Pia kwa kufanya mazoezi kila mara na hasa kabla ya mlo kuna faida nyingi ambazo haziwezi kuonekana kwa haraka, kama vile kuimarisha hali ya kiakili, ambayo matokeo yake ni kuwa na furaha. Hii inatokana na kuzalishwa kwa wingi kwa kemikali aina ya endorphins wakati wa kufanya mazoezi. Kemikali hii ya endorphins ni muhimu kwenye mapambano ya sonono (Depression) na hivyo kumfanya mfanya mazoezi kuwa na furaha zaidi.
Tafiti zinaonesha kuwa mwili huzalisha kemikali hii ya endorphins baada ya mtu kufanya mazoezi ya kawaida kwa dakika 12. Kama wanafamilia wanaweza kufanya mazoezi kwa muda hata wa saa moja, au nusu saa, wanaweza kuwa na furaha na kuzuia kusambaratika kwa ndoa zao.
Pia kuna kemikali nyingine muhimu ambayo tafiti zinaonesha kuwa huzalishwa baada ya kufanya mazoezi. Kemikali hii itwayo “Serotonin” huongezeka kwenye mfumo wa neva baada ya kufanya mazoezi, ambayo hufanya mfanya mazoezi ajisikie vizuri kiafya na kupunguza sonono (Depression). Tafiti pia zinaonesha kuwa kemikali hii, ni muhimu sana katika mwili, kwani hufanya mfanya mazoezi alale usingizi mnono.
Ufanyaji wa mazoezi mara kwa mara husaidia pia mfanya mazoezi ajithamini, na kuondoa uchovu na unyonge. Unapojithamini, huchangia mtu kujiona bora, kujiamini na kuwa mwenye ustawi katika maisha au kazi zake. Mazoezi pia hufanya tendo la ndoa kuwa bora na hivyo kuleta mahusiano bora ya kinyumba na mpwendwa wako.
Nimejaribu kuanisha umuhimu na faida za maozezi na hasa wakati yanapokuwa na tija ili kuleta hamasa ya kufanya mazoezi kwa kila msomaji wa makala hii. Unaweza kufanya mazoezi wewe na familia yako au na wenzako, au pekee yako, chukua muda kidogo katika masaa 24 na ufanye mazoezi, maana utajisikia vizuri na kuwa mwenye afya njema, lakini kumbuka utapata faida zaidi ukifanya mazoezi wakati tumbo likiwa tupu, yaani kabla ya mlo, baada ya kula chakula tembea taratibu ili kukifanya chakula kitulie vyema tumboni.
Usisahau, kabla ya kifungua kinywa asubuhi jitahidi ufanye mazoezi angalau kwa muda wa robo saa.