Image

Vyandarua Vilivyowekwa Dawa

Chandarua hutoa kinga dhidi ya mbu, nzi na wadudu mbali mbali wasambazao magonjwa, hivyo kuzuia magonjwa kama malaria, homa ya dengue na homa ya manjano.

Ufanisi wa kazi wa chandarua huwa maradufu kinapowekwa dawa ya kuua wadudu.

Vyandarua vilianza kutumika lini?

Vyandarua vilianza kutumika kuanzia katikati ya karne ya kumi na nane (mid-18th century), inasadikiwa kuwa hata yule malkia maarufu wa Misri Cleopatra alitumia chandarua. Vilevile vyandarua vilitumika wakati wa ujenzi wa mfereji wa suez baada ya malaria kutishia umaliziaji wa ujenzi wa mfereji huo.

Chandarua hutengenezwa kwa kutumia: pamba, polyester, polyethylene au nylon

Vyandarua vyenye dawa

Vyandarua vyenye dawa vilianza kutumika miaka ya 1980 kwa ajili ya kuzuia malaria. Na hadi sasa vyandarua hivi vinaanza kutumiwa kama mmbadala wa vyandarua vya zamani katika nchi nyingi, Tanzania ikiwa ni mojawapo ya nchi hizo.
Inaaminika kuwa vyandarua vyenye dawa vinafanyakazi maradufu ya vyandarua visivyo na dawa. Chandarua hutoa kinga ya asilimia 70 dhidhi ya malaria kulinganisha na kulala bila chandarua.

Katika tafiti iliyofanywa na Deswal na wenzake iliyochapishwa September 2004, katika kambi za jeshi katika mji wa Allahad, nchini India waligundua kuwa maambukizi ya malaria yalipungua kwa kiasi kikubwa baada ya kutumia vyandarua vyenye dawa, na mbu aina ya Anophiline walipungua kwa asilimia 67.8 wakati culex walipungua kwa asilimia 49. Na watumiaji hawakupata madhara yoyote. Na hivyo walithibitisha kuwa matumizi ya vyandarua vyenye dawa husaidia kupunguza malaria kwa kiasi kikubwa.

Kwa sasa vyandarua vingi huwekewa dawa aina zifuatazo: Deltamethrin na Permethrin. Kwa ufanisi mzuri wa chandarua chenye dawa, ni vyema kila baada ya miezi sita kukiwekea tena dawa,ili kiweze kufanya kazi vizuri.

Kwanini watu wengi hawatumii vyandarua vyenye dawa?

Tafiti mbalimbali zimeshafanyika kuhusiana na kwanini watu wengi hawatumii vyandarua vyenye dawa hata kama watapewa bure na serikali. Katika utafiti uliofanyika pembezoni mwa mto Imo, Nigeria iliyochapishwa machi 2010 “kuhusiana na mtazamo wa matumizi ya vyandarua vyenye dawa na athari yake katika kuzuia malaria kwa wakina mama wajawazito” uliofanywa na chukwuocha UM na wenzake waligundua kuwa mtazamo wa wananchi kuhusu malaria kuwa wanawake wajawazito na watoto wapo kwenye hatari zaidi ya kupata malaria kuliko wanaume na wanawake ambao hawana watoto kabisa kwa sababu miili yao ni dhaifu. Vilevile walipata sababu za kutotumia vyandarua vyenye dawa kuwa ni:

  • Gharama na upatikanaji wake
  • Vilevile wanaamini kemikali za dawa zinazowekwa zinamadhara kwa watu wazima,watoto na wanawake wajawawazito
  • Wengi walipata matangazo kuhusu umuhimu wa vyandarua vyenye dawa
  • Wengi waliamini dawa hizo zitumikazo kwenye vyadarua huleta madhara yafuatayo:
    • huathiri upumuaji hasa kwa wakina mama wajawazito na kama zinaua mbu basi zinaweza kuua hata binadamu.
    • Wapo pia watumiaji wengi walioripoti kuhisi joto kali na kukosa hewa ya kutosha wakiwa wamelala usiku.

Nini mtazamo wa matumizi ya vyandarua vyenye dawa katika nchi nyingi za afrika?

Kwa ujumla kuna imani na mitazamo mbalimbali kuhusiana na matumizi ya vyandarua vyenye dawa kikubwa kikiwa kuhusishwa na kupunguza nguvu za kiume na kuaminini kuwa zinaweza kuleta madhara makubwa kwa binadamu.

Hitimisho

Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa zinathibitisha kuwa Hamna madhara kwa binadamu na matumizi mazuri ya vyandarua vyenye dawa hupunguza maambukizi ya malaria kwa kiasi kikubwa.

Nikisema matumizi mazuri namaanisha kuwa uhakikishe umelala katikati hamna ngozi inayogusa chandarua hasa kwa vile ambavyo havina dawa maana mbu huweza kukuuma, na kuhakikisha hakija chanika na kimechomekwa vizuri. Na kutosahau kukiwekea dawa tena baada ya miezi sita.

Imesomwa mara 30524 Imehaririwa Jumatatu, 31 Julai 2017 11:09
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.