama ya kunyoosha nyoosha viungo yanatosha kuleta kabisa matokeo ya kuridhisha.

Uchunguzi huo ambao ulihusisha watu wazima waume kwa wake waliokuwa wakiendesha baiskeli au mazoezi ya kunyoosha viungo kwa muda wa saa mbili kwa wiki kwa muda wa miezi sita ulionesha kuwepo kwa maendeleo makubwa katika uwezo wao wa kukumbuka mambo na hata kufikiria mambo mapya.

Mmoja wa watafiti hao Kirsten Hotting kutoka chuo kikuu cha Hamburg, Ujerumani anasema kuwa mtu anayefanya mazoezi ya aina mbalimbali kwa pamoja ana uwezekano wa kupata matokeo mazuri zaidi.

Ripoti hii inaweza kutafsiriwa kama changamoto kwa watu walio katika nafasi mbalimbali za kutoa maamuzi kiuongozi kuwa tabia ya ufanyaji mazoezi inaweza kuimarisha sana uwezo wao wa kukumbuka mambo na kufikiria mambo mapya, na hivyo kuzidi kuongeza tija katika utendaji wao wa kila siku. Aidha hii ni changamoto hata kwa watu wengine kuanzisha utaratibu wa kujifanyia mazoezi mepesi kwa ajili ya kuimarisha afya ya akili na mwili kwa ujumla.

Ripoti ya utafiti huu inapatikana katika Jarida la Health Psychology

Imesomwa mara 7153 Imehaririwa Ijumaa, 26 Mai 2017 09:04
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.