Image

Sababu na Dalili za Kuharibika kwa Mimba Sehemu ya Pili (Third trimester miscarriage)

Makala hii ni muendelezo wa makala ya kwanza kuhusu Sababu na Dalili za Kuharibika kwa Mimba, katika sehemu ya kwanza ya Sababu na dalili za Kuharibika kwa Mimba - Sehemu ya Kwanza tuliangalia maana ya kuharibika kwa mimba na baadhi ya visababishi vyake sehemu ya kwanza. Katika makala hii tutaangalia kuharibika kwa mimba miezi mitatu ya mwisho ya kipindi cha ujauzito (Third trimester miscarriage).

Kuharibika kwa mimba kwa kipindi hiki sio sana kama kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo.

Visababishi vya kuharibika kwa mimba ni;

 • Kukaa vibaya kwa kitovu cha mtoto au hata kuwepo kwa fundo (knot) kwenye kitovu cha mtoto
 • Kulegea na kulainika kwa shingo ya kizazi (Cervical Incompetence)
 • Matatizo ya viashiria vya asili ambavyo havikugundulika hapo awali (Chromosomal defects)
 • Bawasiri (Hemorrhages)
 • Kukosekana kwa uwiano wa vichocheo mwilini (hormonal imbalance)
 • Utapia mlo
 • Vipimo vya vina saba kama Amniocentesis or Chorionic Villus Sampling (CVS) ambavyo hufanyika wiki ya 16 ya ujauzito
 • Maambukizi kama ugonjwa wa mafua, surua na ugonjwa wa mishipa ya fahamu au neva
 • Uvimbe katika mfuko wa uzazi (fibroids)
 • Mimba kupitiliza umri wake zaidi ya wiki 41 za ujauzito (post maturity )
 • Matatizo ya maumbile ya mfuko wa uzazi (Uterine structural abnormalities/defects)
 • Matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine
 • Uvutaji sigara na unywaji pombe
 • Matatizo ya kondo la nyuma la uzazi -Abruptio placenta au Placenta Previa

Abruptio Placenta ni kuachia kwa kondo hili kutoka kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi. Ikumbukwe ya kwamba kondo hili ndilo linalohusika kumpa mtoto chakula pamoja na hewa ya oksijeni wakati wa ujauzito.

Chanzo cha tatizo hili hakijulikani isipokuwa kinahusishwa na ugonjwa wa kisukari, presha (140/90mmHg au zaidi), uvutaji sigara, matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine, kuwepo kwa historia ya kupata tatizo hili hapo awali,maumivu kwa mama mjamzito kutokana na kupigwa, kuzaa watoto wengi haya yote huchangia uwezekano wa kupata tatizo hili.

Viashiria vyake ni pamoja na kutokwa damu kwenye tupu ya mwanamke na maumivu makali sana ya tumbo.

Baadhi ya vichagizi (risk factors) vya kuharibika kwa mimba kipindi hiki ni;

 • Kubeba mimba yenye watoto wengi (Multiple pregnancy)
 • Kushika mimba tena ndani ya muda mfupi baada ya kujifungua hapo awali
 • Hypothyroidism-Ugonjwa wa tezi koo
 • Kutopata choo (Constipation)
 • Kuharisha
 • Polycystic ovary syndrome 

Viashiria vya kuharibika kwa mimba kipindi hiki ni kama ifuatavyo;

 • Kutokwa damu sana kupitia tupu ya mwanamke (Heavy vaginal bleeding)
 • Kuona matone ya damu kutokwa na matone ya rangi kutoka kwenye tupu ya mwanamke
 • Maumivu makali na kuhisi maumivu yanavuta sehemu za tumbo (cramps)
 • Maumivu ya kiunoni
 • Kichefuchefu, kutapika na kuharisha
 • Maumivu kwenye bega
 • Kubana na kuvimbiwa tumbo
Imesomwa mara 4806 Imehaririwa Jumanne, 18 Aprili 2017 12:51
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.