Image

Mambo 10 ambayo daktari wako wa meno angependa ufahamu

Watu wengi huwa na hofu ya sintofahamu hasa wanapofikiria kwenda kumwona daktari wa meno. Mambo 10 yafuatayo yatakusaidia sana kufahamu nini utarajie unapokwenda kufuata uchunguzi wa afya ya kinywa na meno ama matibabu ya magonjwa ya kinywa na meno.

1. Uchunguzi wa afya ya kinywa na meno hujuimuisha uchunguzi wa kansa kinywani

Unapokwenda kwa daktari wa kinywa na meno kwa uchunguzi wa kawaida wa kinywa na meno (dental check up visit), kwa kawaida daktari wa kinywa na meno hutazama hali ya kinywa na meno pia huchunguza uwepo wa dalili za kansa kinywani. Inakadiriwa kuwa mtu mmoja hufa kila saa la kutokana na ugonjwa wa kansa kinywani huko Marekani. Ugonjwa huu hatari unaoshambulia zaidi kuta za kinywa, midomo-hasa mdomo wa chini- pamoja na koo unatibika ikiwa utatambuliwa mapema na kutibiwa kikamilifu.

Hivyo, kumwona daktari wa meno walau mara mbili kwa mwaka (kila baada ya miezi sita) na kuepuka matumizi ya tumbaku/sigara vitakuwezesha kujikinga na ugonjwa wa kansa ya kinywa na madhara yake.

2. Magonjwa ya fizi huathiri afya ya mwili kwa ujumla

Magonjwa ya fizi na meno ni chanzo kikuu cha kupoteza meno kwa watu wenye umri mkubwa/watu wazima, na pia magonjwa haya huhusishwa na magonjwa ya moyo na kiharusi (stroke).

Ikiwa magonjwa haya ya fizi yatatambuliwa mapema (gingivitis), yanatibika vizuri na kuepusha madhara zaidi.

Ikiwa tatizo hili halitopata tiba mapema, ugonjwa hukomaa zaidi (periodontitis) ambapo mfupa unaoshikilia jino/meno hushambuliwa na kuharibiwa.

Kusafisha meno kwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku, matumizi ya nyuzi-safishi (dental floss), kumwona daktari wa meno kwa uchunguzi mara kwa mara na kusafisha meno kitaalamu kwa tatibu wa meno, kutasaidia kuepuka madhara ya magonjwa ya fizi.

3. Uchunguzi wa kinywa na kusafisha meno kitaalamu ni tiba muhimu zaidi

Ni wangapi kati yetu wenye desturi ya kumwona daktari wa meno walau mara mbili kwa mwaka (walau kila baada ya miezi sita)? Mara nyingi wengi wetu huhangaika na foleni za kumwona daktari wa meno pale tu tunaposumbuliwa na maumivu ama ya jino ama kidonda kinywani ama kwa sababi ya hali zinginezo zinatotulazimisha kumwona daktari wa meno.

Kusubiri mpaka tusukumwe na maumivu ya meno/kidonda kinywani ama ajali yoyote kunatunyima fursa bora zaidi ya kuchunguzwa afya ya kinywa na meno na kusafishwa meno ili kuepusha madhara ya magonjwa ya kinywa na meno kabla hayajatokea ama kukomaa.

4. Kupiga mswaki mara mbili kwa siku kunaepusha kuoza kwa meno

Kupiga mswaki kwa ufanisi walau mara mbili kwa siku huondoa ukoko unaogandiana kinywani na kusababisha kuoza kwa meno. Ukoko huu ni ute laini unaoganda kwenye sehemu mbalimbali za jino/meno huku ukiwa na mamilioni ya vimelea vya magonjwa (bakteria). Matumizi ya nyuzi-safishi (dental floss) kila siku husaidia kuondosha ukoko maeneo ambako mswaki haufiki, vile vile kuondosha ukoko huu kunasaidia kujikinga na magonjwa ya fizi.

5. Magonjwa ya kinywa na meno husababisha harufu mbaya mdomoni

Takribani asilimia 85 ya watu wenye harufu mbaya kinywani huwa na magonjwa ya kinywa na meno,Ikiwa harufu mbaya kinywani inasababishwa na magonjwa kinywani, dawa za kusafisha kinywa (mouthwash) haziwezi kuondoa tatizo zaidi ya kulifunika kwa muda tu.

Hakuna sababu ya kuona haya kumwambia daktari wa meno kuhusu harufu mbaya kinywani inayokusumbua, kwa vile kumwambia na kujadili tatizo lako ni njia ya kuelekea kwenye tiba ya uhakika. Matumizi ya nyuzi-safishi (dental floss) kila siku, kusafisha meno na ulimi kwa mswaki walau mara mbili kwa siku yaweza kuondoa harufu mbaya kinywani kwa kiasi kikubwa.

6. Chakula bora ni muhimu kwa afya bora ya kinywa na meno

Ulaji wa vyakula na vinywaji vyenye sukari na visivyo na virutubisho vya mwili vinapochanaganyikana na vimelea vya magonjwa (bakteria) hutengeneza tindikali ambayo hushambulia ukuta wa nje wa jino (dental enamel). Kushambuliwa kwa enameli na tindikali husababisha mashimo kwenye meno na magonjwa ya fizi.

Kudhitibi na kupunguza ulaji wa vyakula vyenye sukari kwa wingi itakuepusha na magonjwa ya kinywa na meno.

7. Bila matibabu, magonjwa ya kinywa na meno hayaponi wala kupata nafuu

Pale daktari wako wa meno anapokupa mpango makakati wa matibabu ya kinywa na meno yako, jukumu lako ni kuzingatia maagizo na maelekezo ya daktari ili upate matokeo mazuri. Inapotokea una mashimo makubwa kwenye meno, bado inawezekana kutibu meno kuanzia kwenye mzizi kabla meno hayajang'olewa.

8. Tiba ya mzizi wa jino haina maumivu

Amini usiamini, sio jambo la kustaajabisha kusikia mgonjwa aking'ang'ania jino ling'olewe kwa madai kuwa matibabu ya jino kuanzia kwenye mzizi wake ni yenye maumivu ya kupindukia, yasiyovumilika.

Ukweli ni kwamba, maendeleo ya teknolojia tiba yamefanya matibabu ya jino kuanzia kwenye mzizi kuwa rafiki na rahisi, tena hayana sifa yoyote ya maumivu makali kupindukia kama ambavyo watu wengi wanaamini, tiba hii ni moja ya tiba rafiki sana kwenye ulimwengu wa matibabu ya kinywa na meno.

9. Badili mswaki mara kwa mara

Umri wa miswaki tunayotumia unapaswa kuwa miezi mitatu (siku 90), baada ya muda huu ufanisi wa mswaki hupotea. Ikiwa unasumbuliwa na magonjwa ya fizi unashauriwa kubadili mswaki kila baada ya majuma manne hadi sita (wiki 4 – 6), kwa sababu vimelea vya magonjwa (bakteria) hijificha kwenye brush za mswaki. Vile vile unashauriwa kuosha mswaki wako kwenye maji ya moto kila baada ya kuutumia na kuubadilisha kila unapopata mashambulizi ya ugonjwa wa fizi.

10. Ni rahisi sana kutunza afya ya kinywa na meno

Watu wengi hifikiri kuwa kuwa na afya bora ya kinywa na meno kunahitaji jitihada za ziada, Ukweli ni kuwa, kumwona daktari wa meno mara kwa mara (walau mara mbili kwa mwaka kila baada ya miezi sita), na kusafisha meno kitaalamu, kupiga mswaki walau mara mbili kwa siku (asubuhi baada ya kupata kifungua kinywa, na usiku kabla ya kulala), kutumia nyuzi-safishi (dental floss), ulaji wa chakula bora chenye virutubisho ni vigezo muhimu sana vya kuwa na afya njema ya kinywa na meno, sasa ugumu upo wapi?

Imesomwa mara 10910 Imehaririwa Jumatatu, 15 Mai 2017 09:36
Dr. Augustine Rukoma

Dr Dr. Augustine Rukoma ni daktari na mtaalamu wa meno, anapenda kutumia muda wake wa ziada kuandika makala na kubadilishana mawazo juu ya afya ya kinywa na Meno.

rukomadentalanswers.blogspot.com | Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana