Image

Tatizo la mimba kutoka au kutolewa ni jambo ambalo limewakumba kina mama wengi walio katika umri wa kuzaa. Aidha mijadala kuhusu kuhalalishwa au kuendelea kuharamishwa kwa utoaji mimba ni jambo linalochukua nafasi ya mazungumzo ya kila siku katika maisha yetu.

Kwa baadhi ya nchi, suala la utoaji mimba ni jambo lililohalallshwa kisheria ingawa kwa nchi kama Tanzania, suala hili halijahalalishwa isipokuwa tu pale panapokuwa na sababu za kitabibu zinazolazimisha kufanya hivyo.

Nini maana ya mimba kutoka?

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), utokaji mimba (abortion) hutokea pale ambapo kiumbe (mimba) kilicho chini ya wiki 22 kinapotoka kwa sababu moja ama nyingine, au kinapotolewa kwa njia yeyote ile. Aidha shirika la Afya limekwenda mbali zaidi na kutoa maana nyingine ya utokaji mimba kuwa ni pale mtoto (kiumbe) anapozaliwa akiwa na uzito wa chini ya gram 500.

Aidha baadhi ya matabibu hupendelea kutumia neno 'abortion' kumaanisha kitendo cha utoaji wa mimba kinachofanywa na mtu mwingine ama kwa njia sahihi au zisizo sahihi na 'miscarriage' kumaanisha kitendo cha mimba kutoka yenyewe kwa sababu nyingine yeyote. Ukiacha tofauti hizi za jinsi ya kuharibika kwa mimba, abortion na miscarriage humanisha kitu kilekile cha mimba kutoka.

Aina za utokaji/utoaji mimba (Classification of abortion)

Utokaji mimba umeanishwa katika aina zifuatazo:

Utokaji wa mimba wa hiyari yaani kitendo cha mimba kutoka yenyewe (spontaneous abortion)

  • Mimba inayotishia kutoka ingawa bado haijatoka (threatened abortion)
  • Utokaji wa mimba usioepukika (inevitable abortion)
  • Utokaji wa mimba ulio kamili (.co.tzplete abortion)
  • Utokaji wa mimba usio kamili (in.co.tzplete abortion)
  • Mimba iliyotoka bila kugundulika kuwa imetoka (missed abortion)
  • Utokaji wa mimba unaojirudia rudia (recurrent abortion)
  • Utoaji mimba kinyume cha sheria (illegal abortion)
  • Utoaji mimba kwa sababu za kiafya (therapeutic abortion)

Mimba inayotishia kutoka (threatened Abortion)

Tatizo hili hutokea mapema wakati wa ujauzito. Hali hii hujionesha kwa damu kutoka ukeni wakati njia ya shingo ya uzazi ikiwa bado imefunga. Mara nyingi mimba inayotishia kutoka haina tabia ya kuambatana na maumivu yeyote ya tumbo.

Daktari anapompima mgonjwa hukuta shingo ya kizazi ikiwa imefunga na hakuna dalili zozote za kiumbe kutoka ingawa mgonjwa hutokwa na damu sehemu za siri. Aidha mgonjwa huwa hana maumivu yeyote ya tumbo.

Mimba isiyoepukika kutoka (inevitable abortion)

Hii ni hali inayotokea mapema wakati wa ujauzito pale damu inapotoka ukeni wakati njia ya shingo ya kizazi ikiwa imefunguka au kuwa wazi. Aidha, kwa kawaida, kiasi cha damu kinachotoka ni kingi na mgonjwa hujisikia maumivu makali sana ya tumbo.

Utokaji mimba usioepukika waweza kupelekea

  • Utokaji mimba ulio kamili (.co.tzplete abortion) au,
  • Utokaji mimba usio kamili (in.co.tzplete abortion).

Utokaji mimba usio kamili (in.co.tzplete abortion)

Utokaji mimba usio kamili huambatana na utokaji damu kwa wingi sehemu za siri za mgonjwa, kufunguka kwa njia ya shingo ya kizazi, kutoka kwa baadhi ya mabaki ya kiumbe (products of conception) ingawa mengine hubakia, na mgonjwa kujisikia maumivu makali ya tumbo hususani sehemu za chini ya kitovu.

Utokaji wa mimba ulio kamili (.co.tzplete abortion)

Hali hii huambatana na mama kutokwa damu sehemu za siri, kujisikia maumivu makali ya tumbo pamoja na kutoka kwa kiumbe ikiambatana na kondo lake la nyuma. Aidha baada ya muda, mgonjwa hueleza kupotea kwa maumivu ya tumbo, damu kupungua kutoka sehemu za siri na kufunga kwa njia ya njia ya shingo ya kizazi (cervix).

Mimba iliyotoka bila kugundulika kuwa imetoka (missed abortion)

Hali hii hutokea pale ambapo, kiumbe kinapokuwa kimekufa bila ya mimba kutoka. Mara nyingi, damu huwa haitoki sehemu za siri, na mgonjwa huwa hajisikii maumivu yeyote ya tumbo. Aidha huwa hakuna dalili zozote za ukuaji wa mimba na hata mapigo ya moyo ya mtoto hayawezi kutambulika hata kama vipimo maalum vitatumika.


Utokaji wa mimba unaojirudia rudia (recurrent abortion)

Hali hii hutokea pale ambapo mama huwa na historia ya mimba kutoka mara tatu au zaidi kwa mfululizo.

Utoaji mimba kinyume cha sheria (illegal abortion)

Utoaji mimba kinyume cha sheria ni usitishwaji wa maisha ya mimba au kutolewa kwa kiumbe kinyume na sheria za nchi husika zinavyoagiza. Katika mazingira kama haya, sababu dhahiri za kitaalamu hukosekana isipokuwa wahusika hutenda kulingana na sababu zao binafsi zikiwemo za kutoitaka mimba au kama ni muhusika ni mwanafunzi huogopa kufukuzwa shule.

Utoaji mimba kisheria kwa sababu za kitabibu (therapeutic abortion)

Utoaji mimba ulioidhinishwa kitabibu ni usitishwaji wa mimba kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama. Usitishwaji huu ni hufanywa kitaalamu na daktari. Sababu zinazoweza kufanya mimba ikasitishwa ni pamoja na

  • iwapo kiumbe kina mapungufu mengi ya kimaumbile (fetal anomally) ambayo yatamletea mtoto atakayezaliwa matatizo na hata kusababisha kifo chake
  • iwapo mama mjamzito alipata ujauzito kwa kubakwa na asingependa kuzaa, au
  • iwapo mama mjamzito ana kansa , kwa mfano, kansa ya kiwanda cha mayai ya kike (ovarian cancer), kansa ya damu (leukemia) au kansa ya tezi la goita (thyroid cancer)

Mambo gani hufanya mimba kutoka kwa hiyari?

Kuna sababu kadhaa zinazoweza kupelekea mimba kutoka kwa hiyari (spontaneous abortion). Miongoni mwa sababu hizo ni

  • Matatizo kwenye mfumo wa jenetiki (genetic abnormalities) ambayo husababisha kuharibika na kutoka kwa mimba katika miezi mitatu ya mwanzoni.
  • Matatizo kwenye mfuko wa uzazi (uterine problems): matatizo kama vile kuwepo kwa uvimbe kwenye mfuko wa uzazi wa mwanamke (uterine fibroids), au kulegea kwa milango ya shingo ya kizazi (cervical in.co.tzpetence) husababisha mimba kutoka katika theluthi ya pili ya ujauzito (second trimester).
  • Sababu nyingine ni pamoja na maradhi wakati wa ujauzito kama malaria, kisukari, shinikizo la damu, kifafa cha mimba, matatizo kwenye tezi ya 'goita' (hypothyroidism). Aidha maambukizi kama Rubella, toxoplasmosis na mengineyo nayo pia huweza kusababisha mimba kutoka.
  • Kukosekana kwa ulinganifu katika baadhi ya homoni mwilini (hormonal imbalance)
  • Matumizi ya baadhi madawa kwa mfano zinazotumika katika kutibu msongo wa mawazo kama vile paroxetine au venlafaxine nayo yaweza kusababisha utokaji wa mimba.

Tabia hatarishi zinazoweza kusababisha utokaji wa mimba

  • Unywaji pombe uliopitiliza.
  • Uvutaji sigara
  • Utumiaji madawa ya kulevya kama vile kokeini (cocaine)
  • Utumiaji kwa wingi wa vinywaji vyenye kiasili cha caffeine kama vile kahawa au kakao.

Vipimo na Uchunguzi

Ili kutambua kuwepo kwa hali hii ya mimba kutoka, vipimo vifuatavyo vyaweza kufanywa na tabibu

  • Kipimo cha mimba kwa kutumia mkojo (Urine for hCG)
  • Kupima damu ili kufahamu kiasi cha wingi wa damu (haemoglobin level), kundi la damu (blood group) na muda wa damu kuganda (bleeding and clotting time).
  • Kuchunguza iwapo shingo ya uzazi imefunga au ipo wazi, na pia kuchunguza iwapo kuna dalili ya kiumbe kutoka ama la. Uchunguzi huu huitwa speculum examination.
  • Ultrasound ya nyonga (pelvic utrasound) kwa ajili ya kutambua iwapo kiumbe kipo ama la, na kama kipo je ki hai ama kimekufa.
  • Aidha ni muhimu pia kufanya uchunguzi wa magonjwa mbali ya zinaa ambayo husababisha mimba kutoka.

Matibabu ya utokaji wa mimba

Matibabu ya utokaji wa mimba hutegea sana aina ya utokaji wa mimba. Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia vitu vifuatavyo wakati wa kutoa matibabu kwa mtu aliyepoteza mimba
Wahudumu wa afya huzingatia kanuni zote (ABC) za kuokoa maisha ya mgonjwa kama vile

  • kuhakikisha njia ya hewa ya mgonjwa ipo wazi na hewa inaingia na kutoka vizuri kwenye mapafu
  • kuhakikisha mgonjwa anapumua vizuri bila shida
  • kuhakikisha mishipa ya damu ya mgonjwa imewekwa mrija wa veni (intravenous line) na mgonjwa anapewa dripu ya maji ya normal saline.
  • kuhakikisha mgonjwa anaongezwa damu haraka iwapo vipimo vitaonesha kuwa alipoteza damu kwa wingi

Matibabu ya mimba inayotishia kutoka (threatened abortion)

Kwenye hali hii, mgonjwa hutakiwa

  • kupumzika kitandani bila kufanya kazi yeyote (.co.tzplete bed rest) angalau kwa wiki moja au zaidi mpaka hapo damu itakapoacha kabisa kutoka
  • kumpa ushauri na uhakika mama ili kumfanya atulie kiakili (assurance and proper councelling)
  • Mama pia hupewa dawa za kumtuliza na kumfanya apumzike (sedatives) kama vile phernobabitone
  • Aidha mama hupewa dawa kwa ajili ya kupunguza kusukuma kwa uterus (antispamodics) kama vile salbutamol
  • Kutofanya tendo la ndoa kwa wiki mbili au tatu
  • Aidha mama na mumewe hupewa ushauri juu ya tatizo hilo na jinsi ya kuendelea na matibabu

Matibabu ya mimba iliyotoka kamili (.co.tzplete abortion)

Mara nyingi mgonjwa huwa haitaji matibabu zaidi ya uangalizi wa karibu kwa vile kiumbe pamoja na kondo lake la nyuma vyote huwa vimetoka kikamilifu. Mara chache sana, kulingana na jinsi daktari atakavyoona, mgonjwa anaweza kupewa antibiotiki kwa ajili ya kuzuia uwezekano wa kupata maambukizi.

Matibabu ya utokaji wa mimba usiokuwa kamili (in.co.tzplete abortion)

Matibabu ya aina hii ya utokaji wa mimba uhitaji mgonjwa kusafishwa kwa ajili ya kuondoa mabaki ya kiumbe (products of conception) yaliyobakia. Usafishaji huu huweza kufanywa kwa kutumia njia inayoitwa Manual Vacuum Aspiration (MVA).

Aidha mgonjwa hupewa dawa za antibiotiki kwa ajili ya kuzuia uwezekano wa maambukizi ya vimelea vya bakteria.

Matibabu mimba iliyotoka bila kugundulika kuwa imetoka (missed abortion)

Matibabu ya aina hii ya utokaji wa mimba ni pamoja na mgonjwa kuwekewa maji ya uchungu ili kiumbe kiweze kutoka. Wakati mwingine, daktari anaweza kuamua kusafisha mfuko wa uzazi (uterus) kwa kutumia njia inayoitwa dilatation and curettage. Sambamba na matibabu hayo, mgonjwa pia hupewa dawa za antibiotiki kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya vimelea vya bakteria.

Matibabu ya tatizo la utokaji wa mimba unaojirudia (recurrent abortion)

Jambo la msingi katika matibabu ya tatizo la utokaji mimba unaojirudia (recurrent abortion) ni kugundua na kutambua chanzo kinachosababisha tatizo hilo na kisha kukishughulikia ili kuondoa kabisa kujirudia rudia kwa tatizo hili.

Imesomwa mara 20956 Imehaririwa Jumatatu, 10 Septemba 2018 17:28
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana