Image

Kujumuika kula Chakula kwa Pamoja kama Familia ni Bora kwa Afya ya Mtoto

Watoto ambao hula chakula cha usiku pamoja na familia yao wanakuwa na afya njema kiakili na kimwili na wana uwezekano mdogo wa kupenda kunywa soda na vyakula hatarishi kwa afya (fast food)

Watafiti kutoka nchini Canada wanasema, watoto ambao mara kwa mara hula chakula pamoja na familia zao wanakuwa na afya njema ya kiakili na kimwili ukilinganisha na watoto ambao hawapati nafasi ya kula chakula pamoja na familia zao.

Watafiti hao wamegundua ya kwamba watoto hao wanapofikisha umri wa miaka 10 wanakuwa na afya njema kiakili, wachangamfu na uwezekano mdogo sana wakunywa vinywaji vyenye sukari kama soda ikiwa watakula chakula mara kwa mara pamoja na wazazi, ndugu au walezi wao.

Utafiti huu ulifanyika kwa muda wa miaka 10, na ulihusisha kuwafuatilia watoto tokea wakiwa wachanga mpaka walipotimiza umri wa miaka 10.

Watafiti hao wanasema,matokeo yao yanathibitisha  ile dhana ya kwamba,kula chakula kwa pamoja kama familia ni muhimu sana kwa binadamu na huleta manufaa mbalimbali kwa sababu  hujumuisha vipengele  vyote muhimu sana vya  mfumo  wetu maisha pamoja na afya za wazazi wetu.

Uwepo wa wazazi wakati wa kula chakula huwapatia nafasi muhimu sana watoto ya kujifunza kujumuika na wengine, kujadiliana kuhusu mambo mbalimbali ya kijamii na kutoa duku duku zao za kila siku na ni fursa adhimu ya kujifunza mijumuiko ya kifamilia kwenye mazingira wanayoyafahamu na salama kiakili’’ alisema Professor Linda Pagani, mtaalamu wa wa elimu ya kiakili kutoka Chuo Kikuu cha Montreal, Canada.

Uzoefu wa mawasiliano wanaopata watoto ni muhimu sana katika kuwajengea watoto uwezo  wa kuwasiliana  na watu wengine nje ya familia kwa kwa njia bora zaidi.

Matokeo yetu yameonyesha ya kwamba, chakula cha pamoja cha familia sio tu kinajenga mazingira mazuri nyumbani bali pia ni nafasi nzuri kwa wazazi  kuendelea kuwafunza na kuwaendeleza watoto kama  watu muhimu kwenye jamii,’’ aliendelea kusema Professor Linda Pagani

Professor Pagani alishirikiana na mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD student) Marie-Josee Harbec, katika kuwafanyia uchunguzi watoto waliozaliwa katika Jimbo la Quebec kati ya mwaka 1997 na 1998.

Watoto waliohusika kwenye tafiti hii,walianza kufuatiliwa tokea wakiwa na umri wa miezi mitano mpaka walipotimiza umri wa  miaka 10.

Walipofikisha umri wa miaka sita,wazazi wao walianza kutoa taarifa kama  walikuwa wakijumuika pamoja na watoto wao wakati wa kula chakula au la.Na pia walipotimiza umri wa miaka 10, wazazi,walimu na watoto wenyewe walitoa maelezo kuhusiana na ukuaji wao,tabia zao za maingiliano na watu wengine na afya zao  kiakili na kimwili.

‘’Tuliamua kuangalia faida za muda mrefu za kula chakula kwa pamoja kama familia kwa watoto na kulinganisha na watoto walio na umri sawa na watoto hawa lakini ambao wazazi,ndugu na walezi hawajumuiki nao wakati wa kula chakula,’’ aliendelea kusema Professor Linda Pagani.

Uwepo wa mjumuiko wa pamoja wakati wa kula chakula kwa watoto wenye umri wa miaka sita husababisha watoto hao kuwa na afya njema kiakili na kimwili wanapotimiza umri wa miaka 10.

‘’Kwa sababu tulikuwa na taarifa nyingi za watoto kabla ya kutimiza umri wa miaka sita,zikiwemo taarifa za kiwango chao cha hasira, uwezo wao kiakili,kiwango cha elimu ya wazazi wao, kujumuika  na mwingiliano wa familia, ilikuwa rahisi kwetu kuchanganua taarifa zetu na hivyo kupata matokeo mazuri ya tafiti yetu’’ alisema Dr. Harbec

Ushauri kutoka TanzMED

Ni vizuri kwa familia kuzingatia matokeo ya tafiti hii hasa kupenda kujumuika pamoja wakati wa kula chakula ili kuwasaidia watoto katika kujijengea uwezo wa kuwasiliana, kujiamini na kupata malezi mema.

Imesomwa mara 4829 Imehaririwa Jumatano, 06 Machi 2019 16:45
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.