Kwa miaka mingi, VVU ilikuwa hukumu ya kifo(death sentense). Lakini kutokana na maendeleo ya dawa za kisasa, watu wanaoishi na VVU wanaweza kuishi maisha marefu na yenye afya wakifuata matibabu kwa usahihi. Dawa za antiretroviral (ARVs) zinaweza kupunguza kiwango cha virusi mwilini hadi kiwango kisichoweza kugunduliwa katika vipimo vya kawaida. Hii inamaanisha kuwa hatari ya kuambukiza mtu mwingine ni ndogo sana. Na kama watu wenye maambukizi wana afya njema na tunaishi naokatika maisha ya kila siku, ni muhimu kuzungumza swala hili.
Jibu fupi ni ndiyo, unaweza kufanya mapenzi na mtu mwenye virusi vya UKIMWI. Lakini kuna mambo muhimu sana ya kuzingatia ili kuilinda afya yako na afya ya mwenza wako.
Kwa nini ni muhimu kujadili swali hili?
- Stigma : Bado kuna uelewa mdogo na unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU. Hii inafanya watu wengi kuwa na hofu na kutokutaka mazungumzo ya wazi kuhusu jinsia na VVU. Hii huweza kupelekea kufanya maamuzi yasiyo sahihi.
- Afya: Ili kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya yako ya ngono( sexual health), inabidi
Kuelewa hatari na kinga. Mbali na hivyo, mazungumzo ya wazi kuhusu VVU yanaweza kuimarisha uhusiano wako na mwenza wako endapo mmoja au wote mnaishi na maambukizi ya VVU.
Mambo ya Kuzingatia:
- Matibabu ya VVU: Dawa za kisasa za VVU zinaweza kupunguza kiwango cha virusi au kufubaza virusi mwilini hadi kiwango kisichoweza kuonekana kwenye vipimo vya kawaida. Hii inamaanisha kuwa hatari ya kumuambukiza mtu mwingine ni ndogo sana lakini bado ipo hivyo hatua za ziada zinatakiwa kuchukuliwa.
- Kinga za ziada: Hata kama mwenzako anafanya vizuri kwenye matibabu, bado ni muhimu kutumia kinga za ziada ili kupunguza hatari ya maambukizi ya VVU na magonjwa mengine ya zinaa.
Mifano ya Kinga za Ziada:
- Kondom: Hizi ni muhimu sana katika kuzuia uambukizi wa magonjwa mengine ya zinaa.
- Dawa za PrEP: Dawa hizi zinaweza kuchukuliwa na watu ambao hatari yao ya kupata maambukizi ya VVU ni kubwa.
- Dawa za PEP: Dawa hizi zinaweza kuchukuliwa baada ya kuwa na uhusiano/ajali/tukio ambalo linaweza kusababisha maambukizi ya VVU.
- Uchunguzi wa mara kwa mara: Wote wawili mnahitaji kupimwa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa mko salama.
- Mazungumzo wazi: Mazungumzo ya wazi kuhusu VVU, mapenzi, na mipango ya uzazi ni muhimu sana katika uhusiano wowote.
- Uaminifu : Uaminifu ni muhimu ili kuzuia kupata maambukizi mapya.
- Mipango ya uzazi: Ikiwa unapanga kuwa na watoto, ni muhimu kuzungumza na daktari/ mtoa huduma wa afya kuhusu hatari na njia za kuzuia maambukizi kwa mtoto.
Hitimisho
Kufanya mapenzi na mtu mwenye virusi vya UKIMWI ni kitu ambacho kinawezekana na kinaweza kuwa salama ikiwa mtachukua tahadhari zote muhimu. Kwa kuzungumza wazi na daktari, kupata matibabu sahihi, na kutumia kinga za ziada, unaweza kufurahia maisha ya mapenzi yenye afya na yenye kuridhisha.
Mambo Muhimu ya Kukumbuka:
-
Tuepuke unyanyapaa: Watu wanaoishi na VVU wanastahili kuheshimiwa na kupendwa kama watu wengine wote.
-
Kujua ni silaha: Kujifunza zaidi kuhusu VVU na jinsi ya kujilinda dhidi yake ni njia bora ya kufanya maamuzi sahihi.
-
Usihofu kuzungumza: Ikiwa una maswali au wasiwasi, zungumza na daktari wako au mshauri wa afya.
Kumbuka: Makala hii imeandaliwa kwa madhumuni ya kutoa taarifa za jumla tu, na haipaswi kuchukuliwa kama ushauri wa kitaalamu wa afya. Kwa ushauri zaidi, tafadhali wasiliana na daktari wako.