Image

Ultrasound Yaweza Kugundua Kansa ya Mfuko wa Uzazi Katika Hatua ya Awali?

Ultrasound ni chombo ambacho kimekuwa kikitumiwa na madaktari wengi sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya kuchunguza matatizo mbali mbali yaliyo ndani ya mwili wa mgonjwa.

Mojawapo ya matumizi maarufu ya chombo hiki kwa wanawake ni utambuzi wa jinsi mtoto alivyokaa tumboni mwa mama mjamzito,kuchunguza umbo la mfuko wa uzazi, matatizo katika mfumo wa uzazi na pia kuangalia iwapo kiumbe kilichopo ndani ya tumbo la mama mjamzito ni hai ama la.

Hivi karibuni huko nchini Uingereza, madaktari wamebuni kipimo cha Ultrasound kinachoweza kugundua kansa ya mfuko wa kizazi mapema kabla ya hata dalili hazijaanza kujitokeza kwa mgonjwa. Kipimo hicho kina uwezo wa kugundua kansa ya mfuko wa uzazi kwa mwanamke ikiwa katika hatua za awali kabisa kabla hata ya dalili zake kuanza kujitokeza rasmi.

Watafiti hao wamesema kwamba hii ni hatua kubwa katika kukabiliana na Ugonjwa wa kansa ya mfuko wa kizazi kwa kina mama katika nchi zinazoendelea, na wanatarajia kwamba chombo hiki kinaweza kuanza kutumika muda si mrefu hasa katika nchi zinazoendelea.

Watafiti hao wamedai kuwa ni matarajio yao kuwa chombo hiki kitakapoanza kutumika, kitakuwa ni miongoni mwa vipimo vya lazima kabisa ambavyo mgonjwa anatakiwa kufanyiwa (Routine) wakati wa kuwafanyia kina mama uchunguzi wa afya zao.

Kuna wastani wa wagonjwa wapya 60,000 wa kansa ya mfuko wa kizazi kila mwaka wengi wao wakiwa kwenye umri wa miaka 60. Aidha kwenye nchi zilizoendelea, ugonjwa huu husababisha wastani wa vifo 1,700 kila mwaka. Tangu mwaka 1970, idadi ya wagonjwa wa kansa ya mfuko wa kizazi imeongezeka kwa asilimia 50, huku wataalamu wa afya wakisema imetokana na wanawake wengi kupenda kuzaa watoto kidogo  pamoja na kuongezeka uzito (Obesity).

Watafiti hao kutoka chuo Kikuu cha London, nchini Uingereza wamesema kipimo hicho cha ultrasound (Ultrasound specialist test) kina uwezo wa kupima unene wa mfuko wa uzazi hivyo kutoa picha zinazowezesha kugundulika kwa kansa mapema.

Katika utafiti wao, kati ya wanawake 96 waliopimwa kwa kutumia chombo hicho, asilimia 80 waligundulika kuwa na kansa ya mfuko wa uzazi kwa usahihi kabisa hata kabla hawajaanza kuonesha dalili kama za kutoka damu kwa wingi kwenye sehemu zao za siri.

Watafiti hao bado wanaendelea kuwapima kina mama zaidi ili kujua uhakika wa kipimo chao katika kugundua kansa katika hatua za awali. Kwa kawaida iwapo kansa itagundulika mapema, mgonjwa ana nafasi kubwa ya kuishi iwapo atapata tiba mapema kabla hata kansa haijasambaa au kuenea mwilini.

Kansa ya mfuko wa kizazi huwapata kina mama ambao wameshafikia ukomo wa kupata hedhi kila mwezi na ambao wana umri kati ya miaka  60 hadi 69. Aidha wanawake wanakuwa katika hatari kubwa zaidi iwapo kiwango cha homoni aina ya oestrogen kitakuwa juu kuliko kawaida.

Kwa kawaida homoni hii ya oestrogen huwa katika kiwango cha chini sana wakati wa ujauzito, na wanawake wenye watoto wachache huwa na kiwango kikubwa cha homoni hii hivyo kuwa kwenye hatari ya kupata kansa hii ya mfuko wa uzazi.

Wanawake wanene (Obese) nao wapo kwenye hatari ya kupata aina hii ya kansa kwa vile wengi wao huwa na kiwango cha juu sana cha homoni hii ya oestrogen kwa vile mafuta yaliyolundikana mwilini hubadilisha homoni za aina nyingine kuwa oestrogen.

Ian Jacobs, mtafiti mkuu katika utafiti huo uliochapishwa katika jarida maarufu la afya la The Lancet amesema, “Miaka kadhaa ijayo, wanawake wanene, waliozaa mara chache, na wenye matatizo ya ugonjwa wa shinikizo la damu wanastahili kufanyiwa uchunguzi wa mifuko yao ya uzazi mapema kwa kutumia kipimo hicho ili kutambua kama wana kansa hii ya mfuko wa kizazi au la”.

Mkurugenzi wa kitengo cha utafiti wa kansa nchini Uingereza, ambao ndio waliofadhili utafiti huo, Bi. Kate Law, amesema matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa kipimo cha Ultrasound kinaweza kutumika na madaktari katika kuwawezesha kugundua aina ya kansa hiyo mapema.

Aina mbili ya chembe chembe za asilia za mwanadamu (genes) zinazohusishwa na kansa hii zimegundulika, ambazo pia huongeza hatari ya ugonjwa mwingine wa mfuko wa uzazi unaoitwa  Endometriosis kwa asilimia 20.

Ugunduzi huo ni hatua muhimu katika utengenezaji wa dawa ya kutibu kiini cha kansa hiyo na pia unafungua njia katika kubuni vipimo vya damu vya kugundua kansa hii kwa haraka. Chembe chembe hizo za asili (genes) zinahusika katika utengenezaji wa ukuta wa mfuko wa uzazi pamoja na kutengeza homoni za  aina nyingi, watafiti hao wamesema.

Ugonjwa huu wa Endometriosis ambao husababisha matatizo ya uzazi, hutokea baada ya ukuta wa mfuko wa uzazi kuanza kuota katika sehemu nyingine za mwili wa mwanadamu.

Inatarajiwa kwamba pindi utafiti huu utakapokamilika, kipimo hiki kitaanza kutumika muda si mrefu katika nchi nyingi duniani ili kuokoa vifo vya kina mama wengi duniani.

Imesomwa mara 8125 Imehaririwa Jumatatu, 15 Mai 2017 16:47
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana