Image

Mafunzo kwa picha: Nyonga na Umbo lililojengeka la Ndoto Yako

Hakuna ubaya wowote kwa mtu kutaka kupendeza. Swala la kuonekana mzuri au kuwa mtanashati limekuwa sehemu muhimu kwa maisha ya binadamu hususani upande wa dada zetu. Si kitu cha ajabu maana tangu enzi za mababu , tunasoma katika historia jinsi mwanamke alivyosifiwa kwa uzuri na urembo wake.

Swala la uzuri na urembo wa mwanamke linajadiliwa mara nyingi katika aya mbalimbali za misahafu ya dini zetu, kuonesha ni jinsi gani ambavyo hata Mungu mwenyewe anavyouthamini uzuri na urembo wa mwanamke. Si ajabu kuona jinsi ambavyo makampuni makubwa yanayojishughulisha na utengenezaji wa vipodozi na nguo, vitu ambavyo vinachangia sana katika kumfanya mwanamke aonekane mzuri na mrembo, yanavyotengeneza faida kubwa.

 Sikatai kwamba kuna uzuri wa kuzaliwa, la hasha. Ni dhahiri kabisa wapo watu waliojaliwa kuwa na muonekano mzuri ambao wamezaliwa nao. Na mtakubaliana na mimi kwamba kuna baadhi ya vitu katika miili yetu ambavyo hatuwezi kuvibadilisha hata kama hatuvipendi, lakini habari njema ni kwamba asilimia kubwa ya muonekano wa sura na miili yetu waweza kubadilishwa, na kuendana na matakwa yetu.

Siongelei wala sishauri utumiaji wa madawa au njia nyingine zenye madhara katika mwili wa binadamu. Bali naongelea jinsi ambavyo mfumo wa maisha waweza kukusaidia kupata muonekano unaoupenda bila kuwa na madhara yeyote ya kiafya katika mwili. Usifikirie sana, hapa naongelea vitu vya kawaida kabisa katika maisha yetu ya kila siku visivyo kuwa na gharama yeyote zaidi ya muda. Naongelea mazoezi na lishe bora. 


mazoezi-kwa-kujenga-umbo

Viko vitu vingi vinavyoelezea muonekano wa mtu. Sura na umbo la mwili ni sehemu kubwa na muhimu katika muonekano . Nadhani mtakubaliana na mimi kwamba, kwa dada zetu muonekano wa nyonga na sehemu za makalio unachangia kwa kiasi kikubwa sana katika uzuri na muonekano kwa ujumla. Hili limeonekana dhahiri siku chache zilizopita kulipotokea wimbi kubwa la kina dada kutumia kemikali zilizoaminiwa kuongeza na kuzipa maumbo mazuri sehemu za nyonga na makalio yao.

Habari njema ni kwamba, huitaji kutumia madawa ambayo yanaweza kuwa na madhara kwa afya yako ili kupata nyonga na makalio ya ndoto yako. Mazoezi na lishe sahihi vinaweza kabisa kukupatia nyonga na makalio uliyokuwa ukitamani siku zote. Leo hii nitaongelea aina ya mazoezi yanayosaidia kutengeneza sehemu za nyonga na makalio na kuzipa muonekano unaoutaka.

Wataalamu wa mambo ya mazoezi wanasema, mazoezi mazuri kwa kina dada ni mazoezi ya sehemu ya chini ya mwili. Hapa ninamaanisha mazoezi yanayohusisha misuli ya miguu, mapaja, nyonga na makalio. Sababu ya kusisitiza mazoezi haya kwa kina dada ni kutokana na ukweli kwamba, wakati mazoezi haya husaidia kiafya, pia yanasaidia kuzipa muonekano mzuri sehemu za nyonga, mapaja na makalio.

Mazoezi yanayokuza na kuyapa makalio na nyonga muonekano mzuri

Zoezi muhimu kuliko yote, ambalo kwa bahati mbaya kinadada wengi hulikwepa, ni zoezi lijulikanalo kitaalamu kama ’’squarts’’ yaani kuchuchumaa kwa kiswahili rahisi. Kufanya squarts, waweza tumia uzito au waweza fanya squarts bila kutumia uzito wowote. Unachukua uzito unaoweza kuhimili, na kuuweka mabegani (kumbuka uzito huu unatakiwa uwe umewekwa pande zote kwa uwiano sawa ukiunganishwa na bomba ambalo ndiyo unaliweka mabegani).

Simama wima miguu yako ikiwa imetengana kiasi, halafu chuchumaa taratibu, na kunyanyuka taratibu. Rudia mzunguko huu mara 6 mpaka 8, kwa kila seti, na ni vema kufanya seti tatu mpaka tano. Kumbuka waweza fanya squarts bila kuwa na uzito wowote, cha muhimu ni kuikutanisha mikono yako pamoja nyuma ya kichwa wakati wote unapokuwa unachuchumaa na kusimama.

Ni muhimu kufahamu kwamba, kama unataka sehemu zako za makalio kuongezeka ukubwa, basi ni vema kutumia uzito.

squatrs-tanzmed

Squarts bila uzito

squarts-na-uzito

Squarts na uzito

Zoezi lingine ni lile la kukaa mkao wa wanyama.

Unapiga magoti na kuweka mikono yako chini kama vile unataka kutembea kama mbwa au paka. Taratibu unarudisha mguu wako nyuma kama kwamba unampiga teke mtu aliye nyuma yako (kama ng’ombe au punda anayepiga teke la kinyumenyume). Unafanya hivyo taratibu na kuurudisha mguu bila kuweka goti chini.

Unarudia mara 6 mpaka 12 kwa mguu mmoja, halafu unafanya hivyo hivyo kwa mguu wa pili. Ni vema kufanya mizunguko mitatu mpaka mitano ya zoezi hili. Muhimu ni kwamba, unaporudisha mguu nyuma, usiunyooshe kabisa, ili msukumo mkubwa usikike kwenye sehemu za makalio. Zoezi hili ni zuri sana kuyapa makalio umbo na muonekano mzuri. Pia ni zuri sana katika kuondoa maumivu ya mgongo.

mzoezi-mahelet
Yako mazoezi mengi yanayosaidia kuongeza na kuyapa makalio muonekano mzuri (shape). Ila niliyotaja hapo juu ni baadhi tu ya mazoezi ambayo waweza fanya hata nyumbani. Kwa wenye nafasi na bahati ya kwenda kwenye sehemu maalumu za mazoezi (gyms), ziko mashine nzuri sana zinazosaidia kuyaweka makalio yako katika umbo na ukubwa unaotaka. Waweza tumia smith machine kwa squarts.

Waweza fanya ``quadriceps curls’’, ´´leg press’’ na mazoezi mengi kwa kutumia mashine maalumu zinazopatikana kwenye gyms mbalimbali. Ukweli ni kwamba kupata makalio yenye muonekano na ukubwa unaoutaka, zingatia mazoezi yanayohusisha sehemu ya chini ya mwili . Si swala la kujaribu, bali ni kitu kinachojulikana kisayansi na kiuzoefu.

sukuma-mguu-tanzania

Leg press - Mazoezi ya miguu

Mazoezi ya kupunguza makalio bila kupoteza muonekano wake mzuri

Ni jambo lililo wazi kabisa, kwamba wakimbiaji wengi wa kike wa mbio fupi (mita 100 na 200), wana maumbo mazuri. Je umewahi jiuliza ni kwa nini? Licha ya kwamba hatuwezi kupinga uwezekano wa kuwa wamezaliwa hivyo, lakini ukweli kwamba kukimbia kunasaidia kukakamaza na kuyapa muonekano mzuri makalio, hauwezi pia kupingika. Wako kina dada wengi ambao makalio na sehemu zao za nyonga zinazidi ukubwa wautakao. Hii hutokana na kuongezeka kwa mafuta mwilini, hususani sehemu za makalio. Kukimbia ni zoezi ambalo husaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mafuta na hivyo kuyapa makalio umbo zuri. Waweza kukimbia nje au kwenye mashine ya kukimbilia, kwa kasi ya kawaida. Ni vizuri kukimbia kwa muda usiopungua dakika 30 kama unataka kupunguza mafuta. Hii pia inasaidia kuongeza mzunguko wa damu na kuufanya moyo wako kufanya kazi vizuri. Fanya hivi mara tatu au zaidi kwa wiki.

kimbia

Kukimbia husaidia kupata umbo bora


Kwa kifupi mazoezi yanaweza kabisa kusaidia kupata umbo na ukubwa wa makalio unayoyataka. Mchanganyiko wa kukimbia, na mazoezi ya sehemu ya chini ya mwili ni njia nzuri ya kukusaidia kupata makalio ya ndoto yako. Ukijumlisha na lishe bora hakuna kinachoshindikana katika mwili wako. Na ni dhahiri kwamba, kwa mazoezi, wakati unatengeneza muonekano wako, ni wakati huo huo unatengeneza afya yako.

Shukrani kwa Miss Mahelet (Model) , na Sansan Gym (Wuhan) kwa kutuwezesha kupata picha kamili kwa mazoezi haya.

Nyuma ya Pazia

dk-khamis-akitoa-maelekezo

 Dk Khamis akitoa maelekezo ya njia bora za kufanya mazoezi

Imesomwa mara 10020 Imehaririwa Jumatatu, 31 Mai 2021 10:58
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.