Image

Magonjwa ya Zinaa - 4: Ugonjwa wa Trichomoniasis

Ugonjwa wa Trichomoniasis ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya jamii ya protozoan vinavyojulikana kama Trichomonas vaginalis. Ugonjwa huu huathiri mrija wa kupitisha mkojo unaojulikana kama urethra na tupu ya mwanamke (vagina). Trichomoniasis pia hujulikana kwa majina mengine kama Trichomonas vaginitis au Trich (tamka “Trick”).

Trichomoniasis huathiri watu milioni 8 kwa mwaka Nchini Marekani na watu milioni 170 kwa mwaka dunia nzima. Ugonjwa huu huonekana sana kwa wanawake kuliko wanaume labda kutokana na wanaume kutoonyesha dalili zozote wakati wa maambukizi au kutokana na majimaji ya kwenye tezi dume kuwa na madini ya zinc ambayo huathiri vimelea hivi vya Trichomonas vaginalis. Ugonjwa huu hupatikana kwa njia ya kujamiana bila kutumia kinga na mtu aliyeathirika na Trichomoniasis.

Nakumbuka mwanajumuiya mmoja wa TanzMed aliuliza swali na hapa naomba ninukuu “madaktari, poleni na kazi za kila siku. mimi nina tatizo napata sana hizi yellowish discharge au niseme kama rangi ya maziwa hivi zinatoka huku chini kwenye tupu, asubuhi, mchana na jioni kama dose ya panadol. lakini hazina harufu kabisa, maana nilisoma makala zenu inasema kama zinatoa harufu ni dalili ya infections. Halafu za kwangu ni nzito hasa na zinavutika. Naomba msaada wenu sijui itakuwa ni nini?” mwisho wa nukuu.

Katika jibu langu nilimuahidi kuendelea na makala za magonjwa ya zinaa na leo naendelea na sehemu hii ya nne.

Nini hutokea wakati wa maambukizi/Pathofiziolojia ya ugonjwa (Pathophysiology)

Umbile la vimelea vya Trichomonas vaginalis ni sawa na chembechembe moja ya damu nyeupe kwa upana (10 μm) ingawa wakati mwingine ukubwa waweza kutofautiana kulingana na mazingira. Kutokana kuwepo kwa mfano wa mikono kwa nje inayojulikana kama flagellum ambayo husaidia vimelea hivi kuingia kwenye tishu za mrija wa kupitisha mkojo pamoja na tupu ya mwanamke na hivyo kuharibu seli aina ya epithelium na kusababisha vidonda (microulcerations) katika tishu hizi. Hii ndiyo sababu kubwa ya kwanini watu wanaopata ugonjwa huu wako kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa ukimwi (HIV) na magonjwa mengine.

Wagonjwa huwa na dalili zipi?

Dalili za Trichomoniasis huanza kuonekana kuanzia siku ya 4 mpaka ya 28 baada ya mtu kupata maambukizi ya ugonjwa huu. Kwa wanawake, Trichomoniasis huathiri shingo ya kizazi (cervix), mrija wa mkojo, tupu ya mwanamke, kibofu cha mkojo, tezi zinazojulikana kama Bartholin glands na Skene glands. Kwa wanaume vimelea hivi vya Trichomonas vaginalis hupatikana katika sehemu za siri za mwanamume, sehemu ya nje ya mrija wa kupitisha mkojo (anterior urethra), kwenye tezi dume (prostate), kwenye mirija ya kuhifadhi na kutoa shahawa (epididymis) na hata kwenye shahawa zenyewe.

Dalili kwa wanawake zinaweza kuwa

Uchafu unaotoka kwenye tupu ya mwanamke ambao unakuwa wa rangi mchanganyiko ya njano na kijani, au rangi ya kama kijivu na huwa mzito sana.

 • Maumivu wakati wa kujamiana (dyspareunia)
 • Harufu kutoka kwenye tupu ya mwanamke
 • Maumivu wakati wa kujisaidia haja ndogo (kukojoa)
 • Shingo ya kizazi kuwa nyekundu – hii hugundulika wakati daktari anamfanyia mgonjwa uchunguzi.
 • Kuwasha sehemu za siri – Kwa baadhi ya wanawake sio wote
 • Maumivu chini ya kitovu – Pia kwa baadhi ya wanawake

Ingawa wanawake ndio huonyesha dalili na viashiria vya ugonjwa huu, muda mwengine wanaweza kuwa na vimelea hivi hata kwa muda wa miaka kadhaa hata kama vipimo vya uchunguzi havitaonyesha (negative) kama ameathirika na vimelea hivi.

Wanaume huwa hawaonyeshi dalili zozote lakini baadhi wanaonyesha dalili zifuatavyo

 • Kuwasha ndani ya uume
 • Kutokwa na uchafu au majimaji kutoka kwenye uume wake
 • Kuwasha au kama kichomi (burning sensation) baada ya kujisaidia haja ndogo au baada ya kutoa shahawa.

Vipimo vya Uchunguzi

 • Trichomoniasis hugundulika kwa kutumia kipimo cha hadubini (Microscope), daktari humfanyia mgonjwa uchunguzi kwa kuingiza kifaa maalum katika tupu ya mwanamke kinachojulikana kama speculum na kuchukua kipimo kwa kutumia pamba maalum (cotton swab) na kupeleka maabara kuangalia kama kuna vimelea vya Trichomonas vaginalis. Kwa kufanya uchunguzi huu, daktari pia anaweza kuangalia kama kuta za ndani za tupu ya mwanamke au shingo ya kizazi kama zimeathirika kwa kuwa na vidonda ambavyo ni vyekundu (red ulceration). Kwa mwanamume, daktari huchukua kipimo cha uchafu unaotoka kwenye uume wake au hupangusa sehemu za siri za mwanaume kwa wale ambao hawatoi uchafu au majimaji yoyote kwa kutumia pamba na kupeleka maabara kufanyia uchunguzi.
 • Kipimo kilichochukuliwa na daktari kinaweza kuoteshwa kwenye maabara (culture) na kuangalia kama kutakuwa na uoto wa vimelea vya Trichomonas vaginalis baada ya siku tatu.
 • Daktari pia anaweza kuangalia kiwango cha kiwango cha tindikali (PH) kwenye tupu ya mwanamke kwa kutumia karatasi maalum ya kipimo hiki (PH paper), kiwango kitakuwa alkaline (PH zaidi ya 5). Kwa kawaida PH ya tupu ya mwanamke inakuwa ni ya tindikali (acidic) kuanzia 3.8 mpaka 4.5, magonjwa yanayobadilisha PH hii pamoja na Trichomoniasis ni Bacteria Vaginosis, atrophic vaginitis nk, na hivyo kumfanya mwanamke kuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi tofauti tofauti.
 • Kipimo cha damu kuchunguza Prostate Specific Antigen (PSA): PSA ni aina ya protein inayozalishwa na seli za tezi dume. Uzalishaji wake huongezeka wakati wa BPH, tezi dume inapopata uambukizi (prostitis), na saratani ya tezi dume. Kipimo hiki kifanywe kwa wanaume wanaopata ugonjwa wa Trichomianisis mara kwa mara au wale wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea na ambao wamepata ugonjwa huu, wafanye kipimo hiki angalau mara moja kwa mwaka.
 • Kipimo cha Pap smear – Chembechembe au seli za shingo ya kizazi huchukuliwa na kuchunguzwa kutumia hadubini. Kipimo hiki pia hutumiwa katika uchunguzi wa wanawake ili kujua kama wamepata saratani ya shingo ya kizazi au la. Wanawake wenye zaidi ya miaka 18 au wale wenye upungufu wa kinga mwilini wanashauriwa kufanya kipimo hiki angalau mara moja kwa mwaka ili wajue afya yao.
 • Elisa for HIV – Kipimo cha kuangalia maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi
 • Urinalysis – Kipimo cha mkojo
 • Complete Blood Count ama FBP –Kipimo cha damu kuangalia wingi wa damu, chembechembe tofauti za damu na chembechembe bapa (platelets).

Tiba ya Trichomoniasis

Tiba ya ugonjwa huu ni kutumia dawa aina ya metronidazole au flagyl. Kwa wanawake wajawazito, dawa hii haitumiki kwa wale wenye ujauzito wa chini ya miezi mitatu au kwa wale ambao wananyonyesha. Ni vizuri kumuona daktari kabla ya kutumia dawa hii.

Wale walioathirika, wanashauriwa kupata tiba pamoja na wenza wao. Madhara ya dawa ya metronidazole ni pamoja na mcharuko mwili (allergic reaction), kichefuchefu, kukauka midomo, kuharisha, kuhisi ladha kama ya chuma mdomoni, kushindwa kuhimili pombe na kushuka kiwango cha chembechembe nyeupe za damu (leukopenia) ambazo hutoa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali na hivyo kumuweka mtu kwenye hatari ya kupata maambukizi tofauti tofauti. Kwa wale wanaokunywa pombe ndani ya masaa 24 baada ya kumeza metronidazole, hupatwa na madhara kama kutapika, kuharisha, kichefuchefu, kukojoa na kutokwa jasho kwa wingi.

Madhara ya Trichomoniasis

Marejeo (References)

 • Laga M, Manoka A, Kivuvu M, et al. Non-ulcerative sexually transmitted diseases as risk factors for HIV-1 transmission in women: results from a cohort study. AIDS. 1993 Jan;7(1):95-10
 • Sorvillo F, Smith L, Kerndt P, Ash L. Trichomonas vaginalis, HIV, and African-Americans. Emerg Infect Dis. 2001 Nov-Dec;7(6):927-32
 • Danesh IS, Stephen JM, Gorbach J. Neonatal Trichomonas vaginalis infection. J Emerg Med. 1995 Jan-Feb; 13(1):51-4.

Usikose sehemu ya tano ya muendelezo wa makala za magonjwa ya zinaa

Imesomwa mara 13316 Imehaririwa Alhamisi, 05 Julai 2018 15:17
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.