Katika siku za karibuni, kumekuwa na changamoto kubwa kwa wanawake walio katika umri wa uzazi kutokupata hedhi (Amenorrhea) au kupata hedhi nje ya mpangilio maalumu. Hali hii siyo tuu hupelekea mawazo kwa baadhi ya wanawake bali pia husababishwa kushindwa kupangilia uzazi wa mpango kwa njia ya kufuatilia tarehe. Hivyo, katika makala hii itaangazia aina, sababu, dalili na njia ya matibabu.
Aina za kukosa hedhi
- Primary (ya awali): Hali hii hutokea ambapo binti ambaye ameshapevuka lakini bado hajaanza kupata hedhi.
- Secondary: Hali hiihutokea kwa wanawake ambao wameshapevuka na wameshaanza kupata hedhi ila kuna wakati hawapati hedhi, hali hii huweza kuwatokea hata miezi mitatu au zaid.
Amenorrhea ya awali (Primary Amenorrhea)
Hali hii hutokea wakati msichana hajawahi kupata hedhi kufikia umri wa miaka 15. Sababu zake zinaweza kua:
Matatizo ya Kijenetiki:
- Ugonjwa wa Turner (Turner syndrome): Hii ni hali ya kijenetiki inayowaathiri wanawake na hutokea wakati kromosomu moja ya X inakosekana au haipo kabisa. Hali hii siyo ya kurithi ila hutokea baada ya makosa kwenye ugawanyikaji wa seli wakati wa hatua za awali kabisa za ujauzito. Hali hii husababisha mfuko wa mayai (ovari) kushindwa kufanya kazi hivyo mwili unakosa sababu ya kutenegeneza ukuta wa damu ambao huja kuvunjika kama kusipokuwa na uchavushaji.
- Matatizo ya tezi ya adrenal: Tezi hizi hutumika kutengeneza Homoni mbalimbali ambazo moja ya kazi zake ni kuchunga mzunguko wa hedhi wa mwanamke. Matatizo ya tezi hizi huathiri uzalishaji wa homoni.
Matatizo ya maumbile:
- Kutokuwepo kwa mji wa mimba au uke.
- Imperforate hymen: Bikra iliofunika kabisa au ambayo haina uwazi, hivyo kuzuia damu ya hedhi kutoka.
Matatizo ya Homoni:
- Matatizo ya tezi ya pituitary au hypothalamus katika ubongo.
- Kushamiri kwa homoni za kiume
Amenorrhea ya Sekondari (Secondary Amenorrhea)
Hali hii hutokea wakati mwanamke ambaye alikuwa anapata hedhi kawaida kuacha kupata hedhi kwa miezi mitatu au zaidi. Sababu zake zinaweza kua:
- Ujauzito: Hii ni sababu kubwa ya kawaida inayoweza kusababisha mwanmke asione hedhi.
- Kunyonyesha Mtoto: Wakati wa kunyonyesha, mwili hutengeneza Homoni za Lactation ambazo huzuia hedhi.
- Kukoma kwa Hedhi (Menopause): wanaweke waliofika umri wa kukata kuona hedhi (miaka 45 –60), Ovari huacha kuzalisha Homoni haswa ya Estrogen ambayo husika na mzunguko wa hedhi.
- Matatizo ya Homoni: Ugonjwa wa Polycystic Ovary Syndrome (PCOS). Matatizo ya tezi ya thyroid (hypothyroidism, hyperthyroidism). Matatizo ya tezi ya pituitary kama vile uvimbe kwenye ubongo unaoathiri eneo la pituitary au hypothalamus.
- Matatizo ya Uzito: Uzito mdogo sana (kama watu wenye anorexia nervosa au utapia mlo). Uzito mkubwa sana (unene kupita kiasi).
- Mazoezi Makali: Mazoezi makali sana yanaweza kuathiri homoni. Na kupelekea kukata kwa hedhi.
- Msongo wa Mawazo (Stress): Msongo wa mawazo unaweza kuathiri homoni.
- Matumizi ya Dawa: Baadhi ya dawa zinaweza kusababisha kukata kwa (kama vile dawa za kupunguza msongo wa mawazo, dawa za shinikizo la damu, na dawa za saratani).
- Magonjwa Mengine: Uvimbe kwenye tezi ya Pituitary au Ovari. Asherman's Syndrome (makovu kwenye mji wa mimba). Magonjwa ya mfumo wa Endocrine kama ugonjwa wa Cushing, na kisukari ambacho Magonjwa ya mfumo wa chakula kama ugonjwa wa Celiac. Magonjwa ya mfumo wa kinga kama ugonjwa wa Addison.
Dalili zinazoweza kuambatana na kukata kwa hedhi ni:
- Mwili kupata wakati ambapo joto linapanda na kua kali.
- Chuchu kutoa/kuvuja maziwa.
- Uke kavu.
- Maumivu ya kichwa.
- Matatizo ya macho.
- Chunusi
- Ukuaji wa nywele nyingi kwenye uso(ndevu) na mwili wako.n.k
Umuhimu wa Uchunguzi
- Kama unakumbana na tatizo la kutokuona hedhi au kukata kwa hedhi, ni muhimu kuonana na daktari kwa uchunguzi kamili.
- Daktari atafanya vipimo vya damu ili kuangalia viwango vya homoni, ikiwa ni pamoja na homoni za tezi ya thyroid, pamoja na uchunguzi wa kimwili na labda ultrasound ili kuangalia matatizo yoyote ya anatomia.
Matibabu
Matibabu ya amenorrhea yatategemea sababu inayoisababisha;
- Matatizo ya tezi ya thyroid yanaweza kutibiwa na dawa za homoni.
- PCOS inaweza kutibiwa na dawa za kudhibiti homoni, kama vile vidonge vya uzazi wa mpango.
- Matatizo ya anatomia yanaweza kuhitaji upasuaji.
Ni muhimu kupata matibabu sahihi ili kuzuia matatizo zaidi, kama vile utasa na kudhoofika kwa mifupa.