Image

Aspirin Hupunguza Uwezekano wa Kuugua Kansa

Matokeo ya utafiti mmoja huko nchini Uingereza yameonesha kuwa utumiaji wa wastani wa dawa aina ya Aspirini kila siku hupunguza uwezekano wa mtumiaji kufa kutokana na kansa.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo, watafiti hao wanadai kugundua ushahidi wa uhakika kuwa utumiaji wa kila siku wa kiwango kidogo cha Aspirini hupunguza uwezekano wa kufa kutokana na kansa kwa karibu asilimia 30 ndani ya miaka mitano ya mwanzo ya utumiaji wa dawa hiyo.

Utafiti huo umeonesha kuwa, uwezekano wa kufa kwa sababu ya kansa hupungua kwa karibu asilimia hamsini kwa baadhi ya aina ya kansa na kwa kadiri mtu anavyotumia Aspirini kwa muda mrefu, uwezekano wa kufa kwa Kansa huzidi kupungua zaidi.

Watafiti hao wamedai kuwa watu wa umri wa kati ya miaka 45 hadi 50 na ambao hawana dalili ya magonjwa yeyote yale, ambao huanza kutumia dawa hii ya aspirini kwa kiwango kidogo kwa wastani wa miaka kati ya 20 hadi 30 wanaweza kufaidika zaidi kwa vile imeonekana kuwa uwezekano wa mtu kuugua kansa una uhusiano wa karibu na umri wake.

Inafahamika tangu awali kuwa kutumia kiwango cha milligrams kati ya 50 hadi 75 ambacho ni takribani robo ya kiwango cha kawaida cha kidonge cha Aspirini husaidia sana kuulinda moyo usipatwe na shinikizo. Faida hii imethibitika hata miongoni mwa watu ambao hawakuwahi kuonekana kuwa na magonjwa ya moyo hapo awali.

Watafiti hao wamedai kuwa, mamilioni ya watu ambao walikuwa wanatumia Aspirini katika kiwango hiki kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya moyo, wapo katika nafasi nzuri zaidi ya kuepuka kupata au kufa kutokana na magonjwa ya kansa.

Hata hivyo kumewahi kuwa na hofu huko nyuma kuhusu tabia ya Aspirini katika kusababisha vidonda vya tumbo au kutapika damu kunakoletwa na kukwanguliwa kwa ukuta wa tumbo kunako sababishwa na matumizi yaliyopitiliza ya dawa hii. Hata hivyo Prof. Peter Rothwell wa hospitali ya John Radcliffe jijini Oxford, ambaye aliongoza jopo la watafiti waliofanya utafiti huo anaamini kuwa faida za utumiaji wa Aspirini zinazidi madhara yake.

Prof Rothwell anasema “Matokeo haya ya utafiti wetu yanaonesha kuwa faida zitakazopatikana kwa kutumia Aspirini katika kupunguza vifo vitokanavyo na kansa zitapelekea kubadilishwa kwa kanuni zinazotawala matumizi yaliyozoeleka ya Aspirini.” 

Matokeo ya utafiti huo yaliyochapishwa katika jarida la utafiti la The Lancet yalionesha kuwa kulikuwa na matokeo ya kuridhisha juu ya uwezo wa Aspirini katika kupunguza uwezekano wa kutokea kwa vifo vilivyosababishwa na kansa.

Ilionekana kuwa baada ya miaka mitano ya kutumia Aspirini, kiwango cha vifo kutokana na kansa kilipungua kwa asilimia 34 kwa aina zote za kansa zilizotafitiwa na asilimia 54 kwa kansa zinazoathiri mfumo wa chakula.

Hata hivyo ni idadi ya wanawake waliohusishwa katika utafiti huo ilikuwa ndogo kiasi cha kushindwa kutoa matokeo ya kuridhisha kuhusu uhusiano kati ya matumizi ya Aspirini na vifo visababishwavyo na kansa ya matiti kwa kina mama.

Imesomwa mara 5149 Imehaririwa Alhamisi, 18 Mai 2017 13:29
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana