Image

Je wajua sababu zainazopelekea mapacha kuzaliwa wameungana (Conjoined twins)

Kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazoripotiwa hapa nchini kuhusu watoto wanaozaliwa wakiwa wameungana. Jamii ya watanzania itawakumbuka sana watoto wa aina hiyo waliofahamika kwa majina ya Mariamu na Consolata ambao kwa sasa ni marehemu.Watoto hawa walikuwa faraja kubwa kwa taifa baada ya kuweza kuishi na kusoma hadi ngazi ya kuingia Chuo Kikuu.

Aidha kumekuwa na riporti za watoto wengine walioungana hapa nchini. Ripoti hii ilitolewa  na zahanati ya St. Theresa Health Centre iliopo Kyaka wiliyani Misenye.

Tafiti zinaonyesha kwenye kila uzao wa 50,000-200,000 kunakuwepo na pacha moja iliyoungana. Mara nyingi huzaliwa wamekufa na wengine hufa kipindi kidogo tu baada ya kuzaliwa na wengine huweza kuishi kwa kipindi fulani. Aina hii ya pacha hutokea zaidi kwa jinsia ya kike kwa uwiano wa 3:1 na jinsia ya kiume.

Tafadhali tuungane pamoja katika makala hii ili tujifunze kuhusu watoto hawa wanaozaliwa huku wameungana.

Watoto walioungana (conjoined twins) ni mapacha ambao maumbile yao yameungana tangu wakiwa katika mfuko wa uzazi na baada ya kuzaliwa. Hali hii hutokea kufuatia kuungana au kutokugawanyika kwa yai lililopevushwa wakati wa ukuaji wa awali.

Kawaida yai moja lililopevushwa hugawanyika zaidi katika siku ya 13 baada ya yai hilo kupevushwa (monozygotic twin pregnancy).Kutokugawanyika kwa yai hili lililopevushwa husababisha mapacha kuzaliwa wakiwa wameungana.Kuna aina mbili za mapacha walioungana;

  1. Mapacha wanaotumia kondo moja la nyuma (single placenta) hujulikana kama monochromic twins au
  2. Mapacha wanaotumia amniotic sac moja hujulikana kama monoamniotic twins

Mapacha walioungana husababishwa na kushindwa kuungana au kutengana kwa yai liliopevushwa wakatii wa ukuaji wa awali, japo hii haiwezi kuelezea kila aina ya kuungana (conjuction)

Ziko aina nyingi za mapacha walioungana (conjoined twins) na wanaweza kuwekwa kwenye makundi makubwa mawili;

  1. Non dorsally conjoined twins- Aina hii ya mapacha walioungana huchangia kitovu kimoja (umbilical cord) moja na  baadhi ya viungo vya ndani ya mwili (internal organs) 
  2. Dorsally conjoined twins -Hapa kila pacha anakuwa na (umbilical cord ) yake na mara nyingi hawachangii viungo vya ndani ya mwili.Hii hutokea pindi pacha hawa wamegawanyika na baadaye kuugana tena ( secondary fusion) katika hatua ya ukuaji wa awali.

Pathofiziolojia

Pacha hawa hutokea baada ya mgawanyiko (cleavage or axis duplication) kutokea baada ya siku ya 13 ya kupevushwa kwa yai. Inaaminika kawaida mgawanyiko huu hutokea siku ya 8 hadi ya 12. Sasa ukitokea baada ya hapo mgawanyiko huo ukianza huishia njiani hivyo husababisha aina hii ya mapacha.

Tafiti nyingine husema pacha waliogawanyika vizuri wanaweza kuungana tena katika hatua za awali za ukuaji kwenye mfuko wa uzazi na kupelekea aina hii ya pacha.

Kisababishi cha matukio haya kutokea bado hakijulikani.

Zifuatazo ni aina za mapacha walioungana (conjoined twins)

Thoraco-omphalopagus-Aina hii ya pacha wameungana  kifuani na kwenye tumbo. Hii ndo aina inayoonekana sana kwa asilimia 28. Mara nyingi hawa huchangia moyo mmoja, ini (liver) na hata sehemu ya juu ya utumbo (upper intestine).

Thoracopagus- Aina hii ya pacha wameungana kifuani tu. Ndo aina inafuatia na hutokea kwa asilimia 18. Wanaweza kuchangia moyo mmoja na ini.

Omphalopagus- Aina hii ya pacha huungana tumboni  karibu na kitovu.  Aina hii hutokea kwa asilimia 10. Hawa huchangia ini moja na sehemu ya utumbo mkubwa (colon) na utumbo mdogo wa chini.

Heteropagus (Parasitic twins). Aina hii nayo hutokea kwa asilimia 10. Aina hii kunakuwa na pacha mmoja mwenye hitilafu ameungana na pacha mwingine mzima.

Craniopagus- Aina hii hutokea kwa asilimia 6. Vichwa vinakuwa vimeungana. Na mara nyingi wachangia ubongo mmoja.

Ziko aina nyingine ambazo hutokea mara chache sana kama zifuatavyo;

Pyopagus- Aina hii mapacha wanaungana kwenye mgogo wa chini na makalio. Hawa huweza kuwa wanachangia sehemu ya utumbo na sehemu za siri mfano uume au uke

Rachipagus -Aina hii mapacha wameungana nyuma kwenye mgongo wote juu hadi chini.

Ischiopagus- Aina hii ya mapacha wameungana kwenye nyonga upande au uso kwa uso. Pacha hawa wanaweza kuchangia utumbo wa chini na sehemu za siri. Pia wanaweza changia miguu miwili au mitatu.

Cephalopagus- Aina hii ya mapacha wanaungana kuanzia kwenye kichwa hadi kwenye kitovu. Aina hii hi ngumu kuishi.

Historia ya mama

Mama wa mapacha aina huu hana tofauti na mama mwenye mapacha wa kawaida. Hamna dalili yoyote ya tofauti kwake.

Uchunguzi

Mapacha hawa wanaweza kugundulika kwa kipimo cha ultrasound mwanzo kabisa mwa ujauzito. Au kwa kutumia Prenatal Magnetic Resonance imaging (MRI)

Tiba

Mapacha wanaoishi baada ya kujifungua  wanaweza wekwa kwenye makundi makuu mawili

  1. Wale ambao wanaweza kutenganishwa kwa upasuaji
  2. Wale wasioweza kutenganishwa kwa upasuaji

Kwenye tiba ya upasuaji uchunguzi wa kina unafanywa ili kubaini uwezekano wa kuwatenganisha hasa kama wanachangia baadhi ya viungo muhimu kama moyo. Upasuaji wa kuwatenganisha mapacha walioungana uhusisha timu za wataalamu wa afya wabobezi kutoka fani mbalimbali za afya. Wakati mwingine upasuaji unaweza sabibisha pacha mmoja ua wote kupoteza maisha.

Tanzania ilishafanikiwa kufanya upasuaji wa aina hii wa kutenganisha mapacha walioungana katika hospitali ya taifa ya Muhimbili National Hospital(MNH)

 

Picha: BBC

Imesomwa mara 2938 Imehaririwa Jumatano, 03 Machi 2021 09:50
Dr Hamphrey

Dr. Hamphrey S. Kabelinde MD ni mhitimu wa shahada ya Udaktari katika Chuo kikuu ya afya na sayansi shirikishi Muhimbili. Mwandishi na mhariri wa makala za afya Tanzmed.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.