Image

Ufahamu ugonjwa wa Malaria

Malaria ni ugonjwa unaoathiri watu wengi sana duniani. Malaria husababisha vifo vya watu milioni 2.7 duniani kote, ambapo vifo vingi hutokea barani Afrika. Ugonjwa wa malaria huonekana katika nchi 100 duniani kote.

Kwa Tanzania, mikoa ambayo inaongoza kwa maambukizi ya malaria ni Kagera (41.1%), Lindi (35.5%), Mtwara (36.6%), Mwanza (31.4%), Mara (30.3%). Mikoa ambayo  maambukizi ya malaria ni kidogo  ni Manyara (1%), Kilimanjaro (1%) na Dar-es-salaam (1.2%). Kwa Zanzibar, maambukizi ya malaria ni kwa asilimia 0.8.

Malaria huonekana sana katika kanda ya Tropiki.Ugonjwa huu wa malaria uligunduliwa mwaka 1880 na Charles Louis Alphonse Laveran, katika hospitali ya jeshi ya Constatine, Algeria, baada ya kuona vimelea vya plasmodium, kutoka kwa mgonjwa aliyefariki kwa ugonjwa huo.

Malaria ni kati ya magonjwa ya maambukizi ambao husababishwa na vimelea vya Plasmodium, ambavyo humfikia binadamu kupitia kung’atwa na mmbu aina ya Anopheles jike.

Kuna aina 5 za vimelea viletavyo malaria:

 1. Plasmodium falciparum - Hupatikana sana katika nchi zilizopo katika jangwa la sahara. Asilimia 75 ya wagonjwa wote wa malaria barani Afrika husababishwa na vimelea hivi. Mwaka 2006, kati ya watu milioni 247 duniani waliougua malaria, asilimia 91 walisababishwa na vimelea hivi (Afrika 98%) na kusababisha vifo kwa asilimia 90 mwaka huo huo barani Afrika.
 2. Plasmodium malariae - Pia hupatikana katika nchi zilizopo katika jangwa la sahara, Asia ya Mashariki, Indonesia na katika visiwa vya magharibi mwa Pacific. Kati vya vimelea vyote vya malaria, plasmodium malariae ndio huonekana kwa uchache zaidi.
 3. Plasmodium ovale - Hupatikana Afrika Magharibi, Ufilipino, Mashariki mwa Indonesia, Papua New Guinea, Cambodia, Bangladesh, India, Thailand na Vietnam.
 4. Plasmodium vivax - Huonekana katika bara la Marekani, Latin Amerika na baadhi ya sehemu za bara la Afrika.
 5. Plasmodium knowlesi - Hupatikana katika bara la Asia ya mashariki katika nchi za Bormeo, Myanmar, Malaysia, Ufilipino, Singapore na Thailand. Haipatikani katika bara la Afrika.

Mzunguko wa maisha ya vimelea vya malaria

Mwenyeji wa msingi ya vimelea vya malaria ni mbu aina ya anopheles wa kike, ambae pia ni msambazaji, na binadamu ni mwenyeji wa kati. Mbu anapokuwa anajipatia chakula kwa kunywa damu kwa kuuma binadamu mwenye maambukizi ya vimelea vya malaria, ndio mzunguko wa kwanza huanza, ambapo gametocyte za vimelea vya plasmodium hugawanyika ndani ya mbu na  kutengeneza gametocyte za kike na za kiume na baada ya hapo gametocyte hizo za kike na za kiume, hujiunga ndani ya mfumo wa chakula wa mbu na kutengeneza Ookinete ambayo hupenyeza kwenye kuta za mfumo wa chakula na kutengeneza Oocyst nje ya ukuta wa mfumo wa chakula, na hapo hupasuka na kutengeneza Sporozoites na kuhamia kwenye tezi za mate za mbu, na kuwa tayari kuambukiza binadamu mwengine pindi mbu anapojitafutia chakula.

Kwa mbu jike damu ndio lishe yake wakati dume lishe yake ni nekta ya mimea, hivyo mbu dume hasambazi ugonjwa huu. Na mbu jike aina ya anopheles hupenda kujipatia lishe kipindi cha usiku.

Maambukizi ya malaria yanaweza kupatikana kwa kuongezewa damu ingawa ni nadra sana.

Kwa Binadamu pindi anapong’atwa na mbu hupata maambukizi kupitia mate ya mbu, na vimelea vya plasmodium kwenye hatua ya sporozoites huingia kwenye damu na kuelekea kwenye ini ambapo hutengeneza schizonts na baadae schizonts hupasuka na kuachia merozoites kuelekea kwenye damu na kutengeneza immature trophozoite  kiataalamu zinajulikana kam ring stage ambapo baada ya hapa huwa kuna hatua mbili tofauti zinazofuata,hatua ya kwanza ni mature trophozoites na kutengeneza schizont nyingine kwenye damu na vilevile schizont hii hupasuka na kutoa immature trophozoites na kuendelea kujirudia tena hatua hii. Hatua nyingine ni gametocyte ambayo hubebwa na mbu.

Dalili za ugonjwa wa malaria

 • Homa
 • Maumivu ya kichwa
 • Kichefuchefu
 • Kutapika
 • Maumivu ya misuli
 • Manjano
 • Degedege
 • Kupoteza fahamu
 • Kukua kwa wengu
 • Dalili za mwanzo hutokea kati ya siku 10 hadi wiki 4, na dalili nyingi hutokea pale hatua ya merozoites inapoachiwa nyingi kwenye damu baada ya schizonts kupasuka.


Madhara ya ugonjwa malaria

 • Malaria ya kichwa (cerebral malaria)
 • Matatizo ya kupumua (pulmonary edema)
 • Viungo kushindwa kufanya kazi (organ failure)
 • Upungufu wa damu
 • Upungufu wa sukari mwilini (hypoglycemia)
 • Shinikizo la chini la damu (hypotension)
 • Haemoglobinuria
 • Disseminated intravascular coagulopathy
 • Metabolic acidosis

Vipimo na uchunguzi

 • Kipimo cha damu na kutumia hadubini
  • Thin film--hutumika kutambua aina ya vimelea vya plasmodium (falciparum,ovale,vivax,malariae)
  • Thick film---hutumika kutambua idadi ya vimelea/µL
 • Kipimo cha damu bila kutumia hadubini
  • Malaria Rapid Diagnostic Test
 • PCR

Matibabu

 • Dawa za malaria
  • Mstari wa kwanza (dawa mseto)
   • Artemether plus Lumefantrine
   • Dihydroartemisinin plus Piperaquine
  • Mstari wa Pili
   • Amodiaquine
  • Mstari wa tatu
   • Quinine
 • Dawa za kushusha homa na maumivu
 • Paracetamol

Kama sehemu ya tiba, mgonjwa anashauriwa pia kula na kunywa maji ya kutosha.


Jinsi ya kuzuia maambukizi ya Malaria

 • Kuzuia mazalio ya mbu
  • Fyeka vichaka na ondoa madimbwi ya maji katika  maeneo yanayokuzunguka.
 • Kuzuia kung’atwa na mbu
  • Matumizi ya vyandarua vyenye dawa ya kuua mbu
  • Matumizi ya dawa za kupulizia za kuua mbu majumbani
  • Matumizi ya dawa za kupaka za kuua mmbu
 • Dawa za kuzuia malaria kwa wasafiri watokao nchi sizizo na malaria
  • Proguanil
  • Malarone
  • Mefloquine
 • Dawa za kuzuia malaria kwa kina mama wajawazito (IPT)
  • Sulfadoxine Pyrimethamine (SP) hutolewa kwa kina mama katika wiki ya 20 na wiki ya 36 ya ujauzito.
Imesomwa mara 15116 Imehaririwa Jumanne, 26 Januari 2021 13:36
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana