Image

Magonjwa ya Zinaa -2: (Sexual Transmitted Diseases)

Katika sehemu hii ya pili ya muendelezo wa makala ya magonjwa ya zinaa nitazungumzia kuhusu ugonjwa wa Chlamydia.

Chlamydia ni nini?

Chlamydia ni aina ya ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Chlamydia trachomatis ambao wanaweza kuathiri viungo vya uzazi na pia kusababisha ugonjwa wa homa ya mapafu unaojulikana kama typical pneumonia. Kati ya magonjwa ya zinaa yanayosababishwa na bakteria, Chlamydia ndio ugonjwa unaoongoza kwa maambukizi duniani ambapo kwa nchi ya Marekani pekee inakisiwa watu milioni 4 huambukizwa kila mwaka .

 Kutokana na ukosefu wa takwimu za nchi nyingi barani afrika pamoja na Tanzania, ni vigumu kujua idadi ya maambukizi kamili, lakini bila shaka ndio ugonjwa wa zinaa unaotokana na bakteria unaoongoza kwa maambukizi ukifuatiwa na ugonjwa wa gono. Chlamydia huweza kuambukizwa kupitia njia za kujamiana kama ;

 • Kujamiana kwa njia ya mdomo, njia ya haja kubwa na kupitia tupu ya mwanamke
 • Kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito
 • Au kupitia mbawa, vinyesi vya wanyama kama ndege walioambukizwa aina ya Chlamydia inayopatikana kwa wanyama ( kuku, bata, kasuku nk )na kusababisha aina ya homa ya mapafu inayojulikana kama psittacosis ambayo huambatana na homa kali yenye nyuzi joto kati ya 39.4 celsius na 41.1 celsius

Chlamydia huathiri sehemu tofauti za mwili wa binadamu kama macho, mfumo mzima wa kupumua, sehemu za siri, viungo vya uzazi na tezi (lymph nodes). Ugonjwa wa Chlamydia na gono huwa yanaambatana kwa pamoja (rejea makala ya magonjwa ya zinaa sehemu ya kwanza).

Dalili na viashiria vya ugonjwa wa Chlamydia

Asilimia 75 ya wanawake na asilimia 50 ya wanaume wanaopata maambukizi ya ugonjwa huu huwa hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa wa Chlamydia. Dalili hutokea wiki 1 hadi 3 baada ya mtu kupata maambukizi.

Dalili kwa wanawake zinaweza kuwa;

 • Majimaji ya rangi ya njano yanayotoka kwenye tupu ya mwanamke yenye harufu kali
 • Maumivu wakati wa kukojoa (haja ndogo)
 • Kuhisi kama kuwaka moto wakati wa kukojoa
 • Kutokwa na damu katikati ya kipindi cha hedhi yaani baada ya kumaliza mzunguko wa hedhi na kabla ya kuanza mzunguko mwengine wa hedhi
 • Maumivu sehemu ya chini ya tumbo
 • Maumivu wakati wa kujamiana
 • Kutokwa na damu wakati wa kujamiana
 • Kuvimba na maumivu kwenye tezi zilizopo sehemu za siri

Dalili kwa wanaume nazo zinaweza kuwa;

 • Maumivu wakati wa kukojoa (haja ndogo)
 • Kuhisi kama kuwaka moto wakati wa kukojoa (haja ndogo)
 • Kutokwa na majimaji kutoka kwenye uume ambayo yanaweza kuwa ya rangi nyeupe kama maziwa, kijivu au rangi ya njano
 • Sehemu ya tundu la kwenye uume huwa nyekundu, huvimba na kuwasha
 • Maumivu kwenye korodani
 • Tezi zilizopo sehemu za siri huvimba na huambatana na maumivu

Mara nyingi dalili hizi kwa wanaume zinakuja na kupotea au zinaweza kuonekana tu wakati anaenda kukojoa asubuhi baada ya kuamka kutoka usingizini

Dalili za ugonjwa huu kama umeathiri puru (rectum) ni kama ifuatavyo (kwa wanawake na wanaume);

 • Kuwashwa na kutokwa na damu kutoka kwenye puru
 • Maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa
 • Kutokwa na uchafu kama kamasi kutoka kwenye puru

Dalili za chlaymdia iliyoathiri macho (kwa wanawake na wanaume);

 • Kuvimba sehemu za kwenye macho
 • Macho kuwa mekundu, kuwasha na hata kutokwa na majimaji kutoka machoni

Chlamydia inayoambukiza kwenye macho (Chlamydia conjunctivitis or trachoma) ndio inayoongoza kwa kusababisha upofu duniani.

Vipimo vya uchunguzi

 • Urethral swab for culture – Majimaji kutoka kwenye uume au uke huchukuliwa kwa kutumia swab maalum ambapo hupelekwa maabara ili kuotesha na kuangalia aina ya uoto wa bakteria
 • Urinalysis (urine test) – Vipimo vya mkojo
 • Polymerase Chain Reaction (PCR) – Kipimo cha kuangalia vina saba vya bakteria na hufanyika maabara.
 Tiba ya ugonjwa wa Chlamydia

Chlamydia ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayotibika. Ugonjwa huu hutibiwa kwa dawa aina ya antibiotics zilizopo kwenye makundi ya macrolides, Quinolones na Polyketides.

Madhara ya ugonjwa huu

 • Kwa wanaume, Chlamydia huathiri korodani na kusababisha mwanamume kukosa uwezo wa kutia mimba mwanamke (infertility) na maambukizi kwenye tezi dume (prostatitis)
 • Kwa wanawake, husababisha maambukizi kwenye mirija ya uzazi, mfuko wa uzazi, na mayai ya uzazi hivyo kusababisha ugonjwa aina ya Pelvic inflammatory disease (PID). Pia huongeza asilimia ya mwanamke kupata mimba ambayo inaweza kutunga nje ya mfuko wa uzazi (Ectopic pregnancy). Mbali na hilo, mwanamke anapata maumivu sugu ya kwenye nyonga, ugonjwa wa mifupa arthritis aina ya Reiters syndrome. Vilevile, Chlamydia huweza kusababisha ugumba kwa mwanamke kama hatapata tiba.
 • Kwa wajawazito, Chlamydia husababisha wanawake kujifungua kabla wakati wake. Mtoto anaweza kuzaliwa na maambukizi kwenye masikio, sehemu za siri, macho na kwenye mapafu (homa ya mapafu). Kama mtoto hatapata tiba ya haraka ya macho basi anaweza kuwa kipofu.

Dalili za Chlamydia kwa watoto wachanga hutokea ndani wiki mbili kwenye macho na homa ya mapafu (pneumonia) ndani ya wiki 2 hadi miezi 3 baada ya kuzaliwa.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Chlamydia
 • Kama nilivyoeleza kwenye makala iliyopita, njia sahihi ya kujikinga na magonjwa ya zinaa ni kuacha au kuepuka kufanya ngono au kujamiana.
 • Kwa wanawake wajawazito, ni vizuri kuhudhuria kliniki mapema wakati wa ujauzito
 • Wale wenye maambukizi wanashauriwa kuchukua tahadhari ya kutowaambukiza wapenzi wao kwa kufanya ngono salama (kutumia mipira), kuepuka kushika macho kwa kutumia mikono na hata ikiwezekana kuwaepuka wapenzi wao ili kuwalinda na maambukizi.
 • Kwa wale ambao wapenzi wao wameambukizwa au wameonyesha dalili za ugonjwa huu, wanashauriwa na wao kupata tiba hata kama hawana dalili zozote.
Imesomwa mara 9251 Imehaririwa Jumatatu, 15 Mai 2017 08:45
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana