Katika miaka ya hivi karibuni, kama wewe ni daktari, mfanyakazi wa kada ya afya,binti au kijana hasa wa miaka 15-24 ni dhahirikabisa jina la P2 si ngeni masikioni mwako. Dawa hii imejizoelea umaarufu mkubwa miongoni mwa mabinti hasa wa umri tajwa kama ni njia kuu ya kuzuia kupata ujauzito. Ingawa dawa hii inaweza kuwa na manufaa yaliyokusudiwa, lakini matumizi yasiyo sahihi huweza kuleta madhara makubwa ukizingatia wengi wanaotumia hawana uelewa mpana juu yake.
Kwa uzoefu niliopata nikiwa kazini mabinti wengi wanaotumia dawa hii ni wale ambao bado hawapo kwenye ndoa lakini wamekuwa wanashiriki tendo na wenza wao, pia, wapo wanawake wachache ambao wapo kwenye ndoa lakini wanatumia P2 kama ni sehemu ya uzazi wa mpango.
Ukweli ni kuwa, mabinti wengi wanaotumia dawa hii ya P2 hujikuta wakitumia kwa sababu;
- Hupatikana kwa urahisi katika maduka mengi ya dawa baridi, na huuzwa bila ya maswali mengi ya ‘kwanini kwanini’-unalipa- unapewa dawa-unaondoka.
- Kutokana na kuona aibu ya kuonekana wanashiriki tendo kabla ya ndoa, mabinti wengi wanaogopa kuhudhuria vituo vya afya kupata ushauri wa uzazi salama na uzazi wa mpango, wengi wao huwa na hofu ya kunyanyapaliwa au kukutana na ndugu wanaowafahamu hivyo kuzua taharuki kwenye familia- kuwa sasa binti huyu ameanza kujihusisha na mapenzi- kumbuka kuwa watumiaji wengi ni kuanzia miaka 15 mpaka 24 (inawezekana ikawa chini au zaidi ya umri huo pia) wengi wao bado hawapo kwenye ndoa.
P2 ni nini:
P2 ni kifupi cha dawa (Postinor-2) hii ni dawa/kidonge kilicho na vichocheo vya homoni kwa ajili ya kuzuia mimba zisizotarajiwa (emergency contraceptive pills) au wengine huita (morning after pills).
Hii ni kati ya dawa nyingi za namna hii ambazo huzuia mwanamke asipate ujauzito inapotokea amefanya mapenzi wakati wa siku za hatari (fertile days) bila kutumia kinga au alitumia kinga (kondomu) ambayo labda ilipasuka (kuachana mkeka) wakati wa tendo na akawa na hofu ya kupata ujauzito.
Dawa hii hushauriwa kutumika si zaidi ya masaa 72 toka mwanamke aliposhiriki tendo la ndoa. Pakiti moja huwa na vidonge viwili ambapo kimoja kinatakiwa kunywa mara tu na kingine hutumia masaa 12 baada ya kunywa kidonge cha kwanza. Ifahamike kuwa vichocheo vya homini katika dawa hizi ni vya kiwango cha juu sana kulinganisha na vidonge vingine vya homini vya kuzuia mimba vya muda mrefu.
Je P2 hufanyaje kazi:
Vidonge hivi hufanya kazi kwa namna kadhaa:
- Hatua ya kwanza kabisa ni kufanya yai lichelewe kupevuka hivyo kuchelewesha uwezekano wa haraka wa kukutana na mbegu na kurutubishwa.
- Pili hufanya ute ute wa ukeni kuwa mzito hivyo huzifanya mbegu za mwanamume (sperms) kushindwa kuogelea kwa haraka kulifuata yai kwa ajili ya kulipevusha. Unaweza kusoma makala ya jinsi gani yai linavyochavushwa hapa.
- Pia, Homoni zilizotolewa na dawa hii ya P2, huufanya mji wa mimba kutokuwa tayari kwa ajili ya kupokea yai lililorutubishwa hivyo huondoa uwezekano wa yao lililochavushwa kwenda kujishikiza tayari kwa ajili ya ukuaji.
Hivyo basi, dawa hii haiwezi kutumika kama dawa ya kutoa ujauzito (abortion) kwa mtu ambaye tayari ni mjamzito.
Faida
Ikitumiaka kwa namna sahihi inaweza kusaidia kuzuia ujauzito usiotarajiwa.
Madhara:
- Dawa hii inavichocheo vya homoni vya kiwango cha juu hivo havimpasi mtu kutumia mara kwa mara lasivyo inaweza leta madhara ya kuharibu utaratibu wa kifisiolojia wa upevukaji wa mayai kwani mara nyingi mwili wa binadamu hubadilika badilika kulingana mazingira, madhara ya mabadiliko haya ya kifisiolojia ni kama:
- Kuchelewa kupata ujauzito kutokana na mayai kutopevuka kwa wakati
- Kupata hedhi isiyotabirika
- Kupata hedhi nyingi kuliko kawaida
- Kutokupata hedhi kabisa
- Mimba kutunga nje ya kizani (ectopic pregnancy)
Mimba hutunga nje ya uzazi endapo mimba imetungwa nje ya mji wa mimba (uterus), mara nyingi hutokea kwenye mirija ya folopian ambapo uchavushwaji hutokea na yai lililochavushwa likashindwa kusafiri kwenda mji wa Mimba. Hii huchangiwa na mabadiliko ya Homoni ambapo P2 hufanya lakini ni nadra sana kutokea kwa sababu ya P2.
- Kuleta shida zaidi au dawa kutofanya kazi kwa usahihi kama utakuwa na magonjwa kama homa ya ini, moyo,figo,sukari au saratani-unatoka damu bila mpangilio-au kama unatumia dawa za muda mrefu kama vile dawa za kufubisha virusi vya ukimwi au dawa za kifaa hivyo ni salama zaidi kujua afya yako kwa ujumla au kuzungumza na mtaalam wa afya kabla ya kumeza/kutumia vidonge hivi.
Maudhi mengine yanaweza kutokea ni pamoja na kichefuchefu, kizunguzungu nk.
Mambo ya msingi ya kuzingatia:
P2 inatumika kuzuia mimba kwa dharura, hivyo haupaswi kuitumia kama njia ya kudumu au kunywa mara kwa mara kwa ajili ya kuzuia mimba- tafadhali kama unafanya hivyo basi tembelea kituo cha afya cha karibu kwa ushauri zaidi.
Hata kama umetumia P2, bad kuna uwezekano wa kupata ujauzito, hivyo kama umetumia P2 na ukakosa hedhi hedhi basi ni vizuri ukapima ujauzito. Watu wengi wanaotumia P2 na bado wakapata ujauzito huamua kufanya utoaji wa mimba kwa njia wanazozijua wao ambazo ni hatari zaidi. Unapogundua hali hiyo ni vyema kutembelea kituo cha afya kwa ushauri zaidi.
Lakini pia wanawake wengi wanasahau kuwa dawa hizi hazizuii magongwa ya zinaa kama vile HIV, Kisonono, Kaswende- hivyo kuwafanya waangalie upande mmoja wa afya yao na kuacha upande mwingine ambao pia ni hatari zaidi kwa faya yao ya uzazi kwa ujumla- kwa sababu magonjwa haya yasipotibika yanaweza kuleta athari kubwa kwenye via vya uzazi na kuleta madhara ya kutopata ujauzito ambao kwa sasa wanaukimbia.
Hivyo wazazi na walezi ni vizuri kuchukua hatua za makusudi kutenga muda wa kuongea na vijana wetu`kuhusu afya ya uzazi,kuwasikiliza, kutambua na kufuatilia mienendo yao kwa karibu.
Lakini pia serikali kwa kushirikiana na wahudumu wa afya pamoja na wizara ya elimu kuweka mazingira sahihi ili kuwasaidia vijana kuweza kupata elimu Rafiki ya afya ya uzazi pia uwoga au kunyanyapaliwa- wanapokuwa na uelewa sahihi inawasaidia kufanya maamuzi sahihi ambapo ni pamoja kujizuia kufanya tendo la ndoa kabla ya wakati au kijihusisha na mahusiano yanayoweza kuhatarisha afya yao kwa ujumla.