Image

Masundosundo au vigwaru au Genital warts ni vinyama laini vidogo vinavyoota kwenye ngozi au utando laini unaozunguka maeneo ya siri. Vinaweza kutokea kwenye uume, uke, mrija wa mkojo [urethra], vulva, shingo ya kizazi [cervix], au maeneo ya kuzunguka njia ya haja kubwa au ndani yake.

Huu ni ugonjwa unaoenezwa kwa njia ya kujamiiana [sexually transmitted infection (STI)].

Visababishi

Ugonjwa wa masundosundo husababishwa na jamii ya virusi wanaoitwa Human papilloma virus (HPV). Kuna zaidi ya aina 70 tofauti za virusi wa HPV ingawa si wote wanaosababisha masundosundo kwenye maeneo ya siri [genital warts]. Baadhi ya aina nyingine za HPV husababisha masundosundo kwenye ngozi inayozunguka sehemu nyngine za mwili kama vile kwenye mikono au miguu. 

Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa baadhi ya aina za virusi wa HPV pia husababisha saratani ya shingo ya kizazi [carcinoma of the cervix] kwa wanawake au saratani ya njia ya haja kubwa [anal cancer] kwa jinsia zote mbili. Aina hii ya virusi hujulikana pia kama high-risk HPV.

Pamoja na kwamba ugonjwa wa masundosundo kwenye maeneo ya siri umejitokeza kwa kasi kubwa hasa baada ya kuwepo kwa janga la UKIMWI, watu wengi waliopatwa na ugonjwa huu huwa hawaoneshi dalili zozote zile. Kwa mfano, kwa wanawake, virusi wa HPV wana uwezo wa kusambaa mpaka maeneo ya ndani kabisa ya kuta za uke au shingo ya kizazi [cervix] bila kuonekana wala kuhisiwa kwa urahisi. 

Kama tulivyotangulia kueleza hapo awali, maambukizi ya HPV husambaa kutoka kwa mtu mmoja mpaka mwingine kwa njia ya kujamiiana kunakohusisha njia ya haja kubwa, uke au ngono ya mdomoni. Mara baada ya kuambukizwa, huweza kuchukua mpaka muda wa wiki sita hadi miezi 6 kwa masundosundo kuwa dhahiri, ingawa baadhi ya wagonjwa wanaweza kukaa hata miaka kadhaa bila kuwa na dalili yeyote ile. Aidha imeonekana pia kuwa si kila mtu anayejamiina na aliye na maambukizi ya HPV au mwenye masundosundo anaweza naye kupata ugonjwa huu. 

Vihatarishi

Watu walio katika makundi haya wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupatwa na masundosundo kwenye maeneo ya siri
•    Wenye wapenzi wengi
•    Kufanya ngono isiyo salama/ ngono zembe
•    Kuanza vitendo vya ngono katika umri mdogo
•    Watumiaji wakubwa wa sigara pamoja na pombe
•    Kupatwa na maambukizi ya virusi wa herpes na wakati huo huo kuwa na msongo mkali wa mawazo
•    wajawazito
•    kuwa na upungufu katika mfumo wa kinga mwilini kwa sababu ya magonjwa mbalimbali au kwa sababu ya matumizi ya dawa fulani fulani

kwa watoto wadogo, ukiona mtoto amepata masundosundo basi ni vema kufanya uchunguzi ikiwa amewahi kubakwa au kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

Dalili za masundosundo [genital warts]

Masundosundo [genital warts] huonekana kama vioteo laini vinavyojitokeza juu ya ngozi ingawa wakati mwingine vinaweza kuwa vidogo mno kiasi cha kutoweza kuonekana vizuri kwa macho ya kawaida.

Kwa wanaume, vioteo hivi hutokea zaidi kwenye uume, ngozi ya pumbu, eneo la mitoki, mapajani pamoja na maeneo ya kuzunguka nje ya njia ya haja kubwa au ndani yake; wakati kwa wanawake hutokea ndani ya uke au njia ya haja kubwa, nje ya uke au ngozi ya nje kuzunguka njia ya haja kubwa, au ndani ya uke kuzunguka eneo la shingo ya kizazi.

Kwa wale wanaopenda kufanya ngono ya mdomoni [oral sex], wanaweza kupatwa na masundosundo/genital warts kwenye maeneo ya kuzunguka mdomo, lips, kwenye ulimi na hata kwenye utando unaozunguka koo.

Dalili nyingine ni kama vile mgonjwa kujihisi kukosekana kwa hisia [kufa ganzi] maeneo yaliyozungukwa na masundosundo,

kwa wanawake kuongezeka kwa utoko/ uchafu sehemu za siri, kuwashwa sana maeneo ya siri na wakati mwingine kutokwa na damu ukeni mara baada ya tendo la ngono. Hata hivyo dalili hizi hutokea mara chache sana.

Wanawake wengi vijana wanaojihusisha na vitendo vya ngono [sexually active] huambukizwa sana ugonjwa huu lakini wengi wao hupona bila hata kuhitaji matibabu, wakati wanaume wanaoambukizwa, wengi wao huwa hawaoneshi dalili zozote za ugonjwa ingawa wanaweza kuwaambukiza wenzi wao bila ya wao kujua. 

Uchunguzi na vipimo

Kwa wanawake, uchunguzi wa ugonjwa wa masundosundo/genital warts hujumuisha uchunguzi wa maeneo ya nyonga [pelvic examination] ambapo daktari huchunguza eneo hilo kwa kutumia vifaa maalum vinavyomuwezesha kuona uwepo wa masundosundo na wapi vilipo. Wakati fulani, kunyunyizia dawa yenye tindikali ya acetic acid husaidia kufanya masundosundo kuonekana kwa urahisi zaidi. Wakati mwingine daktari anaweza pia kufanya kipimo cha pap smear kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi [kwa vile kama tulivyoona hapo awali, zipo aina fulani fulani za HPV ambazo husababisha saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake].

Kwa wanaume, uchunguzi wa maeneo ya siri ni muhimu sana ili kufahamu kama kuna masundosundo au la.

Matibabu

Ni vema genital warts zitibiwe hospitali na daktari; haishauriwi kutumia dawa za kununua kujitibu mwenyewe kwa vile kuna uwezekano mkubwa wa kuchanganya aina ya dawa zinazotumika maalum kutibu aina nyingine za warts kwa ajili ya kujitibu genital warts.

Matibabu ya genital warts hufanyika hospitali [OPD] kwa mganga kuondoa vioteo juu ya ngozi iliyoathirika au kwa kutumia dawa utakazoandikiwa na daktari na kuelekezwa namna ya kuzitumia mwenyewe nyumbani kwa siku kadhaa mpaka majuma kadhaa. Dawa zinazotumika ni pamoja na Podophyllin na podofilox, Trichloroacetic acid (TCA) au Imiquimod

Ukiachilia mbali matumizi ya dawa, masundosundo yanaweza pia kutibiwa kwa njia ya upasuaji mdogo kama vile kwa kuvikata, au kuvimaliza kwa kutumia njia ya baridi/barafu [cryosurgery], njia ya umeme [Electrocauterization] au kuvikausha kwa kutumia mionzi maalum ya laser [Laser therapy].

Matibabu ya masundosundo, kama yalivyo matibabu ya magonjwa mengine yanayosambaa kwa njia ya ngono, ni lazima yahusishe pia tiba kwa mwenza wa mgonjwa. Wakati mwingine hata kama utajihisi huna dalili za waziwazi, ni vema kumuona daktari ili uchunguzwe na kutibiwa kuepusha kusambaza ugonjwa kwa watu wengine au kuachia ugonjwa mpaka ukakuletea madhara zaidi.

Aidha matibabu yanaweza kuhitaji kurudiwa rudiwa mara kadhaa mpaka masundosundo yatakapokuwa yametoweka kabisa. 

Kwa wanawake ambao wametibiwa genital warts na kupona au wale ambao wamewahi kuwa na wenza waliowahi kuugua ugonjwa huu, wanashauriwa sana kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa shingo za kizazi [pap smear]. Kwa wanawake waliowahi kuugua genital warts, ni vema kufanya pap smear walau kila baada ya miezi 3 mpaka 6 tangu kupata matibabu ya awali ya genital warts.

Na kwa wale watakaonekana kuwa na dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi, hawana budi kufanyiwa uchunguzi na tiba zaidi li kuepusha uwezekano wa kupata saratani kamili ya shingo ya kizazi.

Baadhi ya nchi zilizoendelea zina utaratibu wa kuwapatia chanjo ya kuwakinga wanawake vijana au wasichana wadogo wenye umri kati ya miaka 10 mpaka 25 dhidi ya maambukizi ya HPV. Chanjo hii hutolewa hata kwa wale ambao wamewahi kuugua genital warts ingawa imeonekana kuwa ufanisi wa chanjo ya HPV dhidi ya kupata saratani ya shingo ya kizazi kwa wale waliowahi kupatwa na genital warts zilivyosababishwa na high risk HPV huwa ni mdogo ukilinganisha na wale ambao hawajawahi kuugua lakini wapo katika hatari ya kupatwa na ugonjwa huo.

Hata hivyo, pamoja na kuwa umetibiwa, bado unaweza kuwaambukiza wengine virusi hawa wa HPV hivyo ni muhimu kuchukua hatua za kujikinga wakati wa kujamiiana.

Madhara ya masundosundo

Kama tulivyoeleza hapo awali, baadhi ya aina fulani za HPV wameonekana kusababisha saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya vulva. Kiujumla, HPV ndiyo kisababishi kikuu cha saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake wengi. Tofauti na wanawake, ifahamike pia kuwa aina za HPV zinazoweza kusababisha genital warts kwa wanaume ni tofauti kabisa na zile zinazoweza kusababisha saratani ya uume [cancer of the penis] au saratani ya njia ya haja kubwa [anal cancer].

Kwa baadhi ya wagonjwa, masundosundo yanaweza kuwa mengi na makubwa sana kiasi cha kuhitaji matibabu ya muda mrefu na ghali zaidi pamoja na ufuatiliaji wa kina.

Kinga dhidi ya genital warts

Njia mojawapo ya uhakika kabisa ya kujiepusha na ugonjwa wa genital warts pamoja na magonjwa mengine ya ngono/zinaa ni kujiepusha na matendo ya ngono na zinaa kabisa. Lakini kwa wale ambao ni ngumu kufanya hivyo, wanaweza kupunguza uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huu kwa kujihusisha kingono na mwenza mmoja tu ambaye una uhakika kuwa hajaambukizwa wala hayupo katika hatari ya kuambukizwa magonjwa haya.

Tofauti na magonjwa mengine ya zinaa, matumizi ya condom hayana uhakika wa asilimia mia moja katika kukukinga dhidi ya HPV kwa sababu virusi wa HPV au hata masundosundo yanaweza kuwa nje nje kwenye ngozi ambayo uwezekano wa kugusana ni mkubwa.

Pamoja na hayo, bado condom inaweza sana kupunguza hatari ya kuambukizwa masundosundo ikiwa tu itatumika vema na inashauriwa kuitumia mara zote unapokutana kingono na mwenza usiye na uhakika naye. Tukumbuke kila wakati kuwa HPV inaweza bado kuambukizwa kwa mtu hata kama mwenza hana masundosundo yanavyoonekana au hana dalili zozote zile. 

Ikiwa kuna uwezekano, ni vema kwa wanawake wote wenye umri wa miaka kati ya 9 mpaka 26 kupata chanjo dhidi ya virusi wa HPV ili kuzuia uwezekano wa kuambukizwa virusi hao ambao hatimaye husababisha saratani ya shingo ya kizazi.

Imesomwa mara 18530 Imehaririwa Jumatatu, 17 Desemba 2018 20:04
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana