Image

Watoto na Tatizo la Kusigina Meno

Naitwa Kissu K. Mpini, ni mwenyeji wa wilaya ya Ifakara,mkoa wa Morogoro, Tanzania, utakumbuka mara ya mwisho nilivyotoa ushuhuda wangu kuhusu shida ya kusigina/kusaga meno-bruxism ilivyonitatiza kwa muda mrefu bila kupata nafuu, kwa kifupi baada ya kupata huduma pale kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili, Kitengo cha Meno, ninaendelea vizuri sana kwa sasa, ninalala usingizi vema, na kazi zangu nazifanya vizuri, hakika nimekuwa mwenye furaha kama wenzangu.

Utakumbuka nilijiuliza sana kama watoto pia hupata tatizo la kusigina meno kama inavyotokea kwa watu wazima, hivyo ili kukata mzizi wa fitina, nilimwandikia barua daktari aliyenihudumia pale Muhimbili siku ile, nimeona ni vema pia elimu aliyonipatia daktari nishirikishe wadau wengine, maana sio wote tunaweza kufika Muhimbili kirahisi, vilevile ninaamini kuwa yeyote atayeweza kusoma maelekezo haya ya daktari itakuwa ni msaada mkubwa sana kwake binafsi, familia na rafiki zake. Majibu ya daktari yamebainisha kwa kirefu kuhusu tatizo la kusigina meno linavyoathiri watoto, ifuatayo ni barua ya daktari kama alivyoniandikia.

Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 20 ya watoto kati ya mwaka 1 hadi miaka 11 husumbuliwa na kusigina/kusaga meno tatizo ambalo kwa kitaalamu linajulikana kama Bruxism. Ingawa takwimu hii inakadiriwa kuwa chini ya hali halisi kwa vile wazazi wengi wanashindwa kutambua tatizo hili kwa watoto wao.

Kama ilivyo kwa watu wazima kwa vyanzo mbalimbali vinavyosababisha kusigina meno, kwa watoto dalili za tatizo hili zinafanana sana na matatizo mengine ya watoto hivyo inawawia vigumu wazazi ama walezi kutambua tatizo hili na hata kupuuzia.

Kusigina meno kwa watoto kunasababishwa na mihemko usiku-nocturnal arousal- na hugawanywa kama tatizo la usingizi-sleeping disorder-, vile vile kusigina meno husababishwa na mwitikio-response- wa mihemko ya usiku ambayo inashabihiana na matatizo ya usingizi-sleeping disorders.

Tatizo hili mara nyingi huwapata watoto ambao huwa na shida ya kupumua vizuri hivyo hupumua kwa kutumia mdomo, watoto walio na vivimbe vya tezi-adenotonsillat hypertrophy-, watoto wenye tatizo la kuziba kwa njia ya hewa wanapokuwa usingizini-obstructive sleeping apnoea, watoto wenye tatizo la meno kuota kwa mpangilio mbaya-dental occlusion- pamoja na watoto wenye matatizo ya akili ama mtindio wa ubongo.

Vile vile tatizo hili hushabihishwa na tatizo la ungano la taya na fuvu – temporomandibula joint disorder pamoja maumivu ya kichwa yasiyokoma.

Matokeo ya kusigina meno kwa watoto mara nyingi hujitokeza kwenye mabadiliko ya tabia na mwenendo wa mtoto kwa sababu ya mihemko na mwitikio wake unaomsumbua akiwa amelala usiku. Tafiti zimeonesha kuwa watoto wenye tatizo la kusigina meno hutatizwa na hofu, mashaka na kukosa utulivu kwenye mambo ya kawaida sana.

Tatizo hili la kusigina meno pia linahisianishwa na Tatizo la kukosa utulivu kitaalamu linajulikana kama Attention Deficit Hyperactivity Disorder (ADHD). Utafiti mwingine ulionesha kuwa tatizo la kusugua meno kwa watoto linashabihiana na msongo wa mawazo kwa mama wakati akiwa mjamzito. Wazazi ambao wameripoti kuwa na tatizo la akili ama mwili , watoto wao pia wameripotiwa kuwa na tatizo la mabadiliko ya tabia mara kwa mara pamoja na mihemko nyakati za usiku.

Matukio ya kusigina meno kwa watoto hudumu kwa sekunde 4 na hutoke kwa wastani wa mara 6 ndani ya saa 1. Matukio haya huwa na kawaida ya kutokea kwa mafungu usiku mzima huku yakiwa na nguvu zaidi kwenye hatua ya pili ya usingizi ambayo kitaalamu hujulikana kama Stage 2 and REM sleep.

Utafiti mwingine umeonesha kuwa asilimia 60 ya matukio ya kusigina meno huambatana na mihemko, ilhali asilimia 40 ya watoto waliojumuishwa kwenye utafiti huu waliripotiwa kuwa na tatizo linalohitaji uangalizi wa tiba wa karibu ama tatizo la kubwa la tabia.

Ni vigumu sana kutambua ikiwa kusigina meno kunasababishwa na mihemko na uangalizi wa karibu na tatizo la tabia, ama ikiwa watoto wanaopata uangalizi wa karibu na tatizo la tabia wanapata shida ya usingizi pamoja na kusigina meno. Hata hivyo, inafahamika kuwa usingizi wa mafungu unaosababishwa na kupumua kwa mtoto akiwa usingizini kunaweza kusababisha matatizo ya tabia, kujali na utawala wa kazi za mwili kwa mtoto.

Kuna uhusiano mkubwa baina ya kusigina meno na kuziba kwa sehemu ya juu ya njia ya kupitisha hewa. Kuvimba kwa tezi-tonsillar hyperplasia- ni moja ya chanzo kikubwa kinachosababisha tatizo la kupumua ukiwa usingizini.hewa. Watoto wanaopumua kwa mdomo mara nyingi huwa na tatizo la kuvimba kwa tezi ambazo huziba sehemu ya juu ya njia ya hewa.

Inaaminika kuwa kuzibwa kwa njia ya hewa wakati ukiwa usingizini husababisha kuongezeka kwa msuguano baina ya misuli ya taya, meno na baina ya mifupa ya taya la juu na chini.

Kuziba kwa njia ya hewa kwa watoto husababisha watoto kusukuma taya la chini mbele kwa nguvu ili waweze kuvuta hewa, kufanya hivi kunachokoza vihisishi vya fahamu kwenye sehemu ya juu ya njia ya hewa hivyo kusababisha kusigina meno.

Kukoroma na kupumua kwa mdomo ni dalili ya watoto kuwa na tatizo ambalo mara nyingi wazazi huwa hawajali sana, kwa sababu hii tatizo la kuziba kwa njia ya hewa wakati mtoto yupo usingizini huchelewa kutambuliwa na kutibiwa kwa miaka mingi.

Utafiti uliofanyika kulinganisha tatizo la kusigina meno kwa watoto kabla na baada ya upasuaji wa vivimbe vya tezi vilivyosababisha kuziba kwa sehemu ya juu ya njia ya hewa, ulionesha kuwa watoto wote walikuwa na wastani wa asilimia 75 ya kuziba kwa njia ya hewa kabla ya upasuaji.

Miezi mitatu baada ya upasuaji , watoto wote waliokuwa na tatizo la kupumua vizuri, walikuwa wametibiwa vema,na hivyo kupunguza tatizo la kusigina meno kwa kiasi kikubwa sana, ingawa asilimia 24 kati yao hawakuacha tabia ya kupumua kwa kutumia mdomo-mouth breathing.

Hii ilikuwa ni barua ya daktari akinijulisha uwepo wa tatizo la kusigina meno miongoni mwa watoto, ambapo kwa kifupi ameandika kuwa vyanzo na madhara ya kusigina meno kwa watoto havina tofauti na wakubwa, ametaja vyanzo hivi kuwa ni mihemko usiku-nocturnal arousal- , mwitikio wa mihemko-arousal response ambayo inashabihiana na matatizo ya usingizi, vilevile kusigina meno hutokea miongoni mwa watoto ambao huwa na shida ya kupumua vizuri hivyo hupumua kwa kutumia mdomo, watoto walio na vivimbe vya tezi-adenotonsillat hypertrophy-, watoto wenye tatizo la kuziba kwa njia ya hewa wanapokuwa usingizini-obstructive sleeping apnoea, watoto wenye tatizo la meno kuota kwa mpangilio mbaya-dental occlusion- pamoja na watoto wenye matatizo ya akili ama mtindio wa ubongo. Tatizo la ungano la taya na fuvu – temporomandibula joint disorder pamoja maumivu ya kichwa yasiyokoma navyo husababisha tatizo la kusigina meno kwa watoto.

Matokeo ya kusigina meno kwa watoto mara nyingi hujitokeza kwenye mabadiliko ya tabia na mwenendo wa mtoto kwa sababu ya mihemko na mwitikio wake unaomsumbua akiwa amelala usiku.

Katika barua yake, daktari ameshauri kuwa ni vema wazazi wasipuuzie wanapoona watoto wao wanakoroma wawapo usingizini, ama wanapopumua kwa kutumia mdomo, pia daktari ameelekeza kuwa, upasuaji wa tezi zilizovimba ni tiba kwa tatizo la kusigina meno kwa watoto.

Imesomwa mara 13335 Imehaririwa Ijumaa, 03 Agosti 2018 09:07
Dr. Barnabas Mbogo

Dr. Barnabas Mbogo ana utaalamu kwenye meno na programu za afya ya jamii kwa ujumla(Community Health Programs))

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana