Image

Uvutaji bangi kwa mzazi husababisha mtoto kupata matatizo ya kiakili kabla ya kuzaliwa

Wanaume wanaovuta bangi wapo kwenye hatari ya kupata watoto wenye matatizo ya kiakili kama kutomudu masomo ya darasani, wamesema wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Pennsylvania, nchini Marekani. Utafiti huu mpya umesema ya kwamba madhara ya bangi kwenye vina saba (DNA) yanaweza kurithishwa kupitia shahawa na hivyo kuathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto.

Cha kushangaza ni kwamba madhara haya ya bangi kwenye ubongo wa mtoto huonekana sana kwa watoto wa kiume kuliko watoto wa kike au mtoto yoyote yule atakayezaliwa na mama ambaye alikuwa mvutaji bangi.

Wakati wanasayansi bado wanajaribu kutafuta ni kwa muda gani athari za bangi kwenye vina saba zinaweza kuwepo hata kama mvutaji ameacha kuvuta bangi miaka mingi iliyopita lakini tafiti hii ni muendelezo wa tafiti za hapo awali ambazo ziliwahi kueleza kuhusu madhara ya bangi kwenye vina saba kwa miaka mingi hata kama mvutaji ameacha kuvuta bangi. Profesa R. Christopher Pierce, mtaalamu wa sayansi ya akili (Neuroscience) katika chuo kikuu cha Pennsylvania pamoja na timu yake ya watafiti ambayo ndio walitafiti nadharia (hypothesis) hii ya kwamba ‘’uvutaji bangi huathiri vina saba kwa miaka mingi hata baada ya mtumiaji bangi kuacha kuvuta bangi’’.

Watafiti hawa walipima nadharia yao kwa kutafiti panya 16 wanaume ambao walipewa uwezo wa kutumia bangi wao wenyewe kwa kuwachanganyia bangi kwenye maji yao ya kunywa kwa muda wa siku 60.Panya wengine wa kiume walikunywa maji ya kawaida kwa muda huo wa siku 60.

Panya hawa walijamiana na panya majike na baadae kugundulika ya kwamba utumiaji bangi kwa mzazi hauna uhusiano wowote na uzito wa mtoto anaezaliwa, jinsia au ukuaji wa mtoto.

Hata hivyo kati ya watoto wote wa panya 46 waliozaliwa, watoto wa kiume ambao walitokana na wazazi ambao walitumia maji yenye mchanganyiko wa bangi walionekana kuwa na matatizo ya kiakili. Baada ya uchunguzi zaidi, watafiti hawa waligundua ya kwamba jeni (genes) ambazo ni muhimu kwa kumbukumbu za kiumbe zimebadilishwa (mutation) kutokana na matumizi ya bangi.

Asilimia ya watoto wa kiume ambao baba zao walitumia maji yaliyochanganya na bangi walikuwa na kiwango kidogo cha molekuli (molecule) aina ya D-serine ambayo ni muhimu kwa ajili ya kumbukumbu. Baada ya watafiti hawa kuwachoma molekuli hii ya D-serine kwenye sehemu ya ubongo ya watoto wa kiume wa panya inayojulikana kama hippocampus kutokana kuwa na kiwango kidogo cha D-serine, waligundua ya kwamba uwezo wao wa uelewa uliongezeka kwa kiwango kikubwa tofauti na hapo awali.

Profesa R. Christopher Pierce na timu yake walipendekeza ya kwamba mfumo wa kiasili (epigenetic mechanisms) ndio chanzo cha tatizo hili kwa wale panya watoto wa kiume. Epigenetics ni matatizo ya mfumo wa kiasili wa jeni ambao hautokani na mabadiliko ya vina saba ya kiumbe bali hutokana na visababishi kutoka nje ya miili ya viumbe.

Watafiti hao wanasema waligundua ya kwamba matumizi ya bangi kwa baba husababisha mabadiliko katika protini aina ya histone kwa watoto wao wa kiume hata kama watoto hao hawajawahi kutumia madawa ya kulevya aina ya bangi.

Mabadiliko katika protini aina ya histone husababisha kutengenezwa kwa wingi kwa kimengenyo (enzyme) kinachojulikana kama D-amino acid oxidase ambacho huvunja vunja molekuli ya D-Serine na hivyo kusababisha matatizo ya kumbukumbu. ‘’Matokeo haya yanaonesha ya kwamba watoto ambao baba zao walikuwa watumiaji wa bangi huathirika kiakili na hivyo hata kuwa na uwezo mdogo wa uelewa wa mambo au masomo yao darasani’’, alisema profesa R. Christopher Pierce. Hata hivyo, kitendo cha matumizi ya dawa ya molekuli aina ya D-serine ambayo iliongeza uwezo wa kumbukumbu za watoto wa kiume wa panya ni jambo la faraja sana .

Uwezo wa molekuli aina ya D-serine katika kubatilisha matatizo ya kumbukumbu imeonesha umuhimu mkubwa wa utafiti wetu’’ aliendelea kusema profesa R. Christopher Pierce. Kuna muelekeo mzuri katika utengenezaji wa dawa ambayo inahimilka vizuri na mwili ya molekuli aina ya D-serine pamoja na vihusika vyake (related compounds).

Tunashauri ya kwamba tujiepushe na matumizi ya aina zote ya madawa ya kulevya ikiwemo bangi kwani pamoja na kusababisha matatizo ya kiakili kwa mtoto kabla hajazaliwa, bangi husababisha magonjwa ya akili kama schizophrenia, kurukwa akili (psychosis), kupoteza kumbukumbu na kuwa na mifupa inayovunjika kwa urahisi kama mifupa ya nyonga, uti wa mgongo (spine) hii ni kwa mujibu ya tafiti zilizowahi kufanyika huko nyuma nk.

Imesomwa mara 6246 Imehaririwa Jumatatu, 04 Machi 2019 10:01
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.