Image

Ugonjwa wa Marbug, Chanzo, Dalili na Tiba

Marburg virus disease (MVD) ni ugonjwa mkongwe na nadra kukutana nao lakini ni ugonjwa mbaya sana ambao mara nyingi hatima yake ni kifo. Ugonjwa huu husababishwa na virusi vya aina mbili,  Marburg virus (MARV) and Ravn virus (RAVV) vilivyo katika kundi la virusi liitwalo  Orthomarburgvirus marburgense. Ugonjwa huu uligundulika kwa mara ya kwanza mwaka 1967 nchini Ujerumani na Serbia. Virusi hivi kwa kawaida hupatikana katika aina ya popo waitwao Rousettus aegyptiacus.

Ugonjwa wa MVD upo kwenye kundi la magonjwa yaitwayo viral hemmorhagic fevers. Viral hemorrhagic fever (VHFs) ni kundi la magonjwa yanayosababishwa na virusi vinavyoharibu mishipa ya damu na kusababisha kutokwa na damu nyingi. Magonjwa mengine kwenye kundi hili ni Ebola, yellow fever, rift valley fever, dengue fever n.k.

Virusi vya Marburg Vinasambazwaje?

Awali, maambukizi ya MVD kwa binadamu yalitokana na kukaa kwa muda mrefu ndani ya migodi au mapango ambapo makoloni ya popo wa  Rousettus huishi.

Lakini baada ya ugonjwa huu kuanza kusambaa kwa binadamu, virusi vya Marburg vimejulikana kua na uwezo wa  kuenea kupitia

  1. Mgusano wa moja kwa moja (kupitia ngozi iliyo na majeraha  au utando wa mucous).
  2. Damu na maji mengine ya mwilini ya watu walioambukizwa kama vile kinyesi,mkojo,jasho, matapishi, manii n.k
  3. Kugusa vitu na mavazi yaliyotumika na mtu mwenye maambukizi au vitu vilivyochafuliwa na majimaji ya mwilini kutoka kwa mtu mwenye maambukizi.( nguo,godoro,mashuka na maforonya, vyombo n.k)
  4. Kula au kugusa mizoga au wanyama walioambukizwa ugonjwa huo kama popo,nyani n.k

Watoa huduma za afya Wako katika hatari kubwa sana na wengi wameambukizwa na wengine kupoteza maisha wakati wa kutoa matibabu kwa wagonjwa na MVD. Hii hutokea kwa kuwasiliana kwa karibu na wagonjwa wakati tahadhari za udhibiti wa maambukizi hazifanyiki kikamilifu. Uambukizaji hutokea kupitia sindano au kupitia majeraha au matone ya maji yanayotoka kinywani mwa mgonjwa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuongea.

Watu hawawezi kusambaza ugonjwa wa MVD kabla ya kuanza kuonyesha dalili. Lakini pindi dalili zinapoanza wataendelea kuambukiza wengine kwa muda wote ambao miili yao bado itakua na virusi hivyo.

 Dalili za Virusi vya Marburg

Dalili za virusi vya Marburg zinaweza kuanza ndani ya siku 2 hadi 21 baada ya kuambukizwa. Dalili za mwanzo zinaweza kuwa kama za homa ya kawaida, lakini hubadilika kuwa mbaya kwa haraka. Dalili hizi zinaweza kujumuisha:

Siku tano za mwanzo

  • Homa kali
  • Maumivu makali ya kichwa
  • Maumivu ya mwili na misuli
  • Uchovu
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Kuhara
  • Upele usiowasha
  • Maumivu ya kifua
  • Ugumu katika kupumua

Baada ya siku tano za kuanza dalili, wagonjwa huanza dalili kali/mbaya za

  • Kutokwa na damu puani, kwenye fizi ,uke na  sehemu nyingine za mwili
  • Kutapika damu
  • Kuharisha damu

Kuathirika kwa mfumo wa fahamu kunaweza kuleta dalili kama :

  • Kuchanganyikiwa (confussion)
  • Kushindwa kutulia (irritability)
  • Uchokozi (Aggression)

Katika hatua za baadae pia imeripotiwa kuwa na maumivu ya korodani moja au zote mbili.

*Vifo vingi huanza kutokea kwanzia siku ya nane kuendelea na mara nyingi husababishwa na upotevu mwingi wa damu.

Jinsi ya Kujikinga na Virusi vya Marburg

  • Epuka mawasiliano  ya karibu na wagonjwa bila kujikinga: Ikiwa unajua mtu anayeugua ugonjwa huu, epuka kugusa maji yao ya mwili na vitu vilivyochafuliwa na maji yao ya mwili.
  • Osha mikono yako mara kwa mara: Tumia sabuni na maji safi wakati wa kuosha mikono na epuka kujigusa usoni,puani, machoni bila kunawa mikono.
  • Pika chakula vizuri: Hakikisha chakula unachokula kimepikwa vizuri.
  • Epuka maeneo yaliyotangazwa kua na mlipuko wa ugonjwa huu.
  • Waambie watoa huduma za afya mapema ikiwa una dalili zozote:
  • Ikiwa una dalili za virusi vya Marburg, ni muhimu kuonana na daktari kwa haraka.

Matibabu ya Virusi vya Marburg

Kwa sasa, hakuna tiba maalum ya virusi vya Marburg. Matibabu yanalenga kupunguza dalili na kurahisisha kazi ya mwili. Wagonjwa wote wanahitaji kutibiwa na kulazwa katika mazingira salama ya hospitali yaliyotengwa maalumu kwa wagonjwa wa MVD.

Kinga ni bora kuliko tiba. Kwa kufuata hatua za tahadhari, unaweza kujikinga na virusi vya Marburg.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Imesomwa mara 152 Imehaririwa Jumanne, 28 Januari 2025 18:29
Dr Ladina Msigwa

Distinguished medical doctor and acclaimed author with a passion for enhancing healthcare and sharing knowledge through the written word.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.