Image

Mawe katika Figo (Kidney Stones)

Baadhi ya watu hukumbwa na tatizo la kuwa na vijiwe katika figo na mfumo wa mkojo kwa ujumla. Mawe haya hutokana na ama madini chumvi au tindikali mbalimbali zinazotolewa mwilini.

Aina za mawe katika figo

Aina za vijiwe katika figo ni pamoja na

 • vijiwe vya calcium oxalate
 • vijiwe vya tindikali ya uric (uric acid)
 • Vijiwe vya struvite (magnesium, ammonium na phosphate)

Vijiwe katika figo husababishwa na nini?

Kwa kiasi kikubwa, vijiwe husababishwa na kukosekana kwa usawa wa maji, madini na tindikali mwilini yaani electrolyte imbalance.

Aidha, kuna magonjwa kadhaa ambayo hupelekea kwa kiasi kikubwa kutokea kwa hali hii kama ugonjwa wa utindikali kwenye mirija ya figo (renal tubular acidosis) ugonjwa wa Dent, matatizo kwenye tezi za parathyroid (hyperparathyroidism), kukojoa chumvi chumvi za oxalate kupita kiasi (primary hyperoxaluria) na hali ya nyama za figo kuwa tepetepe (medulary sponge kidney).

Nani yupo katika hatari ya kupata tatizo hili?

Tatizo hili huwapata zaidi

 • Watu walio na historia ya familia ya kuwa na vijiwe kwenye figo
 • Walio na umri kuanzia miaka 40 na kuendelea ingawa tatizo hili laweza kutokea katika umri wowote
 • Wanaume kuliko wanawake
 • Walio na upungufu wa maji mwilini, kwa lugha rahisi wale wasiopenda kunywa maji katika kiwango kinachoshauriwa
 • Wanaopendelea kula zaidi vyakula vyenye kiasi kikubwa cha protini, chumvi au/na sukari
 • Walio na unene kupita kiasi (obesity)
 • walio na magonjwa ya utumbo mkubwa (inflammatory bowel diseases) au waliowahi kufanyiwa upasuaji wa tumbo (gastric bypass surgery)

Dalili za vijiwe katika figo ni zipi?

Dalili ni pamoja na

 • Kuhisi maumivu makali ya tumbo hasa sehemu za mbavu (colicky loin pain). Maumivu haya huwa na tabia ya kuja kwa ghafla, kudumu kwa sekunde kadhaa kisha kuachia. Maumivu huweza kushuka kuelekea kwenye ncha ya uume (tip of penis) kwa wanaume na kwa wanawake huelekea kwenye kinena.
 • Kujihisi kichefuchefu
 • Kutapika
 • Kukojoa mkojo uliochanganyika na damu (hematuria)
 • Wakati mwingine uwepo wa usaha katika mkojo (Pyuria) hasa iwapo kuna maambukizi ya bakteria
 • Maumivu wakati wa kukojoa (dysuria)
 • Mkojo kutoka kwa kiwango kidogo sana (oliguria)
 • Mkojo hushindwa kupita katika mirija ya ureter na kusababisha figo kushindwa kutoa uchafu mwilini na kusababisha mlundikano wa uchafu kwenye damu hali inayojulikana kama postrenal azotemia
 • Kushindwa kupita kwa mkojo husababisha pia kutanuka kwa sehemu tofauti za figo (renal pelvis na calyces) hali inayojulikana kama hydronephrosis
 • Iwapo kutakuwa na maambukizi katika mkojo, mgonjwa anaweza kuwa na homa

Vipimo na uchunguzi

Vipimo vinavyoweza kugundua tatizo hili na madhara yake ni pamoja na

 • X-ray inayoonesha mfumo mzima wa figo, mirija ya ureta pamoja na kibofu cha mkojo. Kipimo kingine huitwa intravenous pyelogram (IVP)
 • Vipimo vya CT-scan au MRI
 • Ultrasound ya tumbo
 • Kipimo cha mkojo na kuotesha (urine culture and sensitivity)
 • Kipimo cha damu (FBP)

Matibabu

Matibabu ya vijiwe katika figo hutegemea na ukubwa wa vijiwe husika. Iwapo vijiwe vina ukubwa mdogo na dalili alizo nazo mgonjwa ni chache na hazimzuii kuendelea na kazi zake za kila siku. mgonjwa anashauriwa

 • Kunywa maji mengi kiasi cha lita 2 mpaka 3 kwa siku. Hii husaidia kuviondoa vijiwe kutoka katika figo au njia ya mkojo
 • Kutumia dawa za maumivu ili kupunguza maumivu iwapo yatatokea

Iwapo vijiwe ni vikubwa na dalili ni nyingi na zinamfanya mgonjwa ashindwe kuendelea na kazi zake za kila siku, mgonjwa anaweza kutibiwa kwa kutumia

 • mawimbi mshtuko kutoka nje ya mwili (extracorporal shock wave lithotripsy) kuvunjavunja vijiwe na kisha vijiwe hivyo hutolewa nje kupitia kwenye mkojo
 • Upasuaji na kisha kuvitoa vijiwe (percutaneous nephrolithotomy)
 • Kifaa maalum kiitwacho ureteroscope
 • Wakati mwingine upasuaji wa kuondoa tezi za parathyroid hufanyika iwapo chanzo ni tatizo la hyperparathyroidism

Jinsi ya kuzuia tatizo la mawe katika figo

Mambo unayoweza kufanya kuzuia tatizo la vijiwe kwenye figo ni pamoja na

 • Kunywa maji mengi kwa siku, na kuhakikisha unakojoa angalau lita 2.5 za mkojo kila siku
 • Punguza utumiaji wa vyakula vyenye oxalate kama viazi vitamu, spinach, soya, chai na chocolate
 • Kula vyakula vyenye chumvi kidogo na punguza protein hasa itokanayo na nyama hivyo tumia itakonayo na jamii ya kunde na maharage
 • Potassium citrate husaidia kuongeza pH hivyo kuzuia wingi wa tindikali katika mwili
 • Kwa walio na tatizo la uzalishaji uliopitiliza wa tindikali ya uric, wanaweza kushauriwa kutumia dawa aina ya Allopurinol
Imesomwa mara 10653 Imehaririwa Ijumaa, 15 Januari 2021 15:49
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana