Utangulizi
Katika dunia ya leo , msongo wa mawazo ni hali isiyoweza kuepukika ya maisha yetu ya kila siku. Kazi, majukumu ya kifamilia, na shinikizo za kijamii mara nyingi hutufanya tulemewe kihisia . Hata hivyo, kuelewa vyanzo vya msongo wa mawazo na jinsi ya kukabiliana nao kunaweza kuboresha ustawi wetu wa kimwili na kiakili.
Vyanzo vya msongo wa mawazo
Msongo wa mawazo unaweza kusababishwa na mambo mbalimbali yanayotuzunguka. Baadhi ya vyanzo vikuu vya msongo wa mawazo ni:
- Shinikizo la Kazi: Majukumu mengi kazini, ratiba ngumu, malengo makubwa, au mazingira yenye migogoro yanaweza kusababisha msongo wa mawazo kwa mtu.
- Changamoto za Kiuchumi: Wasiwasi kuhusu fedha na mipango ya kifedha, kama vile mikopo, kodi, na gharama za kila siku, ni chanzo kikubwa cha msongo wa mawazo kwa watu wengi.
- Mahusiano:Migogoro au mawasiliano mabaya ndani ya familia, ndoa, au urafiki inaweza kuongeza msongo wa mawazo.
- Mabadiliko ya ghafla ya Maisha: Kupoteza kazi, kuhamia mji mpya, au matukio ya kushtua kama vile kifo au ugonjwa, huchangia kuongezeka kwa msongo wa mawazo
Dalili za msongo wa mawazo
Msongo wa mawazo unaweza kuathiri mwili wako, akili yako, na tabia zako kwa njia nyingi. Dalili za kawaida za msongo wa mawazo ni pamoja na:
- Dalili za Kimwili: Maumivu ya kichwa, matatizo ya kumeng'enya chakula, maumivu ya misuli, na mabadiliko ya hamu ya kula.
- Dalili za Kihisia: Hofu, wasiwasi, kukosa utulivu, kukasirika kwa haraka, au kujihisi kulemewa na hisia.
- Dalili za Kijamii: Kujiondoa kutoka kwa marafiki na familia, kupunguza kushiriki kwenye shughuli unazozipenda, au kuepuka majukumu ya kifamilia na kijamii.
Athari za Msongo wa mawazo kwa Afya
Msongo wa mawazo wa muda mrefu unaweza kusababisha athari mbaya kwa afya, ikiwa ni pamoja na:
- Magonjwa ya Moyo: Msongo wa mawazo sugu huongeza shinikizo la damu, jambo ambalo linaweza kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo.
- Magonjwa ya Kinga: Msongo wa mawazo unaweza kudhoofisha mfumo wa kinga, na hivyo kukufanya uwe na uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi.
Njia za Kukabiliana na msongo wa mawazo
Ikiwa huwezi kuepuka kabisa msongo wa mawazo, kuna njia mbalimbali za kupunguza athari zake kwenye maisha yako.
- Mazoezi ya Mwili: Kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia mwili kutoa homoni za furaha ambazo ni Serotonin, dopamine, endorphins, na oxytocin , ambazo hupunguza msongo wa mawazo na kuboresha hali ya hisia.
- Kupumzika:Mazoezi ya kupumua kwa kina (deep breathing) , kutafakari (Meditation), na yoga ni njia nzuri za kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza utulivu wa akili.
- Matumizi mazuri ya muda : Kupanga ratiba zako kwa uangalifu, kuweka malengo yanayowezekana, na kuzingatia kipaumbele kwa kazi muhimu kunaweza kusaidia kupunguza msongo wa mawazo wa muda mrefu.
- Kujishughulisha na Shughuli Unazozipenda: tenga muda wa kufanya mambo unayofurahia, kama vile kusoma, kupika, au kutumia muda na marafiki, husaidia akili yako kupata pumziko.
- Kuzungumza na Wengine : Kupata msaada wa kihisia kutoka kwa marafiki, familia, au mtaalamu wa afya ya akili kunaweza kusaidia kupunguza hisia za msongo wa mawazo na kuboresha hali ya kiakili.
Mtazamo Chanya
Kubadili jinsi unavyofikiria kuhusu changamoto za maisha kunaweza kusaidia sana kupunguza msongo wa mawazo.
Kukubali kuwa kuna mambo ambayo huwezi kuyabadilisha na kuepuka kujilaumu kunaweza kuongeza uwezo wa kudhibiti msongo wa mawazo.
Hitimisho
Msongo wa mawazo ni sehemu ya asili ya maisha, lakini njia tunayochagua kuushughulikia ina athari kubwa kwa afya zetu za mwili na akili. Kwa kutumia mikakati ya kudhibiti msongo wa mawazo, tunaweza kuimarisha maisha yetu na kuzuia athari mbaya zinazoweza kujitokeza. Ikiwa unahisi kuwa msongo wa mawazo unazidi uwezo wako, usisite kuomba msaada wa kitaalamu.
Je, umewahi kukutana na mtu ambaye anapenda sana utaratibu na anaona vigumu kubadili ratiba yake ya kila siku? Au labda umeona mtoto ambaye anapendelea kucheza peke yake na anaonekana kutojali wengine? Hizi zinaweza kuwa baadhi ya dalili za usonji (autism)
Usonji ni hali ambayo huathiri jinsi ubongo unavyofanya kazi, na kusababisha mtu kuwa na changamoto katika mawasiliano ya kijamii, tabia, nk. Katika makala hii, tutajadili kwa undani zaidi kuhusu usonji, jinsi unavyoathiri maisha ya watu, na njia za kuwasaidia
Usonji, pia unajulikana kama Otizimu (Autism kwa Kiingereza), ni kasoro ya maendeleo ya ubongo inayosababisha ubongo na mfumo wa fahamu kwa ujumla kushindwa kukua kwa njia ya kawaida. Hii ni kasoro ya ukuaji wa mfumo wa fahamu (neurodevelopment) ambayo huathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa mtu kuwasiliana, kujumuika kijamii, na kufikiri. Katika makala hii, tutachambua kwa undani zaidi kuhusu usonji,na athari zake kwa wanaoishi nao.
Usonji ni Nini?
Usonji ni hali inayosababisha mtu kukosa uwezo wa kawaida wa kuwasiliana na kujumuika kijamii. Mtu mwenye usonji anaweza kuwa na shida ya kuelewa lugha na ishara za mawasiliano (expressive and receptive language and gestures), pamoja na kuonyesha Tabia Zilizojirudia Rudia na Zenye Mipaka Maalum (restrictive and repetitive patterns of behaviour) . Aidha, uwezo wa kufikiri wa mtu mwenye usonji pia unaweza kuwa tofauti, na anaweza kuwa na ugumu wa kuoanisha mawazo na hisia zake na mazingira yanayomzunguka.
Dalili za Usonji
Madaktari hutafuta dalili hizi kuu mbili wanapowatambua watu wenye usonji:
1. Changamoto katika Mawasiliano na Mwingiliano wa Kijamii:
- Mwingiliano wa Kijamii:
- Kuanzisha na kubadilishana mazungumzo.
- Kushiriki maslahi au hisia.(sharing of interests and feelings)
- Kuelewa kile ambacho wengine wanawaza au kuhisi.
- Mawasiliano:
- Kutazamana kwa macho (eye contact) kunaweza kuwa kukosa raha kwa baadhi ya watu wenye usonji lakini hii haimaanishi kuwa hawasikilizi.
- Kuelewa lugha ya mwili ya watu wengine, ishara, na sura za uso.
- Kudhibiti sauti, kama vile kuzungumza kwa sauti kubwa au ndogo sana au kutumia sauti ya monotoni. (monotone/flat tone)
- Kuendeleza, Kudumisha, na Kuelewa Mahusiano:
- Kuonyesha hisia na kutafuta faraja ya kihisia kutoka kwa wengine.
- Kufanya marafiki na kucheza na wenzao.
- Kuelewa mipaka na nafasi binafsi.
- Kuhisi kuchoka au kufadhaika katika hali za kijamii.
2. Tabia Zilizojirudia Rudia na Zenye Mipaka Maalum:
- Mienendo ya Kurudia Rudia:
- Kufanya harakati za mwili zinazojirudia rudia kama vile kutikisa mwili, kupiga makofi, au kuzunguka.
- Kupanga vitu kwa mstari, kuzungusha magurudumu, au kuwasha na kuzima swichi mara kwa mara.
- Kuiga mazungumzo ya mtu mwingine, kurudia maneno au misemo (inayojulikana kama echolalia).
- Haja ya Kufanya Mambo kwa Utaratibu Fulani:
- Kukasirika sana hata kwa mabadiliko madogo katika mipango au ratiba.
- Tabia za kimazoea kama vile kuangalia video zile zile mara kwa mara au kugusa vitu kwa mpangilio fulani.
- Haja ya kufuata utaratibu fulani wa kila siku, kama vile ratiba ya kila siku, menyu ya chakula, au njia ya kwenda shuleni.
- Maslahi Makubwa na Yaliyo na Mipaka Maalum: (Restrictive and repetitive patterne of interest)
- Maslahi makubwa au maarifa kuhusu mada maalum na nyembamba.
- Kuwa na shauku kubwa sana kwa kitu fulani kama vile toy au kinyago.
- Hisia za Kupita Kiasi kwa Vichocheo vya Hisia:
- Utofani wa hisia kama vile usikivu mkubwa sana kwa mwanga, sauti, mguso, au umbile la kitu.
- Kukosa hisia kwa maumivu au joto.
- Tabia za kutafuta hisia kama vile kunusa au kugusa vitu, kuvutiwa kwa kuona mwanga au harakati.
Jinsi ya Kuwasaidia Watu Wenye Usonji
Ingawa usonji hauna tiba, kuna mbinu mbalimbali zinazoweza kusaidia kuboresha maisha ya watu wenye usonji na familia zao. Tiba kama vile tiba ya lugha na mawasiliano (speech and language therapy), tiba ya tabia (behavioral therapy), na tiba ya hisia (sensory integration therapy) zinaweza kuwa na msaada mkubwa.
Ni muhimu kwa jamii kuwa na uelewa mzuri kuhusu usonji ili kusaidia kupunguza unyanyapaa na kuboresha ushirikiano wa kijamii kwa watu wenye usonji. Kwa kuzingatia haya, watu wenye usonji wanaweza kufikia uwezo wao kamili na kuishi maisha ya kuridhisha.
Hitimisho
Usonji ni hali inayohitaji uelewa, uvumilivu, na msaada kutoka kwa jamii nzima. Kwa kuelewa vyema usonji, tunaweza kusaidia kuboresha maisha ya watu wenye usonji na familia zao, na pia kuboresha ushirikiano wao katika jamii. Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa watu wenye usonji wanapata nafasi sawa katika jamii na wanapata msaada unaofaa ili kuweza kuishi maisha yenye furaha na mafanikio.
Kumekua na mlipuko barani Africa, nchi za jirani pia zimetangaza kua na wagonjwa wa mpox. Hivi karibuni hata mabara mengine yameanza kutangaza uwepo wa ugonjwa huu kwa kasi, hiii imepelekea WHO kuutangaza ugonjwa wa homa ya nyani kama janga la kimataifa. Hata hivyo nchini Tanzania bado hakujatangazwa kupatikana kesi ya ugonjwa huu.
Homa ya nyani ni ugonjwa unaosababishwa na virusi.virusi hivi ni familia moja na virusi vinavyosababisha smallpox au ndui kwa kiswahili.
Tuone historia ya Homa ya nyani kifupi.
Homa ya nyani sio ugonjwa mpya, umegundulika mwaka 1958 katika nyani waliokua wakifanyiwa tafiti. Kesi ya kwanza ya homa ya nyani kwa binadamu iligundulika mwaka 1970 nchini DRC.
Tangu wakati huo kumekua na kesi chache barani africa hasa africa ya kati na afrika ya magharibi. Lakini mwaka 2022 tumeanza kuona ugonjwa huu ukienea kwa kasi maeneo ambayo sio endemic na hata nje ya bara la Africa.
Unaambukizwaje
- Mji maji au mate yanatotoka kinywani wakati wa Kuongea, kukohoa au kuoiga chafya. (Droplets)
- Aina zote za ngono zinaweza kuambukiza, hii inajuimuisha kumbusu mtu mwenye mpox(All forms of sexual contact including kissing)
- Kukutana au kugusana ngozi na mtu mwenye homa ya nyani (Skin to skin contact)
- Kuvaa nguo au kutumia mashuka na foronya za mtu mwenye homa ya nyani. (Sharing clothes and/or bedding)
- KUgusa au kula wanya walioathirika au mizoga.
Dalili
- Upele (una wezakutokea kwenye ngozi, mdomoni, ukeni, au ndani ya njia ya haja kubwa)
- Homa
- KUskia maumivu kwenye koo. (Sore throat)
- Maumivu Kichwa
- Maumivu ya Misuli
- Maumivu ya mgongo
- Uchovu wa kupitiliza usio elezeka
- Kuvimba tezi
Tiba na chanjo
- Homa ya nyani isiokua na dalili kali (severe) hupona yenyewe ndani ya wiki 2-4 ( self limiting)
- Nenda kituo cha afya kuhakiki kama ni mpox na sio kitu kingine.
- Matibabu ya upele na kutibu dalili zingine kama homa kali na maumivu ya misuli yanaweza kupatikana
Chanjo ya homa nyani ipo lakini bado haipatikani nchi nyingi za Africa.
Watu walio katika hatari Ya kupata Homa ya nyani yenye Dalili Kali (severe).
- Watoto chini ya mwaka mmoja
- Wajawazito
- Watu wenye upungufu wa kinga mwilini.
Watu walio katika hatari ya kupata homa ya nyani
- Watoa huduma ya afya
- Wanaofanya kazi katika mkusanyiko/msongamano wa watu wengi
- Watu wenye wenza wengi ( multiple sexual partners)
- Watu wenye kujihusisha na biashara ya ngono
- Wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja pia wametajwa kuwa na hatari ya kupata.
Jinsi ya kujikinga
- Epuka sehemu zenye msongamano ambazo utagusana na watu
- Nawa mikono kabla ya kujigusa, kula, au unapotoka kwenye mizunguko
- Tumia kinga wakati wa kujamiiana
- Epuka kugusa wanyama wanaumwa au mizoga bila kujua ugonjwa au sababu ya kifo.
Jinsi ya kuwalinda wengine endapo wewe umeathirika.
- Kaa nyumbani au katika chumba chako mwenyewe kama inawezekana.
- Osha mikono mara nyingi kwa sabuni na maji au na vitakasa mikono, hasa kabla au baada ya kugusa vidonda.
- Vaa barakoa na funika vidonda unapokuwa karibu na watu wengine hadi upele wako upone.
- Weka ngozi yako kavu na bila kufunikwa (isipokuwa unapokuwa chumbani na mtu mwingine).
- Epuka kugusa vitu katika maeneo ya pamoja na safisha maeneo ya pamoja mara kwa mara.
- Fuata maelekezo ya daktari katika kutibu vipele/vidonda.
- Tumia dawa za kupunguza maumivu zinazopatikana bila agizo la daktari kama vile paracetamol au ibuprofen.
Nini cha kuepuka
Kupasua au kukuna vipele/malengelenge. Hii inaweza kuweka vijidudu kwenye vidonda na kusababisha vishambuliwe na bakteria au kuchelewa kupona kwa vidoonda. Au kusambaza zaidi mwilili.
Kwa Taarifa, msaada na ushauri zaidi piga simu namba 199
Afya ya Akili
Afya ya akili maana yake ni hali ya kuwa sawa kihisia, kisaikolojia na kijamii inayoambatana na kuwa na uwezo wa kutatua changamoto za kila siku. Ni hali ya kuwa na mawazo chanya, kuwa sawa kijamii na kisaikolojia na kuweza kuchangia katika utendaji wako na uwezo wa kuridhisha wa kimawazo na kitabia. Huhusisha uwezo wa mtu kumudu mfadhaiko wa kihisia kama vile wasiwasi, upweke, hasira, huzuni; ikiwa na maana ya kuwa mstahimilivu na kuwa na mchango katika jamii inayomzunguka.
Afya ya akili inaathiri jinsi tunavyofikiri, kuhisi, na kutenda. Pia husaidia kuamua jinsi tunavyokabiliana na mafadhaiko, kuhusiana na wengine, na kufanya maamuzi yanayofaa. Afya ya akili ni muhimu katika kila hatua ya maisha, kuanzia utotoni na ujana hadi utu uzima. Kumekuwa na tafsiri ambayo si sahihi katika jamii yetu ya kuwa afya ya akili ni hali ya kutokuwa sawa, afya ya akili ni tatizo, afya ya akili ni ugonjwa wa akili, afya ya akili ni upungufu wa akili. Tafsiri hizi zote hazipo sawa. Ukweli ni kwamba afya ya akili ni afya; hakuna afya pasipo afya ya akili. Afya ya akili sio ugonjwa wa akili na hakuna kitu kinachoitwa ugonjwa wa afya ya akili. Kuna umuhimu wa kujifunza maneno haya ili kupunguza unyanyapaa wa afya ya akili katika jamii zetu.
Ugonjwa wa Akili
Ugonjwa wa akili ni hali ya kutokuwa sawa inayoathiri utendaji kazi wa mtu na madiliko huweza kuonekana katika hisia, fikra na matendo tofauti na yale yanayotarajiwa na jamii na hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha. Kuna zaidi ya magonjwa 200 ya akili, ikiwa ni pamoja na sonona, uraibu, wasiwasi uliopitiliza, skizofrenia, baipolar (mawazo mseto).
Ugonjwa wa Sonona
Sonona ni ugonjwa wa akili unaohusisha hali endelevu ya huzuni au kukosa shauku au raha inayoambatana na mabadiliko mbalimbali ya kimwili, kihisia na kiakili pia. Sonona ni hali inayoathiri utendaji kazi mzima wa mtu. Kuna utofauti mkubwa kati ya sonona na msongo wa mawazo. Aidha, msongo wa mawazo uliokithiri huweza kusababisha sonona.
Ugonjwa huu unatokana na namna tunavyotatua changamoto tunazokutana nazo katika maisha yetu ya kila siku. Sonona ni mrejesho wa hisia tulizozibeba ndani yetu kutokana na nyakati mbalimbali tunazozipitia. Hii inaweza kuwa kwa kupanga kutokana na utofauti katika utatuzi wa changamoto zetu. Kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha ndio mwanzo wa kupata sonona. Sonona ni moja kati ya magonjwa ya afya ya akili ulimwenguni ikiwa na zaidi ya watu milioni 264 kwa mwaka wanaoathirika na changamoto hii. Hii ni hali inayoongoza kwa kuleta mzigo mkubwa kwa wagonjwa wengi duniani na katika hali iliyokithiri inaweza kusababisha mtu kuondoa uhai wake.
Watu wengi hupata msongo wa mawazo, ikiwa ni changamoto ya afya ya akili na ni hali ya kawaida kukutana nayo katika maisha. Msongo wa mawazo ukikithiri hupelekea sonona. Sonona pia ikikithiri hupelekea tatizo liitwalo Sonona Kubwa (Major Depressive Disorder, MDD). Sonona Kubwa ni kiwango cha juu cha tatizo ambacho kinahitaji matibabu ya haraka na kitaalamu zaidi.
Takwimu zinaonesha kuwa takriban watu milioni 350 wameathirika na magonjwa ya akili na zaidi ya watu 800,000 kila mwaka hufariki kwa kuondoa uhai wao wenyewe na hii hutokea sana kwa vijana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 29. Ongezeko la changamoto za afya ya akili linakuja kwa kasi ulimwenguni kote ikiwemo Tanzania.
Kutokana na malengo ya maendeleo endelevu (SDG) yaliyooanzishwa mwaka 2015 na Baraza la Umoja wa Mataifa likiwa na malengo ya kufikiwa mwaka 2030, mkusanyiko huo wa malengo 17 yaliyopangiliwa kwa faida ya watu wote; lengo namba tatu ambalo ni “Afya Njema na Ustawi” linahakikisha kila mtu anapata huduma za afya bora. Sonona ni moja kati ya vipaumbele vya Shirika la Afya Duniani kupitia mpango mkakati uitwao WHO’s Mental Health Gap Action Programme (mhGAP) ikilenga kusaidia nchi mbalimbali, haswa kwa nchi za kipato cha chini na kati kuongeza utoaji huduma juu ya afya ya akili na magonjwa mbalimbali ya mfumo wa fahamu.
Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na Lancet Global Health, zinaonesha kuwa kuna uhaba wa takwimu juu ya afya ya akili barani Afrika hali ambayo inaonesha ni jinsi gani bado huduma hizi ni duni barani. Changamoto za afya ya akili zimekuwa zikiongezeka kwa kiasi kikubwa barani Afrika, kitu ambacho kinahitaji kuwekewa mkazo wa hali ya juu. Idadi ya watu barani Afrika inasadikika kuongezeka mara mbili katika miongo mitatu ijayo. Ongezeko la watu linaenda sambamba na ongezeko la changamoto za afya ya akili. Watu wengi hasa vijana wako katika hatari ya kuathirika na changamoto hizi, hii ikitokana na misukumo mbalimbali katika jamii na utumiaji wa dawa za kulevya ukiongezeka ikiwa kama njia kuu ya wahanga hawa kutumia kuepukana na changamoto hizo.
Je, Utajuaje Kama Una Sonona?
Ubaya ni pale ambapo mgonjwa wa sonona hajijui kama anasonona. Hii inapelekea kuongezeka kwa idadi kubwa ya waathirika na kukithiri kwa tatizo. Sonona ni ugonjwa usiofichika. Kupitia muongozo wa magonjwa mbalimbali ya akili (DSM V) pamoja na toleo la Kiswahili – Tiba Baina ya Watu (TBW) kwa International Rescue Committee (IRC) kutoka kwa Shirika la Afya Duniani tunaweza kuona vitu mbalimbali vinavyoweza kuashiria kuwa wewe ni muathirika wa ugonjwa wa akili, sonona. Dalili za sonona hujumuisha:
- Mabadiliko ya usingizi aidha kulala sana ama kukosa usingizi kabisa.
- Mabadiliko katika kula, aidha kukosa kabisa hamu ya kula ama kula sana.
- Hisia za kujiona mwenye hatia au hufai.
- Hisia za uchovu na umakini hafifu kazini.
- Kukosa utulivu wa mwili na kihisia pia.
- Ugumu katika kufanya maamuzi.
- Kupungua uzito bila kutarajia, takribani 5% kwa mwezi ama kuongezeka uzito.
- Kusononeka kila wakati, huzuni endelevu.
- Kujitenga mbali na watu na kupendelea kukaa peke yako muda mwingi.
- Kukosa matumaini kabisa.
- Kupoteza msisimko wa kihisia na kukosa hamu ya tendo la ndoa.
- Kuwa mvivu hata kwenye shughuli za kawaida.
- Kupata maumivu ya mwili kama vile kichwa kuuma mara kwa mara, vidonda vya tumbo, kujihisi mchovu mara kwa mara, kushindwa kuzungumza, kushindwa kutembea.
- Kuwa na hasira mara kwa mara hata sehemu zinazohitaji utulivu.
- Kujawa na chuki juu ya wengine na kutoelewana na watu wanakuzunguka.
- Kutamani kujidhuru na hatimaye kuondoa uhai wa mtu binafsi au pamoja na wale wanaomtegemea.
- ubadilika katika siku za hedhi au kukosa kabisa.
- Uraibu hasa wa pombe.
- Kusahau na kukosa uwezo wa kufikiri vema.
Sababu za Ugonjwa wa Sonona
Visababishi vya ugonjwa wa sonona vinaweza kuwa katika makundi makuu matatu: kibailojia, kisaikolojia na kijamii.
1. Sababu za Kibailojia
- Kurithi kwa vinasaba vya ugonjwa wa sonona. Uwepo wa historia ya ugonjwa huu katika familia huongeza uwezekano wa mtu kupata tatizo hili. Hii inamaanisha ugonjwa huu unaweza ukawa ni wa kurithi kutoka kizazi hadi kizazi, japokuwa kutokuwepo kwa historia ya ugonjwa huu katika familia haina maana ya kuwa hakuna uwezekano wa kupata.
- Magonjwa ya mwili. Magonjwa ya mwili aidha ya muda mfupi kama vile malaria kali ama magonjwa sugu yaani ya muda mrefu kama vile kisukari, homa ya ini, saratani, UKIMWI, figo kushindwa kufanya kazi, nk.
2. Sababu za Kisaikolojia
- Malezi. Watu wengi wanaopata ugonjwa huu wa sonona huwa wanahistoria ya kupata changamoto katika malezi yao walipokuwa watoto. Malezi kwa mtoto yanamchango mkubwa sana katika kujenga ama kuharibu afya ya akili ya mtoto.
- Matukio ya kuhuzun
3. Kijamii
- Matukio kama vile kukosa ajira, matatizo sehemu za kazi, kufukuzwa kazi/chuo, migogoro kazini au kustaafu kazi, kukosa mtoto, kuhamishwa mahali pa kazi, kuoa ama kuolewa.
- Majanga kama vile kimbunga, mafuriko, tetemeko la ardhi, n.k.
- Changamoto za kila siku za maisha kama vile talaka, mimba kuharibika, kutoa mimba, kutengana, kufungwa, kuuguza au kuugua muda mrefu, n.k.
- Madeni, upweke, kukataliwa, kujuta vinaweza kusababisha ugonjwa wa sonona.
Matibabu ya Ugonjwa wa Sonona
Sonona ni ugonjwa unaotibika. Ni muhimu sana kuwahi hospitali au kuonana na mtaalamu husika katika hatua za awali kabisa ili kuzuia kukithiri kwa tatizo. Matibabu ya ugonjwa wa sonona yanagawanyika katika sehemu kuu mbili; ambazo ni:
1. Tiba ya Mazungumzo (Non-Pharmacological)
Mazungumzo na mtaalamu wa afya ya akili ni mojawapo ya tiba madhubuti kwa wagonjwa wa sonona. Njia hii haihusishi dawa ikiwa na maana ya vidonge wala sindano. Hii ni tiba ya kisaikolojia ikiwa na lengo la kubadilisha mtazamo wa muathirika.
2. Tiba ya Kutumia Dawa (Pharmacological)
Hii ni njia inayohusisha utumiaji wa vidonge kama vile amitriptyline, fluoxetine, lorazepam, n.k. Dawa hizi zinafanya kazi katika ubongo kwenye sehemu inayohusika na kupandisha ama kushusha kemikali katika mwili ili kuleta mabadiliko ya kihisia na kitabia kwa mgonjwa husika. Njia hizi zinaweza kutumika zote kwa pamoja kwa mgonjwa mmoja pia.
Njia ya Kuzuia Ugonjwa wa Sonona
Sonona Kazini – Hiki ni kitabu kilichoandikwa katika lugha ya Kiswahili nyepesi na yenye kueleweka na kinachoakisi uhalisia kwa lengo la kujifunza kwa undani zaidi juu ya ugonjwa huu wa sonona na namna gani unaweza kuepuka katika maisha yetu ya kila siku. Kitabu hiki ni kwa ajili ya kila mtu mwenye utashi wa kutambua changamoto anazopitia, aidha akiwa jinsia ya kike au ya kiume.
Hakikisha unapata nakala yako sasa, kokote ulipo utakipata kwa uaminifu kabisa.
"Macho mekundu" ni neno linalotumika kuelezea macho yaliyopata wekundu, kuwasha, na kuwa na viashiria vya damu (bloodshot). Wekundu huu hutokea pindi vimishipa midogo ya damu chini ya uso wa jicho vinapotanuka au kuvimba. Mara nyingi, ni athari ya ukereketaji (irritation) au mashambulizi (infection) ya kwenye jicho.
Macho mekundu yanaweza kuathiri jicho moja au yote mawili. Pia ni hali ambayo inaweza kutokea taratibu au kwa ghafla, kama vile kwa matatizo ya mzio au jeraha la jicho.
Unaweza kuwa na macho mekundu na dalili nyingine kama vile:
- Maumivu ya jicho.
- Kuwasha.
- Kutokwa na matongotongo.
- Kuvimba kwa jicho.
- Mabadiliko katika kuona, kama vile kuona ukungu.
Hatua na viwango tofauti vya ukali wa macho mekundu
Mara nyingi, macho mekundu athari zake huwa kubwa kwa muonekano kuliko jinsi unavyojisikia ndiyo maana kwa wengi huwa hawahisi kitu mpaka wanapoenda kujiangalia na kugundua kuwa jicho limekuwa jekundu. Katika visa vingi, macho mekundu ni ya kawaida na mara nyingi hutibiwa na matibabu ya nyumbani au matibabu ya madawa ya kawaida (OTC).
Lakini ikiwa jicho lako au macho yako yanaendelea kuwa mekundu kwa zaidi ya wiki moja, au una maumivu au matatizo kwenye kuona, hakikisha unaweka miadi ya kuonana na daktari haraka uwezavyo, unaweza kuonana na daktari wa macho ophthalmologist (eye doctor) au daktari wa miwani optometrist.
Ni nini chanzo cha kawaida cha macho mekundu?
Kuna sababu nyingi zinazoweza kupelekea kupata tatizo la macho mekundu, macho yanaweza kupata wekundu kutokana na uvaaji wa lenzi za kuweka machoni kwa muda mrefu au umekaa kwenye kompyuta kwa muda mrefu bila kupata mapumziko. Baadhi ya sababu nyingine za kawaida ni pamoja na:
- Mzio (Allergies).
- Tatizo la Blepharitis.
- Mamabukizi ngozi ya juu ya gololi (Viral Keratoconjunctivitis).
- Jicho kavu.
- Jeraha la jicho.
- Ugonjwa wa Glakoma (Glaucoma).
Mambukizi ya kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu "Viral Keratoconjunctivitis"
Haya ni moja ya maambukizi ambayo hulipuka sana kwenye jamii zetu, Mambukizi ya kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu "Viral Keratoconjunctivitis", ni maambukizi yanayosambaa kwa kasi kubwa. Hakuna tiba maalumu kwa ugonjwa huu na hata bila tiba, dalili huisha zenyewe ndani ya wiki mbili. Usafi ni jambo muhimu kuzuia maambukizi haya kusambaa kwa watu wengine. Mlipuko huu husababishwa na Kirusi kijulikanacho kwa jina la Adenovirus kwa asilimia zaidi ya 80%.
Dalili huonekana kuanzia siku 5 hadi 14 baada ya kupata vimelea vya maambukizi. Aidha, mara chache inaweza kuchukua muda mrefu zaidi. Pia, mtu huchukua siku 1 hadi 2 mpaka kuanza kuonesha dalili na anaweza kuendelea kuambukiza takriban wiki mbili baada ya dalili kuanza kuonekana.
Hadi sasa hakuna tiba maalumu kwa maambukizi ya ugonjwa huu, na dalili huisha kwa muda wa wiki 2, wakati mwingine zinaweza kuendelea kwa wiki hadi 6. Wagonjwa wanashauriwa kufika kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupimwa na kupatiwa dawa za kupunguza madhara kulingana na ishara zitakazoonwa na Daktari.
Maambukizi haya husambazwa kwa njia zifuatazo;
- Kugusa machozi au matongotongo kutoka kwenye macho ya mtu mwenye maambukizi.
- Kugusana mikono na mtu mwenye maambukizi halafu ukajishika machoni.
Macho Mekundu Yanaonekanaje na Kujisikiaje?
Wakati mwingine, jicho lako linaweza kuwa jekundu mahali ambapo palipaswa kuwa kweupe. Hii inaweza kutokea pindi vimishipa vya damu vilivyopo ndani ya macho yako vimevimba kuliosababishwa na kukereketa kwa jicho. Pia, inawezekana kabisa kuwa vimishipa vidogo vidogo vimepasuka.
Ikiwa jicho lako limekuwa jekundu kutokana na jeraha, basi inawezekana kuwa jicho limefungua zaidi (dilate) vimishipa vya damu katika jicho lako ili kuruhusu damu zaidi kufika kwenye eneo hilo kwa ajili ya kuharakisha uponyaji kwani damu ndiyo nyezo inayotumika kwenye uponyaji ndani ya mwili wa binadamu. ufungukaji mkubwa wa vimishipa hivi ndiyo inayosababisha macho kuwa mekundu.
Kulingana na hali inavyoendelea, macho yako mekundu yanaweza kujisikia:
- Halina shida yoyote, kwa wengi wenye hali hii hawawezi kujua kama wana jicho jekundu mpaka wajiangalie au waambiwe na watu wengine.
- Kuwasha au kuwa na kero, mara nyingi kwa wale walipata maambukizi (infection).
Jinsi ya kujisaidia
Kumbuka kuwa, kuna aina nyingi sana za macho mekundu, baadhi yake unaweza kujitibia wewe mwenyewe nyumbani na nyingine utajitaji msaada wa haraka wa daktari.
- Pata mapumziko ya kutosha.
- Weka kitambaa kizito juu ya macho yaliyofungwa.
- Fanyia massage ngozi ya juu ya jicho (eyelid)
- Kwa utaratibu kabisa safisha ngozi ya jicho (eyelid) kwa kutumia maji safi.
- Unaweza kuweka matone ya dawa za kawaida (OTC).
- Wakati mwingine, mtaalam wa huduma ya macho anaweza kupendekeza na kutoa dawa za viua vijasumu (antibiotics), matone maalum ya macho, au dawa za kunywa.
Ni nini hatari au madhara yanayowezekana ikiwa macho mekundu hayatibiwi?
Kwa mara nyingi, macho mekundu si hatari na inaweza hata isiwe na haja ya matibabu. Hata hivyo, kuna hali zinaweza kuwa na athari kubwa zaidi na zitakuladhimu upate matibabu ya kina.
- Ikiwa umekaa na jicho jekundu kwa zaidi ya siku moja au mbili, au ikiwa tatizo hili limempata mtoto mdogo, basi unashauriwa uwasiliane na mtoa huduma za afya kwa uangalizi zaidi.
- Pia, unatakiwa kuwasiliana na mtoa huduma pindi unaposikia maumivu au jicho linatoa matongotongo au uchafu wowote.
- Endapo jicho lako kuwa jekundu ni matokeo ya athari kubwa kwenye jicho, endapo utakaa nalo bila ya matibabu linaweza kupelekea matatizo makubwa ikiwemo kupoteza uwezo wa kuona.
Jinsi ya kuepuka macho mekundu.
Si rahisi kuepuka kila macho mekundu, lakini unaweza kupunguza uwezekano wa kupata macho mekundu kwa kufuata ushauri ufuatao;
- Usipendelee kusugua macho kwa kutumia mkono. Uchafu na vijidudu (germs) vilivyopo kwenye mikono yako vinaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ya jicho kuwa jekundu au kukereketa (irritation).
- Kama unatumia lenzi za ndani ya macho, hakikisha ni safi na usiweke kupitiliza muda ulioshauriwa.
- Kwa wadada, tumia njia sahihi kuondoa urembo (make up) na hakikisha macho yako yanabaki masafi.
- Hakikisha unapata muda wa kupumzika kila utumiapo kompyuta. Usitumie kwa muda mrefu bila kupata mapumziko.
- Epuka vitu vinavyoweza kupelekea jicho kukereketa kama vumbi,moshi nk.
- Hakikisha unajenga desturi ya kunawa mikono kwa maji safi na yanayotiririka kwa sabuni mara kwa mara kuzuia kupata maambukizi.
- Onana na daktari pindi unapoona unapata macho mekundu mara kwa mara au umepata macho mekundu yasiyoisha.
- Usichangie vipodozi na vitu vingine unavyotumia kama vile taulo za karatasi au nguo au dawa za macho.
- Funika mdogo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya ili kuzuia kuambukiza wengine.
Dalili za hatari
Ingawa macho mekundu huisha yenyewe baada ya muda, ila kuna wakati, macho mekundu ni ishara ya ugonjwa mkubwa.Wasiliana na daktari pindi unapoona;
- Jicho linauma.
- Umeanza kuwa na uono hafifu.
- Macho yanakuwa yanaogopa mwanga kupitiliza (extra sensitive to light).
- Una dalili zaidi ya wiki na zimekuwa zikiendelea kuwa mbaya.
- Jicho limekuwa likitoa matongotongo yanayoganda kwenye kope.
- Umepata homa au maumivu yanayoambatana na kujisikia vibaya.
Hakikisha unaenda hospitari haraka iwezekanavyo pindi unapoona moja ya dalili hizi;
- Jicho linauma kupitiliza.
- Unaogopa mwanga kupitiliza.
- Jicho limevimba.
- Unaona ukungu.
Neno kutoka TanzMED
Kimsingi, karibu kila mtu kwa nyakati tofauti amewahi kupata changamoto ya macho mekundu. Kwa wengi wetu, macho mekundu haijawahi kuwa ni tatizo kubwa. Maranyingi husababishwa na mkereketo wa jicho na huondoka pindi mkereketo unapoisha wenyewe. Lakini, kuna wakati kwa baadhi ya hali utatakiwa kwenda kuonana na daktari kwa vipimo zaidi. Hakikisha unawahi hospitali pindi unapoona maumivu ya jicho au changamoto kwenye uono (vision). Ni maamuzi ya busara kupata ushauri wa daktari pindi unapokuwa na changamoto ambayo hauna uhakika nayo. TanzMED inakuwezesha kuweka miadi na kuongea na daktari moja kwa moja kwa njia ya mtandao. Pakua TanzMED App na uweke miadi leo.
Baadhi ya vifungu vimekopiwa kutoka vipeperushi vya Elimu ya Afya kwa uma https://elimuyaafya.moh.go.tz/
Tatizo la kunyonyoka nywele hujulikana kitaalamu kama alopecia (tamka ‘’ alopesia’’). Hali hii ya kunyonyoka nywele husabababishwa na mfumo wa kinga ya mwili kushambulia mwili wa mtu husika (autoimmune disorder).
Kwenye alopecia, mfumo wa kinga ya mwili hushambulia mizizi ya nywele (hair follicles) na hivyo kusababisha kunyonyoka kwa nywele.
Wingi wa kunyonyoka nywele hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.Kwa baadhi ya watu, nywele hunyonyoka sehemu ndogo na kusababisha mabaka mabaka madogo ambayo mwanzoni sio rahisi mtu kugundua.Baadae mabaka haya huungana na kuwa sehemu moja kubwa iliyonyonyoka nywele na hatimaye mtu anaweza kugundua.
Kwa wengine, nywele hunyonyoka kwa wingi sana. Baadhi ya wagonjwa wameota nywele baada ya awali kunyonyoka na kisha nywele hizo hunyonyoka tena. Mara chache hutokea kwa mgonjwa alienyonyoka nywele kuota tena nywele hizo kwa maisha yake yote.
Alopecia haina uhusiano wa umri wala jinsia ya mtu.Kwa hiyo, mtu yoyote anaweza kupata hali hii.
Kwa kawaida, meno ya mtoto ya utotoni (meno ya awali) huanza kutoka kuanzia miaka 6. Kwa baadhi ya watoto, huweza kuchelewa kuanza kutoka meno ya utotoni hadi wanapoanza mwaka wA 7.
Meno ya kwanza yanayoanza kutoka ni yale mawili ya chini ya kati (lower central incisors) na hufuatiwa na yale ya juu ya kati (upper central incisors) (. Baada ya hapo, hufuatiwa na meno ya kutafunia ya kwanza na ya pili.
Kwa kawaida, meno ya ya awali hukaa bila kutoka mpaka pale meno ya kudumu yanapotaka kuanza kuchomoza, hivyo hulisukuma jino la utoto na kusababisha kutoka. Endapo mtoto atatoka meno mapema au jino litatoka kwa sababu ya ajali au kuoza, basi jino la kudumu litaziba pengo hilo baada ya muda kufika. Hii inaweza kusababisha meno kutokuwa na mpangilio mzuri kwakuwa wakati linachomoza kulikuwa na meno mengine ya utotoni, hivyo unashauri kuwasiliana na daktari wa kinywa na meno kwa ushauri zaidi.
Pale mtoto anapoanza kutoka meno, tafadhali zingatia kanuni bora za Afya ya kinywa na meno kama ;
- Kuhakikisha anasubua meno angalau mara mbili kwa siku. Mkazanie kwa sababu umakini unahitajika.
- Msaidie mtoto kusugua meno kila siku
- Hakikisha anakula chakula bora na kupunguza matumizi ya vyakula vitamu
- Weka miadi na daktari wa kinywa nameno
Kwa mazingatio haya, utaweza kuhakikisha afya bora ya kinywa na meno ya mtoto wako. Pia, unaweza kusoma makala zaidi juu ya Afya ya kinywa na meno wakati wa makuzi ya mtoto
Afya bora ya kinywa na meno kwa mtoto ni muhimu sana na ina uhususiano wa moja kwa moja na afya yake kwa ujumla. Humuepusha mtoto kupata maumivu, uwezekano wa uambukizo, kumfanya aweze kutafuna vizuri ili kupata virutubisho muhimu kwa ajili ya kujenga kinga dhidi ya magonjwa, na kusaidia ukuaji. Afya nzuri ya kinywa na meno pia itamfanya mtoto aweze kuhudhuria masomo ipasavyo na hivyo kupata matokeo mazuri.
Umuhimu wa meno ya utoto
Wazazi /walezi wengi hujiuliza kwanini wahangaike kutunza meno ya utoto ambayo yanatarajiwa kung’oka na kuota ya ukubwa. Meno ya utoto ni muhimu kutokana na sababu zifuatazo:
Humsadia mtoto kutafuna na hivyo kumwezesha kupata virutubisho muhimu
Hutunza nafasi kwa ajili ya meno ya ukubwa
Hali ya afya ya meno ya utoto huathiri hali ya afya ya meno ya ukubwani
Husadia uumbaji wa maneno (kuongea)
Kama mzazi / mlezi unatakiwa kuwa mstari wa mbele kutunza meno ya mtoto wako kwani, watoto hupenda kujifunza kutokana na mfano wa wazazi.
Zifuatazo ni dondoo muhimu kwa wazazi/walezi kwa ajili ya kutunza afya bora ya mtoto:
Umri wa kuzaliwa mpaka miezi 6
- Mnyonyeshe mtoto maziwa ya mama pekee hadi umri wa miezi sita.
- Maziwa ya mama ni muhimu sana kwa ukuaji na kinga dhidi ya magonjwa.
Umri wa miezi 7 hadi miezi 18
- Usimlaze mtoto akiwa na chuchu ya maziwa au chuchu ya mama mdomoni ili kuzuia ugonjwa wa kuoza kwa meno (rampant caries)
- Mpatie mtoto maji badala ya juisi akiwa na kiu.
- Iwapo utampa mtoto juisi ya boksi unashauriwa kuongeza kiwango cha maji sawa na kile cha juisi ili kupunguza kiasi cha sukari kilichomo ndani ya juisi.
- Ukitengeneza juisi nyumbani kwa ajili ya mtoto, jiepushe kuiongezea sukari.
- Jino la kwanza litakapoota, anza kusafisha kinywa cha mtoto kutumia kitambaa laini kilicholoweshwa kwenye maji safi au mswaki laini bila dawa.
- Panga miadi ya kwanza ya kumwona daktari wa meno (first appointment) wakati mwanao hana maumivu au shida yoyote ili kujenga mahusiano mazuri kati ya mtoto na daktari
Umri wa miezi 18 hadi miaka 6
- Dhibiti ulaji wa vyakula vyenye sukari na zingatia ulaji wa vyakula vinavyojenga afya ya mtoto kama matunda, mboga mboga, karanga, maziwa na samaki.
- Safisha meno ya mtoto kutumia maji safi na mswaki laini na dawa ya meno (zingatia kiwango cha dawa: kiasi cha mbegu ya kunde) asubuhi na jioni kila siku.
- Mtoto asukutue mdomoni ili kupunguza kiwango cha dawa itakayobaki.
- Chunguza mara kwa mara meno ya mtoto ili kugundua dalili za mwanzo za ugonjwa wa kuoza kwa meno (rangi kuwa nyeupe au kahawia zaidi katika eneo husika baada ya kukausha) na pia matatizo mengine kama uvimbe, vijipu au kutoka damu kwenye fizi.
- Mpeleke mtoto kwa daktari wa meno angalau mara moja kwa mwaka na mara unapogundua tatizo lolote kinywani mwake.
Umri wa miaka 6 hadi 12
- Msimamie mtoto kusafisha kinywa na meno mara mbili kwa siku.
- Mtoto ateme dawa itakayobaki ila asisukutue na maji baada ya kupiga mswaki.
- Mjengee mtoto tabia ya kusukutua na maji kila baada ya kula vyakula vyenye sukari kama keki, chokoleti au juisi.
- Chunguza mara kwa mara meno ya mtoto ili kugundua dalili za mwanzo za ugonjwa wa kuoza kwa meno na matatizo mengine kinywani.
- Mpeleke mtoto kwa daktari wa meno angalau mara moja kwa mwaka na mara unapogundua tatizo lolote kinywani mwake.
Umri wa miaka 12 na zaidi
- Mtoto anaweza kuanza kusafisha kinywa na meno bila ya usimamizi.
- Dhibiti ulaji wa vyakula vyenye sukari na zingatia ulaji wa vyakula vinavyojenga afya ya mtoto kama matunda, mboga mboga, karanga, maziwa na samaki.
- Mpeleke mtoto kwa daktari wa meno angalau mara moja kwa mwaka na mara unapogundua tatizo lolote kinywani mwake.
CREDIT: Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS)
Assalamu’alaikum Warahmutullahi Wabarakatuh. Natumai mu wazima wa afya na mnaendelea vyema na majukumu ya kila siku.
Waumini wa dini ya Kiislam duniani kote wameingia katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hivyo,katika muendelezo wa makala zinazohusu kisukari, tunaoenda tujikumbushe au tujifunze mambo machache ya kufanya kabla, wakati na baada ya kipindi takatifu cha mfungo wa Ramadhani.
Tukiwa tuna amini kuwa watu wengi wanaoishi na tatizo la Kisukari hasa aina ya pili ya kisukari wanatamani sana kufunga Ramadhani katika kutimiza moja ya nguzo za imani ya dini ya Kiislam, na kwa imani Funga ni dawa kiroho na kimwili pia.
Jambo la kwanza kwa mtu mwenye kisukari ni kujiweka tayari kwa funga miezi mitatu au minne kabla, kuitayarisha akili na nafsi,hii itakusaidia kuwa mwangalifu sana katika ulaji wako na mfumo mzima wa ulaji.
Kufanya kipimo cha hba1c ni muhimu kwa sababu inaonesha kiwango cha sukari miezi mitatu na hii inakufanya ujue kama utaweza kufunga ramadhan bila kuwa tatizo lolote au hutaweza kufunga. Kupima sukari kabla na baada ya kula kabla ya mfungo wa ramadhani pia ni muhimu,kabla ya kula ni lazima sukari iwe chini ya sita(6) na masaa mawili baada ya kula iwe chini ya nane (8) na kama majibu yatakuwa hivyo kila mara hii itakuonesha kuwa unaweza kufunga bila tatizo.
Jambo la pili ni kuhakikisha unapata ushauri kutoka kwaa daktari wako wa kisukari, Shauriana naye, usiamue kufunga Ramadhani bila ya kushauriana na daktari wako, hii ni muhimu kwa sababu anaweza kukupa ushauri kulingana na kiwango chako cha sukari kwa miezi mitatu nyuma.(hba1c) na kipimo cha sukari cha kila siku unachopima kabla na masaa mawili baada ya kula.
Wakati wa mfungo ni lazima mtu mwenye kisukari atambue kuwa anaweza kufunga baada ya ushauri na ruhusa dakitari wake,na endapo akifunga, ni lazima pia awe anapima kiwango cha sukar kabla ya kuanza ,mfungo,kwa mfano, kabla ya kula daku ni lazima apima,hii itamsaidia kujua kama ataweza kufunga kwa siku hiyo ama Lah, kama akipima na kiwango cha sukari kikiwa sita (6) au saba(7) anaweza kufunga lakini indapo akipima akikuta kwango cha sukar iki chini ya sita (6), labda ni tano(5) au nne (4) hatoweza kufunga kwa sababu moja ya kisababisho cha sukari kushuka ni kukaa bila kula kwa muda mrefu.
Kutokupata choo au kuhisi kwenda kujisaidia haja kubwa na kutofanikiwa kutoa choo au mtu kupata choo chini ya mara tatu kwa wiki hujulikana kitaalamu kama constipation.Mtu mwenye tatizo hili la kufunga choo hupata choo kigumu,kikavu na chenye kupita kwa taabu kwenye njia ya haja kubwa.
Tafiti nyingi zinaonyesha kwamba angalau kila mtu katika maisha yake huwa anapata tatizo hili la kufunga choo. Kufunga choo ni tatizo ambalo watu wengi bado huhisi ni jambo la aibu sana hata kulizungumzia na hubaki na tatizo kwa muda mrefu mpaka pale wanapopata madhara ya kiafya ndio hutafuta msaada wa kitabibu.
Dalili zifuatazo zinaweza kutumika kuelezea tatizo la choo kufunga;
- Kupata choo kigumu na kinachoambatana na maumivu makali wakati wa kwenda haja kubwa
- Kutokupata choo kwa muda mrefu (infrequent bowel movements)
- Mtu kuhisi kama hajamaliza haja kubwa licha ya kupata choo
Tafiti nyingi zilizowahi kufayika zinaonyesha kwamba takribani asilimia 16 (16%) ya watu wazima hupata tatizo hili la kufunga choo,waathirika wengi wakiwa ni watu wenye umri kati ya 60-110 (asilimia 35%).
Kwa nini wazee hupata tatizo hili la kufunga choo?
Sababu zifuatazo huchangia wazee kutokupata choo au kufunga choo;
- Hali ya uzee husababisha mmeng’enyo wa chakula kufanyika taratibu (slow metabolism)
- Ukosefu wa lishe bora
- Kutokunywa maji ya kutosha
- Kutofanya mazoezi
- Magonjwa ya uzee kama pelvic floor prolapse na utumiaji wa dawa aina ya antacids na dawa za kupunguza maumivu
- Pia uzee husababisha meno kung’oka hivyo wazee huchagua vyakula laini na vyenye ufumwele (fiber) kidogo
Wanawake wajawazito ni miongoni mwa watu wanaopata tatizo hili la kufunga choo mara kwa mara.
Visababishi vya choo kufunga (constipation) ni kama ifuatavyo;
- Kutokula mlo wenye ufumwele (fiber) wa kutosha
- Kutokunywa maji ya kutosha
- Kutumia sana dawa za kulainisha choo
- Kutokufanya mazoezi au
- kuishi maisha ya unyongovu (stressful life)
- Madawa kama aspirin (NSAID), morphine, dawa za presha(thiazides, verapamil, furosemide), dawa za sonono (antidpressants), madawa ya saratani n.k
- Magonjwa ya mfumo wa mmengenyo wa chakula au vichocheo vya mwili (hormonal disorders) kama hypothyroidism
- Ujauzito- Mama mjamzito yupo kwenye hatari zaidi ya kupata choo kigumu au constipation hasa katika miezi ya mwisho ya ujauzaito wake kwa sababu ya kuongezeka kwa vichocheo mwili aina ya sex hormones, kupungua kwa mmeng’enyo kwenye tumbo na kuchelewa kwa tumbo kupitisha chakula (delayed interstinal emptying)
- Magonjwa ya tumbo kama colorectal dysfunction, diverticulitis, irritable bowel syndrome, saratani za matumbo hasa utumbo mkubwa
- Chronic Idiopathic constipation- Sababu zisizojulikana
Kama ambavyo tumejifunza sababu na makundi wa watu ambao wapo kwenye hatari zaidi. Tatizo hili linaweza kumpata mtu yoyote wa rika lolote hata watoto wachanga. Hivyo fuatilia makala zetu zijazo ili kujua uchunguzi,matibabu na jinsi ya kuepukana na tatizo hili la kufunga choo.Kama tayari una tatizo hili tafadhali fika kituo cha afya kilichokaribu nawe kwa ajili ya uchunguzi, matibabu na ushauri wa kitaalamu.