Image

Saratani ya Shingo ya Kizazi (Cervical Cancer)

Utangulizi

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi duniani. Inakadiriwa kuwa asilimia 85 ya vifo hivi hutokea katika nchi zinazoendelea. Kwa Tanzania, wastani wa wanawake 6,241 huugua saratani hii kila mwaka, ambapo 4,355 kati yao hufa, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la afya duniani (W.H.O) ya mwaka 2010

Saratani ya shingo ya kizazi ndio saratani ya kwanza kwa wanawake nchini Tanzania, na Saratani namba moja kwa wanawake walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 44. Tanzania ina wanawake milioni 10.97 walio na umri wa miaka 15 na kuendelea, ambao wako kwenye hatari kubwa ya kupata saratani hii. Kwa afrika mashariki, asilimia 33.6 ya wanawake wote, wanasadikiwa kuwa na virusi aina ya human papilloma virus ambavyo ndio visababishi vya ugonjwa huu.

Je nini kinasababisha saratani ya shingo ya kizazi?

Maambukizi ya human papilloma virus ndio yanayosababisha saratani ya shingo ya kizazi. Kuna zaidi ya aina 150 ya virusi hivi vya human papilloma virus, ambapo aina tatu (yaani ainaya 26,53,66) ndio venye hatari sana ya kusababisha ugonjwa huu, aina ya 16 na 18 ndivyo vinavyojulikana kusababisha zaidi ya asilimia 70 ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi. Virusi hivi huambukizwa kwa njia ya kujamiana au kugusana kwa ngozi ya mtu mmoja na mwengine, na huambukiza wanaume na wanawake.

Vihatarishi vya saratani ya shingo ya kizazi

 • Kuanza kufanya ngono mapema – Wanawake wanaoanza kujamiana wakiwa na umri wa miaka 16 wako kwenye hatari baadae kupata saratani ya shingo ya kizazi.
 • Kuwa na wapenzi wengi – Mwanamke mwenye wapenzi wengi au mwenye mwanamume mwenye wapenzi wengi yupo kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu. Utumiaji wa kondomu hupunguza hatari ya kupata saratani hii, lakini ikumbukwe ya kwamba kondomu sio kinga ya ugonjwa huu.
 • Maambukizi ya human papilloma virus
 • Uvutaji sigara – Kemikali zilizopo kwenye sigara huchanganyikana na seli au chembechembe za shingo ya kizazi hivyo kuleta mabadiliko katika shingo ya kizazi hatimaye kusababisha saratani.
 • Utumiaji wa vidonge vya kupanga uzazi kwa muda mrefu hasa wale wanaotumia kwa zaidi ya miaka mitano (miaka 5)
 • Ugonjwa wa genital warts ( dalili ni matezi na muda mwingine vidonda katika sehemu ya siri ya mwanamke). Hii husababishwa na virusi vya human papilloma virus.
 • Lishe duni au utapia mlo
 • Kuzaa watoto wengi – Wanawake ambao wamepata watoto zaidi ya watano wako kwenye hatari kubwa sana ya kupata saratani ya shingo ya kizazi. Ndio maana mama akishafikisha watoto watano anashauriwa kufunga kizazi.
 • Umri mkubwa – Baada ya kufikisha umri wa miaka 25, hatari ya kupata saratani hii huongezeka. Wanawake wenye zaidi ya miaka 45 wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.
 • Uasili wa mtu – Saratani ya shingo ya kizazi huonekana sana kwa watu weusi kuliko watu weupe.
 • Upungufu wa kinga mwilini – Magonjwa yanayosababisha upungufu wa kinga mwilini kama ukimwi huchangia kupata saratani ya shingo ya kizazi. Hata baadhi ya dawa pia husababisha upungufu wa kinga mwilini, mfano, dawa zinazotolewa baada ya mgonjwa kupewa kiungo cha mtu mwengine kama figo,moyo nk.
 • Historia ya saratani ya shingo ya kizazi katika familia. Saratani hii pia inahusishwa na kiashiria cha aina ya HLA-B7 ambacho kinaweza kurithishwa kwenye familia ya mgonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.
 • Matumizi ya dawa aina ya diethystilbestrol (DES).
 • Kujamiana na mwanaume ambaye hajatahiriwa – Tafiti zimeonyesha ya kwamba wanaume ambao hawajatahiriwa wako katika hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya human papilloma virus, hii ni kutokana na uchafu ndani ya gozi linalofunika kichwa cha uume hivyo kuweka mazingira mazuri kwa virusi vya human papilloma virus kustawi na hatimaye kuambukiza mwanamke wakati wa kujamiana.
 • Dalili na viashiria vya saratani ya shingo ya kizazi

  Saratani ya shingo ya kizazi katika hatua za awali haina dalili au viashiria vyovyote.

  • Kutokwa na damu katika tupu ya mwanamke (vagina) ambayo sio ya kawaida. Damu hii inaweza kuwa matone, au damu inayotoka katikati ya mzunguko wa hedhi (yaani baada ya hedhi kabla ya hedhi inayofuata) au damu itokayo kwa mwanamke ambae ameacha kupata hedhi.
  • Kutokwa na damu baada ya kujamiana baada ya tendo la ndoa.
  • Maumivu wakati wa kujamiana.

  Dalili za saratani iliyosambaa ni kama zifuatavyo

  • Kupungua kwa hamu ya kula
  • Kupungua uzito
  • Kuhisi uchovu
  • Maumivu ya nyonga
  • Maumivu kwenye mgongo
  • Maumivu ya mguu
  • Mguu mmoja kuvimba
  • Kutokwa na damu nyingi kwenye tupu ya mwanamke
  • Kuvunjika mifupa (bone fractures)
  • Kutokwa na mkojo au kinyesi kwenye tupu ya mbele ya mwanamke.

  Vipimo vya saratani ya shingo ya kizazi

  Pap smear

  Chembechembe au seli za shingo ya kizazi huchukuliwa na kuchunguzwa kutumia hadubini. Kipimo hiki pia hutumiwa katika uchunguzi wa wanawake ili kujua kama wamepata saratani ya shingo ya kizazi au la. Wanawake wenye zaidi ya miaka 18 au wale wenye upungufu wa kinga mwilini wanashauriwa kufanya kipimo hiki angalau mara moja kwa mwaka ili wajue afya yao.

  Cervical Biopsy

  Kipimo hiki huhusisha uchukuaji wa nyama kutoka kwenye uvimbe katika shingo ya kizazi na hupelekwa maabara kuchunguzwa kama kuna saratani au la. Kipimo hiki kinathibitisha uwepo wa saratani.

  Colposcopy

  Hii ni aina ya darubini inayotumiwa kuchunguza shingo ya kizazi ili kuangalia kama kuna tishu ambayo si ya kawaida. Kipimo hiki kinaweza kufanywa na daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama.

  Cone Biopsy 

  Kipimo hiki hufanywa kwa kuchukua nyama kutoka katika shingo ya kizazi mfano wa koni kwa uchunguzi zaidi na hufanywa katika chumba cha upasuaji mgonjwa akiwa amepewa dawa ya nusu kaputi. Hiki kipimo kinaweza kutumiwa kama njia moja ya kutibu saratani ambayo haijaenea na ambayo ni ndogo sana kuondolewa kwa njia hii. Kuna aina mbili ya kufanya kipimo hiki

  (a) Kukata nyama kutoka katika shingo ya kizazi kwa kutumia nyaya ya umeme inayojulikana kitaalamu kama loop electrosurgical excision procedure (LEEP) na

  (b) Kukata nyama ya shingo ya kizazi kwa kutumia visu maalum vya upasuaji au laser

  PET Scan

  Kipimo hiki pia huweza kuthibitisha uwepo wa saratani na kuangalia maendeleo ya mgonjwa baada ya kupata tiba

  Blood test

  Vipimo vya damu, kuangalia wingi wa damu, kwa sababu wagonjwa wengi wanakuwa na upungufu wa damu kutokana na kuvuja damu mara kwa mara.

  Picha ya kifua ya X-ray

  Kuangalia kama saratani imesambaa kwenye mapafu au la.

  CT Scan

  Kuangalia kibofu cha mkojo kama kimeathirika au la, na pia kuangalia kama saratani imesambaa kwenye mifupa, ini, figo na sehemu nyingine za mwili.

  Makundi ya saratani ya shingo ya kizazi

  Saratani ya shingo ya kizazi imegawanywa katika makundi kulingana na TNM ama FGO (Classification) kama ifuatavyo;

  Stage 0 

  Saratani iliyo kwenye chembechembe au seli za aina ya epithelium lakini haifiki kwenye nyama za ndani za shingo ya kizazi, Stage I – Saratani iliyopo kwenye shingo ya kizazi,

  Stage II

  Saratani iliyosambaa hadi kwenye tupu ya mwanamke sehemu ya juu kwa 2/3,

  Stage III 

  Saratani iliyosambaa hadi kwenye ukuta wa nyonga na sehemu ya chini ya uke kwa 1/3, Hii inaleta madhara katika figo,

  Stage IV 

  Saratani iliyosambaa hadi nje ya tupu ya mwanamke na pia husambaa hadi kwenye sehemu nyingine za mwili kama mapafu, figo, mifupa nk.

  Tiba ya saratani ya shingo ya kizazi

  Tiba ya saratani hii inategemea na kundi na aina ya saratani mgonjwa aliyonayo.

  Tiba ni kama ifuatavyo:

  Tiba ya kuchoma (cauterization)

  Tiba hii hutolewa kwa wagonjwa wenye matatizo ya shingo ya kizazi kabla hayajakuwa saratani na hutumia joto kali , umeme, na kemikali kuchoma sehemu iliyoathirika.

  Tiba ya dawa (Chemotherapy) 

  Tiba kwa kutumia dawa za saratani ambazo huuwa chembechembe au seli za saratani ya shingo ya kizazi. Dawa hizi hutolewa kwa mgonjwa ambae saratani imeshasambaa mwilini na inahusisha dawa moja pekee au mchanganyiko wa dawa zaidi ya moja ambazo mgonjwa hupewa kwa njia ya dripu au humeza kupitia mdomoni. Dawa hizi hutumiwa zaidi ya mzunguko mmoja na ni za gharama. Dawa hizi zinaweza kutumiwa ili;

  • Kutibu saratani
  • Kuzuia saratani isisambae sehemu nyingine mwilini
  • Kupunguza kasi ya ukuaji wa saratani
  • Kupunguza madhara ya saratani

  Madhara ya dawa hizi yanatofautiana kulingana na aina ya dawa, muda wa utumiaji, na kiwango cha dawa yenyewe. Madhara yake ni kichefuchefu, uchovu, nywele kunyofyoka (hair loss) nk.

  Tiba ya mionzi (radiation therapy)

  Tiba ya mionzi kwa kutumia mionzi ya X-ray, gamma na neutrons ambayo huua seli za saratani hii. Mionzi hii haina maumivu na madhara yake ni uchovu, tupu kuwa nyembamba sana (narrowing of vagina) na mgonjwa kupungukiwa na damu.

  Tiba ya upasuaji (surgical treatment) 

  Aina za upasuaji kwa mgonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ni kama zifuatazo:

  • Cryosurgery: Mpira maalum (probe) huingiziwa kupitia kwenye tupu hadi kwenye shingo ya kizazi na majimaji ya nitrogen hupitishwa yaliyo na baridi ya -160 0 celsius yenye uwezo wa kugandisha na kuharibu seli za shingo ya kizazi hivyo kuzuia saratani.
  • Laser surgery: Aina hii ya upasuaji inatumia mionzi ya laser ambayo huchoma seli za shingo ya kizazi ambazo haziko kwenye hali ya kawaida, mionzi hii haiharibu tishu za pembeni na hutumiwa kwa matatizo ya shingo ya kizazi kabla hayajakuwa saratani.
  • Cone biopsy:  Kama nilivyoeleza kwenye vipimo hapo juu.
  • Simple hysterectomy:  Hii inahusisha kuondoa mfuko wa kizazi (uterus) kupitia sehemu ya tumboni au kupitia kwenye tupu ya mwanamke kwa wagonjwa wa kundi I (Stage I). Madhara yake ni ugumba, kuvuja damu, kupata madhara sehemu ya haja ndogo au utumbo na maambukizi kwenye kidonda.
  • Radical hysterectomy:  Hii inahusiha kuondoa mfuko wa uzazi kupitia kwenye tumbo pamoja na tishu za mfuko wa uzazi, sehemu ya juu ya tupu ya mwanamke, na tezi za kwenye nyonga. Mayai (ovaries) na mirija ya uzazi yanabakizwa. Madhara yake ni kama ya hapo juu pamoja na kuleta karaha na maumivu wakati wa kujamiana.
  • Pelvic exenteration:  Huhusisha uondoaji wa kibofu cha mkojo, uke, puru (rectum) na sehemu ya utumbo mpana (colon). Upasuaji huu hutumiwa kwa wagonjwa wenye na saratani iliyojirudia.

   

  Imesomwa mara 10382 Imehaririwa Alhamisi, 08 Juni 2017 09:44
  Dr Khamis

  Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

  Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

  Makala shabihana