Zamani ilikuwa ni kawaida kuona wanawake wanatoboa masikio, pua, ili kuvaa aina mbalimbali za herini na shemeri. Siku hizi si ajabu kuona wanaume na wanawake wakijitoboa au kuchorwa alama (tattoo) sehemu mbalimbali za miili yao kama kwenye pua, mdomo, ulimi, tumbo, masikio, mikono, miguu, kwenye kichwa, mapaja, mgongo na hata sehemu za siri yote haya kwa ajili ya urembo, miila au desturi zao, kutaka kujinasibu na tabaka fulani au kutaka kuonyesha ubunifu wao (artistic expression).
Kutoboa/kuchorwa mwili kama kutafanywa na mtaalamu wa kutoboa/kuchora mwili hakuna madhara yoyote ya kiafya, madhara ya kutoboa/kuchorwa mwili hupatikana pale tu ambapo kitendo hiki hufanywa na mtu ambaye si mtaalamu na mjuzi wa fani hii bila kutumia njia salama za kiafya.
Katika utafiti uliofanywa nchini Marekani na madaktari bingwa wa ngozi (dermatologists) katika chuo kikuu cha Northwestern University Feinberg School of Medicine na kuchapishwa katika jarida la American Journal of Clinical Dermatology umesema tatizo kubwa la kutoboa/kuchorwa mwili ni maambukizi (infection) yanayokisiwa kufika asilimia 20 ya kutoboa/kuchorwa sehemu mbalimbali za mwili. Maambukizi haya mara nyingi husababishwa na bakteria na huonekana katika sehemu ya mwili iliyotobolewa/kuchorwa.Madhara mengine ya kutoboa/kuchorwa mwili ni kuvuja damu, mzio/aleji, ngozi kuchanika pamoja na ngozi kuwa na baka au scarring.
Ni mambo gani ya kuzingatia kabla ya kutoboa/kuchorwa mwili wako?
- Unatakiwa kujua uwezekano wako wa kupata maambukizi - Kama tayari una maambukizi au una kidonda kilichowazi, ni bora ukaacha kutoboa/kuchorwa mwili mpaka utakapopona na kuwa na afya njema. Hatari ya kupata maambukizi ni kubwa kama utatobolewa/kuchorwa na mtu ambaye si mtaalamu na hana ujuzi wa kufanya kazi hii. Hakikisha anayekufanyia hivi awe anafahamu masuala ya kukinga wateja wake na maambukizi ambayo ni pamoja na kusafisha vifaa vyake kila baada ya kazi, kuvichemsha vifaa hivyo au kuhakikisha vipo salama na havina bakteria wowote kwa kutumia kemikali za kusafishia, kuvifunika vifaa hivyo baada ya kuvisafisha na yeye mwenyewe kuvaa gloves salama (surgical gloves) wakati wa kufanya kazi yake hiyo ili hata kama ana magonjwa ya kuambukiza asiweze kukuambukiza wewe kwani zipo taarifa ambazo watu wameambukizwa ugonjwa wa ukimwi au wamepata ugonjwa wa tetanus wakati wa kutobolewa/kuchorwa miili yao.
- Hakikisha huna maradhi yoyote sugu - Kama una maradhi ya kisukari, ni bora ukaepuka kutoboa/kuchorwa mwili kwani kidonda chake kinaweza kisipone haraka na hatari ya maambukizi kwa wagonjwa wa sukari iko juu kupitia kwenye vidonda.
- Fahamu kuhusu uwezo wako wa kupona - Unatakiwa uwe na ufahamu juu ya uwezo wa mwili wako katika kupona (healing tendencies) kidonda chochote kile. Kuna watu wengine wanapopata mchubuko au kukatika ngozi zao hupona kwa ngozi ile kufanya kama baka na uvimbe unaojulikana kama keloids. Kama wewe ni mmoja wa watu wa aina hii basi unahitaji kuepuka kufanya kitendo hiki cha kutoboa/kuchora mwili wako. Sehemu ambazo huchukua muda mrefu kupona baada ya kutoboa/kuchora mwili ni pamoja na kwenye maeneo ya tumboni, kwenye chuchu na hata sehemu za siri kwa wanawake.

Dr Khamis
Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).
Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.