Image

Je UTI ni ugonjwa wa zinaa (STI)?

Utangulizi:

Mara nyingi tumeona katika mitandao ya kijamii au katika story za vijiweni tunasikia maambukizi ya njia ya mkojo(UTI) yakihusishwa na magonjwa ya zinaa. Je swala hili lina ukweli ndani yake? Katika makala hii tutaenda kuona maana ya maambukizi ya njia ya mkojo, aina zake, visababishi na tabia hatarishi, dalili, matibabu na tutajibu swali letu lililohamasisha Makala hii.

STI ni nini?

Magonjwa ya zinaa (sexually transmitted infections) ni maambukizi yanayosababishwa na vijidudu kama bacteria,virusi, n.k  ambavyo vinaenezwa kwa njia ya ngono. Maambukizi haya huweza kushambulia maeneo tofauti ya mwili ikiwemo mfumo wa uzazi, mfumo wa mkojo, ngozi, macho,mdomo, na hata ubongo.

UTI ni nini?

UTI (Urinary Track Infection) ni maambukizi ya mfumo wa mkojo ambayo mara nyingi husababishwa na bacteria wanaopatikana kwenye mfumo wa chakula (mfano E.choli) au fangasi. Bacteria hawa kupitia vichochezi mbalimbali hupata upenyo wa kuingia kwenye Mrija wa mkojo ambao husafirisha mkojo kutoka kwenye kibofu hadi nje ya mwili (urethra). Kutoka hatua hii maambukizi haya huendelea kushambulia mwili kwa kupanda kufuata njia ya mkojo hadi kufika kwenye figo. Kutokana na kupanda huku kwa mashambulizi haya tunaweza kugawanya UTI katika makundi matatu:

  • Urethritis : maambukizi kwenye urethra
  • Cystitis : maambukizi kwenye kibofu cha mkojo
  • Pyelonephritis: maambukizi kwenye figo

Vichochezi/visababishi hataraishi vya UTI

1. Jinsia (Maumbile)

  50-60% ya wanawake wote hupata maambumbukizi ya mfumo wa mkojo angalau mara moja katika maisha yao. (Medina, 2019, #)

Wanaume pia hupata maambukizi ya mfumo wa mkojo  lakini Idadi hii kwa wanaume ni ndogo zaidi kulinganisha na wanawake kwasababu ya tofauti katika maumbile ya mfumo wa mkojo. Uwezekano huongezeka kwa wanaume ambao hawajatairiwa.Wanaume wasiotahiriwa ni asilimia 32%, ikilinganishwa na asilimia 8.8% kwa wanaume waliotahiriwa. (Morris & Krieger, 2018, #)

Njia ya mkojo ya mwanamke (urethra) ni fupi kuliko ya mwanaume na hufanya mashambulizi ya vijidudu kupanda kwa haraka zaidi. Lakini pia njia ya mkojo (urethra) ya mwanamke ipo karibu na maumbile ya nje ya mfumo wa uzazi na njia ya haja kubwa, hii husababisha wadudu kuweza kuhama kiurahisi na kushambulia njia ya mkojo.

2. Usafi duni

  • Kutokuwa msafi au kujisafisha vizuri katika eneo la haja kubwa na uke kunaweka mazingira rafiki ya vijidudu kuzaliana kwa kasi na kuweza kuhama kiurahisi kuingia kwenye njia ya mkojo. (namna sahihi ya kujisafisha ni kutoka mbele kurudi nyuma)
  • Kutokujikausha vizuri baada ya kujisaidia  na kuvaa nguo zinazobana muda wote kunatengeneza mazingira rafiki kwa vijidudu hivyo kuzaliana kwani vijidudu hivyo hupenda mazingira ya joto na yenye ubichi/unyevu.
  • Kutokujisafisha vizuri baada ya tendo la ndoa. Hii husaidia kusogeza vijidudu karibu na njia ya mkojo.

3. Kutokunywa maji ya kutosha

kutokunywa maji ya kutosha kunasababisha kukojoa mara chache kwa siku na hivyo mkojoo hukaa mda mrefu kwenye kibofu, hali hii hutengeneza mazaliano mazuri ya vijidudu.

4. Kukaa mda mrefu bila kukojoa

kukaa kwa mkojo kwa mda mrefu kwenye kibofu hutengeneza mazingira rafiki kwa vijidudu kuzakliana. Kukojoa mara kwa mara kunaweza kusaidia kusukuma vijidudu kutoka kwenye mfumo wa mkojo.

Umri

kwa jinsia ya kike UTI hushamiri zaidi kwa watoto. Hii ni kwasababu ya ugumu wa kutunza usafi na ukavu wa njia za haja wakati wote. kwa wanaume UTI huongezeka kwa wazee kwasababu ya ongezeko la magonjwa yanayozuia njia ya mkojo.

Magonjwa yanayo zuia njia ya mkojo, mfano

  1. Mawe kwenye figo au njia ya mkojo kutoka kwenye kibofu kwenda nje (urethra ) .
  2. Kuongezeka kwa tezi dume na Kuzuia njia ya mkojo kwa wanaume .
  3. Saratani ya kibofu cha mkojo .
  4. Kupungua kwa njia ya mkojo kutoka kwenye kibofu kwenda nje (urethra ) kutokana na kovu au kuumia.
  5. Shida za mishipa ya fahamu inayodhibiti kibofu cha mkojo.

Kukaa na mpira wa mkojo (catheter) kwa mda mrefu bila kubadilishwa na usafi duni wa mpira wa mkojo ni moja ya visababishi vikubwa vya UTI kwa wagonjwa waliolazwa. Kihatarishi hiki huongezeka mara dufu endapo katheta hio itaakaa mfululizo bila kutolewa au kubadilishwa.

Dalili za uti

Dalili za kawaida:

  1. Maumivu ya kuchoma wakati wa kukojoa (mara nyingi watu husema mkojo unauma)
  2. Kusikia kubanwa mkojo mara kwa mara lakini mkojo unatoka kidogo tu.
  3. Mkojo kuwa na harufu kali au kubadilika harufu.
  4. Maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo.

Dalili kali :hizi mara nyingi huashiria maambukizi yamefika kwenye figo.

  1. Homa (zaidi ya nyuzi joto 38)
  2. Kichefuchefu na/au kutapika
  3. Maumivu ya maeneo ya ubavuni (chini ya mbavu) na mgongo.
  4. Damu kwenye mkojo.
  5. Usaa kwenye mkojo.

Je UTI ni ugonjwa wa zinaa???

Wakati UTI inaweza kuhusishwa na shughuli za ngono na mara kadhaa kusababishwa na wadudu wanao sababisha magonjwa ya zinaa (kama klamidia na kisonono), UTI siyo ugonjwa wa zinaa moja kwa moja.  Magonjwa ya zinaa husambazwa hasa kupitia ngono, wakati UTI inaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usafi duni au matatizo ya kiafya ambayo hayahusiani na ngono.

Vipimo na matibabu ya UTI.

Wewe au mtu wako wa karibu mkihisi mnazo dalili zilizotajwa hapo juu ni vyema kufika kituo cha afya na kuchukuliwa vipimo ili kuthibitisha ugonjwa na kuanza matibabu.

Vipimo hivyo vinaweza kuwa: 

  • Kipimo cha mkojo (urinalysis)
  • Kuotesha mkojo (urine culture)
  • Picha ya damu (full blood picture)

Vipimo vingine vya ziada vinaweza kuongezwa na mtoa huduma  ili kuondoa uwezekano wa magonjwa mengine kulingana na dalili au maelezo utakayompa.

Matibabu:

Maambukizi ya mfumo wa mkojo mara nyingi husababishwa na bacteria hivyo matibabu yake hua ni antibiotiki. Mara chache maambukizi hayo husababishwa na fangasi hivyo dawa za fangasi hutolewa kulingana na majibu ya kipimo cha kuotesha mkojo. Dawa zingine zinaweza kuongezwa kulingana na dalili mfano: dawa za maumivu au kushusha homa, dawa za kuzuia kutapika, n.k.

Mbali na matibabu ya hospitali mgonjwa anashauriwa kunywa maji mengi ya kutosha, kula matunda yenye maji maji kama matango na matikiti.

Kurudia kwa UTI.

Maambukizi ya mfumo wa mkojo yanaweza kujirudia mara kwa mara. Hii inaweza kusababishwa na vitu vifuatavyo:

  • Maambukizi mapya kutokana na Kurudia tabia hatarishi baada ya ya kumaliza matibabu ( mfano usafi duni)
  • Muendelezo wa maambukizi yalele kutokana na kutokumaliza dawa au usugu wa vijidudu kwa dawa.
  • Upungufu wa kinga mwilini (mfano kisukari, VVU)
  • Kuendelea kuwepo magonjwa mbalimbali kama ya figo au yenye vizuizi kwa njia ya mkojo.

Kumbuka

  • Epuka matumizi yakiholela ya antibiotiki !!
  • Pata matibabu
  • Tumia dawa sahihi
  •  Maliza dozi yote, tumia dawa kwa usahihi kulingana na maelekezo ya     mtoa huduma ili kuzuia kutengeneza usugu wa vijidudu.

Marejeleo:

  • Medscape
  • NHS UK
  • Tanzania standard treatment guideline
  • Medical journals
  • 1.Medina M, Castillo-Pino E. An introduction to the epidemiology and burden of urinary tract                    infections. Therapeutic Advances in Urology. 2019;11. doi:10.1177/1756287219832172
  • 2. Morris B, Krieger JN. Male circumcision protects against urinary tract infections. Version: 2018-02-16. In: Bjerklund Johansen TE, Wagenlehner FME, Matsumoto T, Cho YH, Krieger JN, Shoskes D, Naber KG, editors. Urogenital Infections and Inflammations. Duesseldorf: German Medical Science GMS Publishing House; 2017-.
  • DOI: 10.5680/lhuii000015
Imesomwa mara 159 Imehaririwa Jumanne, 08 Oktoba 2024 10:11
Dr Ladina Msigwa

Distinguished medical doctor and acclaimed author with a passion for enhancing healthcare and sharing knowledge through the written word.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.